KATIKA harakati zako za kutafuta mpenzi, unaweza
kukutana na mwanamke ambaye kwa sababu moja au nyingine anakwondolea uwezo wako
wa kufikiri, kutumia mantiki na pia kutumia akili yako ya kuzaliwa. Si lazima
awe amekufanyia kitu, lakini inaweza kuwa ni ulevi wako tu unaosababisha ufanye
mambo yasiyo ya kawaida. Pengine ndiyo maana baadhi ya wasanii huzungumzia
suala la “kudata” kutokana na mapenzi.
Ni jambo jema kudhani kuwa wewe na mpenzi wako mnapendana kwa dhati na kwamba
kila mmoja amefika kwa mwenzake, lakini kama mojawapo ya mambo haya kumi
yaliyoelezwa hapa chini litajitokeza, basi fahamu kuwa yamkini umependa kuliko
kawaida, yaani ni kama umenyweshwa sumu ya penzi. Kumbuka kupenda ni kuzuri,
lakini kupenda kupindukia kunaweza kukutumbukia nyongo, kwani katika kila jambo
kinahitajika kiasi.
1. WIVU WA KUPINDUKIA
Ni jambo jema kwa mwanamume kumtakia heri mpenzi wake na kufanya kila awezalo
kuhakikisha kuwa hapati madhara, lakini iwapo utakuwa mtu wa wasiwasi na
mashaka pale unapomwona mpenzi wako akizungumza na mwanamume mwingine, au
anapotoka na marafiki zake wa kike, au anapovaa nguo inayomfanya atamanishe,
basi fahamu kuwa tayari umekunywa sumu ya mapenzi.
Katika uhusiano wa kimapenzi, kuaminiana ni jambo muhimu sana. Kama kweli
unataka mpenzi wako akupende kwa dhati, mwoneshe kuwa unamwamini na unaheshimu
maamuzi yake, ikiwa ni pamoja na maamuzi ya kutoka na marafiki zake wa kike na
kuwa na marafiki wa kawaida wa kiume. Ondoa hofu na acha kabisa kumpeleleza,
maana wapo wanaume ambao hutumia muda wao mwingi kuwapeleleza wapenzi wao ikiwa
ni pamoja na kuwategeshea kamera na rekoda za simu.
2. KUTOMWACHIA NAFASI MPENZI
Kama huishi na mpenzi wako ni jambo la kawaida kuwa na hamu ya kumwona mara kwa
mara, lakini kumbuka kuwa mpenzi wako naye ana maisha yake na anahitaji nafasi
ya kuwa peke yake kwa ajili ya mambo yake binafsi.
Hisia za kutaka kuwa na mpenzi wako muda wote zinaweza kudhaniwa kuwa ni za
mapenzi ya dhati, lakini kwa hakika hiyo si ishara njema ya mapenzi ya kudumu.
Hebu jiulize kama unaweza kuendeleza hali hiyo maisha yako yote. Ni wazi kuwa
utachoka. Kwa hiyo, mpe mpenzi wako fursa ya kupumua. Namna hii mpenzi wako
atajenga hamu ya kutaka kukutana nawe lakini ukiwa naye muda wote hamu hiyo
itaisha.
3. KUMWAMULIA MPENZI MAMBO YAKE
Unaweza kujikuta ukisukumwa kumwambia mpenzi wako awe anavaa nini wakati gani,
akutane na nani na kwa wakati gani au ale nini. Ukiona hivyo, fahamu kuwa hayo
si mapenzi, bali umepitiliza na pengine mwisho wa uhusiano wenu unanukia.
Hata ukiachilia mbali suala zima la usawa wa jinsia, hakuna mwanamke ambaye
angependa apangiwe kila kitu kuhusiana na maisha yake. Kama ilivyodokezwa hapo
juu, kila mtu ana maisha yake na kilichowaunganisha ni mapenzi tu. Kama utataka
kumpangia kila kitu ni wazi kuwa utaishia kuishi peke yako.
4. KUMUULIZA MPENZI MASWALI
Iwapo utajikuta ukimuuliza mpenzi wako maswali mengi yanayoonesha wasiwasi wako
kuhusiana na mwenendo wake, fahamu kuwa kuna tatizo na tatizo hilo lisipopatiwa
ufumbuzi utakuwa mwanzo wa mwisho wa uhusiano wenu.
Mwanamke angependa umuulize maswali ya kawaida kuhusiana na jinsi siku yake
ilivyokuwa na kama marafiki zake hawajambo au la, lakini kila jambo lina mpaka
wake. Mwanamke hatarajii kuwa kila mnapokutana atakuwa kama ameingia kwenye
chumba cha mtihani au usaili wa kazi.
5. KUTOAMINI ANACHOKWELEZA MPENZI
Wakati mwingine watu hushindwa kuwaamini wenzao, lakini kwa sababu ambazo ni za
msingi, lakini kuna wakati ambapo mtu hushindwa kumwamini mwenzake bila sababu
yoyote ya msingi, au kwa sababu zisizo sahihi, kisingizio kikiwa ni mapenzi.
Kuna tatizo la kisaikolojia la kujishuku au kuwashuku wenzako. Hili ni jambo
ambalo linaweza kukuharibia mustakabali wako katika mapenzi, maana husababisha
kujengeka kwa mazingira ya kutokuaminiana. Ili uweze kwenda sanjari na mpenzi
wako, amini kila anachokweleza hadi pale utakapokuwa na sababu za msingi za
kutokumwamini. Na hata unapokuwa umelithibitisha jambo, endelea kuwa katika
uhalisia wako.
6. KUACHA HOBI, MARAFIKI
Mahusiano ya kimapenzi mara nyingi huhusisha kila mmoja kuacha baadhi ya mambo
yake kwa ajili ya mwenzake. Hata hivyo, lengo ni kuweka tu uwiano wa mahitaji,
si kuacha kila kitu ulichokuwa nacho kwa ajili ya mwenzako, ama kwa shinikizo,
au kwa kulewa penzi.
Iwapo utabaini kuwa marafiki zako sasa wamekuwa ni marafiki zako wa zamani na
hobi zako zimebaki tu katika kumbukumbu japo kwa hakika bado unahisi mapenzi
katika hobi hizo, basi tambua kuwa huyo mrembo wako amekunywesha sumu ya penzi
na sasa huwezi hata kuitumia vema mantiki yako.
Mbaya zaidi, iwapo utabaini kuwa marafiki zako wapya ni marafiki wa siku zote
wa mpenzi wako na hobi zako ni zile za mpenzi wako, basi tambua kuwa huna tena
nafsi yako, bali umejisalimisha mzima mzima kwa mpenzi wako. Lakini msemo mmoja
wa hekima unatwambia usiweke mayai yako yote kwenye kikapu kimoja. Yamkini
unaelewa.
7. KUKUBALI KUPELEKESHWA
Pengine unakumbuka kuwa kuna nyakati ambapo ulikuwa na uwezo wa kujikita katika
jambo moja na kulifanya kwa umakini, huku ukiwa pia mwerevu, mjanja na
unayejisimamia, lakini leo unayeyuka kirahisi tu kama barafu iliyowekwa juani!
Hii ni hatari kwa mustakabali wa maisha yako.
Mbaya zaidi ni pale utakapoiacha kazi yako inayokulipa vizuri na kufanya kazi
nyingine kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako. Ukifika hali hii ujue wewe
mwenyewe kuwa hapo hakuna mwanamume.
8. UTAYARI WA KUFA KWA AJILI YAKE
Umewahi kujisikia kuwa na utayari wa kufa kwa ajili ya mpenzi wako? Kama jibu
ni “ndiyo”, basi fahamu kwa hakika kuwa hayo uliyo nayo si mapenzi bali ni
upumbavu. Pengine huku ndiko kunywesha sumu ya mapenzi. Kwa hakika, hakuna
mwanamke ambaye anastahili kumfanya mwanamume yeyote kufa kwa ajili yake.
Yamkini wanaume wanaolengwa katika makala haya si wavulana wanaosoma sekondari,
waliobalehe majuzi, ambao wakipenda au kupendwa hujiona kama wako katika sayari
yao. Mwanamume aliyepevuka hujiamini na hayaweki maisha yake yote mikononi mwa
mwanamke, hata kama mwanamke huyo angekuwa ndiye mrembo wa dunia.
Iwapo, ama kwa ujinga au kwa kufahamu umewahi kumwambia mpenzi wako: “Ukiniacha
nitajiua,” na ukawa unaamini hivyo kabisa, basi yamkini unahitaji kutafuta
msaada wa ushauri nasaha, maana kwa hakika umepotoka.
9. MUDA WOTE UNAWASILIANA NAYE
Vijana wa siku hizi ni watumiaji wazuri sana wa simu, lakini iwapo utabaini
kuwa asilimia kubwa ya muda wako unautumia ama kwa kuongea au kuwasiliana kwa
ujumbe mfupi na mpenzi wako, basi fahamu kuwa kuna tatizo ambalo linahitaji
ufumbuzi wa haraka.
Kumbuka kuwa mapenzi hayachukui nafasi ya kila kitu. Yamkini huyo mpenzi wako
amekukuta unaishi na kuna mambo ya muhimu ya kufanya. Hebu achana na simu
kwanza ufanye mambo ya muhimu kuhusiana na maisha yako. Kama mpenzi wako
hakwelewi katika hili basi hakufai.
10. NDUGU ZAKE WANAKUFUATILIA
Iwapo utabaini kuwa marafiki, ndugu na jamaa za mpenzi wako wanamtonya mpenzi
wako kuhusiana na kile wanachokiita mwenendo wako mbaya, usipuuze hali hii.
Kuna uwezekano mkubwa kuwa watu hawa wanayo sababu ya kuwa na wasiwasi na
mwenendo wako, kwa hiyo jichunguze na kuangalia jinsi unavyoenenda.
Hata hivyo, jambo hili si ishara njema ya mustakabali mwema wa uhusiano wenu.
Iwapo mpenzi wako ataweka watu wake wakufuatilie, maana yake halisi ni kwamba
hakuamini. Katika hali kama hii, haitarajiwi kuwa mustakabali wa uhusiano wenu
utakuwa mzuri, kwani kutakuwa na uingilizi mwingi wa ndugu, jamaa na marafiki
zake. Unaweza kukubali kuendelea kuishi katika hali hii kwa kisingizio cha
mapenzi, lakini ukweli ni kwamba hayatakuwa mapenzi bali karaha.
KUWA MAKINI
Kama unavyoona, hizi ni baadhi tu ya dalili kuwa mapenzi yako kwa mwanamke sasa
yanaelekea katika ulevi, mithili ya ule wa dawa za kulevya. Jambo moja la
kukumbuka ni kwamba kweli mapenzi ni kitu kizuri, lakini pia mapenzi yanahitaji
kuwa jambo linaloashiria mustakabali mwema kwa wahusika wawili. Yakiwapo mambo
haya kumi hauwezi kuwapo mustakabali mwema katika mapenzi.
No comments:
Post a Comment