CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kipo njiapanda, baada ya vigogo wake ambao
ni wabunge, kuamua kuchukua fomu za kuwania uongozi ndani ya chama
hicho, katika ngazi ya wilaya, kinyume cha kanuni za uchaguzi.
Marekebisho
ya katiba yaliyofanywa na chama hicho katika kikao chake cha Februari
12, mwaka huu yanawazuia wabunge kugombea nafasi za uongozi ndani ya
chama katika ngazi ya wilaya kama hatua ya kutoa fursa kwa wanaCCM
wengine kujaza nafasi hizo za uongozi.
Kwa mujibu wa marekebisho
hayo, mbunge ataruhusiwa kugombea nafasi za uongozi wa chama ikiwa
atapewa kibali cha Kamati Kuu (CC). Pia itafanya hivyo kwa kuzingatia
mazingira maalumu ya maombi yatakayowasilishwa na kamati ya siasa ya
wilaya au mkoa.
Mabadiliko hayo, pia ndiyo yaliyohamishia ujumbe
wa NEC kutoka katika ngazi ya mkoa kwenda wilaya, uamuzi ambao umeanza
kutekelezwa katika mchakato wa uchaguzi unaoendelea hivi sasa.
Hata
hivyo, kipengele hicho cha katiba ambacho kupitishwa kwake kulipata
upinzani mkubwa kutoka kwa wabunge wa chama hicho, kinaonekana kupuuzwa
kutokana na wengi wao kujitokeza, wakiwamo mawaziri na kuchukua fomu za
kugombea uongozi kinyume cha katiba ya chama chao.
Miongoni mwa
vigogo waliochukua fomu ni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),
Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora),
George Mkuchika na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Abdallah
Kigoda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji),
Dk Mary Nagu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine
ni Wabunge Deo Filikunjombe(Ludewa), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk
Hamis Kigwangalla (Nzega ), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Godfrey
Zambi (Mbozi Magharibi), Seleman Nchambi (Kishapu), Luhaga Mpina
(Kisesa), Dk Titus Kamani (Busega), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi),
John Komba Mbinga Magharibi, James Lembeli (Kahama), Ahmed Salum
(Solwa).
Habari kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa suala
hilo tayari limeanza kuwaumiza vichwa vingozi wa CCM, kutokana na wingi,
pia aina ya wabunge walioamua kuingia katika kinyang’anyiro ilhali
mazingira ya kugombea kwao yakithibitisha kutokuwapo kwa udharura.
“Ni
kweli kwamba tupo njiapanda kwa sababu hapa chama lazima kiamue ama
kufuata kanuni au kutumia mwanya uliowekwa kuwaruhusu wote wagombee,
lakini hata kikifanya hivyo maana ya marekebisho hayo haitakuwepo,”
alisema mmoja wa watoa habari wetu ndani ya CCM na kuongeza:
“Wewe
fikiria ikiwa kwa mfano watamkatalia mtu kama Lowassa, Profesa
Mwandosya au Mkuchika (George), hilo unadhani linawezekana? Hapo si
watakuwa wanatafuta ugomvi tu.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu suala hilo, hakuwa tayari
kulizungumzia akisema, bado ni mapema mno kwani kuna vikao vingi vya
chama kabla majina ya wagombea kuwasilishwa mbele ya vikao vya juu
ambavyo ni CC na NEC.
“Mimi nadhani bado ni mapema, ijapokuwa ni
kweli kwamba tulipitisha mabadiliko hayo, lakini naamini kamati husika
katika ngazi za mikoa na wilaya zinafahamu wajibu wake. Kama hivyo
ndivyo, basi tusubiri majina yakifikishwa kwetu ndipo tunaweza kutoa
tamko.
Wabunge hawajui mabadiliko
Baadhi ya
wabunge waliochukua fomu kugombea walisema, wamefanya hivyo kwani
wanavyofahamu, kanuni bado hazijabadilika na kwamba kilichopo ni
mapendekezo ambayo hadi sasa bado hayajapitishwa na vikao husika.
Filikunjombe
alisema: “Kwanza ninavyofahamu, kanuni na katiba havijabadilishwa kwani
yalikuwa ni mapendekezo tu, kwa hiyo hakuna kinachotuzuia sisi wabunge
kugombea. Pili niseme kwamba jambo lolote linalogusa wabunge, linapaswa
kujadiliwa na kupata mwafaka katika vikao vya chama”.
Kwa upande
wake, Zungu alisema CCM hakikuwahi kupitisha azimio la kuwakataza
wabunge kugombea nafasi mbalimbali kwenye chama hicho.
Alisema ni
haki ya mwanachama yeyote kuchagua au kuchaguliwa na kwamba wabunge
wanaruhusiwa kugombea nafasi yoyote kwenye chama… “Sijawahi kusikia kitu
kama hicho katika CCM, ni ruksa kugombea nafasi mbalimbali ikiwa vikao
vitakupitisha.”
Dk Kigwangalla alisema, anakumbuka liliwahi
kutolewa wazo la kuwazuia wabunge kugombea nafasi kwenye chama lakini
halikupitishwa na NEC… “Halikupitishwa wazo hilo hivyo wabunge
wanaruhusiwa kugombea nafasi za uongozi kwenye chama. Hakuna kizuizi
chochote.”
Mabadiliko ya Katiba
Katika kikao
chake cha Februari 12, mwaka huu Nec ilipitisha mabadiliko ya katiba kwa
kuzifanya nafasi za ujumbe wa Nec na wenyeviti wa wilaya na mikoa, kuwa
ni kazi za muda wote kwa lengo la kuwaweka viongozi hao kuwa karibu na
wanachama na kushughulikia matatizo yao.
Kwa kuzingatia mabadiliko
hayo, ni dhahiri kwamba wabunge na madiwani hawezi kuwania nafasi za
uongozi ndani ya chama, kwani wanazuiwa na Kanuni ya Uchaguzi ya CCM,
toleo la Februari, 2010.
Kifungu cha 22 cha kanuni hiyo kinasema:
Mwanachama ambaye anaomba nafasi ya uongozi ambayo ni kazi ya muda wote,
hataruhusiwa kushika nafasi ya aina hiyo zaidi ya moja katika chama
isipokuwa Kamati Kuu imeamua vinginevyo.
Pia, Kifungu cha 23
kinataja nafasi za uongozi za muda wote kuwa ni mwenyekiti wa tawi au
mtaa, mwenyekiti wa kata au wadi, mwenyekiti wa jimbo au wilaya,
mwenyekiti wa mkoa, makatibu wa halmashauri kuu wa ngazi zinazohusika,
diwani, mwakilishi na mbunge.
Uamuzi wa Nec kuongeza nafasi
wajumbe wa wilaya katika orodha ya nafasi za muda wote, uliwaengua
wabunge, wawakilishi na madiwani kugombea nafasi ndani ya chama.
Hata
hivyo, wabunge na wawakilishi hawakuzuiwa kugombea nafasi za Nec katika
viti 10 vya Tanzania Bara na Visiwani au katika jumuiya za chama hicho
ambazo ni Wazazi, UWT na UVCCM.
Katika marekebisho hayo, wajumbe
wa Nec watakuwa ni wajumbe 10 kutoka Tanzania Bara, 10 kutoka Zanzibar,
10 wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, wajumbe wanaoingia kwa nafasi
zao, wajumbe 221 wanaochaguliwa kutoka wilayani na wanaotoka kwenye
vyombo vya uwakilishi; wabunge 10 na wawakilishi watano.
Wengini ni wajumbe kutoka jumuiya za chama; wanaochaguliwa na UWT 15, UVCCM 10 na Wazazi watano.
Wakati
marekebisho hayo yakiwa bado ni mapendekezo, wabunge wa CCM walianzisha
mpango wa kuyapinga, lakini walipokutana na Mwenyekiti wa chama hicho,
Rais Jakaya Kikwete, mjini Dodoma waligeuka mabubu na kushindwa
kuzungumzia.
Miongoni mwa malalamiko hayo, yalikuwa ni kwamba
marekebisho ya Katiba hayakuwashirikisha wakiwa ni wadau na kwamba kwa
kufanya hivyo, kulikuwa na lengo baya la kuwaengua kushiriki shughuli za
chama.
Taarifa hizo ziliwanukuu wabunge hao wakidai kuwa
suala hilo, linahitaji mjadala wa kitaifa ili kutoa wigo mpana kwa
wanachama kutoa mawazo yao. Hata hivyo, baadaye CC na Nec walipitisha
mabadiliko hayo ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika uchaguzi wa sasa.
Chanzo ni Mwananchi
No comments:
Post a Comment