NJOMBE

NJOMBE

Monday, September 3, 2012

Polisi waua tena kikatili • RPC adai anakaribia kustaafu, hawezi kuruhusu mikutano ya CHADEMA

KATIKA hali inayoonyesha watawala wamedhamiria kuigeuza nchi hii dola ya kipolisi, jana Jeshi la Polisi liliua mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyekuwa anaripoti habari za ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani hapa.
Habari za awali zilisema Mwangosi aliuawa kwa bomu lililorushwa na polisi waliotaka kuzuia CHADEMA kufungua tawi katika Kijiji cha Nyololo.
Wakati viongozi na wanachama walipokuwa wakiendelea na ufunguzi wa tawi la pili kijijini hapo, ghafla walivamiwa na askari polisi, ambao walianza kuwashambulia wananchi. Askari wapatao wanane ndio walimvamia Mwangosi.
Wakati askari hao wakiendelea kumshambulia, ghafla lilirushwa bomu kuelekea eneo walikokuwa, likampiga Mwangosi na kumkata vipande vipande na kutoa utumbo wake nje.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia askari hao wakimshambulia mwandishi huyo na wananchi wengine, huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michale Kamuhanda akiwa eneo la tukio.
Alipofuatwa na kuombwa awazuie askari wake kumshambulia mwandishi huyo, kamanda huyo alifunga vioo vya gari lake, akapiga honi mara kadhaa, na akaondoka. Baada ya RPC kuondoka eneo hilo, ndipo bomu lilirushwa na kumfumua mwandishi utumbo.
Baadhi ya akina mama walikatika miguu, wakakimbizwa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu. Baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliokuwapo nao walijeruhiwa kwa kipigo, wakiwamo Hamad Yusuph, Benson Kigaila, Deogratius Sihale na wengine.
Wengine wakiwamo mwandishi wa habari hizi aliyejeruhiwa mkono, Godfrey Mushi wa gazeti la Nipashe na Oliver Moto wa Star TV, walikimbilia katika pori la Nyololo.
Alipopigiwa simu Kamanda wa Polisi hakutaka kuzungumza lolote zaidi ya kusema kuwa yupo kwenye mwendo wa kasi, hivyo hawezi kuzungumza. Akakata simu yake ghafla.
Gazeti hili lilitaka kumuuliza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, kama vitendo hivi vya polisi kuua wananchi ni agizo la serikali au utashi binafsi wa polisi kuzuia wananchi kufanya kazi zilizo haki yao kikatiba, simu ilipokewa na mtu aliyejitambulisha kama PC Seleman, akasema ofisi ya IGP haikuwa na taarifa za tukio hilo. Ilikuwa saa 12:21 jioni.
Alisema, “mwandishi nitakupigia baadaye IGP hadi sasa yupo katika mkutano ngoja tuanze kufuatlia kujua maana hatuna taarifa hadi sasa.” Hadi tunakwenda mitamboni, hakupiga simu kama alivyokuwa ameahidi.
Kabla ya tukio hilo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, alizungumza na waandishi wa habari alisema msisimko wa mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea hivi sasa nchini hauwezi kusimamishwa na Serikali ya CCM, hata kama wataamua kuwaua viongozi wote wa CHADEMA.
Dk. Slaa alikuwa akizungumzia hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yao ya ujenzi wa chama inayoendelea mkoani hapa. Aliahidi kuendelea, licha ya jeshi hilo kuapa kuizuia kwa gharama yoyote.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamuhanda, alisema awali kwamba anaipenda kazi yake, hivyo hawezi kuruhusu mikutano katika mkoa wake mpaka atakapopata maelezo ya ziada.
Alisema: “Ni kweli jana saa mbili tuliwapa barua ya kuruhusu shughuli zao ila hili ni agizo na mimi ninakaribia kustaafu na kazi yangu ninaipenda, hivyo siwezi kuruhusu maandamano kinyume na maagizo yaliyopo.”
Alisema CHADEMA hawawezi kufanya mikutano kwa kuwa hawana jeshi wala vifaa vya kupambana na Jeshi la Polisi, hivyo wakijaribu kutotii sheria ni lazima washurutishwe.
Dk. Slaa alisema alipopata taarifa za kusitisha mikutano juzi, alimpigia IGP Mwema kutaka ufafanuzi kwani makubaliano yao ya awali yalikuwa kwamba wasitishe mikutano kwa siku nne au tano kisha waendelee na ratiba yao.
“Katika nia njema nilimpigia IGP kujadiliana juu ya hili. Hakupokea simu mpaka nilipomtumia ujumbe mkali, akaniambia angepiga saa mbili usiku; pia hakufanya hivyo. Na nilipomtafuta alisema zuio linaendelea.
“Nikamuuliza kwa nini watu ambao ni asilimia tano ya Watanzania wote, tena wakiwa wameelekezwa wawatafute waandikishaji wa sensa kwa namba za simu, wawe sababu ya kuzuia shughuli zetu halali? Mwema hakuwa na jibu,” alisema Dk. Slaa.
Alisisitiza hata baada ya kushindwa kutolea maelezo hoja hiyo, IGP alisema hilo ni agizo na ni lazima litekelezwe kwa sababu ni amri iliyotolewa kisheria.
Dk. Slaa alisema hata alipomuuliza ni sheria gani inayozuia hali hiyo, hakumjibu huku akisisitiza amri yake ifuatwe.
“Sisi hatuna bunduki, hatuna mabomu wala majeshi, lakini Serikali ya CCM na polisi wanapaswa kutambua haya tunayoyafanya ni sawa na gharika. Kuyazuia ni vigumu, hata kama watatuua viongozi wote, watambue mioyo ya Watanzania itaendelea kulilia mabadiliko haya,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kuwa hata barua ya awali ya msajili wa vyama vya siasa haikutoa agizo la kusimamisha shughuli za kisiasa, bali ilikuwa ikitoa rai juu ya umuhimu wa suala hilo, jambo alilosema walilisikiliza kwa ajili ya uzalendo wao kwa nchi.
Naye Mkuu wa Operesheni ya M4C, Benson Kigaila, alisema kuwa mikakati ya polisi kuzuia mikutano ya CHADEMA ni mipango ya CCM.
Alisema Agosti 4, 2012, walipokuwa wakijiandaa kufanya mikutano yao katika Mkoa wa Morogoro, Jeshi la Polisi lilizusha sababu mbalimbali zisizo za msingi na kwamba hata walipotumia busara ya kukubaliana nao bado waliendelea kubuni hila chafu za kuzuia mikutano ya CHADEMA.
Wachambuzi wa kisiasa walisema hii ni dalili kwamba serikali imezidiwa, na sasa imeamua kuigeuza Tanzania kuwa dola ya kipolisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vox Media, Ansbert Ngurumo, alisema katika dola za namna hiyo, serikali hutumia nguvu polisi kuzima na kunyamazisha harakati za kisiasa, kijamii na kiuchumi za watu wake, kwa kisingizio cha usalama.
Katika dola ya kipolisi, serikali huzuia mijumuiko, mikutano na maandamano ya wananchi, ili kudhibiti wananchi kuipinga au kukosoa.
Alisisitiza: “Katika kufanya hivyo, polisi huumiza na kuua wananchi, ikidhani kwa kufanya hivyo inaua upinzani. Lakini historia imeonyesha kuwa mahali pote ambapo serikali imetumia mabavu kutisha na kunyamazisha wapinzani, chama tawala kimeanguka, ama katika sanduku la kura au kwa mapinduzi ya aina yoyote.”
Jukwaa la Wahariri, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Neville Meena, lilisema, “tunalaani kitendo cha polisi kutumia nguvu kiasi cha kusababisha kifo cha mwandishi. Kitendo hiki hakikubaliki, na kinadhihirisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.” Hata hivyo, Meena alisema Jukwaa litatoa taarifa rasmi baadaye leo.
Mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Ndimara Tegambwage, alisema: “Sasa polisi wamewageukia waandishi wa habari. Mabavu yao haya yataishia wapi? Mwandishi kafia vitani; mazingira ya kisiasa hapa Tanzania yanazidi kuwa mabaya. Hii sasa ni vita; ni muhimu waandishi wa habari wapewe mbinu za kuandika habari za kivita.” Baadaye aliandika onyo kwa polisi.
Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment