Waziri wa sheria wa Afrika
Kusini ametaka ufafanuzi zaidi kuhusu wachimba migodi 270, walioshtakiwa
kwa kosa la mauaji ya wachimba migodi wenzao waliouawa kwa kupigwa
risasi na polisi.
Waziri Jeff Radebe alisema kuwa uamuzi wa
kuwafungulia mashtaka wachimba migodi hao, uliwashtua wengi na
kusababisha wasiwasi miongoni mwa watu nchini humo.Inaarifiwa viongozi wa mashtaka waliwafungulia mashtaka wachimba migodi hao kwa misingi ya kanuni za kosa la kutendwa kwa nia moja ambayo ilitumika sana wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi.
Uamuzi huo tayari umekashifiwa vikali na mawakili ya kikatiba.
Katika taarifa yake, waziri Radebe, alisema kuwa kulingana na katiba , waziri wa sheria ndiye ana usemi mkubwa juu ya mamlaka ya kitaifa kuhusu mashtaka.
Alisema kuwa ameagiza kiongozi wa mamlaka hiyo kumpa maelezo kuhusu sababu za uamuzi waliouchukua.
Polisi waliwapiga risasi wachimba migodi 34 wiki mbili zilizopita wakati wa mgomo wao katika mgodi wa madini ya Paltinum wa Marikana , unaomilikiwa na kampuni ya Lonmin, ambayo ni ya tatu kwa ukubwa wa uzalishaji wa madini hayo.
Hata hivyo polisi walitetea hatua yao wakisema walilazimika kuwafyatulia risasi wachimba migodi hao, walipokuwa wanakabiliana nao wakiwa wamejihami kwa mapanga.
Sita kati ya wachimba migodi hao 270 waliokamatwa na polisi wangali hospitalini wakiuguza majeraha yao.
Walifunguliwa mashtaka siku ya Alhamisi baada ya viongozi wa mashtaka kusema kuwa walikuwa miongoni mwa kundi la watu ambao vitendo vyao vilisababisha polisi kuwafyatulia risasi.
No comments:
Post a Comment