Waandishi wa habari nchini
Tanzania hii leo walifanya maandamano ya kimya kimya kulaani kuuawa kwa
mwandishi mwenzao Daudi Mwangosi.
Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam ambalo
ndilo lenye idadi kubwa ya waandishi nchini, maandamano hayo yalianza
katika kituo cha runinga cha Chanel Ten na kumalizikia katika uwanja wa jangwani.Hapo jana chama cha Upinzani nchini Tanzania Chadema, kilimtaka rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kimahakama itakayochunguza kifo cha mwandishi huyo kwa madai kwamba hawana imani na kamati iliyoundwa na waziri wa mambo ya ndani kwa maelezo kuwa haina mamlaka ya kisheria.
Huku mazingira yaliyopelekea kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi yakiwa bado yamegubikwa na utata, chama cha Demokrasia na maendeleo kimewataka waziri wa mambo ya ndani Emmanuel Nchimbi na mkuu wa jeshi la polisi Said Mwema kuachia ngazi mara moja kama njia ya kuwajibika.
Mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe, amesema kuwa Chadema haina imani na kamati iliyoundwa na waziri Nchimbi kwa madai kwamba imekosa mamlaka ya kisheria.
Hivyo amemtaka rais Jakaya Kikwete aunde tume ya kimahakama itakayochunguza kifo cha mwandishi huyo na kwamba, iwapo hayo hayatatekelezwa, chama hicho kitafanya maandamano makubwa.
Katibu mkuu wa jukwaa la wahariri nchini Tanzania, Nevil Meena alisema kuwa tukio la kuuawa kwa mwandishi huyo wa habari marehemu Daudi Mwangosi tarehe mbili mwezi huu katika kijiji cha Nyololo huko mkoani Iringa, kumeibua hisia kali miongoni mwa waandishi wa habari pamoja na wanaharakati huku wengi wao wakihoji usalama wa waandishi wanapokuwa kazini hasa katika mazingira magumu.
No comments:
Post a Comment