Shirika la kuwahudumia wakimbizi la umoja wa mataifa, UNHCR,
limeomba Israel kuruhusu kikundi cha wahamiaji wa kiafrika kuingia nchini
humo.
Wahamiaji hao wamekwama katika mpaka wa nchi hiyo na Misri kwa wiki moja
sasa.Waziri wa mambo ya ndani wa Israeli Eli Yishai, anasema sio kwamba hawahurumii wahamiaji hao kwa sababu ya masaibu wanayopata, lakini hofu yake ni kuwa ikiwa wataruhusiwa kuingia Israel, huenda hatua hiyo ikiwafanya mamia ya wahamiaji wengine kuingia nchini humo.
Israel imekuwa na visa vya ubaguzi wa rangi kwa wahamiaji wa kiafrika serikali ikiwafananisha na saratani.
Mnamo mwezi Juni, wahamiaji wanne wa kiafrika walijeruhiwa baada ya makaazi yao kuteketezwa na watu walioaminika kuwa wenyeji mjini Jerusalem.
Baada ya shambulio hilo ukawekwa ujumbe ukutani kuwataka wageni kuondoka eneo hilo. Katika siku za karibuni kumekua na hisia kali nchini Israel kuhusu jinsi ya kushughulikia wahamiaji elfu 60 kutoka Afrika.
Sheria mpya ilipitishwa nchini Israel kuwapa mamlaka maafisa wa uhamiaji kuwazuilia korokoroni wahamiaji haramu kwa miaka mitatu.Waathiriwa wa shambulio la wakati huo walikuwa raia wa Eriterea ambapo walipata majeraha ya moto mikononi.
Msemaji wa polisi nchini Israel Micky Rosenfeld aliambia BBC kwamba sio siri waafrika weusi wamekuwa wakilengwa na wenyeji.
Katika majuma ya karibuni ghasia zilitokea miji kadhaa ya Israel wanakopatikana wahamiaji wa kiafrika. Kusini mwa jiji kuu Tel Aviv biashara za waafrika zilishambuliwa huku waafrika wenyewe wakikejeliwa hadharani.
Polisi wanasema takriban wahamiaji elfu 60 wa kiafrika wanaishi Israel ambapo 35,000 wakikaa Tel Aviv na 5,000 wakiwa mjini Jerusalem.
No comments:
Post a Comment