Usalama umeimarishwa katika eneo
la Tana River baada ya siku mbili za mashambulizi ya kulipiza kisasi
kati ya jamii za Pokomo na Orma.
Watu arobaini na wawili walifariki katika mashambulizi ya hapo jana ambapo zaidi ya watu miatatu walishambulia vijiji vinne.Waziri mkuu Raila Odinga alisema kuwa mauaji hayo huenda yakatafsiriwa kwa misingi ya mkataba wa Roma.
''Mashambulizi haya yamepangwa na yamekuwa yakiendelea kwa muda. Hili sio tukio la ghafla bali limepangwa kwa umaakini mkubwa na kisha kutekelezwa.'' alisema waziri mkuu. ''Ni makosa yanayoweza kupelekwa katika mahakama ya kimaitaifa ya uhalifu wa kivita'', alisema Raila.
Wabunge wa eneo hilo waliowasilisha hoja hiyo wanataka mkutano na rais Mwai Kibaki kuhusu mgogoro unaoendelea huko.
Hali ya kibinadamu katika eneo hilo inasemekana kuzorota kila kukicha ingawa shirika la Red Cross na mashirika mengine ya kijamii yanatoa misaada kwa waathiriwa.
Mnamo siku ya Jumatatu, watu 38 waliuawa katika mapigano mapya yaliyozuka katika eneo hilo siku tatu tu baada ya watu 12 wa kabila la Pokomo kuuawa katika mashambulizi yaliyofanya na jamii hasimu ya Orma.
Polisi 11 ni miongoni mwa waliouawa katika makabiliano hayo.
Kulingana na Red Cross, nyumba ziliteketezwa moto baada ya kijiji kimoja kuvamiwa.
Tukio hilo linajiri baada ya mashambulizi mengine kutokea kwenye eneo hilo la Tana River na kusababisha vifo vya karibu watu kumi na saba.
Polisi kwa usihirikiano na shirika la msalaba mwekundu waliweza kuokoa manusura. Inaarifiwa watu wameanza kuhama eneo hilo la Tana River kukimbilia usalama wao.
Mwezi jana zaidi ya watu 50 waliuawa katika mapigano mengine kati ya jamii za Pokomo na Orma.
Hizi ni ghasia mbaya zaidi kushuhudiwa hivi karibuni tangu zile za mwaka 2007 kufuatia uchaguzi uliozua utata mkubwa.
Jamii ya wapokomo ambao ni wakulima wanaoishi katika eneo la mto Tana huzozana mara kwa mara na jamii ya wafugaji ya Orma chanzo kikiwa malisho na maji.Lakini wadadisi wanasema sio mzozo kuhusu malisho ndio unasababisha mashambulizi haya bali huenda yamechochewa kisiasa.
Serikali ya Kenya imelaumiwa sana kwa kujikokota katika kuchukua hatua za kusitisha mashambulizi haya ya kulipiza kisasi ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda mrefu huko Tana River.
Wito umetolewa wa kuwapokonya silaha makundi ya watu waliojihami ili kukomesha mashambulizi hayo.
No comments:
Post a Comment