Mahakama nchini
Afrika Kusini inatarajiwa kuwaachilia huru wachimba migodi 270
waliofikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji ya wachimba migodi wenzao 34
waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Mashtaka hayo yaliyofikishwa mahakamani kwa
mujibu wa kanuni ya enzi ya ubaguzi wa rangi, yaliakhirishwa kwa muda
baada ya malalamiko ya umma.Wachimba migodi wa kwanza miamoja wataachiliwa leo wengine wakisubiri kuachiliwa siku ya Alhamisi.
Mazungumzo yanayolenga kusitisha mgomo wa wachimba migodi hao wa mgodi wa madini ya Platinum wa Marikana, yataanza leo.
Polisi wanadai kuwa walilazimika kuwafyatulia risasi wachimba migodi hao kama hatua ya kujilinda kwani na wao walikuwa wamejihami kwa mapanga wakati wakikabiliana nao.
Mgomo wao ulioitishwa kulalamikia nyongeza ya mishahara pamoja na kutaka chama chao kipya cha wafanyakazi kutambuliwa, ungali unaendelea huku mgodi ukisalia kufungwa kwa wiki tatu sasa.
Hata hivyo kampuni inayomiliki mgodi huo, Lonmin, ambayo ndio ya tatu kwa ukubwa wa uzalishaji wa madini hayo, imesema kuwa mgomo huo ni haramu.
Lakini imetupilia mbali matakwa yake kuwa ikiwa wafanyakazi hao hawatarejea kazini , watafutwa kazi.
Baada ya ufyatuliaji risasi, viongozi wa mashtaka wa serikali, walitumia kanuni ya enzi ya ubaguzi wa rangi ya kosa la ujumla kuweza kuwafungulia mashtaka wachimba migodi 270 waliokamatwa wakati wa vurugu baada ya mgomo wao kuwalazimisha polisi kuwafyatulia risasi.
Kanuni hiyo ilitumika na walowezi wa kizungu wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi kuwanyanyasa wapinzani wao waafrika weusi.
No comments:
Post a Comment