NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, September 4, 2012

Wachimba Migodi 122 waachiliwa Afrika Kusini


Wachimba migodi walioachiliwa
Wachimba migodi mia moja ishirini na wawili wa kampuni ya Lonmin yenye kuchimba madini ya Platinum wameachiliwa huru na Mahakama ya Kharankuwa iliyoko kaskazini mwa Pretoria.
Mara tu baada ya kuachiliwa wachimba migodi hao walikaribishwa nje ya mahakama na wenzao ambao walionekana kuimba nyimbo za kushangilia na kuwaelekeza katika eneo kulikotokea mauaji
Hatua ya kuachiliwa kwa wachimba migodi inakuja baada ya viongozi wa mashtaka kufutilia mbali mashtaka dhidi ya wachimba migodi 270 kufutia shinikizo za umma.
Wachimba migodi wa kwanza hao walikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya wenzao 34 waliouawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi.
Wakili wa wachimba migodi hao Bi Mapuli Kesi, alifurahia uamuzi huo wa mahakama na kunukuliwa akisema, "mimi ninayo furaha kubwa na ni ushindi mkubwa kwa kundi letu. Tumefanya kazi kubwa kufikia hapa tulipo."
Mwandishi wetu wa Afrika Kusini, Omar Mutasa, aliyekuweko mahakamani wakati kundi la kwanza la wachimba migodi lilipoachiliwa huru, alisema wachimba madini hao walilalamikia kile walitaja kuwa mateso mikononi mwa maafisa wa polisi.
Mmoja wao ambaye hakutaka kusema jina lake aliambia BBC, "polisi walikuwa wakali sana wakisema tusiwatazame na wakati mwingine walikuwa wakitutoa nguo na kutupiga marungu."
Hapo jana polisi waliwapiga riasasi na kuwajeruhi wachimba migodi wanne katika tukio tofauti .
Inadaiwa kuwa polisi walitumia risasi za mipira kuwatawanya waandamanaji katika Mgodi mwingine wa Gold Miners wanaogoma wakidai nyongeza ya mishahara ndipo wanne hao walipojeruhiwa.
Kisa hiki kinafuatia kuuwawa kwa wachimba migodi wengine 34 wakati walipopigwa risasi na polisi wiki mbili zilizopita.
Mazungumzo yanayolenga kusitisha mgomo wa wachimba migodi hao wa mgodi wa madini ya Platinum wa Marikana, vile vile yalitarajiwa kuanza hapo jana.
Polisi wanadai kuwa walilazimika kuwafyatulia risasi wachimba migodi hao kama hatua ya kujilinda kwani na wao walikuwa wamejihami kwa mapanga wakati wakikabiliana nao.
Mgomo wao ulioitishwa kulalamikia nyongeza ya mishahara pamoja na kutaka chama chao kipya cha wafanyakazi kutambuliwa, ungali unaendelea huku mgodi ukisalia kufungwa kwa wiki tatu sasa.
Hata hivyo kampuni inayomiliki mgodi huo, Lonmin, ambayo ndio ya tatu kwa ukubwa wa uzalishaji wa madini hayo, imesema kuwa mgomo huo ni haramu.
Lakini imetupilia mbali matakwa yake kuwa ikiwa wafanyakazi hao hawatarejea kazini , watafutwa kazi.
Baada ya ufyatuliaji risasi, viongozi wa mashtaka wa serikali, walitumia kanuni ya enzi ya ubaguzi wa rangi ya kosa la ujumla kuweza kuwafungulia mashtaka wachimba migodi 270 waliokamatwa wakati wa vurugu baada ya mgomo wao kuwalazimisha polisi kuwafyatulia risasi.
Kanuni hiyo ilitumika na walowezi wa kizungu wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi kuwanyanyasa wapinzani wao waafrika weusi.

No comments:

Post a Comment