NJOMBE

NJOMBE

Monday, September 3, 2012

Walimu waanza mgomo wa kitaifa Kenya


Mabango ya walimu Kenya wakitaka kuongezwa mishahara
Maelfu ya walimu nchini Kenya wameanza mgomo wao rasmi wakidai kuwa serikali imekuwa ikipuuza kilio chao kuongezwa mishahara kwa miaka mingi.
Walimu hao ni wa shule za misingi na zile za upili na leo wamesusia kazi wakitaka nyongeza ya mishahara huku shule nyingi nchini humo zikiathirika.
Walimu hao wamekiuka agizo la mahakama lililoharamisha mgomo huo. Shule nyingi katika miji mikubwa mfano Mombasa, Nairobi na Nakuru zilisalia kufungwa.
Walimu hao wanadai nyongeza ya kati ya asilimia miamoja na miatatu.
Walimu wa shule za upili pamoja na wahadhiri wa vyuo vikuu wamesema watajiunga na mgomo huo baadaye wiki hii.
Mgomo huu unajiri wakati shule zikifungua kwa muhula wa tatu kitu ambacho walimu hao wanasema sio hoja kwani wamekuwa wakigoma kila muhula wa tatu unapofungua kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita wakidai hiyo nyongeza.
Wanasema kuwa serikali haina usawa katika mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kwani ni hivi maajuzi tu wauguzi na wafanyakazi wengine wa umma walipoongezwa mishara baada ya kugoma. Wanadai kuwa walimu wamepuuzwa.
Mgomo huu umeonekana kufanikiwa kwani shule nyingi zimesalia kuwa bila walimu wanafunzi wengi wakibaki nyumbani.
Walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe kwa serikali kuwa wao hawawezi kula panya kwa mishahara midogo ambayo wanapata. Na vile vile walisema kuwa wamechoka na ahadi za uongo za serikali.
Mgomo huo uliitishwa na mashirika ya wafanyakazi yanayowakilisha takriban walimu laki mbili na nusu.
Wameahidi kuendelea na mgomo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

No comments:

Post a Comment