NJOMBE

NJOMBE

Friday, November 9, 2012

Mbinu za kusoma na kuelewa


Tunapozungumzia uelewa wa wanafunzi darasani tunakuwa tumeingia katika msitu mpana zaidi wa majibu, lakini ukweli unabaki kuwa ndani ya darasa linalofundiswa na mwalimu mmoja hutokea wanafunzi wengine wakaelewa zaidi  na wengine wasielewe kabisa.

Kuna wanafunzi na baadhi ya wanasayansi wanaamini kuwa kuna binadamu huzaliwa na uwezo mkubwa wa kuelewa zaidi ya wenzao, huu ni ukweli lakini si wa kuamini sana kwani kipimo cha kuhakikisha kuwa huyu ameumbwa hivyo hakuna zaidi ya kuangali tu yale ambayo yanatendwa na huyo anayeitwa ana akili za ziada au za kuzaliwa.

Lakini wakati huo huo kuangalia ayatendayo mtu au kuangalia uelewa wake darasani hakutoshi kumpa sifa za kuwa na sababu ya kuwazidi wenzake ambao wameamua tu kutokusoma, kutomsikiliza mwalimu, kutozingatia wanachoelekezwa au wameharibiwa na masumufu ya dunia yakiwemo masuala ya mapenzi.

Kwa maana hiyo, hawa ambao hawaelewi kwa sababu wanasoma huku wanawaza mambo ya kimapenzi au wanafikiria kwenda muziki au  kucheza, hawawezi kuwekwa kwenye kundi la watu ambao hawakuzaliwa na akili bali waliojiharibu kwa kukosa kuufahamu ukweli.

Hivyo basi, kuna kila sababu kwa mwanafunzi kupuuza fikra za kizembe zinazomfanya ajione kuwa anazidiwa na wenzake darasani kwa sababu yeye hakuzaliwa na akili nyingi. Kila binadamu mwenye akili timamu kwa mujibu wa tafiti za watalaamu wa masuala ya ufahamu ana uwezo mkubwa mara 1000 kuliko ule anaoutumia.

Hii ina maana kuwa kama kuna mwanafunzi anaongoza darasa lenye watu 100, uwezo huo wa kuongoza anaweza kusonga nao mpaka akafikia kwa watu 1,000 na akifika hapo anaongeza mara 1,000 tena na tena. Huu ni uwezo wa ajabu sana alionao mwanadamu. Lakini wengi kati yetu tumeshindwa kusonga mbele mara elfu toka tulipo kwa sababu tumeshindwa kutumia kipawa chetu na tumeamini uongo kuwa kuna waliopendelewa tangu wanaumbwa.

Ben Carson mwandishi mashuhuri na daktari bingwa wa magonjwa ya akili ambaye awali alikuwa akiburuza mkia darasani aliambiwa na mama yake aitwaye Sanya Carson maneno haya: �you can do anything they can do, only you can do it better� (Nukuu inapatikana ndani ya kitabu kiitwacho THINK BIG cha Ben Carson ukurasa wa 7) kwa tafsiri isiyo rasimi Ben aliambiwa na mama yake kuwa �unaweza kufanya wayafanyayo, lakini wewe unaweza kufanya zaidi yao�

Mwanamke huyu alidumu kumwambia mwanae kuwa ni bora zaidi ya wengine na kumtaka aongeze bidii kila siku ili afikie lengo. Ben aliaamini aliyokuwa akiambiwa na kwa makusudi aliamua kujibidisha na hatimaye kufikia  kiwango cha kuwa msomi mwenye kuheshimika ulimwenguni.

Kimsingi kuna watu wengi ambao walipuuza kauli za kujiona duni na kufanikiwa katika mambo waliyokusudia kuyafanya. Huu ni ushahidi kuwa hajaumbwa mwanadamu kuwa wa mwisho darasani bali matokeo ya kushindwa ni lazima yapewe kwanza sababu za uzembe na maumbile yawe ni ya mwisho kufikiriwa. Ufuatao ni muongozo wa kumuwezesha mwanafunzi kusoma na kuelewa vema.

-Kumzingatia mwalimu

Wanafunzi wengi wanashindwa kufikia uelewa wa juu kwenye masomo yao kwa sababu hawawi makini wanapofundishwa darasani na waalimu wao. Kitendo cha kuweka mawazo nusu darasani na nusu nje ni kujiwekea kizingiti cha kuelewa kinachofundishwa.

Ni muhimu kwa mwanafunzi kama nilivyosema awali kwamba ampende mwalimu wake na aone furaha kumsikiliza anapofundisha. Itakuwa vigumu kwa mwanafunzi kuelewa anachofundishwa kama anayemfundisha anamchukia eti tu kwa sababu jana alimwadhibu au alimfokea.

Ifahamike kuwa, msingi mkubwa kabisa wa mwanafunzi kuelewa somo lo lote ni kuelewa anachofundiswa moja kwa moja toka kwa mwalimu wake. Kitendo cha kutoka darasani bila kujua kilichofundishwa ni jambo la hatari kwa maendeleo ya mwanafunzi kimasomo.

Inashauri kuwa mwanafunzi anapoingia darasani anatakiwa kuwa makini na kufuata anachoongea mwalimu wake neno kwa neno, huku akinoti anachoelewa na asichoelewa, ili kama ni msaada wa kueleweshwa aombe muda mfupi baada ya mwalimu kumaliza kufundisha.

Kurudia notisi

Mara baada ya mwanafunzi kufundishwa na kuelewa, anatakiwa akifika nyumbani siku hiyo hiyo arudia yale aliyosoma kwa kujikumbusha alichosema mwalimu wake. Hii itamsaidia zaidi kuifanya akili itunze kumbukumbu ya somo alilofundishwa na hivyo kumfanya mwanafunzi kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujikumbusha au kukumbuka atakapokuwa akifanya mtihani.

Haifai kwa mwanafunzi kurejea nyumbani na kufunika madaftari bila kujikumbusha au kurudia siku mbili baada ya kufundishwa, kufanya hivyo kunaweza kutoa nafasi kwa akili kuyatupa aliyofundishwa kutokana na wingi wa masomo au mambo aliyoelekezwa kwa siku mbili au wiki nzima.

-Kufanya uchambuzi

Ni wajibu wa mwanafunzi kufanya uchambuzi wa notisi zake za shule kwa kuandika mchanganuo wenye maneno machache ya msingi kwenye daftari jingine au karatasi. Kufanya hivi kutamsaidia kupunguza wingi wa maneno ya kuhifadhi akilini hasa kwa wanafunzi wa ngazi za chini ambao wengi wao hutumia mbinu za kukariri ambazo ni hatari kwa kusahau haraka.

Kwa mfano, wanafunzi anapofundishwa kuhusu ubadhilifu wa pesa ndani ya Benki Kuu  ya Tanzania �BoT� kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje maarufu kama EPA na kupewa takwimu na mlolongo mzima ulivyokuwa, anachotakiwa kufanya yeye ni kunyambua mambo ya msingi ambayo yatamuongoza katika kujibu maswali, kama kuwajua wahusika, mwaka wa skendo, kiasi kilichoibwa na kilichorudiswa.

Mambo hayo machache akiyafahamu yatamfanya awe na uwezo wa kulielezea jambo hilo kwa kina mbele za watu na kuonekana mwenye ufahamu wa kutosha, lakini pia atajihakikishia uwezo wa kukabili jaribio au mtihani wo wote utakaokuja na swali la EPA.

-Kujipima uelewa

Kumsikiliza mwalimu, kurudia notisi na kufanya uchambuzi kunaweza kusitoe picha sahihi juu ya uelewa wa mwanafuzni katika yale anayosoma pamoja na uwezo wake wa kukumbuka aliyojifunza. Mwanafunzi ili ajipime kama akili yake imenakiri vema anatakiwa kutenga siku ndani ya wiki kwa kujitungia mitihani kutoka kwenye daftari zake, kuifanya na kujisahihisha mwenyewe.

Hii itampa mhusika ufahamu wa kujua ni eneo gani kaelewa zaidi ya jingine na hivyo kujituma zaidi sehemu ambayo hajaelewa kwa kuuliza tena kwa mwalimu au kwa wenzake ambao anadhani wana ufahamu mkubwa kuliko yeye. Ni vibaya kusoma bila kujipima uwezo. Itapendeza kama wanafunzi watakuwa wakifanya mitihani ya kujipima kwenye vikundi kila wiki.

 -Kukuza ufahamu
Ziko njia nyingi za mwanafunzi kukuza ufahamu wake lakini muhimu zaidi ni kusoma vitabu, kusikiliza habari kupitia vyombo vya mbalimbali na kushiriki katika mijadala ya wazi yenye kujadili masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mwanafunzi hawezi kukuza ufahamu kama hajui masuala ya jamii yake, siasa za ulimwengu na hali ya uchumi wa ndani na nje na hayo yote yanapatikana kwa kusoma. Jambo jingine la msingi ni kwa mwanafunzi kuepukana na aibu ya kujieleza mbele za watu. Njia pekee ya kuhifadhi kumbukumbu ya kile alichosoma na kuwa na tabia ya kuwaeleza wengine.

Kwa mfano, kama mwanafunzi atakuwa amefungua mtandao wa inteneti na kusoma habari za kupanda kwa uchumi wa Marekani anatakiwa awaeleze wenzake alichojifunza, vivyo hivyo atakaposoma vitabu au kutazama filamu. Kujua jambo na kutokulitenda ni ujinga sawa na mtu ambaye hajui kabisa. Aibu ya kuzungumza mbele za watu haifai ni vema mwanafunzi akajiamini na kujizoeza kueleza anachokifahamu mbele za watu.

No comments:

Post a Comment