Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa linasema haliko tayari kuunga mkono harakati za jeshi la kanda
ya Afrika Magharibi katika kukabiliana na wapiganaji wa Kiisilamu ambao
wameteka kaskazini mwa Mali.
Baraza hilo limelaani uharibifu,wa makuburi na
minara ya kale katika mji wa Timbuktu ambao umewekwa chini ya urithi wa
dunia na kusema uharibifu huo ni sawa na uhalifu wa kivita. Muungano wa
kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS unanuia kutuma wanajeshi 3,00 nchini
Mali.Kundi la Ansar Dine lenye uhusiano na mtandao wa Al Qaeda liliuteka mji wa Timbuktu mapema mwaka huu.Kundi hilo tayari limeharibu madhabahu ambayo linasema yamejengwa kinyume na imani ya Kiisilamu.
Msemaji wa Ansar Dine Sanda Ould Bamana aliambia BBC Sharia ya Kiisilamu hairuhusu makaburi yaliyojengwa kwa urefu wa zaidi ya inchi sita. Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni{UNESCO} pamoja na serikali ya Mali zimeomba kundi la Ansar Dine kusitisha harakati za kuharibu turathi hizo.
UNESCO pia imeelezea wasi wasi kwamba nyaraka za kale na vifaa vingine muhimu huenda vikaporwa na kuvukishwa kimagendo na imeziomba nchi jirani kuzuia kosa hilo kufanyika.
Timbuktu imepata sifa za kimataifa kutokana na eneo hilo kua moja wapo ya kitovu cha mafunzo ya imani ya Kiisilamu hususan misikiti yake iliyojengwa karne za 15 na 16. Timbuktu pia wanatoka Mawalii 333 ambao wanaheshimiwa sana katika madhehebu ya Sufi.
Ansar Dine ambao wana msimamo mkali{Salafist} wanapinga heshima kwa Mawalii.Waliuteka mji wa Timbuktu baada ya mapinduzi ya kijeshi kutokea. Katika mwanzo wa harakati za kutwaa kaskazini mwa Mali Ansar Dine walishirikiana na wapiganaji wa Tuareg waliotaka kujitenga na Mali.
Hata hivyo makundi hayo yametofautiana katika siku za karibuni hali iliyosababisha makabiliano makali katika maeneo matatu muhimu ya Mali ikiwemo Timbuktu, Gao na Kidal.
No comments:
Post a Comment