NJOMBE

NJOMBE

Thursday, July 19, 2012

ICC kuchunguza uhalifu wa kivita Mali

Wapiganaji wa Kiisilamu tayari kubomoa Msikiti wa Kale
Mahakama ya kimataifa ya Jinai{ICC} imeanzisha uchunguzi dhidi ya dhuluma za kivita kaskazini mwa Mali. Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hio Fatou Bensouda amesema ombi la uchunguzi huo limetolewa na serikali ya Mali.
Makundi ya waasi wakiwemo wapiganaji wa Kiisilamu yamelaumiwa kwa mauaji, ubakaji na kuwaingiza watoto jeshini.Waasi walidhibiti kaskazini mwa Mali baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
Bi Bensouda amesema afisi yake imeanzisha uchunguzi wa uhalifu wa vita baada ya serikali ya Mali kukiri kwamba haina uwezo wa kuwaadhibu wanaotekeleza dhuluma hizo.Hapo mwezi jana Bi. Bensouda alisema uharibifu wa maeneo ya kale hususan katika mji wa Timbuktu utachukuliwa kama uhalifu wa vita.
Wanajeshi walipindua serikali kwa tuhuma kwamba utawala wa Mali ulishindwa kukabiliana na waasi wa Tuareg pamoja na wapiganaji wa Kiisilamu. Msukosuko wa mapinduzi ulitoa nafasi kwa makundi ya Kiisilamu na Tuareg kuyadhibiti maeneo ya kaskazini mwa Mali.
Moja ya kundi la Kiisilamu lina uhusiano na tawi la Al Qaeda Kaskazini mwa Afrika.Huku haya yakiarifiwa taasisi ya kutathmini mizozo ya kimataifa imeonya kwamba Mali inakumbwa na tisho la kungia vitani.
"International Crisis Group", limetaka pande husika katika uwongozi wa Mali na jamii ya kimataifa kuafikia suluhu la haraka kwa mzozo wa sasa.Wiki jana Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius alisema nchi yake inatafakari harakati za kijeshi kuangamiza maasi kaskazini mwa Mali.

No comments:

Post a Comment