KAMBI ya Upinzani Bungeni imelalamikia fedha kidogo zilizotolewa kwa
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika mwaka wa fedha 2011/12.
Kambi
hiyo ilisema kati ya Sh258.35 bilioni zilizoidhinishwa kwa ajili ya
matumizi ya kawaida, fedha za matumizi zilizopelekwa wizarani kutoka
hazina kufikia Mei 31, mwaka huu ni Sh103.06 bilioni, sawa na asimilia
67.62.
Msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika, Rose Kamili alisema kwa upande wa fedha za maendeleo hadi
kufikia Mei 31, zilizokuwa zimepelekwa wizarani kutoka hazina ni Sh72.63
bilioni ambazo ni sawa na asilimia 68.56 ya fedha zilizoidhinishwa.
“Huu
ni uthibitisho kamili kwamba malengo yaliyopangwa kufikiwa mwaka wa
fedha 2011/12 hayakufikiwa,” alisema Kamili alipokuwa akiwasilisha maoni
ya kambi yake kuhusu makadirio ya matumizi ya wizara hiyo.
Aliongeza
kuwa: “Serikali itoe maelezo mbele ya Bunge hili kwa nini tuipatie
fedha inazoomba kwa wizara hii, wakati mwaka jana haikutekeleza bajeti
iliyoidhinishwa na Bunge, hivyo kuzorotesha malengo yake.”
Alisema
taarifa ya utekelezaji ya Wizara ya Kilimo, inaonyesha bajeti imepungua
kutoka Sh258.35 bilioni mwaka 2011/12 hadi Sh237.624 bilioni sawa na
punguzo la asimilia 8.7.
“Pamoja na kupungua kwa bajeti,
matumizi ya kawaida yameongezeka kutoka Sh152.41 bilioni mwaka
uliopita hadi Sh170.364 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia
11.78,”alisema Kamili ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) na
kuongeza:
“Wakati matumizi ya kawaida yameongezeka kwa takriban
asilimia 12, bajeti ya maendeleo katika wizara hii imepungua kutoka
Sh105.94 bilioni mwaka 2011/12 hadi Sh67.260 bilioni ikiwa ni anguko la
asilimia 57.5.”
Alisema kwa takwimu hizo ni dhahiri kwamba
hakuna mkakati wa dhati wa kutekeleza kauli ya Kilimo Kwanza, kwani
licha ya bajeti ya maendeleo kupungua, imeendelea kuwa tegemezi kwa
fedha za nje kwa asilimia 77.7.
“Tafsiri ya utegemezi huu ni kwamba sasa Serikali imeamua kukiweka kilimo chetu rehani,” alisema
No comments:
Post a Comment