BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mhandisi William
Mhando na wafanyakazi wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za
ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka unaoikabili menejimenti hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi
hiyo, Victor Mwambalaswa, ambaye ni Mbunge wa Lupa (CCM), ilisema kuwa
Julai 13 bodi ilikutana katika kikao cha dharura na kujadili masuala
mbalimbali ikiwamo tuhuma hizo.
Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Jenerali
Robert Mboma (Mstaafu), ilisema kuwa kutokana na tuhuma hizo kuwa nzito,
ni vema ukafanyika uchunguzi huru ambao unaanza mara moja kwa kumtumia
mchunguzi huru.
Iliwataja wengine waliosimamishwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi
Mtendaji, Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha,
Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi, Harun Mattambo.
Ilisema kuwa pamoja na hatua hizo, bodi itahakikisha shughuli za
kiutendaji na uendeshaji wa shirika hilo zinaendelea kama kawaida.
Hata hivyo, kusimamishwa kwa vigogo hao kumezua tafrani, huku kukiwa
na habari kwamba hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni kuficha siri nzito ya
kukwama kwa shirika hilo.
Habari zimedai kuwa kumsimamisha kazi Mhando kunatokana na kile
kinachosemwa ‘jeuri’ yake ya kukataa maagizo ya wakubwa ambao wamekuwa
wakitaka kuliendesha shirika hilo kisiasa zaidi badala ya kukubaliana na
uhalisia.
Wakati Mhando akidaiwa kuhujumu shirika, habari zinasema kuwa yeye
mwenyewe ameelekeza lawama kwa serikali na watendaji wake wakuu kwa
kulinyima shirika hilo pesa ilizoahidi kwa ajili ya miradi ya uzalishaji
na usambazaji wa umeme, na kulizuia shirika hilo kuuza umeme kwa faida,
kwa sababu za kisiasa.
Inasemekana hatua dhidi ya Mhando inatokana na woga wa waziri na
katibu mkuu juu ya mjadala mkali unaotarajiwa kuibuka bungeni wakati wa
kujadili bajeti ya wizara yao. Mhando anatolewa kafara kisiasa, lakini
taarifa zinasema naye amejibu barua ya katibu mkuu kueleza jinsi
asivyohujumu shirika hilo.
|
No comments:
Post a Comment