Taarifa kwa Vyombo vya
Habari
Napenda kuwatangazia wana-Bumbuli kwamba ile ahadi
niliyotoa wakati wa kampeni – ahadi ya kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli –
imetimia. Shirika limepata usajili, limefungua ofisi, lina watumishi wa mwanzo
na tayari ipo miradi minne ambayo utekelezaji wake utaanza mara moja. Tutazindua
Shirika hili tarehe 4 Agosti 2012, katika mkutano wangu na wana-Bumbuli waishio
Dar es Salaam na mikoa ya jirani, na baadaye katika mikutano na wananchi jimboni
Bumbuli.
Chimbuko
Nilipoamua kugombea Ubunge wa Bumbuli mwaka 2010,
niliamua kwamba katika utumishi wangu kama Mbunge nitashirikiana na Wana-Bumbuli
pamoja na marafiki na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi katika
kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii Bumbuli. Jimbo letu ni kati ya majimbo
yaliyo nyuma kimaendeleo kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhitaji jitihada za ziada –
zaidi ya zile za Serikali. Katika kufikia lengo hilo, niliahidi kuanzisha
Shirika litakaloratibu shughuli za maendeleo katika Jimbo.
Nilifikia uamuzi wa kuanzisha Shirika nikitambua kwa
dhati uwepo wa jitihada nzuri za serikali katika kuboresha maisha ya watu wa
Bumbuli nikitegemea pia serikali kuendeleza jitihada zaidi. Hata hivyo natambua
kwamba kazi ya maendeleo si kazi ya serikali pekee, inahitaji ushiriki wa kila
mmoja na hasa sekta binafsi ili kuisadia juhudi za serikali kufikia malengo ya
maendeleo. Nilitaka kuchambua uwezo wa watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi
mbalimbali katika kupanua wigo wa ajira na shughuli za kipato kwa watu wa
Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii.
Mpango wa Mageuzi Bumbuli
Mpango huu ulitokana na mawazo
niliyokuwa nayo nilipoamua kugombea ubunge juu ya haja kuunganisha jitihada za
wenyeji wa Bumbuli, wafanyabiashara na taasisi za hapa nchini, na wawekezaji
kutoka nje katika kufanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Niliamini jitihada
za sekta binafsi zikioana na mipango ya maendeleo ya serikali kutachochea kasi
ya ukuaji wa uchumi wa wana-Bumbuli na hivyo kupanua wigo wa ajira na shughuli
za kibiashara za uzalishaji mali katika Jimbo.
Malengo ya mpango wa kuikwamua Bumbuli kupitia
uwekezaji katika jamii ni kama ifuatavyo:
1.
Kuongeza
pato la wakulima wa Bumbuli kutokana na mazao wanayovuna kwa kuboresha mbinu za
kilimo, mbinu za kuhifadhi mazao, na hatua mahsusi za kuongeza thamani ya mazao
hayo (value-addition).
2.
Kuwavutia
wawekezaji kujenga taasisi au shule itakayokuwa na wanafunzi, walimu na
wafanyakazi wengine watakaotumia bidhaa zinazozalishwa Bumbuli, hivyo
kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi.
3.
Kuleta
huduma za kifedha kwa kuanzisha taasisi ya fedha Bumbuli ambayo hatimaye itakuwa
benki ya wananchi wa Bumbuli ambayo itatoa mikopo kwa masharti
nafuu.
4.
Kuchukua
hatua mahsusi za kuhifadhi mazingira ya Milima ya Usambara kwani maisha na
maendeleo ya kiuchumi ya watu wa Bumbuli yanategemea sana mazingira na mandhari
ya milima ya Usambara.
5.
Kuanzisha
Shirika la Maendeleo Bumbuli litakalokuwa na jukumu la kubuni, kuratibu na
kusimamia uendeshaji wa shughuli zilizoainishwa hapo juu. Shirika hili ndilo
litakalokuwa kiini cha mtandao wa kijamii wa uchumi kwa Bumbuli.
Malengo haya yamekusudiwa kuwanufaisha wananchi kwa
kuanzisha mtandao wa kimataifa wa kibiashara ambapo wadau mbalimbali
watashiriki; na hatamu za uchumi zikishikiliwa na watu wa Bumbuli wenyewe.
Shirika la Maendeleo Bumbuli
Shirika la Maendeleo ya Bumbuli ni shirika la
maendeleo lisilotengeneza faida lenye lengo la kukuza uchumi na kuchochea
maendeleo ya Jimbo. Shirika hili limesajiliwa kama kampuni yenye ukomo wa
dhamana, na litafanya biashara ili kulipia gharama za uendeshaji na faida
inayopatikana itatumika kugharamia miradi ya maendeleo ili kufikia malengo ya
kijamii ya Mkakati wa Mageuzi ya Uchumi wa Bumbuli. Shirika litakuwa na kazi
zifuatazo;
1.
Kuihamasisha sekta binafsi kushiriki
katika maendeleo ya Bumbuli kwa kuwekeza katika maeneo mblimbali. Uwekezaji huu
utahusisha wafanyabiashara wa ndani na wale wa kigeni na Shirika litajihusisha
zaidi katika kutoa msaada wa kitaalamu, na kuratibu mtandao wa kibiashara
utakaoenea kuanzia ngazi ya wilaya, taifa na kimataifa.
2.
Kubuni na
kuitangaza ‘Chapa Lushoto’ (Lushoto Brand) pamoja na kutayarisha mafunzo kwa
wakulima juu ya kutayarisha mazao yao ili yapate kuwa na thamani bora zaidi.
Shirika hili litajenga mfumo utakaosaidia kununuliwa kwa mazao ya wakulima na
masoko ya bidhaa, muundo utakaotumiwa na wafanyabiashara binafsi.
3.
Kuvutia
uwekezaji kwa njia ya kuitangaza Bumbuli pamoja na kuishauri halimashauri na
serikali za mitaa kuhusu maeneo ya kuwekeza na miundombinu ya kuboresha ili
kuvutia uwekezaji zaidi.
4.
Kutafuta
fedha kwa ajili ya uwekezaji wa kijamii na kibiashara na kutoa msaada wa
kihuduma kwa makampuni ya biashara ya nyumbani na uwekezaji wa kutoka nje.
5.
Kuratibu
mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wadau mbalimbali wa maendeleo
Bumbuli.
6.
Kuhamasisha ushiriki wa wananchi
katika mpango wa Maendeleo na Mpango wa uwekezaji.
Shirika litaongozwa na bodi itakayokuwa na watu kati
ya nane na kumi na moja na kuendeshwa na timu ya watu watano ambao watakuwa ni,
Mkurugegenzi Mtendaji, Mweka Hazina, Wachambuzi wawili na Mhasibu.
Miradi ya Mwanzo ya Shirika la Maendeleo
Bumbuli
1.
Mradi wa Kituo cha Kukusanya, Kusafisha, Kugredi, Kupaki na Kutafuta
Masoko ya Mboga na Matunda ya Bumbuli (Bumbuli Packing House)
Wilaya ya Lushoto, jimbo la
Bumbuli likiwemo, inasifika kwa kilimo cha mboga na matunda. Hata hivyo,
asilimia hamsini (50%) ya mboga na matunda yanayolimwa Bumbuli yanaharibika –
kwa kutokufika sokoni au kutopata soko la uhakika. Hata yale mazao
yanayonunuliwa, wakulima wanapata mapato kidogo sana ambayo hayaendani na
thamani ya jasho lao.
Mradi wa Bumbuli Packing
House, ambao utajiendesha kibiashara, una dhamira ya kumaliza tatizo hili.
Pamoja na hili mradi huu utawawezesha wakulima kwa pembejeo – mbegu, mbolea,
pampu, nk – na mafunzo ili wazalishe mboga na matunda bora zaidi ya kukidhi
mahitaji ya soko la kimataifa.
Mradi huu, katika awamu ya
kwanza, utagharimu shilingi milioni 780. Utafiti wa Kibiashara (Market Analysis
Survey) umefanyika, Andiko la Kibiashara limekamilika. Na majadiliano na
wadhamini kupata fedha hizi yamefikia mwisho ambapo ndani ya mwezi mmoja fedha
hizo zitapatikana, na baada ya maandalizi kukamilika (ikiwemo kupata
professional management), mradi utaanza.
2.
Mradi wa Kiwanda cha Kusindika Mboga na Matunda
Shirika liko katika hatua za
mwisho za mazungumzo ya kukifufua upya kiwanda cha kusindika Mboga na Matunda
(Natural Choice) kilichopo Soni, jimbo la Bumbuli, ambacho mwanzoni kwa miaka ya
2000 kilikuwa na sifa kubwa ya kutoa bidhaa nyingi, bora na za thamani
kubwa.
Mradi huu utaenda hatua ya
mbele zaidi ya Bumbuli Packing House kwa kutengeneza juisi, jams, concentrates
na bidhaa nyingine za mboga na matunda kwa ajili ya soko la ndani na nje ya
nchi. Mradi huu, sio tu utatoa ajira kwa watu wa Bumbuli, bali pia utahakikisha
soko la uhakika kwa mboga na matunda ya Lushoto linapatikana na kuongeza thamani
ya mazao ya wakulima na hivyo kuwaongezea kipato.
3.
Mradi wa Kutoa Mikopo kwa Masharti Nafuu (Bumbuli Microfinance
Institutition)
Jimbo la Bumbuli halina tawi
la benki yoyote na huduma ya fedha ni tatizo kubwa. Shirika la Maendeleo Bumbuli
limeomba leseni kutoka Benki Kuu kuanzisha taasisi ya fedha kwa ajili ya
ukopeshaji kwa masharti nafuu na pamoja na huduma nyingine za fedha. Andiko la
Mradi huu limefanywa kitaalam sana, baada ya utafiti wa karibu miezi nane kuhusu
njia muafaka ya kutoa huduma ya fedha kwa masharti nafuu kwa watu wa Bumbuli.
Mradi huu utagharimu shilingi milioni 450 kwa kuanzia na baada ya miaka mitatu
mtaji utaongezwa na kufikia shilingi bilioni 1.6. Wakati tunasubiri usajili na
leseni kutoka Benki Kuu tayari wapo wafadhili ambao, baada ya kusoma andiko
letu, wameonyesha nia ya kusaidia mradi huu.
Msingi wa mradi huu ni
kuwezesha vikundi vya kuweka na kukopeshana fedha ambavyo tayari vipo lakini
vina mtaji mdogo, kutoa mafunzo ya fedha kwa vikundi hivi, na kuhamasisha
kuanzishwa kwa vikundi vingine. Kipaumbele na nafuu ya mikopo itatolewa zaidi
kwa vikundi vitakavyotumia fedha hizi kwa uzalishaji mali na shughuli ambazo
zitaajiri watu wengine.
4.
Mpango wa Malipo kwa Kufanya Vizuri
kwa Shule za Sekondari (Cash-On-Delivery for Secondary Education in
Bumbuli)
Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC) litakavyotekeleza
program ya msaada ya Malipo kwa kufanya vizuri** au cash on
delivery (COD), ambayo itaongeza umakini na tija kwenye kujifunza na matokeo
ya mitihani katika shule za sekondari jimboni Bumbuli. Kulingana na utafiti
wetu, jimbo la Bumbuli liko kwenye hali ya kukata tamaa ya kupata msaada kwenye
Sekta yake ya Elimu ya Sekondari. Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC)
litatekeleza program ya majaribio ya malipo kwa kufanya vizuri (COD), ya miaka
mitatu ambayo itafanya malipo kulingana na idadi ya wanafunzi ambao wamefaulu
Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne. Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC)
linalenga kuboresha matokeo ya kujifunza/elimu katika jimbo la Bumbuli kupitia
program hii ya kutoa motisha. Program hii itahusu Shule za Sekondari za Serikali
za Kata.
Malipo kwa
kufanya vizuri (COD) ni utaratibu mpya kutoa msaada ambapo wafadhili hutoa pesa
kwenye maendeleo yanayopimika kwa kuangalia matokeo maalum. Unahusianisha moja
kwa moja malipo na matokeo maalum, ikiwapatia watendaji/wapokeaji motisha ya
kuongeza nguvu zao za kufanyakazi ili kufikia maendeleo.
Msingi na uhalali wa wazo la CDO,
ulioanzishwa awali na Kituo cha Maendeleo ya Kimataifa(Center for Global
Development) mjini Washington, umejikita kwenye mtazamo kwamba kazi za maendeleo
ni lazima zitathminiwe kwenye athari (impact) zinazoletwa. Mbinu inawakilisha
mabadiliko kutoka kufuatilia nguvu na rasilimali ambavyo mashirika huwekeza
katika kutoa misaada - 'nyenzo/rasilimali', na pia shughuli na
vifaa/vitendeakazi vinavyotokana na uwekezaji huo - 'matokeo'. Badala yake,
mbinu hii inalenga kujikita kuangalia namna gani maisha ya watu masikini
yameweza kubadilishwa kutokana na uwekezaji kwenye sekta au eneo fulani la
maendeleo (afya, elimu, n.k).
Mnamo mwezi Septemba 2011, Shirika la
Maendeleo Bumbuli lilifanya utafiti wa kina juu ya mazingira ya kujifunzia
Bumbuli na kugundua kwamba shule nyingi, walimu, na wanafunzi wa Bumbuli hawana
motisha wala rasilimali zinazohitajika kuwawezesha wafanye vizuri kama
inavyotarajiwa.
Kwa wastani, kila shule iliyotoa data
za matumizi ya pesa ilionyesha ni Sh. 5,268 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka 2010
(kiasi kilichotarajiwa kwa shule za Sekondari ni shilingi 25,000 kwa kila
mwanafunzi). Pamoja na hayo, utafiti ulionyesha kuwa ni 71% tu ya walimu
walikuwepo shuleni, ambapo ni 19% tu walikutwa madarasani. Utafiti huo ulionesha
kuwa walimu hupata mishahara yao kwa wakati. Wastani wa mshahara halisi wa
mwalimu wa Bumbuli ni Sh.395,000 kutoa malipo ya deni ya Sh.74,000 kila mwezi.
Wengi walionesha kuwa na shughuli ya ziada ya kiuchumi (67%), hasa kilimo (90%).
Wengi wao (98%) walidai kutokuhusishwa katika hatua za kupanga bajeti za shule.
Wastani wa Pato la Mtanzania anayeishi kijijini (ikiwemo Bumbuli) ni Sh.152,000
(HBS, 2010). Wakati 89% ya wanafunzi wanaonesha kushiriki katika shughuli za
kiuchumi wa familia, bado 70% wanafanikiwa kupata muda kidogo wa kukamilisha
kazi zao za masomo wakiwa nyumbani, huku 34% inaonesha hawakufika shule kwa
mwezi uliopita kutokana na kusaidia shughuli za nyumbani. Matokeo ya Mtihani wa
Kidato cha Nne ya mwaka 2011 kwa Shule za Bumbuli yalikuwa mabaya sana. Kati ya
wanafunzi 1,327 waliofanya mtihani, hakuna aliyepata Division 1, waliopata
Division 2 ni wanne, waliopata Division 3 ni 39, na waliobakia, yaani wanafunzi
1,274, walipata Division 4 na 0.
Pamoja na hatua mahsusi ambazo
Serikali inachukua kuboresha elimu nchini na kuongeza ufaulu, Shirika la
Maendeleo Bumbuli, kupitia Program hii ya COD, linataka kuonesha kwamba fedha
zinaweza kugawika vizuri na kwa usahihi ili kuboresha elimu kwa kupima kiwango
cha ufaulu wa wanafunzi.
Hatua na mikakati inayopendekezwa
Program ya COD kwa Shule za Sekondari Bumbuli
itahusisha makubaliano kati ya Shirika la Maendeleo Bumbuli, Shule za Sekondari
Bumbuli na Halmashauri ya Wilaya kulipa jumla ya kiasi cha Dola za kimarekeni
100 kwa kila mwanafunzi anayefaulu mitihani ya kidato cha IV kwa daraja la
I-III. Malipo ya COD yatafanyika baada ya uthibitisho wa matokeo ya mtihani wa
kidato cha nne. Fedha zitapelekwa Halmashauri ya Wilaya, Shule za Sekondari na
kwa walimu na wanafunzi. Fedha zitakazogawiwa kwa shule zitatumika kwa ajili ya
mahitaji ya kielimu ya shule kama zilivyowekewa vipaumbele na Bodi za
Shule.
Watakaonufaika na mradi:
Kwa kila mwanafunzi atakayefaulu mtihani (Div I-III)
anapomaliza kidato cha nne, Shirika la Maendeleo Bumbuli kupitia program ya COD
litatoa malipo yafuatayo:
1. Walimu: Tsh 60,040/= kwa kila mwanafunzi
anayefaulu mtihani
2. Wanafunzi: Tsh 50,500/= Kwa kila mwanafunzi
anayefaulu mtihani
3. Shule: Tsh
31,600/= Kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
4. Halmashauri ya
Wilaya: Tsh 15,800/= kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
Vipimo na Ukaguzi:
Data za mitihani kuanzia mwaka 2011
zitatoa msingi wa awali, na msingi huo utakuwa ukibadilishwa kila mwaka na
ufanisi wa utendaji wa shule, hivyo kila mwaka unakuwa msingi kwa ajili ya
malipo ya mwaka ujao wa. Kiashiria cha matokeo kitakuwa idadi ya wanafunzi ambao
wamefaulu kidato cha nne kwa kupata daraja la I-III. Ili kuyadumisha matokeo
hayo, hatua mbalimbali zitakuwa vikiripotiwa kila mwaka na shule na halmashauri.
Mkataba, matokeo, na taarifa nyingine zitawekwa wazi kwa wananchi ili kuongeza
uwajibikaji wa wafadhili na wapokeaji
Shirika la Maendeleo Bumbuli halina nia ya kusema
kwamba COD ndio suluhisho pekee la tatizo la maendeleo ya elimu au ufumbuzi wa
matatizo yote katika mfumo wa elimu nchini lakini tunaamini inaonesha matarajio
ya kutosha kuona thamani ya kujaribu, kujifunza na kutathmini.
Uendelevu wa
program
Ili program iwe endelevu, Shirika la
Maendeleo Bumbuli(BDC) litaweka mfumo thabiti wa kufanya tathimini na kutoa
mrejesho, ambao utatumika kama zana ya kupimia uwajibikaji, na kuendeleza uwazi.
Pia ni muhimu kuzingatia ushirikishwaji wa wenyeji wa Bumbuli na umiliki wa
program ya COD. Hili linaweza kufanikiwa kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha
elimu bora kama uwekezaji wa wenyeji, na Mtandao wa Wahitimu wa Shule za
Sekondari Bumbuli kwa ajili ya fedha za COD. Zaidi sana, Shirika la Maendeleo
Bumbuli litahusisha na kutumia Bodi za Shule, ambazo zinahusisha wazazi na
walimu. Hii ndiyo njia itakayowafanya watu wa Bumbuli wathamini juhudi zao
wenyewe katika kuboresha jamii zao.
5. Kambi ya Wanafunzi Wanaojiandaa
na Mtihani wa Kidato cha Nne 2012
Kuanzia tarehe 4 Agosti hadi 5
Septemba, wakati wa likizo za masomo, Shirika limeandaa kambi maalum kwa
matayarisho ya vijana wanaojiandaa na mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu. Kambi
hii itakuwepo kwenye Kituo cha Elimu Soni, ambacho kina mandhari, mazingira na
eneo la kutosha kufundishia na kuishi wanafunzi katika kipindi
hiki.
Kila siku, wanafunzi hao watapigwa
msasa kwa masomo ambayo hawakupata fursa ya kuyasoma vizuri katika mwaka wa
shule, watafundishwa mbinu za kufanya mitihani (ikiwemo time-management), na
kufanya revision ya mitihani ya Kidato cha Nne ya kuanzia mwaka 1984 hadi sasa.
Shirika litatafuta walimu wenye sifa za kufundisha masomo ya Hesabu, Kiingereza,
Historia, Kemia, Fizikia na Biolojia, hata nje ya Jimboni na kuwalipa posho kuja
kufundisha kwenye kambi. Pia tutaomba watu mbalimbali, ikiwemo walimu wastaafu,
wenye moyo wa kujitolea waje kufundisha kambi hii.
Mwisho
Hadi sasa Shirika la Maendeleo Bumbuli
halijapata mfadhili au ufadhili kutoka kokote au kwa mtu yoyote. Miradi hii
niliyoitaja ndio iko katika hatua za kupata ufadhili. Fedha ambazo zimetumika
hadi sasa kuanzisha Shirika, kuweka ofisi, kuajiri watumishi wa muda na kufanya
utafiti na kutengeneza maandiko ya miradi zimetokana na mkopo niliouchukua kama
Mbunge, ikiwemo mkopo wa gari ambao sikuutumia kununua gari bali kuanzisha
Shirika.
Napenda kutoa mwito kwa wana-Bumbuli
wenzangu na Watanzania kwa ujumla kusaidia kuchangia maendeleo ya Jimbo la
Bumbuli, hasa kwa miradi ambayo hatukuitafutia ufadhili kama huu wa COD na
kambi. Kwa kuchangia unaweza kutumia namba ya M-PESA 0762088050. Kwa maelezo
zaidi kuhusu Shirika la Maendeleo Bumbuli, tuma barua pepe: getinvolved@bumbuli.org au piga simu:
+255 22 2129821/6 au tuma fax: +255 22
2129796
Katika miezi ijayo, BDC pia itatekeleza miradi ya kitaifa yenye manufaa kwa
maendeleo na utawala bora kwa nchi yetu. Naamini nchi yetu itapiga hatua za
maendeleo kwa kasi zaidi kama kila mmoja wetu, kwa nafasi na uwezo wake,
atathubutu, lakini pia kama sote tutasaidiana katika kuchangiana na kupeana
mawazo kuhusu shughuli za maendeleo.
January Makamba
Mbunge
Bumbuli
No comments:
Post a Comment