WAKATI vitendo vya uhalifu vikizidi kuongezeka sehemu mbalimbali
nchini, sasa silaha kutoka nchi jirani zinadaiwa kuingia kwa wingi na
kuuzwa mitaani na baadhi yake kubadilishwa na mahindi, Mwananchi
Jumapili limegundua.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa,
kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo ya silaha nchini, bunduki moja
aina ya Short Machine Gun (SMG) sasa inauzwa kati ya Sh300,000 hadi
Sh500,000, huku bunduki aina ya AK 47 ikiuzwa kwa Sh700,000 hadi Sh1
milioni.
Wakati vijiji kadhaa mkoani Tabora vilipokumbwa na uhaba
wa chakula, bunduki aina ya SMG katika Kijiji cha Usinge wilayani
Urambo zilibadilishwa kwa gunia moja la mahindi, huku AK 47
ilibadilishwa kwa magunia mawili ya mahindi.
Gazeti hili huko
nyuma liliwahi kuripoti kuuzwa kwa bastola holela mitaani katika miji
mikubwa ikiwamo Arusha, Mwanza, Moshi ambapo silaha hiyo ilikuwa ikiuzwa
kati ya Sh800,000 hadi shilingi milioni moja.
Uchunguzi wa muda
mrefu uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali iliyopo
mipakani umebaini kuwa, mtandao huo wa uingizaji silaha ni mkubwa na
unawashirikisha matajiri na baadhi ya askari polisi wasiokuwa waaminifu.
Silaha
hizo huingizwa nchini kupitia mkoani Kigoma, mpakani mwa Rwanda,
Kenya, na Burundi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo, magari, pikipiki
na boti kupitia Ziwa Victoria pamoja na baiskeli ambapo bunduki hizo
hufungwa kama mzigo ya kawaida.
Chanzo kimoja cha uhakika
kililiambia Mwananchi Jumapili kuwa eneo la Usinge ndiyo kituo kikuu cha
kupokelea silaha kutoka Burundi na Rwanda ambazo husambazwa mikoa
mbalimbali nchini.
Mawakala
Mmoja wa watu
ambao wamewahi kufanya biashara alisema kuwa mawakala wa silaha hizo
wapo katika mikoa ya Kigoma na Tabora na kwamba ni wafanyabiashara, huku
baadhi wakidaiwa kuwa watu wenye asili ya kabila la Kitutsi.
Lakini
kwa Usinge alimtaja mfanyabiashara mmoja ambaye pia hukopesha fedha kwa
riba (jina tunalo) ambaye inadaiwa kuwa biashara hiyo haramu
anayoifanya inajulikana na mamlaka mbalimbali za juu serikalini.
Habari
hizo zilieleza kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akinunua SMG kati ya
Sh300,000 hadi Sh500,000, na kwamba huzisafirisha kwa kutumia mtandao
wake hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa na huziuza kati ya Sh800,000 hadi
Sh1,000,000.
Mbali na kutumia silaha hizo kwa ujambazi pia huzitumia kufanya uwindaji wa tembo kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Habari
hizo zinaeleza kuwa baada ya kuyapata meno hayo ya tembo na kukatwa
vipande, husafirisha kwa kusaidiwa na maofisa wa maliasili na askari
polisi wasiokuwa waaminifu.
Askari hao inadaiwa wanatumiwa na
wafanyabiashara wakubwa kuuza meno ambapo huwalinda watu hao wanapokuwa
wanasafirisha nyara hizo huku wakiwa wamevalia sare zao za kazi.
Zinafafanua
kwamba wanaposafirisha bidhaa hizo, huyaweka meno katika magunia ya
mkaa kutokea Wilaya za Serengeti, Bunda, Bariadi, Maswa hadi Mwanza
ambapo mtandao wa watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu huipokea mizigo
hiyo na kuisafirisha kwenda kwa mawakala wa biashara hiyo.
Kwa
mujibu wa vyanzo huru vya habari, silaha hizo hupokewa Mwanza ambapo
huuzwa kwa wingi wilayani Serengeti kwa ajili ya kufanyia uhalifu na
uwindaji wa wanyama pori.
“Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa)
kwa kutumia wapelelezi wao wamejitahidi kutoa taarifa Polisi lakini
wanaokamatwa baada ya muda huachiwa…, Polisi ni chanzo kikubwa hapa,”
zilieleza habari hizo.
Silaha kutokea Somalia
Inadaiwa
kuwa silaha hizo zinazotokea Somalia, huingizwa nchini kwa njia ya
panya kupitia Kenya kwa kutumia punda ambao huwa wanakokota mikokoteni
iliyopakiwa magunia ya mahindi au karanga ambayo ndani yake huwa na
silaha hizo.
Tanapa wasaka mtandao
Tangu
kuuawa kwa Tembo ‘George’ maarufu kama tembo wa JK, Tanapa inadaiwa
kutumia gharama kubwa kuusaka mtandao huo bila mafanikio.
Mmoja wa
maofisa wa shirika hilo kwa sababu za kiusalama jina limehifadhiwa
aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa anajua taarifa zote za upatikanaji wa
silaha wanazozikamata.
“Kuna mambo ambayo yanatusumbua sana maana
wenzetu (polisi) wanatangaza kuwa wamekamata silaha, lakini baadaye
waliokamatwa huachiwa baada ya kutoa fedha,” alisema ofisa huyo na
kuongeza:
“Kama rushwa itaendelea hali ya usalama kwa mikoa ya
Kanda ya Wiwa itakuwa mbaya maana silaha ni nyingi na zilizokamatwa ni
kidogo kuliko zilizopo.”
Ofisa huyo alikwenda mbali zaidi kwa
kufafanua kwamba baadhi ya watuhumiwa wanaouza na kusafirisha silaha
hizo wana uhusiano na baadhi ya maofisa wa polisi ambao huvujisha siri
kila inapofanyika operesheni ya kuwakamata watu hao.
“Matatizo
yote yanachangiwana maofisa wa polisi ambao hawana mpango wa kumaliza
tatizo hili hatari, nchi itageuka dampo la silaha za kivita, vyombo vya
usalama vinatakiwa kuwachunguza maofisa wanaotuhumiwa, tena wachunguzwe
mpaka mali zao kwani baadhi yao wanadaiwa kujengewa nyumba,”
kilibainisha chanzo hicho.
Kamanda Simon Sirro
Kamanda wa
operesheni Tanzania, Saimoni Siro aliyeendesha msako wa watuhumiwa wa
ujambazi waliohusika na mauaji ya mtalii na Meneja Msaidizi wa Kambi ya
Ikoma Bush na kupora vitu mbalimbali alikiri hivi karibuni kuwa,
uingizaji wa silaha za kivita unazidi kushika kasi.
"Uhalifu wa
kutumia silaha unazidi kushika kasi, wengine wanahusika na ujangili
katika hifadhi na wengine kwenye matukio kama haya ya uhalifu lakini
tunakabiliana nao kuhakikisha wahusika wanakamatwa, nashukuru hata wazee
wamekerwa na hali hii na wanatoa ushirikiano mzuri maana nimeitwa hadi
kikao cha wazee wakanieleza nao mikakati yao," alisema.
RPC Mara
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa huo,
Emmanuel Lukula kwa nyakati tofauti waliliambia Mwananchi Jumapili juu
ya ongezeko la silaha za kivita mkoani humo na kueleza kuwa hali hiyo
inatishia usalama wa raia na mali zao, ikiwemo uwindaji haramu.
Kamanda
Boaz alisema kwa kipindi cha Januari 2011 hadi Mei 2012, bunduki 25
zimekamatwa na nyingine kusalimishwa kwa hiari ambapo kati ya hizo SMG
ni 19 na Riffle 8.
Risasi zilizokamatwa ni 686 za SMG na 630 za Riffle na short gun zikiwa 56.
“Ni
kweli silaha za kivita zinaingizwa nchini kutoka nchi jirani na idadi
hiyo ni kubwa na bado zipo nyingine hazijakamatwa ila bado tunaendelea
na uchunguzi kwa kuwa inaonyesha zinaingizwa kwa ajili ya kufanya
uhalifu,” alisema Kamanda Boaz.
Aliongeza, “Lakini wapo
wanaonunua na kudai kwamba wanazitumia kwa ajili ya kulinda mifugo yao,
lakini silaha za kivita hairuhusiwi kumilikiwa na mtu,”
alisema.Alipoulizwa kama askari nao wanahusika katika vitendo hivyo Boaz
alisema, “Ndiyo nasikia kutoka kwako, ila sina uhakika.”
Akizungumzia
matukio yaliyotokea Mei mwaka huu alisema zilikamatwa bunduki nne aina
ya SMG pamoja na risasi 436 ambazo ziliingizwa na watu kutoka Urambo na
Kigoma na kwamba, mbili kati za silaha hizo zilikuwa zimeishaingia
wilayani Serengeti kwa mkazi mmoja wa Kijiji cha Bisarara ambaye awali
alitoa risasi 228 na baada ya kubanwa akatoa nyingine.
Inadaiwa
kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amenunua SMG mbili na baada ya kukamatwa
alitaja mtandao wake ambao mmoja wa wenzake alikamatwa mjini Magumu na
mwingine Bunda.
RPC Kagera
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kagera, Henry Salewi alikiri kuingizwa kwa silaha hizo nchini
kutoka nchi za Uganda na Rwanda na kufafanua kwamba, huingizwa kupitia
njia za panya na kwamba ni vigumu kuwadhibiti watu hao.
“Ni kweli
silaha zinaingizwa kwa njia ya mabasi na boti. Eneo la mpaka wa nchi ni
kubwa hivyo kuwakamata ni kazi ila juhudi zinafanyika” alisema.
Alisema
silaha hizo zinatumika katika uhalifu na kuongeza, “Kwa kushirikiana na
wananchi tumekamata SMG na AK 47 pamoja na watu wanaopeleka silaha
hizo mikoa mbalimbali, wananchi wasikubali kukaa kimya wakati
wakiwafahamu watu hawa.”
RPC Shinyanga
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Athumani Diwani aliliambia Mwananchi
Jumapili kuwa silaha hizo zinatoka nchi za Rwanda na Burundi na kwamba
wanaoziingiza wanapitia mkoani Kigoma.
“Tuna changamoto kubwa kwa kuwa kasi hiyo hasa kwa mwaka jana ilikuwa kubwa, wanaingia na silaha za kivita,” alisema Diwani.
Alisema kuwa taarifa za polisi kuhusika katika matukio hayo wamezipata na wanazifanyia kazi.
RPC Kigoma
Kamanda
wa Polisi mkoani Kigoma Kamishna Msaidizi, Frasser Kashai aliliambia
gazeti hili kwamba sababu kubwa ya kushamiri kwa vitendo vya uingizaji
silaha inatokana na udhibiti mdogo katika maeneo ya mipaka ya nchi na
kwamba jambo hilo linavisumbua vyombo vya ulinzi na usalama.
“Burundi
licha ya kuwa ni nchi ndogo, wameathiriwa na migogoro, jambo
linalowafanya waingie nchini kutafuta hifadhi, lakini wanaingia na
silaha na kufanya uhalifu huku wakisaidiwa kuhifadhiwa na wananchi,”
alisema Kashai.
Alisema kuwa bunduki aina ya SMG na AK 47 ndizo zinazotumika katika uhalifu na uwindaji wa wanyama.
”Wanakuja
na nia mbalimbali lakini wakiona hali siyo nzuri wanaingia katika
hifadhi. Hivi sasa tunashirikiana na Tanapa kufanya msako. Tunawaomba
wananchi washirikiane na Jeshi la Polisi ili kukomesha vitendo hivi,”
alisema Kashai.
RPC Tabora
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Tabora (ACP) Anthony Rutha alisema watu hao wanaingiza bunduki
kwa kuzipitisha porini na kwamba huingizwa na wakimbizi ambao hurudi
nchini kwa maelezo ya kuja kusalimia ndugu na jamaa.
“Kambi ya
Ulyanhulu inatusumbua sana kwa kuwa pale zinaingizwa silaha kali kama
SMG na AK 47 na kituo chao kikubwa ni Urambo, Sikonge na hasa Usinge
ambako kunatisha zaidi kutokana na kuzungukwa na mapori,” alisema.
Hata hivyo alisema kwa sasa Usinge kumetulia baada ya kituo cha polisi kufunguliwa mapema mwaka huu.
“Kamati
za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Mwanza, Mara,Tabora, Shinyanga, Kigoma
na Kagera ziliomba kibali ofisi ya Waziri Mkuu ili tufanye operesheni
za pamoja lakini hatujawahi kujibiwa, bila kufanya hivyo hali itakuwa
mbaya.” alisema Rutha.
Rutha alisema mpaka sasa amepata taarifa
kuwa baadhi ya askari wilayani Kibondo wanahusika katika matukio hayo
na kwamba jambo hilo linachunguzwa.
RPC Mwanza
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow alisema kuwa silaha hizo zinaingizwa kutoka nchi jirani za Rwanda na Burundi.
“Kwa
jinsi mazingira yalivyo watu hawa wanaingia nchini kwa kutumia njia za
majini, barabara pamoja na njia zisizo halali jambo linalofanya vikosi
vya ulinzi kushindwa kuwadhibiti watu hawa,” alisema.
No comments:
Post a Comment