KUELEKEA KATIBA MPYA NA SISI TUIGE YA UFARANSA NINI SOMA MAPINDUZI 1789
Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 yalikuwa aina fulani ya maasi ya
wanaokandamizwa na kunyonywa, dhidi ya maisha duni, magumu na
yasiyovumilia miongoni mwa wananchi.
Baadhi ya mambo
yaliyochochea harakati na hatimaye mapinduzi, yaliyozaa moja ya katiba
za kwanza bora kabisa duniani, ni pamoja na mazingira tete ya kisiasa,
kijamii, kiuchumi na mchango wa wanaharakati wasomi walioiamsha jamii,
kama inavyotokea leo hapa kwetu.
Serikali ya Ufaransa,
ilijengeka juu ya utawala wa Mfalme mwenye mabavu (absolute monarch).
Licha ya kukua kwa mawazo mapya na mwamko juu ya utawala bora na haki za
binadamu, bado Mfalme alijiona ndiye chanzo cha mamlaka yote. Alizoea
kujitapa kwa kusema: “Mimi ndiye Taifa, na Taifa ndilo mimi”.
Kufikia nusu ya pili ya karne ya 18, ufalme ulikithiri kwa rushwa, udhaifu mkubwa kiutendaji na Taifa kukosa mwelekeo.
Nchini Ufaransa, kila mwananchi aliwekwa kwenye kundi la kitabaka,
maarufu kama estate. Tabaka la kwanza na la juu kabisa lilikuwa la
makasisi wa kanisa, wakiwamo ma-askofu, maparoko na viongozi wengine wa
kanisa. Hawa hawakuzidi 100,000 kwa idadi, katika nchi ya watu
25,000,000 wakati huo. Walikuwa na upendeleo maalumu katika jamii, kama
vile kusamehewa kodi zote, kutoshitakiwa na walikuwa matajiri
kupindukia.
Tabaka la pili lilikuwa la Wafaransa kutoka familia
zenye nasaba bora na maarufu. Kama ilivyokuwa kwa wale wa tabaka la
kwanza, hawa nao walikuwa matajiri, walisamehewa kodi; walishika nafasi
za juu serikalini na jeshini. Waliposhitakiwa mahakamani, waliweza
kuchagua wao wenyewe mahakimu wa kusikiliza na kuhukumu kesi
zilizowakabili.
Tabaka la mwisho, lilikuwa tabaka la tatu
lililojumuisha wananchi wengine wote, wakiwamo wafanyabiashara,
wanasheria, madaktari, wakulima wa kati na wadogo na wafanyakazi.
Zaidi ya asilimia 80 ya Wafaransa waliishi vijijini kwenye vishamba
vidogo vidogo kwa kuwa karibu ardhi yote ilimilikiwa na kanisa. Hawa
walichakaa kwa kodi lukuki walizotozwa na serikali ambazo tabaka la
kwanza na la pili hawakulipa.
Walitozwa kodi ya kanisa (tithe),
ambayo ilikuwa moja ya kumi ya mapato yote, walitozwa kodi ya ardhi
(taille) na walitozwa kodi ya kichwa (capitation).
Walilipa pia
kodi ya mapato (vingtiene), kodi ya chumvi (gabelle ) na walijitoa
nguvu kwa shuruti kujenga barabara za Mfalme kila wiki (corvee) na kodi
nyinginezo.
Ukiangalia hali ilivyo nchini kwetu sasa ni kama
tunapita njia hiyo ya matabaka kujengeka mithili ya Ufaransa ya kale,
huku tabaka la mwisho, la wakulima na wafanyakazi likionja adha ya kodi
lukuki na huduma duni lakini za gharama kubwa (maji, umeme, tiba, bei
duni za mazao).
Kufikia mwaka 1788, jamii ya walalahoi iliuona
utawala wa Mfalme Louis wa XVI kuwa usio na manufaa kwao na uliopitwa na
wakati. Maswali matatu yalitawala katika jamii wakati huo: Ni kwa namna
gani utawala huo wa mabavu ungefikia mwisho katika nchi isiyo na
katiba? Namna gani tabaka hizo tatu zingeweza kushirikiana kuuondoa
madarakani kwa njia ya kura? Tabaka hizo zitakaaje na kupiga kura?
Mei 5, 1789, Bunge Kuu la Ufaransa (The Estates General) la tabaka zote
tatu, liliketi mjini Versailles, kuzungumzia namna ambavyo katiba ya
nchi ingeweza kupatikana ili kukabiliana na madaraka makubwa ya Mfalme.
Wakati wabunge kutoka tabaka la tatu walitaka tabaka zote tatu zikae
kwa pamoja na kupiga kura kila “kichwa” kura moja, tabaka mbili za
kwanza, kwa kuhofu kuzidiwa kura na tabaka la tatu (lililokuwa na
wawakilishi mara mbili ya tabaka mbili za kwanza) na kuhatarisha maslahi
yake, zilitaka kila tabaka lipige kura peke yake na kutoa matokeo.
Kama tabaka la kwanza na la pili yangepiga kura juu ya kuwa au kutokuwa
na katiba kwa lengo la kulinda maslahi yake, tabaka la tatu
lingeshindwa kwa tabaka mbili kwa moja (2 – 1). Hapo bunge likaendelea
kukaa bila suluhu juu ya jambo hili.
Baada ya kuchoshwa na
udhalimu wa tabaka la kwanza na la pili; Juni 17, 1789, wabunge wa
tabaka la tatu walichukua uamuzi mgumu: walijitangaza kwa nguvu kuwa wao
ndio bunge pekee la Ufaransa.
Huku wakiwa wamefungiwa milango
wasiingie bungeni, wabunge hao walikusanyika kwenye kiwanja cha mpira na
kuapa kutotawanyika hadi hapo watakapoipatia Ufaransa katiba. Kiapo
hiki maarufu kinajulikana kama The Tennis Court Oath. Hapa Mapinduzi ya
Ufaransa yakawa yamekwishaanza.
Kuona hivyo, na kwa hofu kuu
juu ya nguvu ya umma kuanza kufanya kazi yake, Mfalme Louis wa XVI
aliitisha haraka kikao cha tabaka zote tatu na kuagiza zikae na kupiga
kura kila tabaka kivyake; lakini tabaka la tatu na baadhi ya wabunge
kutoka matabaka mawili ya kwanza, walikataa kutii amri.
Mmoja
wa wabunge wa tabaka la tatu, Count Mirabbeau, alisimama na kunguruma:
“Tupo hapa kwa matakwa ya watu; ni singe (bunduki) pekee zitakazotutoa
hapa, vinginevyo hatutoki”.
Kwa ushauri wa mke wake Marie
Antoinnete, Mfalme Louis wa XVI alituma jeshi kuvunja bunge. Lakini, kwa
mshangao wa kila mtu, askari walipofika eneo walipokusanyika, walitupa
silaha na kuungana na “waasi” hao, huku ghasia na maandamano yakizidi
kupamba moto mitaani kuwaunga mkono. Siku mbili baadaye, viongozi wa
dini na wale wenye nasaba bora, waliungana na walala hoi hao.
Juni 27, 1789, huku akiwa amejawa hofu, Mfalme Louis wa XVI alisalimu
amri na kuagiza wabunge wa tabaka zote tatu kukutana. Kufikia hapo, kile
kilichoanza kama bunge lililoitishwa kushauri tu, lilikuwa limegeuka
kuwa serikali ya kitaifa.
Wakati bunge la umoja wa kitaifa
likijadili nini cha kufanya, mmoja wao kutoka tabaka la wenye “nasaba
bora” alitoa mawazo kwamba, “wakulima walikuwa wakiasi dhidi ya
ukandamizaji, na kwamba, badala ya kwenda kinyume nao, bunge lipambane
na udhalimu huo”.
Agosti 4, 1789, bunge lilifuta maslahi na
marupurupu yote manono ya tabaka mbili za kwanza. Na kama hatua ya
kwanza kwa kazi ya kuandika katiba, bunge (au bunge la katiba kama
lilivyokuja kujulikana) lilitoa azimio juu ya haki za binadamu na za
raia.
Azimio hilo liliweka misingi mikuu ya serikali ambayo katiba iliyotarajiwa ilitakiwa kuzingatia, kama ifuatavyo:
Kwanza: Binadamu huzaliwa na kubakia huru na mwenye haki sawa.
Pili: Haki hizo ni haki asilia na ni pamoja na uhuru wa mtu binafsi, umiliki wa mali, usalama na haki ya kukataa kukandamizwa.
Tatu: Sheria ni kielelezo cha matakwa ya wananchi. Kila raia ana haki
kushiriki yeye mwenyewe, au kupitia wawakilishi (wabunge) wake katika
kuzitunga.
Nne: Mtu asituhumiwe, asikamatwe au kufungwa ila kwa kushitakiwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
Chini ya azimio hili, mambo kama uvumilivu wa kidini, uhuru wa
kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, yalitajwa kuwa moja ya mihimili
ya uhuru wa mtu na kwa serikali yenye uhalali wa kutawala.
Septemba 1791, katiba iliyokuwa ikisubiliwa kwa hamu na wananchi,
ilikamilika. Ilitoa na kufafanua kwa mara ya kwanza katika historia,
mgawanyo wa madaraka kati ya utawala, bunge na mahakama. Kazi ya kutunga
sheria ilikabidhiwa kwa bunge.
Jambo moja lisilo la kawaida
lililofanywa na bunge hilo la katiba ni kwamba, baada ya kukamilisha
kazi yake na kabla ya kujivunja, lilitangaza wajumbe wake kutostahili
kugombea ubunge wa bunge jipya.
Katiba ni mapambano; haiji kwa
ridhaa ya watawala. Mfalme Louis wa XVI alijaribu kuligawa Bunge ili
lisipate muafaka juu ya katiba wakilishi kwa ajili ya wananchi wote ili
kumwezesha kuendeleza udikteta wake kwa manufaa yake na maswahiba wake.
Bila nguvu ya umma wa wanyonge, inayoshinda nguvu ya mtutu wa bunduki,
Ufaransa isingepata Katiba bora na yenye kuzingatia utawala wa sheria na
haki za binadamu. Baada ya hapo, dunia yote, hadi sasa, iliiga katiba
hiyo ya Ufaransa.
Yaliyotokea na yanayotokea hapa nchini kuhusu historia ya michakato ya katiba hayatofautiani na yaliyotokea Ufaransa.
No comments:
Post a Comment