Watu 16 wameripotiwa kuuawa na
wengine kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kuvamia makanisa mawili
katika mji wa Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya hii leo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Upelelezi nchini Kenya, Muhoro Ndegwa, watu waliouawa saba ni raia na maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda maeneo ya ibada katika kanisa la Africa Inland Church, AIC.
Kanisa jengine lililoshambuliwa ni Kanisa Katoliki ambapo magruneti mawili yalirushwa, ambapo moja liliripuka na kujeruhi watu kadha.
Hakuna mtu wala kikundi kilichodai kuhusika na mashambulio hayo, japo katika mashambulio kadhaa ya siku zilizopita yalihusishwa na wanamgambo wa Kiislam wa Somalia wa kundi la Al-Shabaab.
Kenya ilipeleka vikosi vyake nchini Somalia mwaka jana kuwasaka wapiganaji wa Al-Shabaab ambao wametajwa kutishia usalama wa nchi.
Matukio ya mashambulio dhidi ya maeneo ya ibada na yenye mikusanyiko ya watu wengi yamekuwa yakiripotiwa katika siku za karibuni nchini Kenya, na mwishoni mwa wiki iliyopita watu watatu waliuwawa katika klabu moja mjini Mombasa, baada ya kushambuliwa kwa magruneti.
Aliyeshuhudia tukio hilo, aliiambia BBC kwamba barabara sasa hazina watu, isipokuwa tu askari wa usalama.
No comments:
Post a Comment