Vijana wengi tumeshapitia au tunapitia kwenye kipindi kigumu sana
maishani. Nina uhakika wengi wetu tumeshawahi kukosa usingizi wakati
tupo kitandani na kubaki tu kuangalia dari na kujiuliza maswali mengi
sana; nitafanya nini maishani? Mustakabali wa maisha yangu ni upi?
Nitakuwa wapi baada ya miaka miwili, mitano au hata kumi?
Bahati mbaya Watanzania hatuna hulka ya kujadili mambo kama haya kwa
uwazi tukiwa na ndugu, jamaa na marafiki zetu. Na matokeo yake
(tunaonekana kama) hatujifunzi kutoka kwa wenzetu — hili suala ndilo
linalonipa misongo kwenye mijadala mbalimbali. Kwahiyo, ni matumaini
yangu kuwa nasaha zilizopo kwenye makala hii zitabadilisha fikra za
angalau kijana mmoja na kutambua kuwa maisha yake ya baadae yako kwenye
viganja vyake! Kwa maneno mengine, wewe msomaji ndio mwenye uwezo mkubwa
wa kuamua maisha yako huko mbeleni yaweje.
Je, unajua una kipawa, kipaji au talanta ipi? Baada ya kumaliza elimu
ya sekondari au chuo kikuu, ulikuwa au unajua unataka ufanye nini; uwe
mtu wa aina gani kwenye jamii?
Kama unashindwa kujibu hayo maswali haraka na kwa ufasaha, usiogope
na wala usitetereke. Hauko mwenyewe, kijana. Wengi tumeshapitia na
tunaendelea kupitia kwenye kipindi ambacho fikra zetu zinakuwa zimejawa
na mawazo ya utata. Lakini utakubaliana nami kuwa wenzetu ambao tayari
wanajua wana vipaji fulani na kuvifanyia kazi, maisha yao huonekana
marahisi machoni mwa wengi.
Amini usiamini, majibu ya maswali mengi hupatikana hapa — kwenye tovuti ya Bongo Celebrity.
Jeff na timu yake wamekuwa wanajitahidi kutuletea mahojiano murua ya
watu maarufu wanaofanya vizuri Bongo kwenye nyanja mbalimbali, ili mimi
na wewe tujifunze mawili matatu kutoka kwao na kutumia ‘maujanja’
kwenye maisha yetu; kukuza vipaji vyetu na kuviendeleza.
Jifunze kutoka kwa waliofanikiwa
Kwa mfano, Profesa Jay akihojiwa huwa anatoa nasaha nyingi
sana ambazo binafsi naamini zinatakiwa kuhamasisha kila kijana
anayezisikia kwa namna moja au nyingine. Cha kusikitisha wengi wetu
tutakumbuka tu ni lini Mzee wa Mitulinga atatoa album mpya. Basi.
Sielewi kwanini tunafumbia macho ukweli kuwa Jay huwa anatembea na
karatasi na kalamu karibia muda wote, na akiona kitu ambacho anadhani
kitakaa vizuri kwenye mashairi yake huwa anakiandika papo kwa papo. Muda
mwingine hata akiwa na marafiki zake. Kama bado hujanielewa, Jay ni
mwandishi mzuri sana na huwa anaandika mashairi muda wote! Na suala la
kipaji chake kukua, kupevuka na kukomaa linajidhihirisha kila kukicha.
Kasikikilize wimbo unaoitwa Chuzi limekubali wa Hard Blasters Crew, halafu linganisha na mashairi yaliyojaa busara kwenye wimbo Machozi, Jasho na Damu aliouimba takribani miaka miwili baadae.
Ninachojaribu kukuasa kijana mwenzangu ni kama ifuatavyo: Fungua
macho ukiwa kwenye pita-pita na mihangaiko yako; ukiona kichuguu kizuri
angalia kwa makini na jifunze jinsi kinavyojengwa na siafu, badala ya kukisifia tu na kuendelea na safari.
Tambua una vipaji
Safari ya kutambua una kipaji au vipaji gani, kuvikuza na kuvifanyia
kazi inaweza ikawa ngumu au rahisi kutegemeana na mazingira na mazingara
uliyokulia na uliyomo. Huo ni mjadala mrefu sana ila sitaki kuzama
huko, kwasababu naamini vitu ambavyo vinampa mtu motisha vina nguvu
zaidi.
Kama nilivyosema hapo awali, usikubali mtu mwingine akuamulie maisha
yako ya baadae yaweje kwasababu tu amekuzidi umri au ana mamlaka
fulani. Aghalabu kauli zenye mamlaka zinaweza kukufunga mawazo yako na
kukusukuma kufanya jambo ambalo labda sio ile kitu roho inapenda. Pia,
usifuate mkumbo; jaribu kufikiria mustakabali wako binafsi kwanza.
Kwa mantiki hiyo, ni jukumu lako kugundua una vipawa gani. Sidhani
kama kuna njia rahisi ya kukwambia, “Aisee, bwa’ mdogo una kipaji
(fulani)! Kifanyie kazi.” Njia pekee itakayokuwezesha kufaulu huo
mtihani ni kujaribu kufanya na kufuatilia mambo mbalimbali — iwe kwa
kusoma vitabu vya taaluma au magazeti, kuongea na kubadilisha mawazo na
watu n.k. Huwezi kung’amua kuwa wewe ni mchezaji mzuri wa mpira kwa
kukaa kijiweni, wakati u mvivu wa hata kupiga danadana tu.
Jiulize, ingekuwa vipi kama Man Dojo na Domo Kaya wangekaa tu vijiweni Arusha na kutothubutu kujaribu kupiga gitaa na kuimba?
Usiogope kukosolewa
Changamoto kubwa mwanzoni ni kuondokana na hofu ya kufanya makosa au
kuogopa kukosolewa. Ni kawaida kila binadamu kuogopa, ila
kinachotufautisha ni jinsi tunavyokivuka hiki kihunzi. Unadhani sikujawa
na hofu hata chembe nilipopewa fursa ya kuandika hii makala na kuanika
mawazo yangu hadharani? Kilichonipoza ni ile motisha ya kutumia kasoro
zozote zitakazojitokeza na kuhakikisha naandika makala nzuri zaidi
nitakapopewa fursa nyingine.
Lengo langu kubwa ni kuanzisha mjadala mzuri, kwasababu ninaamini
kuna Watanzania wengine wengi wenye uzoefu na mawazo mazuri zaidi yangu,
na nina kiu na njaa ya kujifunza kutoka kwao!
Hadithi nzuri kuhusu kujua jinsi ya kutumia vema ukosolewaji inatoka kwa Sir Juma Nature. Sir Nature alitoka kwa njia ya kushirikishwa kwenye nyimbo kama Mtani Jirani, Mtulize na Maskini Jeuri. Mimi ni mmojawapo wa mashabiki wake wakubwa na nilivutiwa sana na kisa alichokiimba kwenye wimbo Mtani Jirani. Ila Juma wa kipindi kile ni tofauti na yule Juma aliyetikisa na Hili Gemu, Kighetto-ghetto (remix), Jinsi Kijana na nyimbo nyingine lukuki.
Juma alikuwa anatumia lugha ‘ngumu’ iliyokuwa inaeleweka kwa vijana
wa Kurasini, Keko, Temeke, Tandika, Mtoni na Mbagala. Nakumbuka P-Funk,
Bonny Luv, Sebastian Maganga na wengine wengi walimkosoa na kumshauri
‘alainishe’ mashairi yake. Kijana hakuzira wala kunywea, akaufanyia kazi
ushauri.
Jiamini na amini unachofanya
Labda hii ndio nguzo kubwa kuliko zote. Sijui kama inajengwa kwa
mambo niliyoyajadili kwa kifupi hapo juu, au ndio msingi unaohimili
niliyoyataja. Kama wewe hujiamini na wala huamini kuwa unachofanya ni
kizuri na kina manufaa kwa jamii, unategemea wanaokuzunguka wakuamini?
Hakika kauli za kutia moyo kutoka kwa wazazi, ndugu, marafiki na watu
ulio nao karibu zinaweza kukusaidia. Ila huwa napenda kusisitiza zaidi
ile motisha mtu binafsi aliyonayo.
Huyu Fid Q kipenzi cha wengi, safari yake haikuanzia na wimbo Mwanza au FidQ.com.
Kijana ilibidi atoke Mwanza kwa hela ndogo aliyokuwa nayo hadi Dar ili
aje kufanya alichoamini ni kipaji chake. Unaweza ukadhani alikuwa
anacheza karata tatu au kamari, kwasababu lolote lile lingeweza kutokea
kwenye safari yake na labda tusingepata kumsikia hata mara moja.
Bahati mbaya (kwa wapinzani wake) na nzuri (kwa mashabiki wake), alipewa nafasi ya kughani kwenye wimbo mmoja unaoitwa Ukweli na Uwazi uliopo kwenye album
ya Wachuja Nafaka. Fid Q akatoka rasmi. Ukisikiliza nyimbo zake mbili
za kwanza, utaafiki kuwa alikuwa anajiamini na anaamini alichokuwa
anafanya.
Sio kazi na dawa, bali ni kazi na kazi
Ingawa sipendi kurusha mawe ya lawama, nitajiona mwenye hatia kama nisiposema haya yafuatayo kwa wale ma-DJ na waandishi wa habari wanaopata fursa ya kuwahoji watu waliofanikiwa kwenye fani mbalimbali.
Wachache wenu mmesahau kuwa kazi mliyokuwa nayo ni dhamana. Mna zana
zote za kubadilisha fikra za watu wanaosikiliza vipindi vyenu. Mimi
siridhiki mnapotaja tu wimbo au kitabu fulani cha mhusika kitatoka lini
na mambo mengine kama hayo kwa dakika thelathini!
Mnasahau kuwa kazi mnazoletewa ni matunda yanayotokana na juhudi,
jasho na uwajibikaji wa wahusika. Kwanini mnashindwa kusisitiza kazi
nzuri hutokana na watu kujituma? Vipi, mbona mnashindwa kutuambia zile shows nzuri za Waunaume Halisi au TMK zinatokana na vijana kufanya mazoezi kila siku?
Ukiongea na watu waliofanikiwa utagundua kuwa, ukiacha vipaji
walivyonavyo, ni wavumilivu na wanajituma. Kwahiyo, kijana mwenzangu,
ukishagundua kipaji chako, huna budi kukilea, kukitunza na kukilinda
kama mboni za macho yako. Na muhimu zaidi ni kukifanyia kazi kila siku;
hakika hiyo ndio njia pekee itakayokuletea matunda.
Ukiangalia kulia, kushoto, mbele na nyuma utaona ‘vita baridi’ kati
ya kizazi cha vijana wa sasa na wa zamani. Bahati mbaya vijana wa sasa
(wanaonekana) wamepoteza matumaini na wamebakia kulaumu, ilihali
wanaweza kuamka, kugundua vipaji vipaji vyao, kujenga moyo wa kujiamini
na kufanya kazi ili kuleta mabadiliko.
Nchi inahitaji kina Modesta, Zitto na January kwenye kila mkoa;
viongozi wapya wanahitajika. Magazeti yanahitaji waandishi wanaoweza
kuakisi mawazo yetu. Jenerali Ulimwengu akistahafu,
hatuna budi kuliziba pengo lake kwa kuwa tutaendelea kuhitaji makala
zitakazotufanya tufikirie. Wahandisi na wanasheria wanahitajika na
wataendelea kuhitajika.
Kijana, huu ni waraka kwako: Tambua na tumia kipaji chako ipasavyo — usijidharau.
No comments:
Post a Comment