Dola kuu za Magharibi
zimetangaza kwamba zinawafukuza mabalozi wa Syria kama hatua ya kulaani
mauaji ya zaidi ya raia 100 katika eneo la Houla Ijumaa wiki jana.
Ufaransa, Uingereza, Ujeremani, Italia, Hispania Canada na Australia zimethibitisha kuwafukuza mabalozi hao.Wengi wa raia waliouawa wakiwemo watoto na wanawake waliuawa kinyama kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Wakaazi wa eneo hilo wamesema wapiganaji wanaounga mkono serikali waliingia makaazi ya raia na kuwaua watu kiholela.Tukio la sasa linajiri wakati Mjumbe maalum wa Kimataifa Koffi Annan amefanya mkutano na Rais Bashar al Assad mjini Damascus.
Waangalizi wa Umoja wa Mataifa ambao walizuru eneo la Taladou wamesema waathiriwa wengi waliuawa kwa kupigwa risasi au kudungwa visu.
Utawala wa Syria umelaumu makundi ya waasi kwa mauaji haya kama hatua ya kuhujumu mpango wa amani na kutoa nafasi kwa dola za magharibi kuendelea kulalamikia utawala huo.
Urusi ambayo imeendelea kutoa silaha kwa utawala wa Syria imesema mauaji yalitekelezwa na pande zote.Koffi Annan ametaja mauaji haya kama ya kinyama na ameonya athari mbaya kufuatia matukio ya sasa.
Kabla ya kukutana na Rais Assad, Bw. Annan amesema serikali ya Syria sharti ionyeshe nia ya kufanikisha majaaliwa ya amani.
Mpango wa amani uliopendekezwa na Koffi Annan kwa Syria ulizitaka pande zote kumaliza mapigano hapo Aprili 12, kutumwa kwa waangalizi wa kimataifa pamoja na wanajeshi wa serikali kuondoka maeneo ya raia.
No comments:
Post a Comment