NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, May 15, 2012

Rais mpya wa Ufarnsa Hollande aapishwa


Rais Francois Hollande

Francois Hollande ametawazwa kama rais mpya wa Ufaransa, na kumfanya kuwa rais wa kwanza wa kisosholisti kuapishwa katika miaka kumi na saba.
Bwana Hollande alisema kuwa anafahamu vyema changamoto ambazo Ufaransa inakabiliana nazo ikiwemo, madeni na uchumi unaojikokota.
Baadaye hii leo rais Hollande atamteua waziri mkuu na kisha kwenda nchini Ujerumani kwa mazungumzo na Chansella Angela Merkel.
Bwana Hollande angependa kufanya mazungumzo zaidi kuhusu mpango wa Ujerumani wa kutafuta suluhu kwa mgogoro wa kiuchumi unaokumba bara la Ulaya.
Hapo jana thamani ya Euro ilishuka masoko ya hisa nayo yakishuka huku hali ya kisiasa nchini Ugiriki ikiendelea kuwa tete.
Mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa fedha wa ulaya, Jean-Claude Juncker, alisisitiza hapo jana kuwa watafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa Ugiriki inasalia katika muungano wa Ulaya.
Bwana Juncker anasubiri kuundwa haraka kwa serikali mpya ya Ugiriki siku tisa baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Lakini pia alionya kuwa Ugiriki haina budi ila kuendelea na juhudi muhimu zilizoanzishwa kuweza kuokoa uchumi wake licha ya sera hizo kupingwa na wapiga kura wengi.
Wengi mjini Berlin wanamshuku bwana Hollande. Hawapendi kuwa wakati wa kampeini zake alionekana kupinga mipango ya kupunguza matumizi ya serikali kwa lengo la kuokoa uchumi pamoja na kuukuza.
Wengi walitafsiri hilo kama juhudi za Ufaransa kutaka kuongoza tena muungano wa Ulaya.

No comments:

Post a Comment