Kikosi cha kwanza cha wanajeshi
wa usalama kutoka Afrika Magharibi, kimewasili nchini Guinea-Bissau
kusaidia kuleta uthabiti nchini humo. Hii ni baada ya tukio la mapinduzi
ya kijeshi yaliyofanyika mwezi jana.
Takriban wanajeshi 70 wote kutoka Burkina Faso
ni sehemu ya vikosi vya usalama vilivyopangiwa kufika nchini humo na
jumuiya ya Ecowas.Takriban wanajeshi 600 wanatarajiwa kufika nchini humo katika siku chache zijazo kulingana na taarifa iliyotolewa na Ecowas.
Guinea-Bissau ilikuwa imesalia na wiki kadhaa kuandaa duru ya pili ya uchaguzi wa urais, wakati jeshi lilipofanya mapinduzi.
Wanajeshi hao waliwasili siku moja na waziri mkuu wa serikali ya mpito, Rui Duarte Barros, aliyetawazwa baada ya mapinduzi.
Viongozi wa mapinduzi hayo, walikubaliana hapo awali kuhusu kipindi cha mwaka mmoja wa ukabidhi wa mamlaka, kama ilivyotakiwa na jumuiya ya Ecowas.
Vikosi hivyo vya usalama, vinapelekwa nchini humo kuweza kusaidiana na wanajeshi kutoka Angola na vile vile kuweza kusaidia harakati za kurejesha utawala wa kikatiba.
No comments:
Post a Comment