JK AWATUPA MKULO,NGELEJA,MAIGE,NUNDU NA DK MPONDA,ATEUA
WATATU WAPYA,PROFESA MAGHEMBE,MKUCHIKA WAPONA MAKAMBA SIMBACHAWENE SASA
MANAIBU.
Rais Jakaya Kikwete akitangaza Baraza jipya la Mawaziri, Ikulu jana.
RAIS Jakaya Kikwete amefanya
mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua wapya watatu na
manaibu 10 huku akiwaacha wanane.
Katika
mabadiliko hayo, Rais Kikwete amewapandisha manaibu mawaziri wanne kuwa
mawaziri kamili na kuwahamisha wizara mawaziri wanane na manaibu waziri
sita, huku mawaziri na manaibu waziri 22 wakibaki katika wizara zao za
awali.
Kutokana na mabadiliko hayo, idadi ya mawaziri na manaibu
wao sasa imeongezeka kutoka 50 katika baraza la awali hadi 55. Mawaziri
kamili wameongezeka kutoka 29 hadi 30 huku manaibu waziri wakiongezeka
kutoka 21 hadi 25.
Mawaziri ambao wameng’olewa na wizara
walizokuwa wakiziongoza kwenye mabano ni Mustafa Mkulo (Fedha), Dk Hadji
Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) William Ngeleja (Nishati na Madini),
Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omar Nundu (Uchukuzi) na Ezekiel
Maige (Maliasili na Utalii).
Panga hilo la mabadiliko limewakumba
pia Manaibu Waziri wawili, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk
Athumani Mfutakamba (Uchukuzi).
Akitangaza baraza hilo Ikulu
jana, Rais Kikwete alisema mabadiliko hayo yametokana na mjadala mkali
ulioanzia bungeni baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba ametumia fursa hiyo
kufanya marekebisho kadhaa ili kuimarisha utendaji wa Serikali.
“Baada
ya kuwasilishwa kwa taarifa ile kulikuwa na mjadala mkali bungeni,
lakini pia kwenye kikao cha wabunge wa chama na Waziri Mkuu (Mizengo
Pinda), alinipa taarifa hiyo na wanasema mawaziri wote waliotajwa
waondolewe,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Tumekaa kwa pamoja na
kumwangalia kila mmoja na tuhuma zake, kwa Kiingereza tunasema ‘case by
case’ na tukaona kwamba wawili kati yao tuwahamishie katika wizara
nyingine lakini tukatumia fursa hiyo kufanya mabadiliko mengine kwa
lengo la kuimarisha utendaji wa Serikali.”
Mawaziri wengine ambao
walikuwa wakikabiliwa na shinikizo la kuondolewa madarakani ni
aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George
Mkuchika na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne
Maghembe.
Mkuchika sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais – Utawala Bora
wakati Maghembe amehamishiwa Wizara ya Maji akichukua nafasi ya Profesa
Mark Mwandosya ambaye ameteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais,
asiyekuwa na Wizara Maalumu.
Rais Kikwete alisema ameteua manaibu
waziri wawili katika Wizara ya Nishati na Madini; mmoja
atakayeshughulikia masuala ya nishati na mwingine madini.
“Kulikuwa
na mjadala mkali kuhusu kutenganishwa kwa wizara hii ya nishati na
madini, lakini tumeangalia kwamba kuunda wizara mpya katikati hivi
halafu kuna masuala ya kibajeti, tukaona itatusumbua, hivyo tumeamua
kuwe na manaibu waziri wawili halafu hayo mapendekezo mengine tukasema
tuangalie mbele ya safari,” alisema.
Alisema uamuzi huo
umezingatia ukubwa wa wizara hiyo na changamoto zake akisema nishati ni
sekta inayokua hasa kutokana na kugundulika kwa kiasi kikubwa cha gesi
pia kuwapo kwa dalili za kupatikana kwa mafuta.
Alisema kwa
upande wa madini, pia sekta hiyo imekuwa ikikuwa kwa kiasi kikubwa na
kwamba kwa miaka mitano mfululizo imekuwa ikishika nafasi ya pili katika
kuliingizia taifa mapato, baada ya utalii.
Mbali na kuongezwa
kwa naibu waziri katika wizara hiyo, Rais Kikwete pia ameteua manaibu
waziri katika wizara ambazo awali hazikuwa na nafasi hizo.
Wizara hizo ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Katiba na Sheria na Maliasili na Utalii.
Mawaziri wapya
Mawaziri
wapya walioteuliwa na Wizara zao kwenye mabano ni Mbunge wa Handeni,
Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Mbunge wa Kalenga, Dk William
Mgimwa (Fedha) na Mbunge wa Kuteuliwa Profesa Sospeter Muhongo (Nishati
na Madini).
Walioteuliwa kuwa Manaibu Waziri ni Mbunge wa Rufiji
Dk Seif Suleiman Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Kibakwe,
George Simbachawene (Nishati na Madini), Mbunge wa Bumbuli, January
Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Mbunge wa Buchosa, Dk
Charles Tizeba (Uchukuzi) na Mbunge wa Mvomero, Amos Makala (Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo).
Wengine ni Mbunge wa Makete, Dk
Binilith Mahenge (Maji), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Maselle
(Nishati na Madini – Madini), Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki
(Katiba na Sheria) na Wabunge wa Kuteuliwa Janet Mbene na Saada Mkuya
Salum wote Fedha.
Naibu Mawaziri waliopandishwa na kuwa mawaziri
kamili wamo, Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk
Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Fenella Mukangala (Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo) na Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).
Kabla
ya kuwa mawaziri kamili, Chiza na Dk Mukangara walikuwa Naibu mawaziri
katika wizara walizopangiwa wakati Dk Mwakyembe alikuwa Naibu Waziri wa
Ujenzi na Kaghasheki alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mawaziri
wengine waliohamishwa kutoka wizara zao za awali ni, Celina Kombani
kutoka Katiba na Sheria kwenda Ofisi ya Rais (Manejimenti ya Utumishi wa
Umma) ambako amechukua nafasi ya Hawa Ghasia ambaye amehamishiwa Ofisi
ya Waziri Mkuu (Tamisemi).
Shamsi Vuai Nahodha amehamishiwa
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambako amechukua nafasi ya
Dk Hussein Mwinyi ambaye amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Dk
Emmanuel Nchimbi amehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
kuchukua nafasi ya Nahodha akitokea Wizara ya Habari, Utamaduni na
Michezo wakati Waziri wa Katiba na Sheria ni Mathias Chikawe ambaye
alikuwa Ofisi ya Rais Utawala Bora.
Manaibu waziri waliohamishwa ni
Charles Kitwanga ambaye amepelekwa Ofisi ya Makamu wa Rais akitokea
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Adam Malima ambaye
amehamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika akitokea Nishati na
Madini na Pereira Ame Silima ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Fedha sasa
anakuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Gregory Teu
ambaye pia alikuwa Wizara ya Fedha amehamishiwa Wizara ya Viwanda na
Biashara ambako anachukua nafasi ya Lazaro Nyalandu ambaye amehamishiwa
Wizara ya Maliasili na Utalii, wakati aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji,
Gerson Lwenge, amehamishiwa Wizara ya Ujenzi, kuchukua nafasi iliyoachwa
wazi na Dk Mwakyembe.
Waliobaki kwenye nafasi zao
Mawaziri
waliobaki kwenye nafasi zao ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Wengine
ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa
Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk
Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia
Simba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo.
Pia
wamo Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka; Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Kwa upande wa
Manaibu Waziri wamo Kassim Majaliwa (Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi -
Elimu), Aggrey Mwanry (Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi), Dk Makongoro
(Kazi na Ajira) na Benedict Ole-Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).
Wengine
ni Mahadhi Juma Maalim ( Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa),
Goodluck J. Ole-Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Ummy
Mwalimu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Philipo Mulugo (Elimu na
Mafunzo ya Ufundi), Dk Abdulla Juma Abdulla (Ushirikiano wa Afrika
Mashariki).
Uwajibikaji
Kuhusu uwajibikaji Rais Kikwete
alisema baada mawaziri kuwajibika kisiasa, wanaofuta ni watendaji katika
wizara na taasisi nyingine za umma ambao ndiyo chanzo cha mawaziri hao
kuwajibika.
Alisema mawaziri wamekuwa wakijiuzulu hata kwa makosa
ambayo si yao na kwamba hivi sasa Serikali itaanza kuchukua hatua kwa
watendaji wakiwamo makatibu wakuu, wakurugenzi wa wizara, watendaji
wakuu wa mashirika na taasisi za umma pamoja na bodi za mashirika
husika.
“Pamoja na kuwa na utaratibu huu mzuri wa kuwajibika kwa
wanasiasa, sasa lazima tuwawajibishe hata hao wanaosababisha mawaziri
hawa kujiuzulu, maana wakati mwingine wanawajibika kwa makosa ambayo si
yao,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Kuna watu ambao kazi yao ni
kupiga fitina tu … wao wana kazi ya kusema kaja hapa ataondoka kwani
yeye ni nani bwana …… sasa watu wa aina hii hatuwezi kuendelea
kuwavumilia hata kidogo, lazima hatua zichukuliwe kwa watendaji wakuu
awe ni katibu mkuu wa wizara, ofisa mtendaji mkuu wa shrika la umma,
mkurugenzi wizarani au hata bodi ambazo zinasimamia taasisi hizi.”
Mawaziri wapya na waliohamishwa wataapishwa keshokutwa Jumatatu kuanzia saa 5:00 asubuhi katika Viwanja vya Ikulu.
No comments:
Post a Comment