GHARAMA za kifaa kilichoharibika kwenye rada kutoka Kampuni ya
BAE System ya Uingereza na kuibua utata mkubwa nchini, kitagharimu sh
milioni 40.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Fadhili
Manongi, alisema kuwa wahandisi wamebaini kuwa kifaa hicho, Power Supply
Unit kiliharibika wiki tatu zilizopita.
Rada hiyo iliyonunuliwa kwa ushauri wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Andrew Chenge, iligharimu sh bilioni 40 na kuibua mjadala
mzito ndani na nje ya nchi kwamba imenunuliwa kwa bei kubwa kuliko bei
halisi.
Manongi alisema kutokana na tatizo hilo, wahandisi na wataalamu wa
rada hiyo wamelazimika kuzima mtambo wake, huku wakifanya mawasiliano na
Kampuni ya BAE Systems ili kupata kifaa kingine.
“Ubovu wa kifaa hicho ulibainika wiki tatu zilizopita na tukalazimika
kuzima mtambo la sivyo kama tusingebaini hilo mtambo ungeweza kuharibika
kabisa. Jumatatu ya wiki ijayo tutakipeleka kifaa hicho nchini Afrika
Kusini kuona kama wanaweza kukitengeneza na wasipoweza tutaagiza BAE
System kutupatia kifaa kingine,” alisema Manongi.
Hata hivyo, alisema ni kawaida kwa mtambo huo kuzimwa kwani kuna
wakati wahandisi hulazimika kuzima ili kuweka mafuta mazito ya grisi.
Manongi, alisema kifaa hicho hakiwezi kupatikana mara moja kwani
lazima utoe taarifa kwa kampuni husika ili iweze kukitengeneza.
Alisema pamoja na kuharibika kifaa hicho, bado huduma za usafiri wa
anga zimeendelea kufanya vizuri, huku kukiwa hakuna malalamiko kutoka
kwa wateja wa ndani na nje ya nchi.
Kuhusu usalama wa anga, Manongi, alisema wamekuwa wakifuatilia kwa
karibu suala hilo na hakuna tatizo lolote lililojitokeza tangu
kuharibika kwa kifaa hicho.
“Hii sio mara ya kwanza kuharibika na kubadilisha vipuri katika mtambo
huo kwani tumekuwa tukifanya hivyo mara nyingi tu…ikumbukwe kuwa huu ni
mwaka wa 12 tangu tuwe na rada hiyo,” alisema.
Alisema kuwa huduma za anga zimekuwa zikiendeshwa sio na rada peke
yake, bali kuna vitu mbalimbali vinavyosaidia na kuvitaja kuwa ni Non
Directional Beacon (Non), Very High Omni Direction Range (VOR) na
Distance Measuring Equipment (DME).
Ununuzi wa rada hiyo uliogharimu sh bilioni 40, umekuwa ukipigiwa
kelele na watu wa kada mbalimbali wakidai kulikuwa na rushwa.
Hata hivyo hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete alisema hakuna rushwa
katika ununuzi wa rada hiyo na baadaye kuungwa mkono na Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye aliwahi kuahidi
kwamba angewataja watuhumiwa hao.
Membe aliyewasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake
bungeni hivi karibuni, alishindwa kutekeleza ahadi yake licha ya
kutakiwa kufanya hivyo na baadhi ya wabunge, wakiongozwa na Waziri
Kivuli wa wizara hiyo, Ezekia Wenje (CHADEMA) ambaye pia ni Mbunge wa
Nyamagana.
Kabla Membe hajasoma hotuba yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias
Chikawe alitoa taarifa rasmi ya serikali bungeni kuhusu suala hilo na
alisema hakuna mtuhumiwa wa rada anayeweza kupelekwa mahakamani na
kutamka kwamba mjadala kuhusu suala hilo umefungwa.
Kashfa hiyo ya rada, imekuwa ikimhusisha Chenge ambaye pia aliwahi
kukutwa na kiasi cha sh 1.2 bilioni, kisiwani Jersey, Marekani ambazo
Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, ilikuwa
ikichunguza kama zilikuwa na uhusiano na biashara hiyo.
Chanzo cha Habari Mtanzania Daima
No comments:
Post a Comment