Mbowe: Tupeni madaraka kwa masharti
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, amewataka Watanzania kukiweka kando Chama cha Mapinduzi
(CCM) na badala yake wakichague CHADEMA kwa masharti kwamba kikishindwa
kusimamia masilahi yao nacho kiondolewe.
Alisema ni makosa makubwa kwa wananchi kufikiria kuwa CCM ndicho baba
na mama yao, hivyo kuwataka wakinyime kura katika chaguzi mbalimbali kwa
kuwa kimeshindwa kuwaondolea kero zao.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na
Mbunge wa Hai, alitoa kauli hiyo juzi jioni katika Kata ya Hembeti,
jimboni Mvomero, mkoani Morogoro, alipozuiliwa kwa muda na wananchi
wakitaka awahutubie.
Alisema kuwa kwa sasa wananchi wanapaswa kuachana na CCM badala yake
wakichague CHADEMA lakini akaweka bayana kuwa endapo nacho kitashindwa
kusimamia masilahi yao, kiwekwe pembeni.
“Mimi Mbowe leo nikiona CHADEMA haiendani na mahitaji ya wananchi na
kushindwa kuongoza, sitakuwa na sababu ya kuendelea kuwa
mwana-CHADEMA, sasa ninyi mnang’anga’nia CCM kwa nini?” alihoji huku
akishangiliwa na wakazi hao.
Mbowe alipita eneo hilo akitokea mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria
vikao vya Bunge, akielekea Kata ya Mtibwa mkoani humo, kuungana na
viongozi wenzake katika operesheni ya vuguvugu la mabadiliko ( M4C)
ndipo akazuiliwa kwa muda katika Kata ya Hembeti ambako kulikuwa na
mkutano wa chama hicho.
Mkutano huo ambao ulikuwa ukihutubiwa na Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar,
Hamad Yusuph, ulisimama kwa muda huku wananchi wakizuia gari la Mbowe
lisiendelee na safari wakitaka awahutubie.
Hali hiyo ilimlazimu kada wa chama hicho, Arcado Ntagazwa, aliyekuwa
akihutubia kumpa kipaza sauti Mbowe kwa ajili ya kusalimia umati huo.
Akihutubia mkutano huo, Mbowe alisema kuwa dhamira ya CHADEMA kuwapo
mkoani Morogoro ni kuwaondoa wananachi wa mkoa huo katika
wimbi la usingizi wa kuishabikia serikali ya CCM aliyodai imeshindwa
kutatua matatizo ya msingi ya nchi.
“Tunapita kila kata ya Mkoa wa Morogoro kujenga mtandao wa chama bila
kujali dini, kabila wala rangi, ujumbe wangu kwa wana-Hembeti ni kujua
wajibu wa chama cha siasa ni kupata viongozi na sera mbadala
zitakazowezesha nchi kusonga mbele,” alisema Mbowe.
Mbowe aliongeza kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuwatoa watu
katika matatizo na kuwapeleka katika neema huku akiwataka wakazi hao
kutafakari miaka 50 ya Uhuru imewafikisha wapi.
Alisema kuwa Mkoa wa Morogoro umefunga ndoa na CCM, hali
inayowafanya wasiwe na sauti ya moja kwa moja hadi matatizo yao
yaongelewe na wabunge wa vyama vya upinzani kutoka maeneo mengine.
“Tunawaunganisha wana CCM, CUF na vyama vingine na wengine katika
kuikomboa Tanzania, tunawaomba msiwacheleweshe wakazi wa mikoa mingine
katika kusonga mbele kwa kuwa ninyi mmefunga ndoa na Chama cha
Mapinduzi,” aliongeza.
Naye Ntagazwa, akihutubia katika vijiji vya Kambala, Hembeti na Mkindo
kunakokaliwa na jamii ya wafugaji na wakulima, alisema migogoro ya
ardhi nchini inakuzwa kwa makusudi na watawala kwa vile wana masilahi
nayo.
Alisema watendaji na watawala wa serikali ya CCM badala ya
kuwakutanisha wakulima na wafugaji kwa ajili ya kuondoa tofauti zao wao
hutumia fursa hiyo kuchukua fedha kwa mmoja wao na kisha kuacha uhasama
miongoni mwa wafugaji na wakulima.
“Msidhani matatizo yenu yanashindwa kutatuliwa ila huo ni mradi wa
watu kwa maana leo ng’ombe wa mfugaji akiingia katika shamba la
mkulima na akapelekwa kwa mtendaji kwa ajili ya kulipwa fidia, mtendaji
anachukua fedha kwa mfugaji na mkulima, hali inayomfanya mfugaji
aendelee kuwa na kiburi cha fedha na mkulima awe na uchungu wa
kuharibiwa mali yake,” alisema Ntagazwa
No comments:
Post a Comment