Rais wa Nigeria, Goodluck
Jonathan, ameonya kuwa hapatakuwa na chaguo jingine ila kuingilia
kijeshi mzozo uliopo nchini Mali iwapo hakutakuwa na mwafaka na makundi
ya kiislamu yaliyojihami.
Akizungumza katika ziara yake nchini Senegal, rais huyo amesema kuwa wanajeshi 3000 kutoka Jumuiya ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, watatumwa nchini humo lakini azimio la Umoja wa Mataifa pamoja na msaada utahitajika.
Alisema kuwa wajumbe watatumwa Bamako kukutana na serikali mpya kufuatia malalamishi kwamba maeneo mbali mbali ya Mali hayajawakilishwa kwenye serikali.
Kulingana na Rais Jonathan, hilo litakapoafikiwa, basi watakuwa radhi kuzungumzia mzozo wa Kaskazini mwa nchi hiyo.
Alisema mzozo wa Mali unapaswa kusuluhishwa kwa mazungumzo, lakini iwapo hayatafaulu basi hakutakuwa na budi ila kutumia nguvu za kijeshi, "njia za kidiplomasia na mashauriano ndio zitakazopowa kipaumbele. Na iwapo mashauriano hayatafaulu, basi tutatumia jeshi kusuluhisha mzozo huu. Jumuiya ya kiuchumi kwa mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, itatumia majeshi kuingilia kati kwenye mzozo huu lakini hata kabla ya kufanyika hivyo lazima Umoja wa Mataifa ikubali kwa sababu tuko chini ya sheria sawa na mikataba sawa.''
Rais Jonathan alikiri kuwa mataifa ya Magharibi mwa Afrika pekee hayawezi kuingilia kati mzozo wa Kaskazini mwa Mali.
Ecowas inasema kuna kikosi cha wanajeshi 3000 ambacho kiko tayari kupelekwa Mali.
Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, majeshi hayo bado hayajakusanywa na mradi wapate msaada wa kifedha kutoka kwa mataifa ya Magharibi kabla ya kuelekea Mali.
Mali kwa upande wake imepinga mzozo huo kuingiliwa na mataifa ya kigeni huku ikishikilia kuwa jeshi yake ikipata msaada wa kifedha itaweza kukabiliana na mzozo huo.
No comments:
Post a Comment