NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, August 28, 2012

Wafungwa tisa wauawa nchini Gambia

Rais wa Gambia Yahya Jammeh
Wafungwa tisa wameuawa nchini Gambia licha ya wito kutoka kwa jamii ya kimataifa dhidi ya sera rasmi nchini humo ya kutekeleza hukumu zote za kunyongwa kwa wafungwa mwezi ujao.
Wafungwa hao, waliuawa kwa kupigwa risasi siku ya jumapili , kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani.
Rais wa nchi hiyo, Yahya Jammeh aliahidi kuwauwa wafungwa wote arobaini na saba waliohukumiwa kunyongwa ifikapo katikati ya mwezi Septemba.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa ushirikiano na jamii ya kimataifa yameelezea wasiwai na kutoa wito kwa rais Jammeh kutotekeleza adhabu hiyo.
Shirika la kimataifa la Amnesty International, lilikemea sera hiyo wiki jana wakati lilipofichua kuwa vifo hivyo vilitekelezwa siku tatu zilizopita.
Wengi wa wafungwa wa Gambia ambao wamehukumiwa kunyongwa ni maafisa wakuu wa zamani pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi ambao wamekuwa wakifungwa kwa madai ya uhaini tangu mwaka
1994, wakati rais Jammeh alipoingia mamlakani kwa njia ya mapinduzi.
Mkuu wa sera ya kigeni katika muungano wa Ulaya, Catherine Ashton, ameitaka serikali ya Gambia kukoma kutekeleza hukumu ya kuwanyonga wafungwa mara moja.
Hotuba ya siku ya Eid
Mwanamke mmoja ni miongoni mwa wale walionyongwa kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya ndani. Baadhi ya makosa aliyopatikana na hatia nayo ni, mauaji, uhaini, biashara haramu ya madawa ya kulevya, ulanguzi wa watu na mengineyo. Yote hayo hukumu yake ikiwa kunyongwa.
Hukumu ya kunyongwa ilifutiliwa mbali na rais wa zamani, Dawda Jawara lakini ikarejeshwa mwaka 1995 pindi rais Jammeh alipochukua mamlaka.
"ifikapo kati kati ya mwezi ujao, wafungwa wote waliohukumiwa kunyongwa, hukumu zao zitakuwa zimetekelezwa. Hakuna namna ambavyo serikali yangu itaruhusu asilimia 99 ya watu wa nchi hii kuishi katika hofu ya wahalifu." alisema rais Jammeh katika hotuba ambayo ilipeperushwa moja kwa moja kuliptia runinga ya taifa tarehe kumi na tisa mwezi Agosti wakati wa sherehe ya siku ya Idd.
Kwa upande wake, rais wa Benin Benin, Thomas Boni Yayi, ambaye ndiye mwenyekiti wa muungano wa Afrika alituma waziri wake wa mambo ya nje nchini Gambai kutoa onyo kwa rais Jammeh dhidi ya kuendelea kutekeleza hukumu ya kunyongwa.

No comments:

Post a Comment