CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa
kutokana na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola,
Rais Jakaya Kikwete, anapaswa kuingilia kati kuunda tume huru ili
kuwezesha uchunguzi wa kina.
Hata hivyo, wakati CHADEMA ikitaka tume huru ya kuchunguza matukio
hayo likiwemo lile la kuuawa kwa kijana Ally Hassan Singano maarufu kama
Zona katika maadamano yao juzi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro,
limejivua lawama za mauaji hayo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
wa CHADEMA, John Mnyika, alisema wanapinga kauli za serikali, Jeshi la
Polisi na CCM zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauaji
yanayoelezwa kufanywa na askari mkoani Morogoro.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa kauli zilizotolewa
na Waziri wa Mambo ya Ndani juzi, Dk. Emmanuel Nchimbi zina mwelekeo wa
kulilinda Jeshi la Polisi, ambalo askari na maofisa wake ni sehemu ya
watuhumiwa wa mauaji badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua
kuchukuliwa kwa wahusika.
“Ikumbukwe kuwa Agosti 27 mwaka huu, polisi mkoani Morogoro walifyatua
risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi wananchi na wanachama wa
CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye mkutano
halali, na kusababisha kifo cha raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi
wengine wawili,” alisema.
Alisema kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo mbalimbali nchini,
Serikali ya CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka ibara ya 14
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba
uhai ni haki ya msingi wa raia wote.
Mnyika alibainisha kuwa, hawakubaliani na hatua zilizochukuliwa na
serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa
na Waziri Nchimbi juzi, ambayo alidai kwa sehemu kubwa yametokana na
taarifa zisizo za kweli kutoka polisi.
“CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi
kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya machozi na
kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na jeshi hilo wametoa
maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Kwamba wakati serikali na polisi wakisema kuwa marehemu alikutwa
umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda
wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja
akaonesha ishara, na ndipo mabomu ya machozi na risasi za moto
zikafyatuliwa na mojawapo kumpata na kudondoka.
Mnyika alidai kuwa mashahidi wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki
ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee
yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za
moto na wengine wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya
machozi.
Aliongeza kuwa sababu zilizotolewa na serikali kuwa polisi walizuia maandamano ya
CHADEMA mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za
kweli kwa vile sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa
yalipangwa siku ya kazi.
Kwa mujibu wa Mnyika, ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la
Polisi ya Agosti 23, 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL.II/202 na
kwamba polisi mkoani Morogoro ndio waliacha kuheshimu utawala wa sheria
na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo ya pande zote.
“Kwa kuzingatia
utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na serikali na Jeshi la
Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA
kinasisitiza kuwa uchunguzi huru ufanyike kwa mujibu wa sheria ya
uchunguzi wa vifo sura ya 24 ya sheria za Tanzania,” alisisitiza.
Wajitetea Moro
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema kuwa
matokeo ya uchunguzi wa tukio hilo, yalionesha kwamba jeraha lililokuwa
kichwani kwa marehemu lilitokana na kugongwa na kitu kizito
kilichorushwa na si risasi.
Alisema kuwa uchunguzi huo ulifanywa na madaktari wawili wa mkoani
humo pamoja na Dk. Ahmed Makata kutoka jijini Dar es Salaam na
kushuhudiwa na mwanasheria wa CHADEMA, Aman Mwaipaya na baadhi ya
askari.
Kamanda Shilogile alisema kuwa baada ya matokeo hayo ya daktari,
polisi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kubaini kitu hicho kilichorushwa
na kusababisha kifo cha kijana huyo.
Alisema kuwa baadaye Jeshi la Polisi litachukua hatua za kisheria kwa
askari ama mtu mwingine atakayebainika kuwa alirusha kitu hicho, ikiwa
ni pamoja na kumkamata kiongozi wa CHADEMA aliyechochea maandamano hayo yaliyozua vurugu.
Kamanda Shilogile alisema kuwa ili kubaini hayo yote, serikali imeunda
tume ya kuchunguza na kwamba inayoundwa na askari polisi na watu
wengine ambao watasaidia kukamilisha uchunguzi huo.
Aliongeza kuwa tume hiyo ambayo tayari imeshafika mkoani Morogoro
itatafuta maelezo na ushahidi kutoka kwa watu mbalimbali walioshuhudia
tukio hilo, wakiwemo wanahabari na hivyo kuwaomba wote watakaohitajika
kutoa ushirikiano.
Kuhusu majeruhi Hashimu Seif aliyejeruhiwa mguu katika vurugu hizo,
Shilogile alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa alijeruhiwa na bomu
lililomuangukia mguuni na kwamba anaendelea vizuri ikiwa bado yuko
hospitali ya mkoa kwa matibabu zaidi.
Wadaiwa kumtesa mtoto
Katika hatua nyingine jeshi hilo Mkoa wa Manyara, limeingia katika
kashfa nzito likidaiwa kumpiga na kumuumiza vibaya mtoto wa kiume,
Kadogoo Kalanga (16), ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya
Selina kwenye chumba cha uangaliazi maalumu (ICU) akiwa hajitambui.
Mtoto huyo ambaye taarifa za polisi juu ya kilichompata
zinatofautiana, yuko mahututi akiwa amevimba sehemu za siri na nyuma ya
kichwa (kichogoni).
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Akili Mpwapwa alisema kuwa mtoto huyo
alipatwa na hali hiyo baada ya kufikishwa kwenye kituo cha polisi cha
Orkasumeti wilayani Simanjiro kwa tuhuma za wizi wa mbuzi wawili na
kupandisha mori, na hivyo kujipigapiga chini hali iliyomsababishia
kupoteza fahamu.
Hata hivyo, maelezo yake yanapingana na polisi waliompeleka mtoto huyo
kwenye kituo cha afya Orkasumeti, ambao waliwaeleza madaktari kuwa
alipata ajali ya pikipiki.
Daktari aliyempokea mtoto huyo kituoni hapo, aliyejitambilisha kwa
jina moja la Ester, alimweleza mwandishi wa habari juzi kwa njia ya simu
kuwa, mtoto huyo alifikishwa hapo Jumatatu wiki hii na askari ambao
walimweleza kuwa alipata ajali ya pikipiki.
Alisema kuwa walimpa huduma ya kwanza, lakini kutokana na hali
aliyokuwa nayo ya kutojitambua, walishindwa kubaini anaumwa wapi, hivyo
siku iliyofuata akashaurina na madaktari wenzake wakaamua kumpa rufaa
kwenda hospitali yenye vifaa kwa ajili ya vipimo zaidi.
Kamanda Mpwapwa alipoelezwa kuwa taarifa yake inatofautiana na ile ya
askari wake kwenye kituo cha afya, aliendelea kusisitiza kuwa taarifa
anazotoa ni zile alizopewa na Mkuu wa Polisi (OCD) wa Wilaya ya
Simanjiro, na kwamba kama inatofautiana na nyingine hilo halimuhusu.
“Maelezo ninayokupa mimi ni yale niliyopewa na OCD wangu, kama kuna “contradiction” (mkanganyiko) kati ya taarifa niliyopewa na ambayo imetolewa mahali pengine hilo si tatizo langu,” alisema.
Naye mama wa mtoto huyo, Paulina Kalanga, aliwaeleza waandishi wakati
akisubiri mtoto wake apatiwe matibabu kwenye hospitali ya Selian kuwa,
alipata taarifa kwamba Kadogoo yuko kituo cha afya saa tano asubuhi ya
Jumatatu na alipofuatilia alimkuta akiwa hajitambui.
Alisema madaktari walimweleza kuwa mtoto huyo alipelekwa hapo na
askari polisi watatu na alipomkagua akishirikiana na ndugu zake,
walibaini kuwa ameumizwa vibaya sehemu za siri ambazo zimechubuka na
kuvimba, huku kaptula aliyokuwa ameivaa ikiwa imelowa mkojo na kuchanika
eneo la katikati.
Paulina aliongeza kuwa, tangu wakati huo hadi jana asubuhi mtoto huyo
hajaongea zaidi ya kuzungusha kichwa sana wakati fulani, hali
inayomlazimu amsaidie kukishikilia kuepuka asijiumize.
Alisema kuwa mtoto huyo anaonekana kuumia kila anapoguswa maeneo ya
nyuma ya kichwa, kwenye mbavu na kwamba anahisi mfumo wake wa haja ndogo
huenda umepata tatizo kwani tangu Jumatatu hapati choo kidogo licha ya
kuwekewa chupa kadhaa za maji ya kumwongeza nguvu mwilini.
Kadogoo alilazimika kuhamishiwa katika Hospitali ya Agha Khan ya mjini Arusha
kwa kutumia gari la wagonjwa la Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro
lenye namba za usajili SM 5004 ili kufanyiwa kipimo cha kichwa, CIT
SCAN.
Mama mzazi wa mtoto huyo pamoja na ndugu wengine waliokusanyika
hospitalini hapo, walieleza masikitiko yao juu ya kitendo hicho cha
kinyama wakidai mpaka sasa polisi imeshindwa kuwapa namba ya taarifa
iliyofunguliwa kwao (RB) kuhusu kosa linalomkabili Kadodoo.
Chanzo Mtanzania daima
|
No comments:
Post a Comment