KATIKA siku za hivi karibuni, wanawake nchini wamekuwa
wakilalamika kuwa kila wanapokwenda kujifungua basi hukutwa na uvimbe katika
nyumba ya uzazi.
Uvimbe huo, ambao si saratani, umekuwa ni tishio kwa maelfu ya wanawake
nchini jambo linalosababisha wengi wao kuondolewa vizazi vyao.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi wa kitengo cha Patholojia wa Chuo
Kikuu Sayansi ya Tiba Muhimbili, Henry Mwakyoma, anaulezea ugonjwa huu na
kusema kuwa fibroids kwa kitaalamu ‘leimyoma’ ni uvimbe unaowapata
asilimia 25 ya wanawake wa Kiafrika na asilimia 50 ya Wazungu.
“Nasisitiza kuwa, uvimbe huu si saratani, unajitokeza ama katika ukuta wa
kati, wa nje au ndani kabisa ya nyumba ya uzazi,” anasema.
Anasema; “uvimbe huu huwa katika umbile la misuli myembamba na
laini na hukua siku hadi siku,” anabainisha Dk Mwakyoma na
kuongeza kuwa, sababu kuu ya ugonjwa huu, bado haijajulikana.
Anafafanua kuwa, pamoja na kuwa sababu kuu haijajulikana, lakini zipo
sababu ambazo zimehakikiwa kusababisha mwanamke kupata uvimbe wa
fibroids.
“Sababu inayopewa kipaumbele zaidi ni wingi wa vichocheo vya ‘estrogen’ ambavyo
vipo katika miili ya wanawake,” Anasema.
Dk Mwakyoma anafafanua kuwa, vichocheo hivi ndivyo hufanya kazi katika mwili wa
mwanamke na kumsababishia kupata siku zake za hedhi.
“Ndiyo maana wengi wanaopata uvimbe huu, huwa ni wanawake walio katika balehe
au ambao tayari wamevunja ungo, kwani ndiyo ambao huzalisha vichocheo vya
estrogen,” anabainisha mtaalam huyo.
Lakini, pia anasema kuwa endapo inatokea mwanamke akapata matibabu ambayo
yatamtaka kuongezewe vichocheo hivi, huwa katika hatari ya kupata uvimbe huu.
Aidha, daktari huyu anabainisha kuwa, ndiyo maana wanawake walio katika
kikomo cha hedhi(menopause) na watoto hawawezi kupata uvimbe huu.
Anazitaja sifa kuu za ugonjwa huu na kusema, huwa ni nyingi kwa sababu ni
uvimbe ambao asili yake ni mishipa midogo midogo na inapokuwa huweza kufikia
urefu wa sentimeta tano na zaidi na uzito wa kilogram 10.
Anaongeza kuwa, uvimbe huu unaweza kutokea katika kuta zote za kizazi cha
mwanamke na kusababisha mwanamke ang’olewe kizazi chake.
“Hata hivyo, wanawake wengi hupata uvimbe huu katika ukuta wa ndani kabisa wa
kizazi,” anasema.
Anataja sifa nyingine za uvimbe huu ni kuwa na tabia yake ya
kubadilikabadilika sana.
Kwa mfano, fibroids huweza kubadilika rangi na kuwa ya njano, ikabadilika
na kuwa katika hali ya kimiminika, baadaye kuwa ngumu au kuwa laini yenye
kutomasika.
Dalili za Fibroids
Dk Mwakyoma anazitaja sababu za ugonjwa huu na kusema kuwa, ni vigumu mwanamke
kubaini au kuhisi dalili zake.
“Dalili hutegemeana na eneo ulipokaa uvimbe na ukubwa, wengi hugundulika wakati
wa kujifungua, na ujauzito au endapo mwanamke atapata uvimbe katikati ya
kizazi, basi huweza kutokwa damu kwa wingi,” Anasema.
Anasema: “Hata hivyo, asilimia 35 hadi 50 ya wanawake wanaougua maradhi
haya huonyesha dalili wakati wa kujifungua,”
Dalili nyingine ni mwanamke kutokwa damu zake za hedhi kwa wingi na kwa siku
nyingi.
Damu za hedhi huweza kuwa nyingi au kidogo sana zikiambatana na maumivu
makali.
“Asilimia 30 ya wanawake wanaopata maumivu na damu nyingi wakati wa
hedhi huwa na uvimbe wa aina hii” anasema
Anasema wakati mwingine mwanamke huweza kuhisi ana ujauzito kwani uvimbe huu
huwa mkubwa na huchezacheza kana kwamba ni kiumbe.
“Nina mifano hai, wapo wanawake waliowahi kuhisi wana ujauzito, wakakosa
kabisa siku zao za hedhi, wakapata dalili zote za ujauzito na kumbe walikuwa na
uvimbe wa fibroids,” anasema.
Anasema, mara nyingi uvimbe unaojitokeza katika ukuta wa nje wa kizazi na
kuning’nia, ndiyo hucheza na kuleta dalili za ujauzito.
Mwanamke huweza kuvimba miguu kwa sababu uvimbe huu husababisha damu isitembee.
Anataja dalili nyingine kuwa ni mwanamke kupata maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Wakati mwingine, fibroids hukua na kuzuia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula
na kusababisha mwanamke avimbiwe.
Vile vile, uvimbe huo huweza kuzuia kibofu cha mkojo, na kumfanya mwanamke
apate haja ndogo kwa taabu , au akatokwa na uchafu ukeni.
“Hatari kuu ya uvimbe huu ni ugumba, asilimia 27 hadi 40 ya wanawake wanaopata
uvimbe katika kuta zote za kizazi, hushindwa kupata watoto,” anafafanua Dk
Mwakyoma
Hatari nyingine ni kwa wanawake wajawazito wenye uvimbe huu ambao wengi
hufanyiwa upasuaji kwani fibroids huweza kuzuia mlango wa kizazi na mwnamke
kushindwa kujifungua.
Imebainishwa kuwa, asilimia 30 ya wanawake hutolewa vizazi mara baada ya
kujifungua kutokana na uvimbe huu.
Mtaalam huyo anatahadharisha kuwa, wanawake walio katika umri wa kuzaa lakini
hawazai wapo katika hatari ya kupata maradhi haya.
“Hii ni kwa sababu vichocheo vya estrogen hukua kwa wingi na kusababisha misuli
ya fibroids kukua, lakini vichocheo hivyo huacha kukua wakati wa ujauzito,”
anasema.
Anataja walio katika hatari hii ni watawa ambao hawatakiwi kuzaa au wale
wanaopitiliza umri wa kuzaa.
Matibabu ya maradhi haya mara nyingi ni kufanyiwa upasuaji na kuondoa
uvimbe huu au kutolewa kabisa kizazi.
“Hii inategemeana na umri wa mgonjwa, idadi ya watoto na maamuzi yake binafsi,”
anasema
Katika mahojiano na Mwananchi na wanawake wenye umri tofauti waliowahi
kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa fibroids, wengi wanauzungumzia kuwa
ugonjwa unaosumbua.
Mmoja wapo ni Janeth Ngaiza (23) ambaye anasema, alikuwa akitokwa damu wakati
yu mjamzito, ndipo daktari alipomfanyia vipimo na kugundua uvimbe huo.
“Kwa kuwa uvimbe wangu ulikuwa bado mdogo, alinishauri kufanyiwa upasuaji
wakati wa kujifungua, nilifanyiwa upasuaji na uvimbe ulitolewa,” anasema Janeth
ambaye hiyo ilikuwa ndiyo mimba yake ya kwanza.
Mwanamke mwingine, Juliana Kasembe anaeleza kuwa, alipata ujauzito kwa
mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 28, baada ya kujifungua tu, ndipo
alipoanza kupata maumivu makali wakati wa hedhi.
“Damu zilikuwa zikinitoka kwa wingi, maumivu makali mno, nilipofanyiwa
uchunguzi daktari aligundua uvimbe huo uliokuwa na kilo tano,” anasema.
Kwa kuwa uvimbe wa Kasembe ulikuwa mkubwa mno, daktari alishauri atolewe
kabisa kizazi chake, kwa usalama wa maisha yake.
Watalaamu mbalimbali wa afya ya uzazi wanashauri wanawake kwenda kufanyiwa
uchunguzi mara kwa mara ili kubaini maradhi ambayo mengine yanaweza kutibika au
kuzuilika.