Polisi nchini Kenya wamesema
kuwa wafanyikazi sita wa shirika la kutoa misaada kwa wakimbizi
wametekwa nyara katika kambi ya wakimbizi ya Ifo ilioko kaskazini
mashariki mwa nchi hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Lagdera ambako kambi hiyo ipo Robert Kimanthi amesema waliotekwa ni raia wa Canada, Norway, Mfilipino, Mpakistani na Wakenya wawili. Wote ni wanaume.
Kulingana na polisi watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki walishambulia msafara wa magari katika kambi hiyo ambayo inatoa makaazi kwa zaidi ya wakimbizi nusu milioni kutoka Somalia. Mtu mmoja aliuawa kwenye tukio hilo.
Polisi wanashuku kuwa wapiganaji wa kiisalamu wa Al shaabab walihusika na shambulio hilo.
Visa vya mashambulio ya kigaidi vimeongezeka katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya, baada ya wanajeshi wake kuingia nchini Somalia mwaka jana kupambana na wanamgambo wa al shabaab.
Katika miezi ya hivi karibuni, wafanyakazi kadhaa wa mashirika ya kutoa misaada wametekwa nyara katika kambi hiyo ya Daadab.
Wawili kati yao ni wanawake wawili raia wa uhispania ambao walitekwa nyara mwezi Oktoba mwaka uliopita.
No comments:
Post a Comment