NJOMBE

NJOMBE

clock

Saturday, June 30, 2012

Msafara wa JK warushiwa mawe Kinondoni


MSAFARA wa Rais Jakaya Kikwete uliokuwa ukielekea Bagamoyo jana ulilazimika kusimama kwa muda baada ya kuzuka kwa vurugu kubwa za kurushiwa mawe katika eneo la Namanga Tegeta Manispaa ya Kinondoni jiji la Dar es salaam.
Wakazi wa eneo hilo walifunga barabara kwa muda, na hivyo kuzuia msafara wa Rais Kikwete kwa kile walichodai aweze kuona namna matajiri wanavyotumia uwezo wao wa kifedha kuwanyanyasa raia wanyonge.
Vurugu hizo zilisababisha mabaunsa wawili kujeruhiwa vibaya na wananchi na wamelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu zaidi.
Vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa mbili, zilitokana na kitendo cha watu (mabaunsa) wanaoaminika kukodiwa na mmiliki wa kituo cha mafuta cha GAPCO aliyetajwa kwa jina Hemed Salum, kuvunja nyumba zao na mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo, msafara huo wa Rais uliweza kuendelea baada ya askari wengi kumwagwa na kuanza kuwatawanya wananchi waliokuwa na hasira.
Wakiongea kwa hasira, wananchi hao walidai kuchoka na vitendo wanavyotendewa na baadhi ya wawekezaji.
“Watu wenye pesa wanafanya kila wanaloliona kuwa linawafaa bila hata kujali sheria za nchi, sasa sisi wananchi tulifanya makusudi ili Rais aone mambo tunayofanyiwa na hawa wawekezaji atusaidie, lakini kinyume chake tunapewa bakora,” alisema mwananchi mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Watu waliobomolewa nyumba zao wamesema kuwa wamesikitishwa na kitendo cha mmiliki wa kituo hicho kuwavunjia nyumba zao akidai kuwa wamejenga kwenye eneo lake.
“Hili eneo ni letu tunalimiki kihalali, kwani tuliachiwa urithi na baba yetu na sisi tuko watoto kumi, kila mmoja alipewa eneo lake tukajenga, na eneo la barabarani halikuwa letu hivyo aliuziwa yeye (Salum) na mtu mwingine akajenga kituo cha mafuta.
“Kinyume chake ametafuta nyaraka za kugushi na kuanza kudai kuwa sisi tunaishi katika eneo lake tuondoke tumwachie, lakini hakuna mtu yeyote asiyejua kwamba eneo hili ni letu na tumeachiwa urithi na baba yetu,” alisema Fikiri Saidi mmoja wa waliobomolewa nyumba huku akitokwa na machozi.
Fikiri aliongeza kwamba kabla ya tukio hilo siku mbili zilizopita, mmiliki huyo aliwafuata nyumbani kwao kwa lengo la kutaka wamuuzie eneo hilo kwa shilingi milioni 100 ili wagawane lakini walikataa, ndipo akatoa vitisho akiwambia kuwa, kwa kuwa wamekataa pesa hizo atawapa wanaozihitaji ili wabomoe na hawataambulia kitu chochote.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela alisema polisi wanamshikilia mmiliki huyo kwa kosa la kujichukulia hatua mkononi na kuwavunjia wakazi hao nyumba na kusababisha upotevu wa mali.
Hata hivyo, Kenyela alisema polisi watafanya msako wa watu waliohusika kupopoa mawe msafara huo, huku akiwataka wakazi hao kuwa watulivu wakati serikali ikiangalia namna ya kuwatafutia hifadhi ya muda.
Watu walioathirika na tukio hilo ni Fikiri Saidi, Rashid Said, Farida Said na Ally Mkwandu, wengine ni Shabani Said, Kassim Said, Sijali Said Rajab Said na Waziri Rashid, ambapo inakadiriwa kuwa thamani ya nyumba na mali zilizoharibiwa inafikia zaidi ya sh milioni 300.
Chanzo cha Habari Tanzania daima

No comments:

Post a Comment