• Vigogo serikalini wamzidi nguvu, abaki njia panda
DHAMIRA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven
Ulimboka ya kutaka kuwafichua polisi na watu wengine wanaodaiwa
kuhusika katika tukio la kumteka, kumpiga, kumtesa na kumtupa katika
Msitu wa Mabwepande, imezimwa na vigogo wa serikali, Tanzania Daima
Jumatano limebaini.
Uchunguzi ambao gazeti hili limekuwa likiufanya tangu Dk. Ulimboka
awasili nchini, umebaini kuwa kinara huyo wa mgomo wa madaktari
uliotikisa nchini, amekuwa na vikao na vigogo wa idara za ulinzi na
usalama na kumshawishi awe mtulivu katika kipindi hiki ambapo serikali
inafanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika kumteka nyara.
Watu wa karibu na daktari huyo, walilieleza gazeti hili kuwa, katika
kipindi kifupi amekutana na vigogo kadhaa wa serikali wakimtaka asiseme
chochote kwa hofu ya kuvuruga uchunguzi.
Wakati vigogo wa serikali wakifanikiwa kumzima Dk. Ulimboka, upande wa
pili wa wanaharakati, ndugu na madaktari wenzake, wamekuwa wakimbana
kumtaka awe jasiri kueleza umma ukweli, na hata kuwataja kwa majina
waliohusika kumteka.
Hata hivyo, Joshua Mulundi aliyetajwa kuwa raia wa Kenya amefikishwa mahakama akituhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Habari kutoka ndani ya uongozi wa Chama cha Madaktari (MAT), zilidai
kuwa, hali ya ushawishi kutoka kwa vigogo wa serikali na mbinyo
anaoupata kutoka kwa wanaharakati na madaktari wenzake, umemweka njia
panda Dk. Ulimboka kiasi cha kushindwa kuamua kama atoke hadharani
kueleza ukweli au atulie ili kulinda maisha yake.
Mara baada ya kurejea nchini akiwa na afya njema, Dk. Ulimboka amekuwa
akikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari, kwamba anajiandaa kueleza
ukweli wa tukio nzima na hata kuwataja waliohusika na unyama
aliofanyiwa.
“Kwa jinsi hali ilivyo, Dk. Ulimboka atabaki na siri moyoni maana
amekutana na watu wazito, wamezungumza nae na kumshawishi anyamaze,
ndiyo maana hadi sasa hayuko tayari kuueleza umma kile alichopania
kusema. Lakini pia wanaharakati na hata wanasiasa kila siku wanajaribu
kumshawishi atoke hadharani kusema ukweli kabla tukio hilo halijaanza
kusahaulika masikioni mwa watu,” alisema daktari mmoja ambaye ni mtu wa
karibu na Dk. Ulimboka.
Katika kuthibitisha kwamba Dk. Ulimboka hayuko tayari kusema chochote,
juzi gazeti hili lilikutana nae katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Usharika wa Ubungo ambapo alisema kuwa kitendo cha
kinyama alichofanyiwa, anamwachia Mungu.
Dk. Ulimboka ambaye aliongozana na familia yake kanisani hapo kwa nia
ya kutoa sadaka na kumshukuru Mungu, alipobanwa hakuwa tayari kusema
chochote zaidi ya kusema muda ukifika ataweka ukweli hadharani na
kukanusha tuhuma za kunyamazishwa na vigogo.
Duru za kiintelijensia zililieleza gazeti hili kuwa, katika hali ya
kawaida Dk. Ulimboka hawezi kusema chochote kama ilivyotokea kwa Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe aliporejea kutoka kwenye matibabu.
Dk. Mwakyembe ambaye aliugua ugonjwa ambao hata mwenyewe aliamini
ulitokana na sumu, uliosababisha aoze kucha, kutoka unga mwilini na
miguu kupasuka, alipata kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba
atakuja kueleza ukweli jinsi alivyopewa sumu iliyomsababishia ugonjwa
huo.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe tangu aliporejea hadi kuteuliwa kuwa Waziri
wa Uchukuzi, hajawahi kueleza chochote kama alivyoahidi na kumweka
mahali pabaya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel
Sitta ambaye ndiye aliyeshikia bango kwamba Dk. Mwakyembe alipewa sumu.
Dk. Ulimboka ambaye alipelekwa Afrika Kusini akiwa hawezi kutembea
wala kula mwenyewe baada ya Juni 27 mwaka huu kutekwa na watu
wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha
kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam,
amekuwa akiwakwepa wanahabari na anaishi kwa kujificha.
Kiongozi huyo wa madaktari amerejea nchini huku serikali na madaktari wakiwa hawajafikia mwafaka kuhusu madai yao.
Madai ya madaktari hao ni hali bora ya mazingira ya utoaji afya
nchini, ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira
magumu, posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za
kuitwa kazini.
Safari ya Dk. Ulimboka kwenda kwenye matibabu nchini Afrika Kusini
ilitawaliwa na usiri mkubwa alipoondoka nchini Juni 31 mwaka huu,
akisindikizwa na Dk. Pascal Lugajo, kaka yake, Dk. Hobakile Ulimboka na
mke wake, Dk. Judith Mzovela.
Kutekwa
Dk. Ulimboka alitekwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili wakati
akiratibu mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea na aliokotwa na
msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya.
Kutokana na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu waliituhumu
serikali kuhusika na tukio hilo, huku yenyewe ikikana na kuliagiza Jeshi
la Polisi kuwasaka waliohusika.
Wakati Dk. Ulimboka alipokuwa akiendelea na matibabu Afrika Kusini,
Rais Jakaya Kikwete alisema serikali haihusiki na kilichomtokea daktari
huyo kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano baina ya serikali
na madaktari.
Rais Kikwete alisema hayo katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
“Dk. Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya
serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa serikali,
hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya
kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini
kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na
serikali,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alichofanyiwa Dk. Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa
kuwa ni kitendo cha kinyama na kinyume kabisa na mila na desturi za
Tanzania.
Kauli ya Rais Kikwete kuhusu mgomo wa madaktari inafanana na ile
iliyokuwa imetolewa awali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema
wanatambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa
shaka kuhusu kilichomtokea Dk. Ulimboka, lakini ameshangazwa na hisia
hizo akisema haoni sababu ya serikali kufanya hivyo.
Chanzo Mtanzania daima