NJOMBE

NJOMBE

Thursday, January 26, 2012

Mgomo wa madaktari wasambaa mikoani

Mwenyekiti wa Madaktari ,Dk.Ulimboka Steven (katikati) akizungumza wakati wa mkutano wa madaktari kutoka katika Hospitali zote za Rufaa kuhusu kuendeleza mgomo wao kama serikali haitawatimizia madai yao,mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Don Bosco Upanga jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Dk Edwin Chitage na Kulia ni DK Rahma Hingera.
SASA WAINGIA DODOMA, MBEYA, PINDA AWAANGUKIA ATAKA WAZUNGUMZE

MGOMO wa madaktari ulioanza juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umesambaa na kuingia katika Hospitali za Mwanyamala na nyingine katika Mikoa ya Dodoma na Mbeya.Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoa tamko akiwataka wawakilishi wa madaktari hao wafike ofisini kwake wakati wowote ili wazungumze naye na kupata suluhu ya tatizo hilo.Katika hospitali ya Muhimbili, mgomo huo jana uliingia katika siku ya pili huku madaktari wastaafu wanaofanya kazi kwa mkataba, wakipanga kuwasilisha pendekezo kwa uongozi wa hospitali hiyo kutaka kuwapunguzia kazi kwa kuondoa shughuli za upasuaji.
“Tunadhamiria kupeleka pendekezo kwenye uongozi wa hospitali hii ili kuwaeleza dhamira yetu ya kupunguza baadhi ya huduma zinazotolewa ikiwamo upasuaji. Hilo ni kutokana na madaktari wanaotakiwa kufanya kazi hiyo kuwa kwenye mgomo,” alisema mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe.“Sisi katika idara hii tupo wawili tu, wagonjwa wanaokuja ni zaidi ya 150 tutawahudumiaje na wakati huohuo tunaitwa wodini? Alihoji daktari huyo.
Katika chumba cha wagonjwa wa dharura ambako juzi huduma ziliendelea, hali ilikuwa tofauti jana, kulikuwa na madaktari wawili tu ambao wameeleza kuwa wenzao wameingia kwenye mgomo.
Ocean Road
Katika Hospitali ya Ocean Road, wahudumu waligoma kuwapokea wagonjwa wapya, hivyo huduma kutolewa katika kitengo cha mionzi na madaktari bingwa.“Hili ni jambo la kusikitisha na ni aibu kwa Serikali kwani mgomo huo utasababisha vifo vya mamia ya watu,” alisema mmoja wa wagonjwa katika hospitali hiyo, Florence Mushi.
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alithibitisha wauguzi kutopokea wagonjwa wapya jana na kueleza kuwa ni kwa kuwa madaktari hawapo kazini.“Hatuwezi kuwapokea wagonjwa wakati watu wa kuwatibu hawapo. Hapa huduma zipo kwenye kitengo cha madaktari bingwa, mionzi na wagonjwa walioko wodini tu,” alisema.
Mwananyamala
Huduma katika Hospitali ya Mwananyamala pia zilikuwa za kusuasua jana baada ya madaktari wanafunzi wanaotoa huduma hospitalini hapo kuendesha mgomo baridi.Jana mchana madaktari walionekana wakiingia na kutoka wodini bila kutoa huduma huku ndugu wa baadhi ya wagonjwa wakieleza kusikitishwa na hatua hiyo. Baadhi wa wafanyakazi wa hospitali hiyo walisema kuwa mgomo hospitalini hapo upo ingawa haujashamiri.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Kaliameli Wandwi hakutaka kuzungumza lolote kuhusu mgomo huo, alipobanwa alisema: “Sina muda wa kuongea na waandishi wenzako nimewakatalia tangu asubuhi.”
Mbeya
Mkoani Mbeya madaktari 75 wamegoma katika Hospitali ya Rufaa huku wagonjwa katika kitengo cha Wazazi Meta, wakilalamika kukosa huduma bila kupata maelezo yoyote kutoka kwa wauguzi.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wagonjwa walisema kuwa mgomo huo ni hatari kwa wananchi ambao hali zao ni duni kumudu matibabu katika hospitali za kulipia.
“Tungekuwa na uwezo kifedha tungekwenda katika hospitali za kulipia lakini sasa ni vigumu kwetu ambao hali zetu ni duni,” alisema Neema Emmanuel.Mgonjwa mwingine Winfrida Rashid alisema: “Hapa rufaa inaonekana kuna huduma zinaendelea kwa baadhi ya madaktari na manesi, lakini kasi imepungua, inawezekana wengine wakafanya kama kuigiza.”
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Eleuter Samky alisema madaktari waliogoma ni 75, kati yao 10 wakiwa waajiriwa na 65 wanafunzi.
Alisema hali ni mbaya kwa wagonjwa kutokana na kuwepo kwa mgomo huo na kwamba wanaofanya kazi ni wafamasia na madaktari bingwa na kitengo cha upasuaji na baadhi ya wauguzi katika kitengo cha mifupa.
Madaktari hao waliogoma, kila walipokutana na waandishi wa habari waliwaonyesha karatasi zilizokuwa zimeandikwa baadhi ya madai yao kwa Serikali.
Dodoma
Mkoani Dodoma nako mambo si shwari baada ya madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mkoa kugoma na kutumia siku nzima ya jana katika mkutano.Kitengo kilichoathirika zaidi na mgomo huo ni cha wagonjwa wa nje ambako kimsingi hakuna huduma yoyote iliyokuwa inatolewa huku baadhi ya madaktari wakisema kuwa wataendelea na mgomo wao huo hadi Serikali itakapotoa majibu ya madai yao.
“Ndugu yangu amelazwa tangu jana (juzi) asubuhi kwa ajili ya operesheni kubwa na hatakiwi kula chochote tangu hiyo jana (juzi) tukitegemea kuwa angefanyiwa operesheni leo,” alisema ndugu wa mgonjwa mmoja ambaye hakutaka kutajwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia madai ya watumishi wa Afya katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Yahya Magaswa alisema wanaungana katika mgomo na madaktari wenzao nchini kote ili kuishinikiza Serikali kufanyia kazi madai yao ya msingi.
“Tumemweleza Katibu wa Mkoa madai yetu ya msingi na sababu za kuungana na wenzetu katika mgomo ulioanza kote nchini... ameahidi kuyafanyia kazi na sisi tumekubaliana kutoa huduma za dharura tu mpaka kesho jioni tutakapokutana tena kujadili majibu yatakayotolewa na Serikali,” alisema Magaswa.

Pinda ataka mazungumzo
Akizungumzia Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema haoni sababu ya kukwama kwa mazungumzo kati ya serikali na madaktari.Waziri mkuu Pinda alisema Dar es Salaam jana kuwa yuko tayari kukutana na wawakilishi wa wanataaluma hao na kutuma salamu popote walipo wakisikia ujumbe wake, wafike wamwone kabla hajaenda bungeni Dodoma, Jumamosi.
“Kupitia kwenu vyombo vya habari, naomba mfikishe ujumbe huu kwamba niko tayari kufanya mazungumzo na madaktari hao. Sijali kama ni uongozi gani jambo la msingi uwe unawakilisha madaktari,” alisema.
Alisema anaumia roho kuona wagonjwa wanapata shida hospitalini hasa Muhimbili kutokana na mgomo huo ambao unazungumzika na kutatulika.
Alisema akikutana na madaktari hao, atawabembeleza wasitishe mgomo na kuendelea kutibu wagonjwa huku, wao na Serikali wakiendelea na mazungumzo ya kudai maslahi yao.
Alisema kimsingi, madaktari hao ambao wako kwenye mafunzo ya vitendo walikuwa na madai ya msingi baada ya kukosa posho zao za Novemba na Desemba, lakini jambo hilo halifungi mlango wa mazungumzo.
Pinda alisema kinachofanyika kwa madaktari hao ni kulipwa posho ambazo si mshahara hivyo, fedha zake zinatoka katika matumizi ya kawida (OC), ambayo wakati mwingine huchelewa.
Kwingine shwari
Katika baadhi ya mikoa ikiwamo Pwani na Mwanza madaktari walikuwa wakiendelea na kazi kama kawaida.
Wagonjwa waliohojiwa jana katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha walisema huduma ziliendelea kama kawaida hali ambayo iliripotiwa pia katika hospitali nyingine mkoani Pwani kama Kituo cha Afya Chalinze na Hospitali za Wilaya Mkuranga, Rufiji na Bagamoyo.
“Mimi si msemaji wa mkoa lakini kwa vile ni kiongozi wa ulinzi na usalama nakuthibitishia hakuna mgomo ingawaje kuna watu pengine walipenda uwepo lakini leo hakuna,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Henry Clemence.
Katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, madaktari waliendelea na kazi. Mmoja wa madaktari waliokuwa kazini, Dk Denis Kashaija alisema wanaendelea kuchapa kazi za kutoa huduma kwa wagonjwa.“Kama unavyoshuhudia, sisi na wauguzi hatujagoma kutoa huduma kwa wagonjwa tunaendelea na kazi labda itokee kuanzia kesho,” alisema Dk Kashaija.
Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Kenneth Goliama na Ellen Manyangu, Dar; Julieth Ngarabali, Pwani; Anthony Gervans, Mwanza; Hamisi Mwesi, Dodoma; Brandy Nelson na Godfrey Kahango, Mbeya.




Pinda: Sifikirii kuwania urais

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ikulu, Dar es Salaam . Picha na Emmanuel Herman

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amezungumzia mambo muhimu kumi na moja yanayogusa nchi kwa sasa yakiwemo ya kiuchumi na kisiasa huku akiwashangaa wanaotumia nguvu nyingi kuwania nafasi ya urais akisema hawajui mzigo mkubwa wa kuongoza taasisi hiyo.

Katika mkutano wake na wahariri na wawakilishi wao uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam jana, Pinda alisema: “Kwa dhati sifikirii kugombea nafasi hiyo ya juu kwani ni mzigo mkubwa.”

Alisema kuna watu wanautaka urais kwa nguvu na kuhoji kama wanajua mzigo mkubwa uliopo katika taasisi hiyo au wanafurahia mazingira yake ili wakanufaike kiuchumi na kibiashara.

“Kuna watu wanautaka kweli urais... wanautaka kwelikweli, lakini kuutaka na kuupata ni vitu tofauti. Sijui kama wanautaka ili wawatumikie Watanzania au kwa sababu tu ya mazingira mazuri yaliyopo pale ili waweze kufanya biashara au wanufaike kiuchumi.”

Alisema mtu anayejua mzigo mkubwa uliopo Ikulu kamwe hawezi kuutaka kama baadhi wanavyofanya: “Wakati mwingine huwa nikienda Ikulu namwambia ndugu yangu Rais pole. Ikulu ni mzigo mkubwa.”

“Sasa hawa wanaoutaka kwa nguvu, ni kweli wanataka kwenda kubeba mzigo huo mzito ? Mimi siko tayari. Sasa wanaoutaka urais kwa nguvu labda wawe wanakwenda pale kufurahia mazingira ya Ikulu kama kufanya biashara lakini si kutumikia Watanzania.”
Alisema Watanzania wanahitaji Rais ambaye atawatumikia kwa dhati na anayejua matatizo yao na huyo ndiye ambaye wenyewe watamchagua mwaka 2015 wakati wa uchaguzi.

Alisema anajivunia muda mwingi alioutumikia umma tangu Ikulu na hadi nafasi ya Waziri Mkuu na kuongeza: "Sasa hivi ni Waziri Mkuu. Hapa ni shule tosha najivunia kutumikia umma hadi hapa nilipo. Panatosha nasema hili kwa dhati.”

Wakuu wa Wilaya
Waziri Mkuu alikiri kuwepo wilaya ambazo zinakaimiwa na wakuu wa wilaya na kuongeza kwamba mchakato wa kukamilisha uteuzi wao umeshakamilika na kinachosubiriwa ni kutangazwa na Rais.

Alisema kuchelewa kukamilika kwa mchakato huo kulitokana na matatizo ya kisheria katika baadhi ya maeneo, kwani kulikuwa na mchakato wa kupokea maoni ya wapi kuwe makao makuu lakini, hilo na mengine yamekamilika na anayesubiriwa sasa ni mkuu huyo wa nchi.

Katiba
Akizungumzia mchakato wa Katiba, Pinda alisema Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha nchi inapata Katiba bora ambayo itagusa maslahi ya makundi tofauti ya kijamii.

Alisema hivi sasa imeundwa timu ndogo ya wataalamu ambayo itaangalia namna ya kufanya maandalizi ya kufanikisha utendaji kazi wa tume ya kuratibu mchakato huo punde itakapoundwa.

Alifafanua kwamba timu hiyo haina uhusiano wala haitafanya chochote kuhusu mapendekezo ya uteuzi wala kuingilia mchakato wa kisheria wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011, bali itaangalia namna ofisi ya tume itakavyopatikana, maslahi kama mishahara, vitendea kazi, magari na miundombinu ya mawasiliano katika utendaji.

Pinda alisema timu hiyo ambayo imeundwa na Katibu Mkuu Kiongozi, itafanya kazi hiyo kwa umakini ili kuhakikisha tume itakapoundwa na kuanza kazi, maandalizi yote ya msingi yanakuwa yamekamilika.

Kuhusu mapendekezo ambayo Rais amekuwa akiyapokea katika kipindi hiki ambacho tayari sheria imekwishapitishwa na Bunge, alisema anasubiri maelekezo kutoka kwa mkuu huyo wa nchi kuona kama kuna mapendekezo ambayo yanaweza kupelekwa bungeni na sheria hiyo kufanyiwa marekebisho madogo ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya wadau wote.

Alisema dhamira ya Serikali na Rais ni kuhakikisha kwamba Katiba inayopatikana inakuwa yenye matakwa ya pande zote husika, huku akitoa mfano kwamba kama Chadema inataka Serikali tatu za katika muundo wa muungano hilo litajulikana katika kura za maoni na kama CCM wanataka Serikali mbili pia litajulikana katika kura za maoni.

Posho za wabunge
Akizungumzia posho za wabunge, Pinda alisema tatizo kubwa lilijitokeza tangu mwanzo ni ukosefu wa taarifa sahihi kwa umma hali iliyoibua mjadala na mgongano wa lugha kati ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wake, Dk Thomas Kashillilah.

Alisema wakati mjadala ulivyoibuka, ni kweli Spika alimwandikia barua Rais kuomba nyongeza hiyo ya posho lakini mkuu huyo wa nchi alikuwa bado hajaidhinisha posho hizo.
“Kwa hiyo, kwa lugha rahisi ingekuwa ni kusema hivi... ni kweli tumeomba nyongeza ya posho kwa mheshimiwa Rais lakini hadi sasa hajaidhinisha, atakapoidhinisha au vinginevyo tutasema. Lakini, ikatokea huyu anasema hivi na yule hivi.”

Hata hivyo, alisema tayari Rais Kikwete amekwisharejesha suala hilo kwake (Pinda) ili kuendelea na taratibu nyingine zaidi ambazo atatoa maelekezo bungeni kuona namna ya kulimaliza suala hilo bila mvutano.

Pinda alisema ingawa kumekuwa na malalamiko, lakini wabunge wana matatizo ya msingi ambayo yanatokana na makato makubwa ya mikopo, kusaidia wapiga kura majimboni na mengine mengi.

Alisema serikalini kiwango cha posho ya vikao kwa siku kwa watumishi wa ngazi za juu ni Sh200,000 kwa ngazi ya kati Sh150,000 na nyingine Sh100,000 na kuongeza: “Hivyo, siyo vibaya sana na hata wabunge wakiongezewa. Ni jambo linaloweza kueleweka kama watu watalizungumza jambo hili kwa utulivu.”

Pinda alisema tofauti na viongozi wa Serikali kama yeye, wabunge wanajigharamia wenyewe nyumba, magari, mafuta, matengenezo na huduma nyingine za kuwasaidia wananchi, hivyo akataka jambo hilo lizungumzwe bila jazba.

Uchumi
Akizungumzia mwenendo wa uchumi, alikiri kwamba mfumuko wa bei ni tatizo kubwa linalotikisa nchini lakini, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inafanya kila jitihada kuhakikisha unashuka.

Alisema mfumuko huo umechangiwa na matatizo ya uchumi wa dunia ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta ambayo kwa sasa pipa moja ni Dola 100 za Marekani katika soko la dunia na matatizo ya mgawo wa umeme.

Alisema kipindi cha Julai mwaka jana, mfumuko ulikuwa asilimia 13, Septemba asilimia 16.8, na kushuka kidogo hadi 12.7 ikilinganishwa na asilimia 5.5 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2010.

Hata hivyo, alisema mwelekeo wa ukuaji wa uchumi si mbaya kwani lengo kwa mwaka 2011 ilikuwa ni ukuaji wa asilimia sita, lakini robo ya kwanza ya mwaka huo uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.8, ya pili asilimia 6.7 na robo ya tatu iliyoishia Septemba ilikuwa kwa asilimia 6.3, hivyo kuonyesha uchumi mpana wa taifa bado uko imara.

Alisema katika kipindi hicho, sekta ya ujenzi ilichangia kwa asilimia 13.2 mawasiliano asilimia 12.9, sekta ya fedha asilimia 11.3 na sekta ya biashara ilichangia kwa asilimia saba.

Kuhusu chakula, alisema ingawa baadhi ya mikoa kama Arusha na Kilimanjaro mazao kama mahindi yameathiriwa na ukame, bado uwezo wa  nchi kujitosheleza kwa chakula kuelekea kipindi cha  Januari hadi Februari bado upo kwani maeneo ya kanda ya ziwa yanatarajiwa kuzalisha mazao ya kutosha.

Akizungumzia mpango wa dharura wa umeme uliopitishwa na Bunge alisema unaendelea vizuri ingawa hadi sasa zimepatikana megawati 270 kati ya 300 zilizokuwa zimekusudiwa, ambazo ni sawa na asilimia 90.
Katika Bunge la Bajeti la mwaka jana, Serikali iliomba Sh1.2 trilioni za mpango huo wa dharura wa kukabiliana na mgawo wa umeme, ambazo zingeanza kuzalisha umeme kuanzia Agosti hadi Desemba, kwa awamu ya kwanza.

Jairo
Kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge katika sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo alisema kwa sasa hatua za Serikali ziko Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili atoe mapendekezo yake ya kitaalamu.
Habari na Ramadhan Semtawa

Tanesco, Dowans waendelea kuvutana mahakamani

James Magai
MVUTANO mkali baina ya Shirika  la Umeme  Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Dowans, kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu  ya Tanzania iliyoamuru Tanesco iilipe Dowans zaidi ya Sh 94 bilioni, bado unaendelea.

Mvutano huo unafautia hatua ya Tanesco kutafuta njia za kisheria baada ya kuomba kibali cha kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga hukumu na  kuepukana na malipo hayo, lakini Dowans nayo ikaendelea kuibana kwa kuiwekea pingamizi ili inyimwe kibali hicho.

Septemba 28  mwaka jana, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, aliamua tuzo ya Dowans iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), isajiliwe ili kuwa hukumu halali ya mahakama hiyo.

Kwa uamuzi huo, Tanesco sasa inatakiwa iilipe Dowans Sh 111 bilioni badala ya Sh 94 bilioni za awali.

Tanesco inapaswa kulipa fidia hiyo pamoja na riba ya asilimia 7.5.

Hata hivyo shirika hilo la umeme limeeleea kutokuridhishwa na hukumu hiyo na hivyo kutoa taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Maombi ya kutaka kibali cha kukata rufaa hiyo, yalitarajiwa kuanza kusikilizwa jana na Jaji Dk. Fauz Twaib lakini mahakama ilishindwa kuyasikiliza baada ya Dowans kuweka pingamizi, ikiomba mahakama isiipe Tanesco kibali.

 Dowans iliiwekea Tanesco pingamizi hilo mwezi huu ikidai kuwa kwa mujibu wa mkataba baina ya pande hizo, hukumu ya ICC haiwezi kukatiwa rufaa.

Ni hoja kama hizo ilizozitoa Dowansa wakati wa pingamizi la Tanesco kutaka Mahakama Kuu isiisajili tuzo yake na baadaye Jaji Mushi alikubaliana na hoja za Dowans na kuamuru tuzo hiyo isajiliwe.

Jana Jaji Dk Twaib aliziambia pande hizo mbili kuwa mahakama haitaweza kusikiliza maombi ya Tanesco kuhusu kibali cha kukata rufaa hadi hapo pingamizi la Dowans litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Jaji huyo, alizitaka pande hizo, kuwasilisha hoja zao kwa njia ya maandishi na kwamba pingamizi hilo litaamuliwa Februari 16 mwaka huu, baada ya kupitia hoja zote.

Ikiwa mahakama itatupilia mbali pingamizi la Dowans, basi Tanesco itapewa kibali cha kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Lakini kama mahakama itakubaliana na pingamizi la Dowans basi harakati za Tanesco kujinusuru katika malipo hayo kwa njia za kisheria zitakuwa mashakani.

Hukumu ya Jaji Mushi ilionekana dhahiri kwenda sambamba na kile alichowahi kukisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema kuwa hakuna uwezekano wowote wa kisheria kuepuka malipo hayo.

Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama  alisema hadi wakati hukumu hiyo inatoka, Tanesco ilipaswa kuilipa Dowans kiasi cha Sh 111bilioni badala ya Sh94 bilioni.

 “Fidia ya awali katika uamuzi wa ICC ilikuwa ni Dola za Marekani 65milioni, lakini kwa sasa ukiweka na riba ya asilimia 7.5 fidia hiyo imeongezeka hadi takribani Dola za Marekani 72milioni ambazo ni kama Sh111bilioni,” alisema Fungamtama.

Katika hukumu yake Jaji Mushi alisema baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote nimebaini kwamba si sawa kwa mahakama hiyo kuingilia uamuzi wa ICC.

“Hivyo ninaagiza kuwa tuzo hiyo isajiliwe na iwe huku halali ya mahakama hii,” alisema Jaji Emiliani Mushi ambaye kabla ya kusoma hukumu hiyo alisema kuwa anatambua kuwa suala hilo limekuwa na msukumo mkubwa wa kisiasa lakini akabainisha kuwa anafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Tuesday, January 24, 2012

Ofisa Bodi ya Mikopo adaiwa kuiba mil. 90/-Aghushi majina hewa ya wanafunzi

MFANYAKAZI wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), Ester Budili, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na tuhuma tisa za kughushi majina hewa ya wanafunzi na kisha kujipatia sh zaidi ya sh milioni 90.7 kwa udanganyifu.
Akisomewa mashtaka yake jana mbele ya Hakimu Mkazi Binfi Mashabala, Wakili wa Serikali, Frida Mwale, alidai kuwa kati ya Agosti 5 mwaka 2010 na Aprili 24 mwaka jana katika ofisi ya Bodi ya Mikopo, iliyoko Msasani, alighushi majina ya wanafunzi na kuyaingiza kwenye orodha ya majina ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bugando kuwa ni miongoni mwa wanafunzi wanaoomba mikopo.
Mwale aliyataja majina ya wanafunzi hao hewa kuwa ni John Suzane, Peter Bahati Mombo Yusuf, Bitaliho Gordian, Kwangaya Ibrahim, Majaliwa Nandu, Mtitu Catherine, Happy Alfred, Simon Isack na Julian Nyangige.
Alidai kuwa katika shtaka la pili anadaiwa kuwa katika kipindi hichohicho alighushi majina mengine ya wanafunzi hewa ambayo ni Catherine Nkya, John Nkya, Andrew John, Goliama Ally, Simon Pamela, Gash Damian na Suzane John na kuyaingiza kwenye orodha ya majina ya wanafunzi wa Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) na kuonyesha kuwa ni miongoni mwa wanafunzi wanaomba mikopo kwa ajili ya elimu ya juu, huku akifahamu jambo hilo si la kweli.
Wakili Mwale aliendelea kudai kuwa katika shtaka la tatu, mtuhumiwa anadaiwa kughushi majina hewa ya wanafunzi Suzane John, Mella Christopher, Zake Ezra, Goliama Ally, Simon Michael, Peter Massawe, Naruo Peter, Pamela Simon na Catherine Nkya na kuwaingiza kwenye orodha ya wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo na Ustawi wa Jamii wanaoomba mikopo.
Aidha, alidai katika kipindi hicho alighushi majina ya wanafunzi Pamela Simon, Munisi Grace na Hamza Goliama kwamba ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaostahili kupewa mikopo ya elimu ya juu.
Alidai kuwa pia alighushi majina hewa ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Uuguzi cha Kilimanjaro kinachomilikiwa na taasisi ya kidini ya Kikristo, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Tumaini,Chuo cha Makumila na Ruaha na kwamba wanafunzi hao walikuwa wanastahili kupewa mikopo na bodi hiyo.
Katika shtaka la kumi, wakili wa serikali alidai kuwa katika kipindi hicho mtuhumiwa aliiba sh milioni 90.7, mali ya bodi hiyo.
Hata hivyo, mtuhumiwa alikana tuhuma hizo na yuko nje kwa dhamana ya bondi ya sh milioni 45. Kesi imeahirishwa hadi Februari 7 itakapotajwa tena.
Habari na Happiness Katabazi

Mdaktari waanza mgomo nchi nzima

JUMUIYA ya madaktari nchini, imetangaza mgomo utakaoanza leo nchi nzima hadi hapo serikali itakaporidhia kulipa madai yao ndipo madaktari watakaporudi kuendelea na kazi.
Akitangaza mgomo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Madaktari, Dk. Ulimboka Stephen, alisema mgomo huo utakuwa wa nchi nzima kwa madaktari kutotoa huduma.
Alisema kuwa madaktari wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu hali ambayo wanashindwa kutoa huduma bora kutokana na kuwa na malipo finyu ya utendaji wao wa kazi.
“Sisi tumeazimia kugoma na hatutaki daktari yeyote aende kutoa huduma kwa wagonjwa mpaka hapo serikali itakaporidhia madai yetu ambayo kila siku yamekuwa yakipuuzwa,” alisema Dk. Stephen.
Aliongeza kuwa katika madai hayo wanaitaka serikali iboreshe mazingira ya kazi kwa wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na wagonjwa katika hospitali zote nchini.
Dk. Stephen alisema kuwa madai ya madaktari yamekuwa yakiipuzwa na baadhi ya watendaji serikalini kwa kupotosha wananchi kwa masilahi ya kuwaumiza wagonjwa walioko hospitalini.
Alisema katika madai mengine, wanataka nyongeza ya mshahara kutokana na kuwa hii wanayolipwa sasa haikidhi mahitaji ya kuendesha maisha yao, hatua inayowafanya kuhangaika kuhudumia katika hospitali zingine ili kuweza kukabiliana na mahitaji.
Wanadai nyongeza ya kulala kazini kutoka sh 10,000 hadi kufikia asilimia 10 ya mshahara wao sanjari na bima ya afya kwa kupewa kadi ya kijani ambayo inatambulisha juu ya kuweza kuhudumiwa.
Alisema kuwa katika mazingira ya kazi yao wanahitaji kukopeshwa magari ili kuweza kuwafikia wagonjwa kwa muda mwafaka.
“Serikali irudishe madaktari walio katika mafunzo bila ya kuwepo masharti yoyote kwa ajili ya kuwaandaa kwenda kutoa huduma bora kwa Watanzania,” alisema Dk. Stephen na kuongeza kuwa kutokana na kufanya kazi katika mazingira hatarishi, wanahitaji serikali iwape asilimia 30 ya mshahara baada ya kupata madhara wakati wa utoaji huduma.
Juzi, uongozi wa Chama cha Madaktari (MAT), ulishindwa kwenda na madaktari wanafunzi ‘intens’ kwenye mkutano wao na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja, alisema mkutano huo uliitishwa baada ya MAT kukwama kuonana na Waziri Mkuu na kutakiwa kurudi katika meza ya majadiliano na wizara hiyo.
Mwamwaja alisema kikao hicho kilichofanyika mchana wizarani hapo, ilibidi kuacha kujadili suala la wanafunzi hao na badala yake ikajadili malalamiko mengine yanayowasibu madaktari kwa ujumla.
Aliyataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na madaktari kupewa nyumba, kuongezewa posho na mazingira magumu ambayo wamekuwa wakifanyia kazi.
Katika kikao hicho, Mwamwaja alidai kuwa iliamriwa kwamba suala la interns lingejadiliwa jana baada ya MAT kufika na wanafunzi hao lakini kabla ya muda uliopangwa kufika, chama hicho kiliifahamisha wizara kwamba wanafunzi hao wamekataa.
Kutokana na hali hiyo, Mwamwaja aliahidi kuwa jana angetoa taarifa ya mazungumzo yaliyojiri katika kikao hicho cha juzi, ikiwemo maamuzi waliyoafikiana kati ya MAT na wizara lakini hakufanya hivyo.
Habari na Chalila Kibuda

Mengi awalipua wapambanaji ufisadi

  Awatuhumu kuhongwa, akerwa na mbio za urais

MWENYEKITI wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, amesema anakerwa na wapambanaji wa ufisadi kunyamaza kimya kwa kile alichokiita kuhongwa na mafisadi au wameanzisha mikakati inayolenga kuzorotesha nguvu ya vita dhidi ya ufisadi.
Licha ya Mengi kutowataja wapambanaji hao, kauli hiyo inaelekea kuwalenga baadhi ya wanasiasa ambao walijimbapambua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi hasa katika Bunge la tisa lililokuwa chini ya Spika wake Samuel Sitta.
Katika Bunge hilo wabunge waliojipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi ni Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), James Lambeli (Kahama), Lucas Selelii (Nzega), Beatrice Shelukindo (Kilindi) na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro).
Mengi alitoa kauli hiyo juzi katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam kwenye tafrija ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na IPP kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Alisema katika siku za hivi karibuni wapambanaji wa ufisadi, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari, wamenyamazishwa kwa njia mbalimbali kutokana na nguvu za mafisadi kifedha.
Alisema ingawa vitendo vya ufisadi vimeongezeka kwa nguvu na kasi kubwa, nguvu na kasi ya wananchi kwa kushirikiana na vyombo vya habari katika vita hiyo zimepungua ambapo hivi sasa kelele za kulaani ufisadi hazisikiki kama awali.
“Kuna watu wanaofikiri kwamba kupungua kwa kelele hizo kunaashiria kupungua au kutokomea kwa ufisadi, kumbe si kweli bali ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya rushwa ya fedha za mafisadi,” alisema.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kutochukuliwa kwa hatua kwa watu wanaohusishwa na vitendo vya ufisadi ambao wanajulikana kwa majina lakini wameachwa wakiendelea kula maisha ya raha na yenye jeuri.
“Ripoti nyingi za uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari zimefichua ufisadi mkubwa wa aina mbalimbali ambao haukupata kukanushwa, kwa mfano Kagoda na Meremeta, ikiwa na maana kwamba ripoti hizo ni za kweli. Ripoti hizi ni za muda mrefu sana, lakini hadi sasa waliohusishwa na ufisadi huo hawajachukuliwa hatua.
“Wananchi wanashangaa kuona mchota fedha za EPA anakiri uporaji huo na anatamba amerudisha fedha, lakini hachukuliwi hatua yoyote, eti kwa sababu hakuna ushahidi. Kama kurudisha si ushahidi, ni ushahidi wa aina gani unatakiwa?” alihoji.
Alisema wananchi wanashangaa wanapoona wauzaji wa rada iliyonunuliwa kwa bei ya kulangua wanarejesha nchini fedha walizoongeza katika uuzaji huo lakini serikali ya Tanzania haijawachukulia hatua zozote za kisheria waliofanikisha rada hiyo kununuliwa kwa bei ghali.
Mengi alisema mfumo mzima wa jamii umechafuliwa na ufisadi unaohusisha viongozi wa serikali, wanasiasa na baadhi ya vyombo vya habari katika vitendo vya rushwa na viongozi wa umma katika wizi na uporaji wa mali za umma.
Aliongeza kuwa kutokana na kutochukuliwa hatua za kisheria dhidi ya wale wanaohusishwa na ufisadi na uchafuzi uliosababishwa na ufisadi katika mfumo wa jamii, wananchi wamekata tamaa ya ushindi katika mapambano dhidi ya ufisadi.
Alionya kuwa ufisadi unavunja amani na ni mchezo hatari na wa mauti, hivyo ni lazima vitendo vya ufisadi vichukuliwe hatua za kisheria haraka vinapobainika.
Pamoja na hayo, alieleza kuwa mapambano dhidi ya ufisadi ni lazima yawe endelevu na kwamba dhamira ya kutokomeza ufisadi huo bado wanayo ingawa mapambano ya awali yalizaa matunda yasiyoridhisha.
“Mafanikio haya yawe chachu ya kuongeza nguvu katika mapambano na tusikubali kukata tamaa kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha hatua zilizochukuliwa. Kukata tamaa ni kukubali kushindwa. Bado hatujashindwa.
“Tusikubali kurubuniwa na nguvu ya kifedha za mafisadi, tusikubali kunyamazishwa. Tukikaa kimya tumewasaidia mafisadi na kuwasaliti ndugu zetu walalahoi.
Mbio za urais
Alisema mbio za kutaka kuwania urais hasa kupitia chama tawala (CCM), zimefikia hatua mbaya kutokana na baadhi ya wanasiasa na watendaji kusahau kuwatumikia wananchi.
Alisema baadhi ya viongozi wa umma wenye dhamana ya kushughulikia matatizo ya wananchi wameyapa kisogo matatizo hayo na badala yake kushughulikia mambo yao binafsi, kiasiasa na kiuchumi.
“Badala ya kushindana katika kuwasaidia wananchi wanashindana katika kujitajirisha na kutafuta madaraka ya kisiasa kuelekea mwaka 2015,” alisema Mengi.
Alisema sababu hiyo na nyinginezo zinachangia maisha ya wananchi kuwa magumu na kubainisha kuwa zipo sababu ambazo haziepukiki, lakini zipo ambazo zinaweza kuepukika.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo aliwashukia watendaji wa halmashauri wa miji na wilaya kwa ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.
Alisema miradi mingi ya maendeleo haitekelezwi na hata kama ikitekelezwa inakuwa ya kiwango cha chini na kwa gharama kubwa na kusababisha hasara kubwa, jambo ambao linaashiria kuwapo kwa rushwa katika utoaji wa zabuni.
“Halmashauri za miji na za wilaya ni kitovu cha maendeo ya jamii, lakini maendeleo katika halmashauri nyingi yamekuwa hafifu na ushahidi umeonyesha kwamba baadhi ya viongozi wa umma katika halmashauri hizo wamekuwa wabadhirifu, waporaji na wezi wa fedha za maendeleo,” alisema.
na Tamali Vullu

Monday, January 23, 2012

Mchakato kutafuta mrithi wa Regia Mtema waanza

                                 Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema
Aziza Masoud na Ellen Manyangu
WIKI moja tangu kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema kilipotokea, mchakato wa kumtafuta mrithi wa nafasi yake umeanza.

Regia alifariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu mkoani Pwani na kuzikwa Jumatano wiki hii nyumbani kwao Ifakara, mkoani Morogoro.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zinasema tayari maofisa husika ndani ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wameanza kushughulikia suala hilo la kuziba nafasi ya mbunge huyo kijana ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba alisema jana kwamba ofisi yake itatumia orodha ya majina yaliyopendekezwa na Chadema mwishoni mwa mwaka juzi.

“Nadhani tunayo orodha ya mapendekezo ya Chadema, basi kwa jinsi taratibu zilivyo, tutarejea katika orodha hiyo na pale tulipopitisha msitari ndipo tutakapoanzia, lakini lazima huyo anayefuata katika orodha awe na sifa za kuwa mbunge,” alisema Mallaba kupitia simu yake ya kiganjani.

Hata hivyo, Mallaba alisema hivi sasa ni mapema mno kufahamu ni lini uteuzi huo utafanyika na kwamba taratibu za ndani zikikamilika, mamlaka husika zitaarifiwa ili umma pia uweze kufahamu.

Awali, Mallaba alikataa kuonana na waandishi wa habari na mmoja wa maofisa wa Tume hiyo alisema: “Amesema majina yametoka hukohuko Chadema ndipo yakaja huku kwa hiyo kama mnayahitaji mnapaswa kwenda katika ofisi za Chadema ili muweze kupata majina hayo.”

Dk Slaa, Zitto wanena
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema chama chake hakifahamu atakayechukua nafasi hiyo na kwamba hiyo inatokana na ukweli kwamba jukumu hilo liko mikononi mwa NEC.

“Majina ya wagombea wa viti maalumu yapo NEC na wao ndiyo wanaoangalia kuchagua nani anayefuata katika orodha iliyopo Tume, kwa utaratibu, mgombea anayefuata ndiye atakayechukua nafasi hiyo,” alisema Dk Slaa.

Alisema Chadema kilipeleka NEC orodha ya majina 28 ya wabunge wa viti maalumu, Desemba 30, 2010 na kati ya hayo majina 25 tayari wameshachaguliwa ni jukumu la NEC kuangalia jina gani linalofuata kwenye orodha hiyo iliyopo.

Alisema kati ya hayo majina matatu yaliyobaki yeyote atakuwa na uwezo wa kuchukua nafasi hiyo kulingana na vigezo vya NEC na kulingana na utaratibu na Katiba ya Chadema.

“Sina mamlaka ya kujua nani anayefuata na ofisini kwangu hata majina sina majina yapo NEC mimi nawategemea wao waniletee  jina kwa mujibu wa taratibu zao nitaliangalia kama muhusika bado ni mwanachama hai nitawajibu na nitawarudishia na ndiyo watalitangaza kwa wananchi,” alisema Dk Slaa.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, jina watakalopewa kama muhusika atakuwa amefukuzwa katika chama, basi jina litakalofuata baada ya huyo mwanachama ndilo litakaloandikwa na kufanyiwa kazi.

Alisema si rahisi kwa NEC kumtangaza mrithi wa nafasi hiyo bila kuwasiliana kwanza na chama na kuthibitisha kuwa bado ana sifa za kushika nafasi hiyo.

Alisema NEC inajua wazi kuwa haiwezi kumtangaza mtu moja kwa moja pasipo baraka za chama kwa sababu siku hizi kumekuwa na wimbi la migogoro ndani ya vyama vya siasa nchini na wengine kujivua uanachama au kufukuzwa.

Wakati Dk Slaa akisema jukumu hilo ni la NEC, Naibu Katibu wake,  Zitto Kabwe alitaja jina la mmoja wa madiwani wa viti maalumu wa chama hicho kuwa ndiye anayefuata katika orodha iliyopelekwa NEC.

Akizungumza jana, Zito alisema kwa mujibu wa orodha yao ya viti maalumu anayefuata baada ya wabunge walioteuliwa mwaka juzi ni diwani huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa.

“Kwa mujibu wa orodha tuliyonayo ya wabunge wa viti maalumu anayefuata baada ya Regia ni diwani kutoka (anataja wilaya na jina lake), ndiye atakayechukua nafasi ya kiti hicho kilichoachwa na marehemu,” alisema Zitto.




Mabadiliko makubwa yaja uchaguzi CCM

                       Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC),Nape Nnauye

WABUNGE WAPIGWA ‘STOP’,TAKUKURU WATANGAZA VITA
MABADILIKO makubwa yanatarajiwa katika uchaguzi wa ngazi zote ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao mchakato wake umepangwa kuanza mwezi ujao.Miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuzuiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama, ikiwa ni hatua ya kufanya mageuzi yenye lengo la kuondoa tatizo la baadhi ya watu kujilimbikizia madaraka.

“Ikiwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi anataka kugombea uongozi wa chama, basi lazima apate kibali cha Kamati Kuu ya CCM na si vinginevyo,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya chama hicho.

Habari ambazo Mwananchi lilizipata na kuthibitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Nape Nnauye zinasema uchaguzi ndani ya chama hicho tawala unatarajiwa kufanyika kwa kuzingatia marekebisho yanayofanywa katika katiba yake.

Nape alikiri jana kwamba kuna mchakato wa marekebisho ya katiba ya CCM. Hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani marekebisho hayo.

Jumatano wiki hii, CCM kilitangaza ratiba ya uchaguzi huo wa ndani ya chama pamoja na jumuiya zake, ambao uchukuaji  fomu utaanza Februari 4, mwaka huu kwa ngazi ya shina, tawi na kata.
 Ratiba iliyotolewa na Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam inaonyesha kwamba katika uchaguzi wa ngazi ya wilaya, mkoa na taifa, fomu zitaanza kutolewa Juni 2, mwaka huu.  Uchaguzi huo unapewa umuhimu mkubwa na wachunguzi wa masuala kisiasa ambao wanauchukulia kama sehemu ya maandalizi ya chama hicho kutwaa tena dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Mchakato wote uchaguzi huo kwa ngazi zote, unatarajiwa kukamilika Novemba 11,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyotangazwa wiki hii na Radio Uhuru inayomilikiwa na CCM.

Mabadiliko ya Katiba
Katika mabadiliko ya katiba yanayofanywa na chama hicho, imeelezwa kwamba hatua ya kuwaengua wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kinyang’anyiro cha nafasi za uongozi wa chama ni kuondoa tatizo la baadhi ya watu kujilimbikizia madaraka.
Kazi hiyo inafanywa na Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya CCM chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa na inatarajiwa kuwasilisha matokeo ya kazi yake katika vikao vya juu vya CCM vinavyotarajiwa kukutana Dodoma mwezi ujao.

Nape alikiri kwamba kuna mabadiliko yanayotarajiwa na kutaja moja tu kwamba ni lile la kufutwa kwa nafasi za wajumbe wa NEC wa mikoa na badala yake nafasi hizo kurejeshwa katika ngazi za wilaya.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi alisema pia wajumbe wa NEC kutoka katika jumuiya za chama wanapendekezwa kuchaguliwa na jumuiya husika badala kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM kama ilivyo sasa.

Alipoulizwa kuhusu kupitishwa kwa mabadiliko hayo na vikao husika Nape alisema: “Najua  unachotaka kufahamu ni iwapo kuna mgogoro wa kikatiba, haupo kwani katiba yetu ina vipengele ambavyo vinaruhusu NEC kutekeleza jukumu hilo.”

“Kwa hiyo mapendekezo yatapelekwa kwenye kikao kijacho cha NEC na yakishapitishwa, basi yataanza kutumika isipokuwa tu kwa mujibu wa katiba lazima Mkutano Mkuu wetu uarifiwe kuhusu hatua hiyo.”

Juzi, Nape alinukuliwa akiwataka watu wanaoona kwamba anakivuruga na kukigawa chama hicho kutokana na kauli zake za kutilia mkazo miongozo na kanuni, watoke CCM na kuanzisha chama chao.  Alitoa kauli hiyo alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni ya Taifa ya TBC1 juu ya maadhimisho ya miaka 35 ya CCM, uchaguzi ndani ya chama na matembezi ya mshikamano, mwaka huu. 
“...Mimi navuruga ulaji wa wachache, si kuvuruga chama, naamini nipo sahihi kwa sababu natetea wengi. Kama ninakigawa chama kwa kuvuruga ulaji wa wachache, basi nitaendelea kukigawa, wachafu waanzishe chama chao cha wachafu na wasafi wabaki upande wao (CCM).”  Alisema sasa ni wakati wa kukirejesha chama hicho katika misingi yake na siyo wachache kukitumia kujinufaisha. 
Ratiba ya uchaguzi
Ratiba inaonyesha kuwa uchaguzi huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili; uchaguzi wa viongozi wa chama na ule wa Jumuiya zake.  Kwa mujibu wa ratiba hiyo, wanachama watakaowania uongozi kwenye jumuiya katika ngazi ya shina, wataanza kuchukua fomu kuanzia Februari 4 na uchaguzi utafanyika Februari 29, mwaka huu.
Kwa upande wa uongozi wa chama ngazi hiyo ya shina, uchukuaji fomu, utaanza Machi 23 na uchaguzi utafanyika Aprili 30.

Katika ngazi ya tawi, fomu kwa wagombea wa jumuiya zitaanza kutolewa Machi 3 na uchaguzi wake utafanyika Aprili 22, wakati fomu za kuwania uongozi wa chama zitaanza kutolewa Februari 20 na uchaguzi utafanyika Machi 31.

Katika ngazi ya kata, wagombea wa jumuiya wataanza kuchukua fomu Mei 4 na uchaguzi wake ni Juni 30, wakati kwa wagombea wa chama fomu zitaanza kutolewa Mei 13 na uchaguzi utafanyika Julai 4.  Ngazi nyingine
Visiwani Zanzibar, fomu kwa ajili ya uchaguzi wa majimbo zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kufanyika Julai 26 kwenye jumuiya na Agosti 2 kwa wagombea wa uongozi wa chama.
Kwa upande wa wilaya, ratiba hiyo inaonyesha kwamba fomu za uchaguzi wa viongozi wa wilaya wa jumuiya Tanzania Bara, zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kumalizika Agosti 22, huku fomu kwa ajili ya viongozi wa chama, zikipangwa kuanza kutolewa Juni  2 na uchaguzi kufanyika Septemba 26. 
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba  katika ngazi ya mkoa, uchaguzi wa jumuiya utaanza Juni 2 na uchaguzi utafanyika Septemba 26 na fomu za uchaguzi wa viongozi wa chama, zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kufanyika Oktoba Mosi mwaka huu.
Ngazi ya taifa, fomu zitaanza kutolewa Juni 2 kwa wagombea wa jumuiya na uchaguzi wake utafanyika Oktoba 5 na fomu kwa ajili ya wagombea wa ngazi ya chama, zitaanza kutolewa Oktoba 25  na uchaguzi utafanyika Novemba 11.  Mkutano Mkuu wa taifa unatarajiwa kufanyika Oktoba 9 ili kukamilisha Uchaguzi Mkuu na kuunda Sekretarieti ya Taifa.
 Takukuru waonya  Wakati hayo yakiendelea, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza vita kwa  wote watakaotoa na kupokea rushwa ili kushinda katika nafasi mbalimbali za uchaguzi huo ndani ya CCM.

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, ambako uchaguzi ngazi ya taifa unatarajiwa kufanyika, Sostenes Kibwengo amesema kuwa taasisi hiyo imejipanga kukabiliana na vitendo vya rushwa vitakavyojitokeza.
“Hatutamwonea haya mtu yeyote hata kama ni mkubwa kiasi gani, maana uchaguzi huo huwa unajaa vibweka ukizingatia mwaka huu wanapanga safu zao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015,’’alisema Kibwengo na kuongeza:   “Tusipokuwa makini na jambo hilo, CCM kitaingiza viongozi wabovu na wazembe ambao mwisho wa siku, wataifanya Serikali yote kuwa ni ya wala rushwa.’’
Kauli hiyo imeungwa mkono na Takukuru Taifa. Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwan alisema kimsingi suala hilo limo ndani ya taasisi hiyo mkoani Dodoma hasa kwa kuzingatia kuwa mkutano huo unafanyika kwenye eneo lake.

Habari hii imeandaliwa na Exuper Kachenje, Keneth Goliama na Habel Chidwali, Dodoma

                                                             

Lembeli, Mgeja wageuka kama wanamasumbwi


MBUNGE wa Kahama, James Lembeli, ambaye ametangaza kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, amemtuhumu Mwenyekiti wa sasa, Hamisi Mgeja, kuwa ana ugonjwa wa kusahau.

Kauli hiyo imekuja baada ya Mgeja kudai kuwa, Lembeli hamnyimi usingizi na kumfananisha na sisimizi ambaye hawezi kumwathiri kwa sababu hana uwezo wa kushinda nafasi hiyo.

Lembeli alisema Mgeja siyo saizi yake katika nafasi yoyote ya kuchaguliwa na kwamba, hata yeye (Mgeja) anajua hasa kupitia uchaguzi mbalimbali uliopita ndani ya chama.

Alisema tayari amesahau mwaka 2005 alikuwa mgombea ubunge wa Kahama na kushindwa vibaya kura za maoni, alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 170 na kuongeza kuwa, hicho ni kielelezo tosha.
Mbunge huyo alisema Mgeja kwa kusahau, mwaka 2010 aligombea ubunge wa Kahama baada ya kukatwa Jimbo la Ushetu, lakini lilipofutwa hilo jipya alimkimbia kwa kujitoa.

“Mgeja siyo saizi yangu, alinikimbia uchaguzi wa kura za maoni za chama kwa mwaka 2005 na mwaka 2010, nilimshinda vibaya sasa hapo ndipo unapombaini kuwa anasahau,” alisema Lembeli.
Kuhusu kanuni ya CCM inayotaka mbungeau mtumishi wa Serikali kujiuzulu kwanza kabla ya kuwania wadhifa ndani ya chama, Lembeli alisema chama kinatoa vibali maalumu kwa wagombea wenye nafasi nyingine za uwakilishi, hivyo atafuata taratibu hizo mpaka amng’oe Mgeja.

Kwa upande wake, Mgeja alisema alimtaka mbunge huyo kuachana kumfuatafuata kwa sababu ana siri nyingi zinazomhusu, ikiwamo kujikita kupambana na ufisadi huku akitekeleza wapiga kura wake.

Mgeja alisema Lembeli anataka kucheza ngoma asiyolingana nayo na kwamba, ndani ya chama hakuna ushindani isipokuwa kuna kupangana, ndiyo maana (Lembeli) akapangwa kuwania ubunge, lakini siyo kwamba alimshinda.

“Mimi sitaki malumbano na Lembeli namheshimu sana, lakini akizidi nitafumua yake yote ninayofahamu ninayo na nitayaripua, yeye kama anataka uenyekiti agombee tu, lakini masuala ya kuzungumzia kitambi changu hayamhusu naona kama vile analionea wivu tumbo langu,” alisema Mgeja.

Mwaka jana, Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Shinyanga, iliwaita Lembeli na Mgeja na kuwaonya vikali kuacha malumbano, huku Mgeja akitolewa nje ya kikao baada ya Lembeli kugoma kujieleza mbele yake.

Arumeru waupokea mwili wa Mbunge kuuzika leo

MAMIA ya wakazi wa wilayani Arumeru na Jiji la Arusha, jana walijitokeza barabara kuupokea mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Jeremiah Sumari ambaye atazikwa leo katika  eneo la Akeri wilayani Arumeru.


Mwili wa mbunge huyo, ambaye alifariki akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Januari 17, mwaka huu, uliwasili jana majira ya saa 12:30 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ndege ya kampuni ya 540 ukisindikizwa na wabunge na mawaziri kadhaa.


Baadhi ya mawaziri waliowasili uwanjani hapo na ndege nyingine ya kusindikiza   mwili huo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (mahusiano) Steven Wassira, Waziri wa Habari,Vijana ,Utamaduni na Michezo, John Nchimbi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera na Bunge), William Lukuvi.


Pia alikuwapo Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye alikuwa kwenye ndege moja na mwili wa Sumari na uwanjani hapo walikuwapo Manaibu Mawaziri kadhaa, akiwamo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Godluck Medeye ambaye ni mbunge Jimbo la Arumeru Magharibi.


Magari zaidi ya 50 yaliyokuwa na watu mbalimbali wakiwamo mawaziri, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa hususan  CCM yalionekana na kuvuta hisia za huzuni kwa wakazi wa mitaa mbalimbali yalikopita.
Wengine ni pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Vijana ambao waliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa( UVCCM), Beno Malisa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu Sumari, Msemaji wa Familia ya Sumari, Chifu Esrom Sumari alisema wamepokea msiba huo kwa  masikitiko makubwa.


Chifu Sumaru ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa ukoo za Kabila la Wameru alilishukuru Bunge kwa kugharamia usafiri na mazishi ya Sumari na pia Serikali kwa kujitolea kumtibu Sumari nchini India na alipokuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Chifu Sumari alisema kifo cha Mbunge huyo ni pigo kubwa kwa familia yao, kwani alikuwa mshauri muhimu na alitoa msaada mkubwa kwa familia na wakazi wa Jimbo la Arumeru Mashariki.


Hadi jana jioni, kamati ya mazishi ya mbunge huyo, ilikuwa inakutana ambapo ratiba ya awali iliyotolewa ilieleza shughuli za mazishi zitaanza saa 2:00  asubuhi.

Ratiba hiyo, inaeleza kuwa ibada ya mazishi itaanza saa 7:00 mchana katika Kanisa la Kiijili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lilipo jirani na nyumbani kwa Sumari ambapo pia uwanja maalumu umeandaliwa kwa shughuli hiyo.


Viongozi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria mazishi leo, akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye tayari yupo mjini hapa na kulikuwa na taarifa za Rais Jakaya Kikwete pia kuhudhuria mazishi hayo.

Marehemu Sumari ameacha mke na watoto wanne, na alichaguliwa kuwa mbunge tangu mwaka 2000 ambapo pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi.



Raia wa Nigeria anaswa na dawa za kulevya Dar

RAIA wa Nigeria mwenye miaka 34 amekamatwa na polisi wa Uwanja wa Ndege Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na dawa za kulevya tayari kuelekea nchini Nairobi.

Kukamatwa kwa Mnigeria  huyo  kumekuja siku chache baada ya polisi kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya zipatazo kilo 210 mkoani Lindi, ambazo zilikuwa tayari kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam zikivunja rekodi tangu kuanzishwa kwa Kitengo cha Dawa za Kulevya.

Juzi, Polisi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere walimkamata Mnigeria huyo jambo ambalo lilithibitishwa na  Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege nchini, Ulrich Matei akisema lilitokea  saa 10:20 alfajiri.

Matei alisema kutokana na kuimarishwa kwa shughuli za upekuzi uwanjani hapo, waliweza kumbaini raia huyo akiwa na pipi 14 za dawa za kulevya ambazo zinaendelea kuchunguzwa kujua ni za aina gani.

Alifafanua kwamba, mtuhumiwa huyo mwenye hati ya kusafiria namba A02425579 iliyotolewa Nigeria mwaka 2010, alikuwa akijiandaa kuondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ).

Kamanda Matei aliongeza, baada ya kupekuliwa raia huyo alikutwa na kiasi hicho ambacho alikificha kwenye fulana na kuongeza kwamba alikuwa akisafiri na ndege hiyo kwenda Kenya kisha Lagos, Nigeria.

"Hapa uwanjani tunajitahidi kwa uwezo wetu wote kuhakikisha uwanja wetu hauwi njia ya wahalifu. Hatuwezi kuruhusu watu wachafue taswira nzuri ya nchi yetu. Sasa tulivyompekua, tulimkuta akiwa na kiasi hicho cha pipi akiwa amezifunga kwenye fulana.

 Alikuwa anasafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya yenye namba KQ481 akielekea Nairobi kisha Lagos, Nigeria," alifafanua Kamanda Matei.

Hata hivyo, Matei alisema raia huyo bado alikuwa akishukiwa kuwa na dawa nyingine alizomeza tumboni lakini hadi jana hakuwa ameweza kutoa nyingine na alikabidhiwa kwenye kikosi cha Kudhibiti za Dawa za Kulevya kwa taratibu zaidi za kisheria.

"Tulimshuku alikuwa amemeza dawa tumboni lakini hadi jana asubuhi hakuwa ameweza kutoa. Tulichofanya sisi Polisi wa Uwanja wa ndege ni kumkabidhi Kitengo cha Dawa za Kulevya ili waweze kuendelea na taratibu nyingine ikiwa ni pamoja na kumpiga X-ray na vipimo vingine kubaini aina ya dawa hizo alizokamatwa nazo kwani zinahitaji vipimo," alifafanua kamanda Matei.

Alisema licha ya kumshikilia kwa siku nzima ya juzi raia huyo ambaye alikamatwa Terminal Two, hakuweza kutoa dawa nyingine zaidi na kwamba  taratibu nyingine za kisheria zitaandaliwa.

Ofisa wa Bunge afariki dunia kwa kupigwa risasi

                                          Shughuli za Bunge zikiendelea Bungeni

WAKATI Bunge likiendelea kuomboleza vifo vya wabunge wake wawili, Regia Mtema (Viti Maalumu Chadema) na Jeremiah Sumari Arumeru Mashariki CCM), limepata pigo jingine baada ya mfanyakazi wake, Nicolaus Luther Senge kufariki dunia kwa kupigwa risasi na askari polisi katika tukio ambalo lilisababisha vifo vya watu watatu.
Hata hivyo, kumekuwa na taarifa za kutatanisha na zenye kupingana kati ya polisi na Bunge kuhusu jina halisi la mfanyakazi huyo na mahali ambako mwili wake umehifadhiwa.
Habari zilizotufikia jana zimeeleza kuwa Senge (49) alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika mauaji yaliyofanyika kwenye kikao cha wanafamilia Kibaha mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu amethibitisha kifo hicho lakini akamtaja mtumishi huyo wa Bunge kuwa ni Nkolo Senge.
Kamanda Mangu alisema katika tukio hilo lililotokea nyumbani kwa Pendael Senge ambaye ni Mratibu wa Tasaf Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, wengine waliofariki dunia ni Andrew Nkolo (30) na askari polisi Nicodemus Senge ambaye ndiye anayetuhumiwa kuwaua wenzake.
Alisema siku ya tukio, watu hao walifika nyumbani kwa Pendael ambaye ni baba yao mdogo kwa ajili ya kupatanishwa juu ya ugomvi wa urithi wa ekari mbili za ardhi zilizoko kijijini kwao Singida.
“Ugomvi huo ulianzia Singida ambako walishtakiana lakini hakimu akawataka waumalize kiukoo. Ndipo Pendaheli ambaye ni baba yao mdogo akaamua kuwaita nyumbani kwake ili wazungumzie suala hilo,” alisema Kamanda Mangu na kuendelea:
“Wakiwa kweye kikao hicho kabla ya kufikia mwafaka, Nicodemus ambaye ni askari polisi wa Kituo cha Usalama Magomeni, Dar es Salaam alichomoa bastola yake na kuwamiminia risasi ndugu zake hao kisha kujimaliza mwenyewe.”
Kwa mujibu wa Kamanda Mangu, miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha na hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Kauli ya Ofisi ya Bunge
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amethibitisha kutokea kwa kifo cha mfanyakazi huyo wa Bunge na kueleza kuwa hadi jana mchana, lakini akasema maiti yake ilikuwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Ndugai alisema Ofisi ya Bunge imesikitishwa na kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia jana, siku chache baada ya taasisi hiyo ya kutunga sheria kupoteza wabunge wawili.
“Kwa sasa nipo Arusha lakini taarifa za kifo cha Senge nilizipata jana. Bado sina taarifa zaidi kuhusu kifo hicho kwa sababu kimetokea kwa njia ambayo lazima ihusishe uchunguzi wa kipolisi,” alisema Ndugai.
Hilo ni pigo jingine kwa taasisi hiyo katika kipindi cha juma moja baada ya Mtema kufariki dunia Januari 14, kwa ajali ya gari iliyotokea Ruvu, Kibaha na Sumari alifariki dunia Januari 17, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu saratani ya ubongo.
Kauli ya familia
Baba mdogo wa marehemu hao Pendael Senge naye alithibitisha mauaji hayo na kueleza kuwa yalitokana na ugomvi wa shamba.
Pendael alisema askari huyo aliwaua ndugu yake Nicolaus Senge ambaye alikuwa mtumishi wa Ofisi ya Bunge, pamoja na binamu yake Andrew Nkolo (mtoto wa shangazi yake).
Akisimulia tukio hilo Pendael alisema kabla ya mauaji hayo, ndugu hao walifika nyumbani kwake Kongowe Kibaha kwa ajili ya kikao cha usuluhishi kuhusiana na ugomvi huo wa shamba. Hata hivyo, alisema usuluhishi huo ulishindikana na badala yake ukazuka ugomvi baina ya ndugu hao uliwafanya wapigane ngumi kabla ya wanandugu kuwaamulia.
Alisema muda mfupi baada ya ndugu kuwaamulia, askari huyo aliwapiga risasi ndugu zake kisha naye kujimaliza.
Alisema chanzo cha ugomvi huo ni shamba la ekari mbili lililoko katika Kijiji cha Ilunda Wilaya ya Iramba, Singida... “Shamba hilo ni la mpwa wangu Andrew ambalo alirithishwa na mama yake aliyefariki dunia takriban miaka 15 iliyopita,” alisema Pendael na kuongeza:
“Lakini kwa kuwa Andrew anafanya shughuli zake za Steshenari Dar es Salaam, basi binamu yake Nicodemus Senge akajenga nyumba katika kiwanja hicho.”
Alisema baada ya Nicodemus kujenga katika kiwanja cha Andrew, walishtakiana katika baraza la ardhi kijijini hapo ambalo liliwaagiza wazungumze wenyewe kwanza ili kuona kama wanaweza kufikia mwafaka.
“Kwa kuwa wote wako hapa Dar es Salaam ndipo jana wakaamua kuja kwangu kwa ajili ya kufanya kikao cha usuluhishi. Wao walifika saa 10 na baada ya ndugu wengine kufika saa 12 jioni ndipo tukaanza mazungumzo:

“Niliwasihi kuwa nikiwa baba yao mdogo ningefurahi kuona jambo hilo linamalizika kindugu,” alisema Pendaeli
Hata hivyo, alisema wakati wa mazungumzo hayo Nicodemus akamshutumu ndugu yake Nicodemus (wa Bunge) kuwa ndiye anayempa msaada binamu yake wa kifedha na kiushauri.
“Alikuja juu (polisi) na kuongea kwa hasira sana. Mimi baada ya kuona kuwa hakuna uelewano tena nilishauri kuwa ni vyema tuliachie baraza la ardhi liamue,” alisema Pendaeli na kuongeza:
“Nico wa Bunge na Andrew walikuwa upande mmoja na huyu askari na baadhi ya ndugu wengine walikuwa pia upande mmoja, hivyo wakaanza kupigana ngumi lakini watu wakawasihi wakaacha.”
“Lakini kabla ya kuondoka huyu askari akaomba maji, walipomletea akakataa glasi akanywea kwenye kidumu kile cha lita tano. Alipokunywa mara moja tu akapiga chini lile dumu kisha akakimbia hadi kwenye gari alimokuwa Nico wa Bunge akampiga risasi moja ya usoni kisha akamfuata Andrew akampiga risasi ya begani, wakati akikimbia akampiga risasi nyingine kiunoni, akaanguka na kufariki dunia,” alisema Pendaeli.
Baada ya matukio alisema watu wote walikimbia akiwamo askari huyo ambaye hata hivyo, alisema alikimbia kama mita 50 kutoka  nyumbani hapo kisha naye akajipiga risasi kifuani na kufariki dunia papohapo.
“Nilikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi na askari walipofika na kumpekua mfukoni mwake (muuaji) wakakuta kikaratasi kilichosema: mtu yeyote asisumbuliwe kwa mauaji haya,” alisema Pendaeli.
Habari hii imeandaliwa na Sanjito Msafiri na Julieth Ngarabali, Kibaha, Aidan Mhando, James Magai

RAIS JAKAYA KIKWETE,CHADEMA WAJADILI KATIBA KWA SAA NANE

 

Rais Jakaya Kikwete akimsikiliza katibu Mkuu wa CHADEMA Dk Willbrod Slaa (kushoto) usiku wa kuamikia jana Ikulu jijini Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya mazungumzo ya mchakato wa Katiba. Katikati ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe. Picha na Ikulu
NI KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA JUZI, KAMATI KUU YAJIFUNGIA KUJADILI, NCCR- MAGAUZU WATOA TAKMO LAO
Fidelis Butahe
MKUTANO kati ya Rais Jakaya Kikwete na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliofanyika juzi Ikulu, Dar es Salaam ulichukua saa nane kutokana na uzito wa hoja zilizokuwa zimetolewa na pande zote mbili.

Novemba mwaka jana, Chadema ilikutana na Rais Kikwete kwa mara ya kwanza Ikulu na kumkabidhi kabrasha lililokuwa na mapendekezo mbalimbali kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambayo pamoja na mengine, kilitaka mchakato huo urejeshwe upya bungeni na kumtaka mkuu huyo wa nchi asitie saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulipitishwa na Bunge. Hata hivyo, siku moja baada ya mazungumzo hayo, Rais alitia saini muswada huo na kuwa sheria.

Vyanzo vya habari kutoka Ikulu, vililiambia gazeti hili jana kwamba Chadema ilipewa ratiba hiyo kuanzia saa 10:30 hadi saa 5:45 usiku ili kutoa wigo mpana wa majadiliano hayo yenye nia ya kupata Katiba kwa njia za amani na umoja.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, katika chumba cha mazungumzo kulitawaliwa na majadiliano ya kina ambayo wakati mwingine, yaliambatana na utani wa hapa na pale kwa mfano, Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbrod Slaa alimwambia Rais: “Watu wanasema nakukwepa Rais.” Ilielezwa kwamba katika mazungumzo hayo, wajumbe wa pande zote mbili walijadili kwa uhuru mkubwa na mkuu huyo wa nchi namna ya kupata Katiba bora bila mikwaruzano.

“Mazungumzo yalikuwa ni mazuri tu, pande zote mbili zilizungumza na kutoa hoja zake, kulikuwa na utani wa hapa na pale. Yale ambayo yalionekana kuwa magumu kidogo kila upande uliomba kuyachukua na kwenda kuyafanyia kazi zaidi kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.”

Novemba 28 mwaka jana, Rais Kikwete alisaini muswada huo na kukamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limeupitisha.

Tangu wakati huo Rais Kikwete amekuwa akitutana, kusikiliza na kuchukua maoni na mawazo ya wadau mbalimbali kutoka vyama vya siasa, asasi za kijamii na makundi mengine ya kijamii kuelekea mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Mchakato huo umekuwa ukipingwa na kwa hoja mbalimbali zikiwamo za kuundwa kwa tume ya kuratibu mchakato huo, hadidu za rejea, mamlaka ya uundaji  wa tume na uteuzi wa wajumbe na wapi tume itapaswa kuwajibika.

Kauli ya Ikulu
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na kusainiwa na Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga ilisema Rais Kikwete alisema licha ya nchi kuwa na Katiba ambayo imelilea vizuri taifa,  inahitajika Katiba mpya inayokwenda na wakati.
Alisema baada ya kumalizika kwa kikao na viongozi wa NCCR-Mageuzi, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chadema, ikiwa ni mwendelezo wa mazungumzo yao yaliyoanza mwishoni mwa  Novemba, 2011 kuhusu Katiba Mpya.


“Katika mazungumzo haya na vyama vya siasa, Rais amesisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa hatimaye Watanzania wote watakiri kuwa Katiba Mpya ni yao wote na hatimaye ifikapo mwaka 2015 nchi iweze kufanya uchaguzi wake na Katiba Mpya,” alisema Kibanga.

Chadema wajifungia Dar
Kwa upande wa Chadema, jana Kamati Kuu (CC) chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ilikuwa katika Hoteli ya Protea Dar es Salaam kujadili mkutano huo na Rais, Ikulu juzi.

Katika kikao hicho, Kamati Maalumu ya Chadema kuhusu mchakato huo wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, iliwasilisha taarifa yake.

Taarifa ya chama hicho, iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika ilisema uamuzi wa CC kuhusu mkutano na Rais  Kikwete utatolewa baada ya kikao hicho kumalizika.

Akizungumzia mkutano wa Ikulu, Mnyika alisema kamati hiyo maalumu ya Chadema iliyokutana na Rais Kikwete ikiongozwa na Mbowe, ilitaarifiwa hatua ambayo imefikiwa na Serikali katika kuanza kuiboresha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, ili ikidhi mahitaji ya kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na ushauri wa wadau mbalimbali.

Kauli ya NCCR-Mageuzi
NCCR-Mageuzi kwa upande wake, kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kikidai kwamba Rais Kikwete amekubali kuifanyia marekebisho  sheria hiyo.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye aliongoza na ujumbe wa watu sita kwenda Ikulu Dar es Salaam juzi, alisema jana kwamba baada ya kuwasilisha ajenda zao mbili kuhusu katiba na umeme, waliambiwa sheria hiyo itafanyiwa marekebisho katika kikao kijacho cha Bunge.

Mbatia aliwaambia waandishi wa habari kwamba pamoja na sheria hiyo kurudishwa bungeni, pia walimwomba Rais Kikwete aifanyie marekebisho Ibara ya 98 ya Katiba ya sasa kwa kuwa inachangia kukwamisha mabadiliko ya Katiba.

“Lengo la kuanzishwa kwa NCCR-Mageuzi ni Watanzania kuwa na Katiba yao na hata Rais wa Awamu ya Tatu (Benjamin Mkapa), tuliwahi kumweleza kwamba Katiba ni ya kudumu na lazima iundwe kwa maslahi ya wananchi na ndicho tulichomweleza Rais Kikwete,” alisema Mbatia.

Alisema tangu wakati huo nchi imekuwa na katiba yenye mfumo wa chama kimoja, licha ya kuwa ilipitishwa sheria ya kuwa na vyama vingi.

Mbatia alisisitiza kwamba, katika msafara wa chama hicho Ikulu, Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa chama hicho, Dk Sengondo Mvungi alitumia zaidi ya saa moja kumfafanulia Rais Kikwete na timu yake jinsi mchakato wa kuandika Katiba Mpya unavyotakiwa kuwa.

Alisema walimweleza Rais Kikwete kwamba  suala la Katiba ni la kisiasa, hivyo si vyema Tume itakayoundwa ikaachwa chini ya uangalizi wa wanasheria pekee.

“Katika tume hii wanatakiwa kutumiwa wataalamu mbalimbali hata kama watakuwa wanasiasa… kinachotakiwa ni kuangalia uwezo wao,” alisema Mbatia.

Katika kikao hicho cha Rais na NCCR-Mageuzi, viongozi wa Serikali waliokuwapo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi na ujumbe wa chama hicho uliwajumuisha pia Makamu Mwenyekiti wake, Zanzibar, Ambary Hamisi, Naibu Katibu Mkuu George Kahangwa, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, Mweka Hazina Taifa, Mariam Mwakingwe, na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaituni Buyogela.

Sunday, January 22, 2012

MKUU WA MKOA WA RUVUMA ATEMBELEA PROJECT YA NISHATI MPYA YA MTO MKUJU

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mh.Said Mwambungu jana jumamosi alitembelea project ya nishati mpya ya mto Mkuju.Project hiyo inaendelea mkoani humo wilayani Namtumbo kijijini Likuyu Seka ndani ya Hifadhi ya mbuga ya wanyama ya Selous.Mkuu wa mkoa huyo Mh.Said Mwambungu aliweza kujionea shughuli mbalimbali zinazo endelea katika Project hiyo yenye matarajio baadae ya kuwa mgodi.Project hiyo iliyopo inajishughulisha na utafiti wa madini ya uranium (urani).Utafiti unafanywa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited chini ya Uranium1 kampuni inayotokea nchini Urusi.Mpaka sasa utafiti huo unaendelea maeneo mbalimbali chini ya kampuni hizo.Utafiti huo umeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana hadi kuweza kusababisha mradi huo kuwa mgodi wa madini hayo ambayo ni muhimu sana dunia kote.
Licha ya mkuu huyo wa mkoa kujionea shughuli za mradi,mkuu huyo nae pia aliongea machache juu ya mtazamo wake katika shughuli izo katika mkoa wake,mkuu wa mkoa Mh.Said Mwambungu alisema namna shughuli za project hiyo inayotarajiwa kuwa mgodi ni nzuri kwani zimeweza sana kusaidia uchumi wa watu wake katika mkoa huo kwa kuweza kutoa ajira kwa vijana katika mkoa wake nakusema anatarajia mkoa kuwa ni mkoa wenye maendelea makubwa sana kutokana na mradi huo na kusema yeye kwa upande wake amelipokea hilo kwa mikono yote kuwa mradi huo uendelea kwasababu unamafanikia makubwa siku za usoni.
                                                         Matukio ya Picha
      Mh.Said Mwambungu kiweka sahihi katika kitabu cha wageni katika camp ya project ya nishati mpya
Hawa ni baadhi ya mameneja katika mradi huo kuanzia kushoto ni Colline Grammar meneja wa site,Benard Mihayo meneja mausiano,Emmanuel Nyamusika meneja wa utafiti,John Ntukula meneja mazingira,Peter Kaluwa administration officer.
Mh.Emmanuel Nyamusika meneja utafiti akielezea juu ya shughuli za mradi nini maana na nini kanachofanyika na nini kinachotafutwa.
Mh.John Ntukula meneja mazingira akielezea juu ya mazingira namna wanavyofanya katika swala la utunzaji wa mazingira ikiwemo uwoto wa asili.
Mh.Said Mwambungu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi katika mradi wa mto Mkuju
Imeandikwa na Makali Machechi picha na Clever Perfect









Saturday, January 21, 2012

Wanakijiji Mbeya waenda hospitali na taa zao

WANANCHI wa Kijiji cha Mbebe Wilaya ya Ileje mkoani Mbeya wamelazimika kutoka na taa zao nyumbani mpaka Kituo cha Afya cha kijiji hicho ili kupatiwa huduma baada ya kituo hicho kukosa umeme kwa muda mrefu.

Watumishi wa kituo hicho waliojitambulisha kwa jina moja moja la Pagale na Kaponda walisema tatizo la umeme limekuwa kero hasa kwa wanawake wajawazito wanaojifungua usiku.

Wahudumu hao walisema wagonjwa wanaopatiwa huduma katika kituo hicho ni kutoka vijiji saba vinavyoizunguka zahanati hiyo na wengi wao wakiwa wanatoka umbali wa kilometa saba na wengine tano.

Aidha, walisema tatizo hilo linawalazimu mara nyingine kutumia mafuta yao ya taa huku nishati hiyo ikiwa imepanda bei kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwa kero kwao.

Kwa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), baadhi ya wananchi walihoji pesa wanazotoa katika kituo hicho kuwa zinafanya kazi gani mpaka kituo hicho kinakosa umeme.

“Hapo nyuma umeme ulikuwepo lakini kutokana na wananchi kusuasua kulipia bili za umeme, umeme ukakatwa,” alisema mmoja wa wauguzi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Aidha alisema kitendo hicho kimewasababishia wachukiwe na wananchi kwa kuwa wagonjwa wafikapo kituoni hapo hukuta kukiwa giza na ndugu wa mgonjwa hulazimika kutafuta mafuta ya taa.
Imeandikwa na Neema Kidumba, Mbeya;