NJOMBE

NJOMBE

Monday, November 19, 2012

MIAKA HATARI YA KUVUNJIKA KWA NDOA



Watafiti wa masuala ya uhusiano na ndoa wana kalenda za miaka ya hatari iliyotafsiriwa sambamba na sababu zinazoweza kuvuruga uhusiano na kuwafanya watu waliokuwa wakipendana kuachana.
 Hivyo kwa dondoo tu nimeona ni vyema niwafundishe watu wanaoishi kwenye ndoa sababu zinazotafsiri ukomo wa mapenzi yao kulingana na miaka husika iliyotafsiliwa na watalaamu wa masuala ya ndoa na uhusiano.
 Wanasaikolojia mbalimbali ulimwenguni kupitia tafiti zao walikubali kuuweka UGOMVI kuwa katika sababu zinazoweza kusababisha ndoa kuvunjika ndani ya mwaka 1-2. Wanasema endapo watu waliooana wakianza kugombana kati ya mwezi wa kwanza na kuendelea, basi ujue kuwa wanandoa hao hawawezi kuvuka miaka miwili kabla ya ndoa yao kuvunjika.
 Jambo la kuzingatia katika sababu hiyo ya ugomvi iliyotajwa ni  kwamba watafiti hao hawachukulii hitilafu na migongano ya kawaida kama sababu, bali mikwaruzano mikubwa yenye kuumiza mwili au roho kwa kiasi kikubwa.
  Watafiti hao wanasema wanandoa wapenzi wanaogombana kwa kipindi hicho huwa na kasoro ya ulinganifu wa tabia, mawazo na mwelekeo hivyo kuwafanya wasiweze kuishi pamoja kwa muda mrefu.
 Hivyo ili wanandoa wasiweze kuachana katika miaka miwili ya mwanzo wanashauriwa kuoana baada ya kuchunguzana vema tabia na kulingana katika hali. (Soma TITANIC 1 njia za kutafuta mchumba)
 Mwaka mwingine wa hatari ni wa NNE. Baada ya kuoana mwaka wa nne unatajwa na watafiti kuwa ni wa hatari katika kuwafikisha wapendanao  ukingoni mwa mapenzi yao. Sababu ambayo inapewa uzito katika kizuizi hiki cha ndoa ni kufanikiwa kupata MTOTO.  

Kuwekwa kwa mtoto katika kizingiti hiki kunaonekana na tafiti nyingi kuonesha kuwa wanandoa wanapofanikiwa kupata mtoto hujisahau na kuhamisha mapenzi yao kwa mtoto, huku wakijisahau kuwa wao pia wana jukumu la kupendana.
 Watafiti hao wanasema wapendanao wanapokuwa na mtoto, muda mwingi humfikiria zaidi yeye.  Kama ni suala la kuchukua zawadi za kurudi nazo nyumabani hazitakuwa kwa ajili ya mume/mke bali itakuwa ni kwa mtoto.  Pia msukumo wa kujali, kuhudumia kubembeleza na ukaribu utahamia kwa mtoto, jambo ambalo litawafanya wapendanao hao kujiona kama watu wasiohitajiana sana na hivyo kuleta hatari ya ndoa kufikia ukomo.
 Ili kukwepa ndoa kuvunjika katika mwaka huu, wanandoa wanashauriwa kuwa baada ya kupata mtoto wasisahauliane, wawe na vipindi vya kuwa pamoja na kushirikiana kama mwanzo, kwa lengo la kulinda upendo wao usiharibike.
 Baada ya kuvuka miaka hivyo, mwaka wa saba tangu kuoana unawekwa kuwa ni mwaka wa kizingiti cha mwisho cha wanandoa kuachana.  Kinachosababisha hatari za mwaka huu kuwemo katika fungu hilo ni MAISHA, MAJUKUMU NA MAZOEA.  
Katika kufafanua mwaka huu watafiti hao wameeleza sababu nyingi, lakini za msingi ni hizo ambazo nimezitaja.
 Wanasema katika mapito ya maisha kuishi kwa wanandoa ndani ya ndoa kwa miaka hiyo saba kutakuwa kumewatumbukiza katika kukabili matatizo mengi ya kimaisha na hivyo kuwafanya wazidiwe na harakati za kujikimu.  Kwanza watakuwa wamepata majukumu ya kulea familia, kutunza watoto wao, ambao tayari watakuwa wameanza kusoma n.k.
 Lakini sababu ya kuzoeana inatajwa kuchangia kuondoa msisimko wa kupendana na hivyo kuamsha hisia potofu kuwa mwanandoa anaweza kuishi bila mume au mke wake. Hivyo ili kulinda ndoa katika kipindi hiki cha miaka saba, wanandoa wanashauriwa kutotumia muda wao mwingi kwenye pilika pilika za kimaisha kiasi cha kukosa muda wa kuwa pamoja.
 Hata hivyo wakati watafiti hao wanakubaliana kuwa miaka iliyotajwa ni ya hatari katika kuvunjika kwa ndoa, bado wanarudi katika kapu hilo kwa kusema wanandoa ambao wanaachana baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka hiyo iliyotajwa, yaani miaka minane na kuendelea wanaingia katika kundi la wazembe na wavivu wa kufikiria misingi ya ndoa yao.
 Wanasaikolojia wanasema watu walioishi kwa miaka hiyo huwa hawana majibu sahihi yanayoweza kushibisha sababu za kuachana kwao.  Wanachokiamini wataalamu hao ni kuwa, hakuna tabia, mwenendo, migongano mabishano na purukushani mpya za kimaisha zinazoweza kuwatokea wanandoa hao kiasi cha kuonekana kuwa ni sababu za kupiku mazoea na kushindwa kuvumiliana.

Katika kuhitimisha hilo niseme tu kwamba, ili kuepukana na kikwazo cha kwanza watarajiwa wa ndoa wanashauriwa kuchanguana kwa kuzingatia ulinganifu wa tabia. Vijana wengi siku hizi hawazingatii ulinganifu wa kitabia, badala yake wanachagua wenza kwa kufuata uzuri na pesa, huku wakilenga kupata sifa toka kwa rafiki zao

Katika kikwazo cha pili, ushauri uliopo ni kuwa makini juu ya malezi ya watoto na kuepuka kusahauliana.  Watoto wanapaswa kuwa ndani ya upendo wa mume na mke.  Kuhusu kizingiti cha miaka saba, ushauri na kuepuka kuzoeana na daima kujizatiti kukabiliana na changamoto za kimaisha bila kukata tamaa.

No comments:

Post a Comment