Kukoroma ni tatizo linalowapata watu wengi wakati wanapolala ambalo
linaweza kuwatokea watu wa kila umri ingawa hutokea mara nyingi kwa
wanaume au watu wanene. Kukoroma huzidi kwa kadri umri unavyoongezeka na
asilimia 54 ya watu wazima hukoroma baadhi ya wakati huku asilimia 25
ya wengine wakiwa na tabia ya kukoroma kila wakati. Kukoroma baadhi ya
wakati kwa kawaida sio tatizo kubwa na mara nyingi huleta tu karaha kwa
mtu anayelala karibu na mkoromaji. Hata hivyo kukoroma huko sio tu
kwamba huharibu usingizi wa anayekoroma bali pia huwasumbua na
kuwakeresha wanaolala karibu na mkoromaji. Wale wenye tabia ya
kukoroma, hukoroma kila wanapolala na mara nyingi huchoka wanapoamka, na
watu wa aina hii hushauriwa kumuona daktari na kushauriwa kuhusiana na
tatizo hilo. Lakini kabla hatujaendela mbele ni bora tujue kukoroma hasa
ni nini au hutokea vipi?
Mtu huwa anakoroma pale kunapokuwa na
kitu au sababu yoyote itakayoziba kuingia au kutoka kwa hewa mdomoni na
katika pua. Kuta za koo hutikisika wakati wa kupumua na matokeo yake ni
sauti inayosikika ya kukoroma. Kuingia au kutoka kwa hewa huweza
kuzuiwa na sababu mbalimbali kama vile:
• Kuziba tundu za pua kusiko
kamili ambako husababisha nguvu zaidi zitumike katika kupitisha hewa
kwenye pua wakati mtu akiwa amelala. Kitendo hicho hupelekea nyama laini
za pua na koo zijikusanye na kusababisha mkoromo. Kuna baadhi ya watu
wanakoroma tu kipindi cha allergy (allergy season) au wanapatwa na
matatizo ya sinus. Baadhi ya matatizo kama vile kupinda pua (deviated
septum) au ukuta unaotenganisha tundu za pua na polyps za pua pia huweza
kufanya pua zizibe na kusababisha kukoroma. Watu wengi wanaofanya
operesheni za pua pia hupatwa na tatizo la kukoroma.
• Kuwa na
misuli dhaifu katika koo na ulimi. Misuli au nyama za koo na ulimi
zinapokuwa dhaifu sana hulegea na kuanguka upande wa nyuma wa sehemu
inayopita hewa. Suala hilo hutokea pale mtu anapolala fofofo au kuwa na
usingizi mzito na kusababisha kukoroma.
• Kuwa na misuli minene ya
koo. Hii ni kwa wale watu wanene ambao hata nyama zao za koo pia
hunenepa na kupanuka na suala hilo husababisha kukoroma, Pia watoto
wenye tonsesi kubwa na adenoids baadhi ya wakati hukoroma.
• Kuwa na
kilimi kikubwa ni mojawapo ya sababu zinazosababisha kukoroma. Kilimi
kirefu kinaweza kuzuia koo na pale kinapotikisika wakati hewa inapita
kwa msukumo husababisha kukoroma.
• Sababu nyinginezo zinazoweza
kumsababishia mtu akorome anapolala ni kuwa na umri mkubwa au uzee,
imeshuhudiwa kuwa watu wa makamo na wazee hukoroma, kwani misuli na
nyama za koo huanza kuzeeka na kulegea kadri umri unayoongezeka.
Vilevile wanaume wanakoroma zaidi kuliko wanawake hii ni kutokana na
wanaume kuwa na njia nyembamba zaidi ya hewa kuliko wanawake. Kukoroma
pia kunaweza kuwa ni tatizo la kurithi. Pombe, kuvuta sigara na matumizi
ya baadhi ya dawa pia husababisha misuli ya koo ilegee na hivyo
hupelekea mtu akorome. Kulala vibaya pia husababisha kukoroka kama vile
kulala kichalichali, kwani hufanya nyama za koo zilegee na kuziba hewa.
Je, Dawa ya kukoroma ni nini?
Swali
hilo limeulizwa sana na mimi katika kulijibu ningependa kusema kuwa,
kujua sababu inayosababisha mtu akorome na kuitatua au kuiondoa sababu
hiyo ndiko kunakotibu kukoroma. Sote tunajua adha inayotokana na
kukoroma, na sauti hiyo inavyosumbua hasa iwapo anayekoroma ni mtu wako
wa karibu kama vile mumeo, mwenzi wako au yoyote yule inayekubidi ulale
naye karibu au katika kitanda kimojana hata chumba kimoja. Kukoroma pia
huathiri usingizi wa mkoromaji kwani anayekoroka humbidi aamke mara
kadhaa usingizini akijua au bila kujua kutokana njia zake za hewa
kufunga kwa sekunde kadhaa ambapo usingizi pia hukatika. Wanaokoroma pia
hushindwa kulala vizuri suala linalopelekea asubuhi wawe wamechoka na
kutofanya majukumu yao vyema, na pia wale wanaolala nao karibu hupatwa
na matatizo kama hayo. Vilevile tunapaswa kujua kuwa kukoroma kuna
athari za kiafya za muda mrefu kwa mtu anayekoroma hivyo si jambo la
kufanyia mzaha na ni tatizo ambalo linapaswa kushughulikiwa na
kutatuliwa.
Wataalamu wanatuambia kuwa ili kujua kukoroma kwako
kunasababishwa na nini ni bora ushirikiane na mwenzi wako au yoyote
unayelala naye ili akuchunguze pale unapolala na kujua jinsi mwili wako
unavyokuwa pale unapokoroma. Ni bora aandae orodha na kuchunguza
yafuatayo:
1. Kufunga mdomo na kukoroma kunaonyesha kuwa kuna matatizo ya ulimi.
2. Kufungua mdomo na kukoroma kunaonyesha unaweza kuwa na tatizo katika misuli au nyama za koo.
3. Kukoroma unapolala kichalichali kunaonyesha kuwa pengine kwa kubadilisha namna unavyolala kukoroma nako kunaweza kwisha.
4. Kukoroma wakati unapolala kwa kila mlalo kunaonyesha kwamba tatizo lako ni kubwa na pengine kunahitajia tiba kubwa zaidi.
Iwapo umebadilisha namna unavyolala na haikusaidia, unashauriwa ujaribu yafuatayo: Punguza uzito Safisha njia yako ya hewa. Kuwa na pua iliyoziba hufanya kupumua kuwe
kugumu na kusababisha kukoroma. Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia dawa
za kusaidia kupumua kwa urahisi (nasal decongestants) zinazopatikana kwa
urahisi katika maduka ya dawa. Wacha kuvuta sigara. Lala
mapema na pata usingizi wa kutosha kila mara huku ukijiepusha na kuchoka
sana. Kunyanyua kichwa kwa nchi 4 huweza kupunguza kasi ya kupumua na
kusaidia ulimi na taya kwenda mbele hali ambayo hupunguza kukoroma.
Fanya hilo kwa tumia mito maalum ya kupunguza kukoroma au lala bila mto.
Wataalamu
pia wanasema kwamba unaweza kupunguza kukoroma kwa kutokula baadhi ya
vyakula au dawa kabla ya kulala ambavyo huongeza kukoroma. Vitu hivyo ni
kama vile
. Kutokula mlo mkubwa kabla ya kulala.
. Kutokula vyakula vinavyotokana na maziwa au maziwa ya soya.
. Kutokunywa pombe kabla ya kulala.
. Kutotumia dawa aina ya antihistamines.
. Kutotumia vyakula au vinjwaji venye kafeini.
Vilevile
wanaokoroma wanashauriwa kufanya mazoezi ya koo ambayo ni pamoja na
kuimba, kusoma kwa kurudia rudia voweli (a,e,i,o,u) kwa nguvu kwa
dakika tatu mara kadhaa kwa siku, kuweka ncha ya ulimi chini ya meno ya
mbele na kurudisha ulimi nyuma kwa dakika 3 kila siku au huku mdomo
ukiwa wazi pelekea taya yako upande wa kulia na wacha ibakie katika hali
hiyo kwa sekunde 30. Huku mdomo ukiwa wazi, kaza misuli ya nyuma ya koo
na rudia kitendo hicho kwa sekunde thelathini. Unaweza kutizama kwenye
kioo na kuona jinsi kilimi kinavyokwenda juu na chini.
Iwapo
kukoroma hakutoisha kwa kutumia njia hizo tofauti zilizoelezwa, usife
moyo jaribu kumuona daktari na akupe ushauri wa kitiba kuhusiana na
tatizo hilo. Madakatari wataalamu wa magonjwa ya pua, masikio na koo au
ENT wanaweza kukusaidia zaidi kutatua tatizo hilo. Siku hizi kuna vifaa
mbalimbali vinavyotumiwa mahospitalini ili kuondoa kukoroma kama vile
kifaa kinachowekwa kwenye meno, CPAP, kidude kinachowekwa mdomoni au
hata kufanyiwa operesheni ili kuondoa tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment