Tunapozungumzia
uelewa wa wanafunzi darasani tunakuwa tumeingia katika msitu mpana zaidi wa
majibu, lakini ukweli unabaki kuwa ndani ya darasa linalofundiswa na mwalimu
mmoja hutokea wanafunzi wengine wakaelewa zaidi
na wengine wasielewe kabisa.
Kuna wanafunzi na
baadhi ya wanasayansi wanaamini kuwa kuna binadamu huzaliwa na uwezo mkubwa wa
kuelewa zaidi ya wenzao, huu ni ukweli lakini si wa kuamini sana kwani kipimo cha kuhakikisha kuwa huyu
ameumbwa hivyo hakuna zaidi ya kuangali tu yale ambayo yanatendwa na huyo
anayeitwa ana akili za ziada au za kuzaliwa.
Lakini wakati huo huo
kuangalia ayatendayo mtu au kuangalia uelewa wake darasani hakutoshi kumpa sifa
za kuwa na sababu ya kuwazidi wenzake ambao wameamua tu kutokusoma,
kutomsikiliza mwalimu, kutozingatia wanachoelekezwa au wameharibiwa na masumufu
ya dunia yakiwemo masuala ya mapenzi.
Kwa maana hiyo, hawa
ambao hawaelewi kwa sababu wanasoma huku wanawaza mambo ya kimapenzi au
wanafikiria kwenda muziki au kucheza,
hawawezi kuwekwa kwenye kundi la watu ambao hawakuzaliwa na akili bali
waliojiharibu kwa kukosa kuufahamu ukweli.
Hivyo basi, kuna kila
sababu kwa mwanafunzi kupuuza fikra za kizembe zinazomfanya ajione kuwa
anazidiwa na wenzake darasani kwa sababu yeye hakuzaliwa na akili nyingi. Kila
binadamu mwenye akili timamu kwa mujibu wa tafiti za watalaamu wa masuala ya
ufahamu ana uwezo mkubwa mara 1000 kuliko ule anaoutumia.
Hii ina maana kuwa
kama kuna mwanafunzi anaongoza darasa lenye watu 100, uwezo huo wa kuongoza
anaweza kusonga nao mpaka akafikia kwa watu 1,000 na akifika hapo anaongeza
mara 1,000 tena na tena. Huu ni uwezo wa ajabu sana alionao mwanadamu. Lakini wengi kati
yetu tumeshindwa kusonga mbele mara elfu toka tulipo kwa sababu tumeshindwa
kutumia kipawa chetu na tumeamini uongo kuwa kuna waliopendelewa tangu
wanaumbwa.
Ben Carson mwandishi
mashuhuri na daktari bingwa wa magonjwa ya akili ambaye awali alikuwa akiburuza
mkia darasani aliambiwa na mama yake aitwaye Sanya Carson maneno haya: �you can
do anything they can do, only you can do it better� (Nukuu inapatikana ndani ya
kitabu kiitwacho THINK BIG cha Ben Carson ukurasa wa 7) kwa tafsiri isiyo
rasimi Ben aliambiwa na mama yake kuwa �unaweza kufanya wayafanyayo, lakini
wewe unaweza kufanya zaidi yao�
Mwanamke huyu alidumu
kumwambia mwanae kuwa ni bora zaidi ya wengine na kumtaka aongeze bidii kila
siku ili afikie lengo. Ben aliaamini aliyokuwa akiambiwa na kwa makusudi
aliamua kujibidisha na hatimaye kufikia
kiwango cha kuwa msomi mwenye kuheshimika ulimwenguni.
Kimsingi kuna watu
wengi ambao walipuuza kauli za kujiona duni na kufanikiwa katika mambo
waliyokusudia kuyafanya. Huu ni ushahidi kuwa hajaumbwa mwanadamu kuwa wa
mwisho darasani bali matokeo ya kushindwa ni lazima yapewe kwanza sababu za
uzembe na maumbile yawe ni ya mwisho kufikiriwa. Ufuatao ni muongozo wa
kumuwezesha mwanafunzi kusoma na kuelewa vema.
-Kumzingatia mwalimu
Wanafunzi wengi
wanashindwa kufikia uelewa wa juu kwenye masomo yao kwa sababu hawawi makini wanapofundishwa
darasani na waalimu wao. Kitendo cha kuweka mawazo nusu darasani na nusu nje ni
kujiwekea kizingiti cha kuelewa kinachofundishwa.
Ni muhimu kwa
mwanafunzi kama nilivyosema awali kwamba
ampende mwalimu wake na aone furaha kumsikiliza anapofundisha. Itakuwa vigumu
kwa mwanafunzi kuelewa anachofundishwa kama
anayemfundisha anamchukia eti tu kwa sababu jana alimwadhibu au alimfokea.
Ifahamike kuwa,
msingi mkubwa kabisa wa mwanafunzi kuelewa somo lo lote ni kuelewa
anachofundiswa moja kwa moja toka kwa mwalimu wake. Kitendo cha kutoka darasani
bila kujua kilichofundishwa ni jambo la hatari kwa maendeleo ya mwanafunzi
kimasomo.
Inashauri kuwa
mwanafunzi anapoingia darasani anatakiwa kuwa makini na kufuata anachoongea
mwalimu wake neno kwa neno, huku akinoti anachoelewa na asichoelewa, ili kama ni msaada wa kueleweshwa aombe muda mfupi baada ya
mwalimu kumaliza kufundisha.
Kurudia notisi
Mara baada ya
mwanafunzi kufundishwa na kuelewa, anatakiwa akifika nyumbani siku hiyo hiyo
arudia yale aliyosoma kwa kujikumbusha alichosema mwalimu wake. Hii itamsaidia
zaidi kuifanya akili itunze kumbukumbu ya somo alilofundishwa na hivyo kumfanya
mwanafunzi kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujikumbusha au kukumbuka
atakapokuwa akifanya mtihani.
Haifai kwa mwanafunzi
kurejea nyumbani na kufunika madaftari bila kujikumbusha au kurudia siku mbili
baada ya kufundishwa, kufanya hivyo kunaweza kutoa nafasi kwa akili kuyatupa
aliyofundishwa kutokana na wingi wa masomo au mambo aliyoelekezwa kwa siku
mbili au wiki nzima.
-Kufanya uchambuzi
Ni wajibu wa mwanafunzi
kufanya uchambuzi wa notisi zake za shule kwa kuandika mchanganuo wenye maneno
machache ya msingi kwenye daftari jingine au karatasi. Kufanya hivi kutamsaidia
kupunguza wingi wa maneno ya kuhifadhi akilini hasa kwa wanafunzi wa ngazi za
chini ambao wengi wao hutumia mbinu za kukariri ambazo ni hatari kwa kusahau
haraka.
Kwa mfano, wanafunzi
anapofundishwa kuhusu ubadhilifu wa pesa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania
�BoT� kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje maarufu kama EPA na kupewa takwimu na
mlolongo mzima ulivyokuwa, anachotakiwa kufanya yeye ni kunyambua mambo ya
msingi ambayo yatamuongoza katika kujibu maswali, kama
kuwajua wahusika, mwaka wa skendo, kiasi kilichoibwa na kilichorudiswa.
Mambo hayo machache
akiyafahamu yatamfanya awe na uwezo wa kulielezea jambo hilo kwa kina mbele za watu na kuonekana
mwenye ufahamu wa kutosha, lakini pia atajihakikishia uwezo wa kukabili jaribio
au mtihani wo wote utakaokuja na swali la EPA.
-Kujipima uelewa
Kumsikiliza mwalimu,
kurudia notisi na kufanya uchambuzi kunaweza kusitoe picha sahihi juu ya uelewa
wa mwanafuzni katika yale anayosoma pamoja na uwezo wake wa kukumbuka
aliyojifunza. Mwanafunzi ili ajipime kama akili yake imenakiri vema anatakiwa
kutenga siku ndani ya wiki kwa kujitungia mitihani kutoka kwenye daftari zake,
kuifanya na kujisahihisha mwenyewe.
Hii itampa mhusika
ufahamu wa kujua ni eneo gani kaelewa zaidi ya jingine na hivyo kujituma zaidi
sehemu ambayo hajaelewa kwa kuuliza tena kwa mwalimu au kwa wenzake ambao
anadhani wana ufahamu mkubwa kuliko yeye. Ni vibaya kusoma bila kujipima uwezo.
Itapendeza kama wanafunzi watakuwa wakifanya mitihani ya kujipima kwenye
vikundi kila wiki.
-Kukuza ufahamu
Ziko njia nyingi za
mwanafunzi kukuza ufahamu wake lakini muhimu zaidi ni kusoma vitabu, kusikiliza
habari kupitia vyombo vya mbalimbali na kushiriki katika mijadala ya wazi yenye
kujadili masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Mwanafunzi hawezi
kukuza ufahamu kama hajui masuala ya jamii yake, siasa za ulimwengu na hali ya
uchumi wa ndani na nje na hayo yote yanapatikana kwa kusoma. Jambo jingine la
msingi ni kwa mwanafunzi kuepukana na aibu ya kujieleza mbele za watu. Njia
pekee ya kuhifadhi kumbukumbu ya kile alichosoma na kuwa na tabia ya kuwaeleza
wengine.
Kwa mfano, kama
mwanafunzi atakuwa amefungua mtandao wa inteneti na kusoma habari za kupanda
kwa uchumi wa Marekani anatakiwa awaeleze wenzake alichojifunza, vivyo hivyo
atakaposoma vitabu au kutazama filamu. Kujua jambo na kutokulitenda ni ujinga
sawa na mtu ambaye hajui kabisa. Aibu ya kuzungumza mbele za watu haifai ni
vema mwanafunzi akajiamini na kujizoeza kueleza anachokifahamu mbele za watu.
No comments:
Post a Comment