Jifunze kusamehe na kusahau uishi zaidi
UKITAKA kuwa na maisha marefu na yenye amani, mojawapo ya mambo ambayo unatakiwa kufanya ni kupenda kusamehe na kusahau.
Kama wewe ni mtu wa kuweka moyoni, amini ninachokwambia subiri
kuingiwa na magonjwa mabaya kama ya moyo, figo na mengine yanayohusiana
na mfumo wa damu kwa ujumla.
Kitaalamu ni hatari zaidi kuweka mambo na kisha kuyarudia, ni kwa
sababu unapokuwa na hasira au chuki, mapigo ya moyo yanakwenda kwa kasi
au pengine yakaenda kidogo kidogo tofauti na ilivyo kawaida.
Matokeo ya hali hii ni kwamba damu inaweza ikawa inaingia kwa wingi
zaidi kwenye moyo au pengine ikawa inaingia kidogo zaidi na hapo huwa ni
mwanzo wa matatizo katika mwili.
Ni nzuri ndugu yangu kufahamu kuwa matatizo ni sehemu ya maisha,
pekee wasio na shida za dunia hii ni wale ambao wamekufa, lakini kama
uko hai, kama si mapenzi, basi mambo ya kibiashara, kazi au hata jirani
ama ndugu na wazazi wanaweza kuwa ni kero kwako.
Ni ngumu kufikiri kwamba unaweza kuishi bila kuwa na vikwazo
vyovyote; ndio nasema ni suala la msingi kuwa mwangalifu unapokuwa na
matatizo kwa kuelewa kwamba shida tumepatiwa wanadamu, kwa hiyo
zinapokuwepo ni kuangalia nini cha kufanya ili mambo yaweze kuwa mazuri.
Kufikiria kuachana kwa sababu kuna hali ya kutoelewana, ni ishara
kuwa kichwa chako hakina akili nzuri sana tunapolima shamba na kisha
tukaona magugu yanaota kwa kasi, tunachokifanya huwa ni kutafuta dawa
kwa ajili ya kuua magugu ili mimea ambayo tumepanda iote vizuri, sasa
kwanini tunapokuwa na shida kwenye ndoa mnafikiria kuachana? Sio sawa.
Cha msingi kama nilivyosema angalia chanzo hasa cha tatizo ni nini na nini cha kufanya ili muwe wanandoa wenye uhusiano mzuri.
KWA WATU AMBAO SI WANANDOA
Ni ujinga mkubwa kukubali kununua gari ambalo tayari linafuka moshi ndio
kusema kwamba kama hamjaoana na tayari mna migogoro, ni vizuri kupata
muda wa kutafakari zaidi kama ni lazima kuendelea au la, lakini si jambo
zuri sana kuingia kwenye ndoa kama kwenye uchumba tu hakuna amani ya
kutosha.
Ni makosa kuamini kwamba leo nanunua gari bovu, halafu ukafikiri
kwamba kesho nitapata fundi wa kulitengeneza hatimaye likawa sawasawa.
Kama mna hiyo imani ni vizuri basi kuhakikisha kwanza mnaiponya migogoro
iliyopo na kupeana muda zaidi, kabla ya kuoana.
KWA WANANDOA TU
Kama nilivyosema, kwa wasio na ndoa, si hekima sana kumsamehe mtu ambaye
tabia zake zinaonekana kuwa mbaya; uchumba ni wakati wa kuangaliana,
kama unaona mtu hafai, hata kama amefikia hatua gani, mpe nafasi ya
kuangaliana zaidi. Usiwe na haraka katika maisha ndugu yangu, utajuta.
Katika ndoa ambacho unatakiwa kufanya ni kujifunza namna ya kuishi pamoja, kusamehe na kusahau pale mnapokoseana.
Hata katika dini tunafundishwa kwamba ni furaha ya Mungu kuona watu
wanasameheana, kiasi kwamba baadhi ya vitabu vitakatifu vinaandika
kwamba Mungu huwa anakuwa nao wale ambao wanasamehe.
Katika maisha mapya utatakiwa usamehe na kusahau kwa ajili yako
mwenyewe, ili kuomba kwako kusizuiliwe na baraka zako zisizuiliwe. Ndio
kusema kwamba kama husamehe, ni ngumu nawe Mungu kukusamehe makosa yako.
Kuna wengine katika ndoa unaweza kusikia anakwambia nimekusamehe,
halafu siku inayofuata unamsikia tena akisema kwamba aaah nimekusamehe
lakini kwa kweli jambo ulilonitendea ni baya sana.
Ndugu yangu jambo moja la msingi sana ambalo ningependa ubaki nalo ni
kwamba yuko wapi ambaye hatakukwaza kwa asilimia 100? Hayuko, kwa maana
hiyo ni vizuri kujifunza namna ya kuishi na uliyenaye kabla bado hauko
kwenye ndoa, pata muda wa kumjua kwa kina kabla ya kuamua. Mkishaingia,
mnapaswa kuendelea milele. Mungu awabariki sana.