NJOMBE

NJOMBE

Sunday, July 15, 2012

Clinton amzuru Mursi Misri

Waziri wa mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, yuko nchini Misri kukutana na kiongozi mpya, rais kutoka chama cha muslim brotherhood, Mohamed Morsi.
Hillary Clinton katika ziara yake ya karibuni barani Asia

Miaka iliyopita, waziri mmoja wa mashauri ya nchi za nje wa Marekani, alitangaza Marekani haizungumzi na muslim brotherhood, na daima haitafanya hivo.
Sasa, serikali ya Rais Obama, imefanya haraka kuwasiliana na rais mpya wa Misri wa muslim brotherhood, Mohamed Morsi.
Marekani imekubali kuwa ukweli hauepukiki, na inajaribu iwezavyo.
Bila ya shaka Hillary Clinton atataka kupata ahadi ya Rais Morsi, juu ya siasa za Misri kuhusu mambo ya nje na ya ndani ya nchi.
Serikali ya Marekani inataka kuona demokrasi na haki za kibinaadamu zinalindwa nchini Misri.
Kwa upande wao, muslim brotherhood wamesisitiza mara kadha kwamba hawataki kutengwa na ulimwengu, hasa kwa sababu nchi hiyo inategemea sana biashara za kimataifa na utalii.

CHADEMA yalitikisa Bunge

WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) sasa wamedhihirisha wazi kuwa kero kwa uongozi wa Bunge.
Hali hiyo imedhihirika waziwazi juzi baada ya kiti cha Spika kuchukua uamuzi mzito dhidi ya wabunge wawili machachari wa CHADEMA, Tundu Lissu na John Mnyika.
Juzi kiti cha Spika kilichukua uamuzi mzito dhidi ya hotuba kali ya kambi ya upinzani ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa bungeni mjini hapa na mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani, ambaye pia ni Mbunge wa  Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lisu na kusababisha kiongozi huyo kupelekwa kwenye  Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.
Hatua hiyo ilifikiwa  baada ya mnadhimu huyo kukataa kufuta maneno aliyoyaandika na kuyasoma katika hotuba yake ambayo yalikuwa yakieleza kuwa baadhi ya majaji wanaoteuliwa hawana uwezo, hivyo wanashindwa kufanya kazi zao ipasavyo.
Imedaiwa kuwa maneno hayo ni ya kashfa kwa majaji na serikali kwa ujumla.
Awali baada ya kumalizika kwa hoja za wabunge waliokuwa wakichangia mjadala wa bajeti ya Sheria na Katiba iliyojadiliwa kwa siku moja na kupitishwa jana. Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Muhagama, alimpa nafasi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ili kuzungumza kuhusiana na kauli zilizotolewa na kiongozi huyo wa kambi ya upinzani.
Mwanasheria huyo alieleza kuwa ana wajibu wa kuwaelekeza mawakili popote walipo na hasa walioko bungeni kufuata na kusimamia misingi ya taaluma hiyo bila kuathiri wadhifa wao wa ubunge.
“Kwa kweli nimefedheheka sana na maneno yaliyotolewa bungeni leo na jambo la kwanza ni maoni ya msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kuhusiana na bajeti ya Katiba na Sheria,” alisema Werema.
Aidha, Werema alitumia nafasi hiyo kumtaka mnadhimu huyo wa kambi ya upinzani kufuta maneno yake hayo ambayo alisema kuwa hayana ukweli wowote kwani majaji wote wanaoteuliwa wana uwezo mkubwa na wanateuliwa kwa kufuata misingi na taratibu husika ambazo zimewekwa za kuwapata majaji.
“Kauli hiyo ni ya ajabu sana na sikutegemea mtu kama Lisu unaweza kuzungumza kauli kama hiyo  na kuwataja watu ambao hawana uwezo wa kuingia humu ndani ya Bunge kujitetea huku ukijua dhahiri kuwa kanuni zetu zinakataza kuwataja watu wa aina hiyo.
“Mwenyekiti namtaka mbunge afute kauli yake hiyo na vinginevyo kama akikataa basi inabidi apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baada ya Mwanasheria Mkuu kutoa muongozo huu kwa mwenyekiti wa Bunge, shughuli za kupitisha bajeti ya Katiba na Sheria ziliendelea na zilipomalizika mwenyekiti alimtaka afute maneno yake kama alivyoagizwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baada ya kukataa kufuta mwenyekiti huyo alisema jambo hilo analipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili liweze kuchukuliwa hatua.
“Naiagiza kamati hiyo ipitie mwenendo wa shughuli zote kwa siku ya juzi, pamoja na “Hansard’’ na mtiririko wote wa miongozo iliyotolewa na kulishauri Bunge nini lifanye katika hatima ya jambo hilo, kwa kufanya hivyo tutajenga heshima ya Bunge katika kufanya maamuzi na kushughulikia mambo mengine,” alisema Mhagama.
Mbali na hilo, mwenyekiti huyo alisema kwenye ukurasa wa tisa wa hotuba ya kambi ya upinzani Lissu alitamka kuwa kuna baadhi ya majaji ambao waliteuliwa na rais hawana uwezo na hawakufanyiwa usaili.
Mwenyekiti huyo alisema kauli hiyo inaingilia mambo ya mhimili mwingine ambao ni Mahakama, hivyo ni kinyume cha kanuni za Bunge.
Alisema pia kwa kuondoa maneno hayo kutalinda heshima ya  uteuzi wa majaji uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni pamoja na kuwatendea haki majaji hao kwa kutoendelea kuvunja kanuni namba 64 kwa kujadili mwenendo wa majaji hao ndani ya Bunge.
Baada ya Mhagama kutoa nafasi hiyo Lissu alianza kwa kukilaumu kiti kwa kukiuka kanuni na kudai kuwa wanaotaka kutoa maneno hayo katika hotuba yake hawakuzingatia kanuni.
“Mwenyekiti kwa heshima kubwa sana nimeshangazwa sana na utaratibu ambao unataka kutumika hapa, kwani haupo katika kanuni za Bunge na haupo mahali popote,” alisema.
Lisu alisema kama  kuna jambo ambalo mtu hakulipenda ama kama amesema kitu ambacho si cha kweli alipaswa kuomba utaratibu kwa mujibu wa kanuni 68 (1) ili akae na anielekeze kama nilichosema kipo kinyume na utaratibu na si vinginevyo.
Mnadhimu huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa kama alisema uongo utaratibu wa kanuni upo kwenye kanuni ya 63, ambayo inazungumzia kutosema uongo bungeni na hatua za kuchukuliwa dhidi ya mtu huyo na si kutakiwa afute bila kufuata kanuni kama ilivyo hivi sasa.
“Sasa natakiwa nifute tu bila kufuata kanuni, hapa tutagombana sana na kwa kitendo hicho cha kuniambia nifute bila kiti chako kufuata kanuni ni kuniambia mnataka kukanyaga kanuni za Bunge hili, hivyo mimi sitakuwa tayari,’’ alisema Lissu.
 Kwa upande wa Mnyika, Naibu Spika Job Ndugai alilazimika kuagiza mbunge huyo afikishwe katika kamati hiyo kwa madai ya kutoa tuhuma za uongo dhidi ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba akidai kuwa anakabiliwa na tuhuma za EPA.
Agizo hilo hata hivyo lilipingwa vikali na Mnyika pamoja na kambi ya upinzani, likihoji maamuzi ya kiti hicho juu ya suala hilo.
Mara kadhaa wabunge wa CHADEMA na wale wa NCCR Mageuzi, wameshambuliwa vikali na wabunge wa CCM, huku ikidhihirika kutetewa kwa nguvu kubwa na kiti cha Spika.
Mathalani, wabunge wa CCM wamekuwa wakishambulia wale wa upinzani kwa maneno ya kudhalilisha, lakini kiti cha spika kimekuwa mara kadhaa kikifumbia macho, kinyume cha hali inapokuwa hivyo kwa wabunge wa upinzani.
Itakumbukwa kwamba wakati Mnyika akichukuliwa hatua hiyo, hadi sasa mwongozo wa spika kuhusiana na kauli ya waziri mkuu kulidanganya Bunge, na lile sakata la Zitto dhidi ya Mkulo havijachukuliwa hatua yoyote kwa mwaka sasa.
Chanzo Mtanzania Daima

Mkurugenzi Mtendaji, vigogo TANESCO wasimamishwa kazi


BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mhandisi William Mhando na wafanyakazi wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka unaoikabili menejimenti hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Victor Mwambalaswa, ambaye ni Mbunge wa Lupa (CCM), ilisema kuwa Julai 13 bodi ilikutana katika kikao cha dharura na kujadili masuala mbalimbali ikiwamo tuhuma hizo.
Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Jenerali Robert Mboma (Mstaafu), ilisema kuwa kutokana na tuhuma hizo kuwa nzito, ni vema ukafanyika uchunguzi huru ambao unaanza mara moja kwa kumtumia mchunguzi huru.
Iliwataja wengine waliosimamishwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi, Harun Mattambo.
Ilisema kuwa pamoja na hatua hizo, bodi itahakikisha shughuli za kiutendaji na uendeshaji wa shirika hilo zinaendelea kama kawaida.
Hata hivyo, kusimamishwa kwa vigogo hao kumezua tafrani, huku kukiwa na habari kwamba hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni kuficha siri nzito ya kukwama kwa shirika hilo.
Habari zimedai kuwa kumsimamisha kazi Mhando kunatokana na kile kinachosemwa ‘jeuri’ yake ya kukataa maagizo ya wakubwa ambao wamekuwa wakitaka kuliendesha shirika hilo kisiasa zaidi badala ya kukubaliana na uhalisia.
Wakati Mhando akidaiwa kuhujumu shirika, habari zinasema kuwa yeye mwenyewe ameelekeza lawama kwa serikali na watendaji wake wakuu kwa kulinyima shirika hilo pesa ilizoahidi kwa ajili ya miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme, na kulizuia shirika hilo kuuza umeme kwa faida, kwa sababu za kisiasa.
Inasemekana hatua dhidi ya Mhando inatokana na woga wa waziri na katibu mkuu juu ya mjadala mkali unaotarajiwa kuibuka bungeni wakati wa kujadili bajeti ya wizara yao. Mhando anatolewa kafara kisiasa, lakini taarifa zinasema naye amejibu barua ya katibu mkuu kueleza jinsi asivyohujumu shirika hilo.

Libya ina maelfu ya wafungwa

Wakuu wa Libya wanachagizwa kuchukua dhamana ya watu wanaokisiwa kuwa 5000, ambao wanazuwiliwa na makundi ya wanamgambo bila ya kufanyiwa mashtaka rasmi.
Gereza nchini LIbya
Shirika la kutetea haki za kibinaadamu, Human Rights Watch, linasema limeorodhesha kesi za watu ambao wameadhibiwa sana wakati wanazuwiliwa na wapiganaji hao wa zamani.
Human Rights Watch inasema, wengi kati ya wale wanaozuwiliwa ni wale waliokuwa wafuasi wa kiongozi wa zamani wa Libya, Moammar Gaddafi, kabla ya kupinduliwa mwaka jana.
Wakuu wa Libya wakitakiwa wawe wameshapeleka kesi zote hizo mahakamani, ilipofika tarehe 12 Julai.

Saturday, July 14, 2012

Mwandishi afungwa jela miaka 18 Ethiopia


Mwandishi Eskinder Nega afungwa miaka 18 Ethiopia
Mwanahabari maarufu ambaye pia ni mwandishi wa Blogi amefungwa jela miaka 18 nchini Ethiopia kwa madai ya kukiuka sheria ya ugaidi.
Eskinder Nega na wenzake 23 walipatikana na hatia mwezi uliopita.
Walikamatwa kwa madai ya kuwa na uhusiano na kundi moja la upinzani lililo na makao yake Marekani kwa jina Ginbot Seven.
Serikali ya Ethiopia inadai kuwa kundi hilo ni la kigaidi.
Mahakama hiyo ya Addis Ababa pia ilimfunga jela maisha mwanaharakati wa upinzani,Andualem Arage.
Kutokana na kazi yake ya uwana-habari na kuandika Blogi, Mwezi wa May, Eskinder alipewa tuzo maarufu la kimarekani la Pen America's Freedom to Write.
Makundi ya kutetea haki za kibinadamu zimekuwa ikiilaumu serikali kwa kubuni sheria hiyo ya kukabiliana na ugaidi yakisema sheria hiyo haifai.
Siku ya Ijumaa Mwanahabari ,Eskinder na mwanachama wa chama cha upinzani cha Unity for Democracy and Justice party walikuwa mahakamani kuhukumiwa.
Washukiwa wengine 16 waliopatikana na hatia mwezi wa Juni wako ukimbizini.
Walipokuwa wakiingia mahakamani wawili hao waliwapungia mikono jamaa zao na marafiki pamoja na maafisa wa kibalozi waliokuwemo ndani.
Eskinder alikamatwa mwezi wa Septemba mwaka jana baada ya kuandika makala iliyokuwa ikiilaumu serikali ya Ethiopia kwa kukamata wapinzani wake kwa kutumia sheria ya ugaidi.
Miongoni mwa watu ambao wamekamatwa chini ya sheria hiyo ni msanii na mcheza filamu maarufu nchini Ethiopia, Debebe Eshetu ambaye ni mkosoaji mkuu wa serikali.

Kamanda wa Afghanistan auliwa harusini

 
Mwanasiasa mmoja maarufu nchini Afghanistan ameuliwa na mtu aliyejitolea mhanga, kwenye harusi ya mtoto wake wa kike.
Ahmed Khan Samangani
Watu zaidi ya ishirini waliuwawa kwenye mripuko wa bomu na wengine wengi kujeruhiwa.
Mwanasiasa huyo, Ahmad Khan Samangani, alikuwa akiamkia wageni kwenye harusi, pale mtu aliyekuwa na bomu alipomkumbatia, na kuripua bomu.
Bwana Samangani kutoka kabila la WaUzbek, aliwahi kuwa kamanda wa wapiganaji.
Baadae akachaguliwa kuwa mbunge, lakini aliendelea kuongoza kundi kubwa la askari waliokuwa na silaha.
Msemaji wa Taliban, alikanusha kuwa wao walihusika na shambulio hilo.

Friday, July 13, 2012

THE INTERNATIONAL MODEL OF THE YEAR 2012 COMPETITION - WASHINGTON ( DMV )- SATURDAY JULY 21 :

MEET TOP 10 HOT MODELS COMPETING FOR THE CROWN,CELEBRITY JUDGES AND CELEBRITY PHOTOGRAPHERS,TICKETS STARTS @ $10 - 25,ALL TICKETS INCLUDES (PRE-NETWORKING PARTY FRM 7-8PM,THE RUNWAY COMPETITION FROM 8-10:30PM & THE AFTER PARTY FRM 10:30 -2AM,ALL AT THE ROCKVILLE ROOFTOP,FOR INFO OR AND TICKETS CALL "DMK"

MARIDADI FASHION SHOW CASTING IN DAR ES SALAAM... KAMA UNAWEZA JIUNGE.

DAR ES SALAAM get ready!Gyverlatrend modelling agency casting for Maridadi fashion show is this Saturday ( 14th July 2012 ) at SLIPWAY - The Terrace from 10am - 3pm. Male and Female models are welcomE

Thursday, July 12, 2012

Zaidi ya watu 50 wateketea Baharini


Watu 54 wamefariki dunia wakati wakijaribu kuvuka bahari kutoka Libya kwenda Italia kwa kutumia boti la mpira wa kujaza pumzi, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi.
Mtu pekee aliyenusurika balaa hilo, aliyeokotwa na wavuvi kutoka Tunisia,amesema kuwa wenzake walizama kutokana na kiu baada ya kusafiri kwa zaidi ya siku kumi na tano baharini.
Ameliambia shirika la UNHCR kuwa walikaribia pwania ya Italia lakini wakasumbuliwa na mawimbi makali yaliyowasukuma hadi boti lao lilipoishiwa na pumzi.
Inasadikiwa kuwa wengi wa watu hao ni kutoka Eritrea.
Manusura ambaye ni raia wa Eritrea pia, aliokolewa na wavuvi wa Tunisia nje ya pwani ya Tunisia na kwa wakati huu anatunzwa kwenye hospitali ya nchini Tunisia.

Aliliambia shirika la UNHCR kuwa kundi la watu 55 liliondoka Libya mwishoni mwa mwezi Juni.
Manusura huyu aliendelea kumfahamisha msemaji wa Umoja wa Mataifa Laura Boldrini kuwa "matatizo yalianza punde baada ya kuvua nanga, na kwa bahati mbaya hatukuruhusiwa kuchukua hata chupa moja ya maji ya kunywa, kwa hiyo tulipokosa njia na mwendo wetu kuendelea watu wakaanza kujihisa wagonjwa na kufariki kutokana na kukosa maji.
According to the UNHCR, around 170 people have died this year trying to reach Europe from Libya.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wakimbizi,UNHCR limesema kuwa hadi watu 1,300 wamefanikiwa kuvuka hadi Italia kupitia bahari tangu kuanza kwa mwaka huu 2012.
Raia wengi wa Eritrea hujaribu kila njia ili kufika sehemu yoyote ya Ulaya au Israil kutafuta maisha bora.
Wakosoaji wanasema wanaikimbia serikali dhalimu inayowakandamiza, umasikini na kulazimishwa kujiunga na Jeshi la Taifa wanapotimizia umri wa miaka 40.

Umoja wa Mataifa waapa kulinda Goma

Majeshi ya Umoja wa Mataifa yanaelekea Goma
Jeshi la kulinda usalama la Umoja wa Mataifa linapelekwa katika mji wa Goma ili kuulinda.
Balozi wa Umoja huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema watahakikisha kuwa mji huo hautekwi na waasi wa M23.
Balozi huyo ,Roger Meece amesema jeshi hilo pia litawalinda raia kutokana na waasi hao.
Kwa wakati huu kuna taarifa kwamba waasi hao wa M23 wanaukaribia mji huo uliyo mashariki mwa Congo.
Wakati huo huo , vyanzo vya habari vimeiambia BBC kuwa jeshi la Congo limekomboa miji miwili ambayo hivi karibuni ilikuwa imetekwa na waasi.
Lakini waasi hao wa M23 wamesema kuwa hawana haja ya kuuteka mji wa Goma bali lengo lao kubwa ni kujadiliana na serikali.
Serikali ya Joseph Kabila na Umoja wa Mataifa imekuwa ikidai kuwa Rwanda inawasaidia waasi wa Congo. Hata hivyo Serikali ya Paul Kagema imekanusha madai hayo.
BBC imefahamishwa kwamba majeshi ya Congo yameonekana yakiingia mji muhimu wa Rutshuru ulio kilomita 70 kaskazini mwa Goma.
Nao mji wa Kiwanja, ambao uko kilomita 20 kaskazini na ambao pia ulikuwa umetekwa na waasi wa M23 nao pia umekombolewa.
Waasi hao ambao walianza vita mwezi wa Aprili waliamua kujiita M23 kufuatia mkataba waliotia saini tarehe 23 Machi . Hata hivyo mkataba wenyewe uliporomoka.
Siku ya Jumanne kiongozi wa waasi hao aliambia BBC kwamba watajificha katika maeneo ya milima hadi serikali ikubali kujadikiana nao . Kiongiozi huo alisisitiza kwamba hawana haja ya kuteka maeneo zaidi ya Congo.
M23 linaungwa mkono na Jenerali mtoro Bosco Ntaganda, ambae anatakikana na mahakama ya uhalifu wa kimataifa -ICC.
Jenerali Ntaganda ni M'tutsi sawa na wakuu wengi wa serikali ya Rais Kagame wa Rwanda.

Wednesday, July 11, 2012

KUELEKEA KATIBA MPYA NA SISI TUIGE YA UFARANSA NINI SOMA MAPINDUZI 1789


Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 yalikuwa aina fulani ya maasi ya wanaokandamizwa na kunyonywa, dhidi ya maisha duni, magumu na yasiyovumilia miongoni mwa wananchi.

Baadhi ya mambo yaliyochochea harakati na hatimaye mapinduzi, yaliyozaa moja ya katiba za kwanza bora kabisa duniani, ni pamoja na mazingira tete ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na mchango wa wanaharakati wasomi walioiamsha jamii, kama inavyotokea leo hapa kwetu.


Serikali ya Ufaransa, ilijengeka juu ya utawala wa Mfalme mwenye mabavu (absolute monarch). Licha ya kukua kwa mawazo mapya na mwamko juu ya utawala bora na haki za binadamu, bado Mfalme alijiona ndiye chanzo cha mamlaka yote. Alizoea kujitapa kwa kusema: “Mimi ndiye Taifa, na Taifa ndilo mimi”.


Kufikia nusu ya pili ya karne ya 18, ufalme ulikithiri kwa rushwa, udhaifu mkubwa kiutendaji na Taifa kukosa mwelekeo.


Nchini Ufaransa, kila mwananchi aliwekwa kwenye kundi la kitabaka, maarufu kama estate. Tabaka la kwanza na la juu kabisa lilikuwa la makasisi wa kanisa, wakiwamo ma-askofu, maparoko na viongozi wengine wa kanisa. Hawa hawakuzidi 100,000 kwa idadi, katika nchi ya watu 25,000,000 wakati huo. Walikuwa na upendeleo maalumu katika jamii, kama vile kusamehewa kodi zote, kutoshitakiwa na walikuwa matajiri kupindukia.


Tabaka la pili lilikuwa la Wafaransa kutoka familia zenye nasaba bora na maarufu. Kama ilivyokuwa kwa wale wa tabaka la kwanza, hawa nao walikuwa matajiri, walisamehewa kodi; walishika nafasi za juu serikalini na jeshini. Waliposhitakiwa mahakamani, waliweza kuchagua wao wenyewe mahakimu wa kusikiliza na kuhukumu kesi zilizowakabili.


Tabaka la mwisho, lilikuwa tabaka la tatu lililojumuisha wananchi wengine wote, wakiwamo wafanyabiashara, wanasheria, madaktari, wakulima wa kati na wadogo na wafanyakazi.


Zaidi ya asilimia 80 ya Wafaransa waliishi vijijini kwenye vishamba vidogo vidogo kwa kuwa karibu ardhi yote ilimilikiwa na kanisa. Hawa walichakaa kwa kodi lukuki walizotozwa na serikali ambazo tabaka la kwanza na la pili hawakulipa.


Walitozwa kodi ya kanisa (tithe), ambayo ilikuwa moja ya kumi ya mapato yote, walitozwa kodi ya ardhi (taille) na walitozwa kodi ya kichwa (capitation).


Walilipa pia kodi ya mapato (vingtiene), kodi ya chumvi (gabelle ) na walijitoa nguvu kwa shuruti kujenga barabara za Mfalme kila wiki (corvee) na kodi nyinginezo.


Ukiangalia hali ilivyo nchini kwetu sasa ni kama tunapita njia hiyo ya matabaka kujengeka mithili ya Ufaransa ya kale, huku tabaka la mwisho, la wakulima na wafanyakazi likionja adha ya kodi lukuki na huduma duni lakini za gharama kubwa (maji, umeme, tiba, bei duni za mazao).


Kufikia mwaka 1788, jamii ya walalahoi iliuona utawala wa Mfalme Louis wa XVI kuwa usio na manufaa kwao na uliopitwa na wakati. Maswali matatu yalitawala katika jamii wakati huo: Ni kwa namna gani utawala huo wa mabavu ungefikia mwisho katika nchi isiyo na katiba? Namna gani tabaka hizo tatu zingeweza kushirikiana kuuondoa madarakani kwa njia ya kura? Tabaka hizo zitakaaje na kupiga kura?


Mei 5, 1789, Bunge Kuu la Ufaransa (The Estates General) la tabaka zote tatu, liliketi mjini Versailles, kuzungumzia namna ambavyo katiba ya nchi ingeweza kupatikana ili kukabiliana na madaraka makubwa ya Mfalme.


Wakati wabunge kutoka tabaka la tatu walitaka tabaka zote tatu zikae kwa pamoja na kupiga kura kila “kichwa” kura moja, tabaka mbili za kwanza, kwa kuhofu kuzidiwa kura na tabaka la tatu (lililokuwa na wawakilishi mara mbili ya tabaka mbili za kwanza) na kuhatarisha maslahi yake, zilitaka kila tabaka lipige kura peke yake na kutoa matokeo.


Kama tabaka la kwanza na la pili yangepiga kura juu ya kuwa au kutokuwa na katiba kwa lengo la kulinda maslahi yake, tabaka la tatu lingeshindwa kwa tabaka mbili kwa moja (2 – 1). Hapo bunge likaendelea kukaa bila suluhu juu ya jambo hili.


Baada ya kuchoshwa na udhalimu wa tabaka la kwanza na la pili; Juni 17, 1789, wabunge wa tabaka la tatu walichukua uamuzi mgumu: walijitangaza kwa nguvu kuwa wao ndio bunge pekee la Ufaransa.


Huku wakiwa wamefungiwa milango wasiingie bungeni, wabunge hao walikusanyika kwenye kiwanja cha mpira na kuapa kutotawanyika hadi hapo watakapoipatia Ufaransa katiba. Kiapo hiki maarufu kinajulikana kama The Tennis Court Oath. Hapa Mapinduzi ya Ufaransa yakawa yamekwishaanza.


Kuona hivyo, na kwa hofu kuu juu ya nguvu ya umma kuanza kufanya kazi yake, Mfalme Louis wa XVI aliitisha haraka kikao cha tabaka zote tatu na kuagiza zikae na kupiga kura kila tabaka kivyake; lakini tabaka la tatu na baadhi ya wabunge kutoka matabaka mawili ya kwanza, walikataa kutii amri.


Mmoja wa wabunge wa tabaka la tatu, Count Mirabbeau, alisimama na kunguruma: “Tupo hapa kwa matakwa ya watu; ni singe (bunduki) pekee zitakazotutoa hapa, vinginevyo hatutoki”.


Kwa ushauri wa mke wake Marie Antoinnete, Mfalme Louis wa XVI alituma jeshi kuvunja bunge. Lakini, kwa mshangao wa kila mtu, askari walipofika eneo walipokusanyika, walitupa silaha na kuungana na “waasi” hao, huku ghasia na maandamano yakizidi kupamba moto mitaani kuwaunga mkono. Siku mbili baadaye, viongozi wa dini na wale wenye nasaba bora, waliungana na walala hoi hao.


Juni 27, 1789, huku akiwa amejawa hofu, Mfalme Louis wa XVI alisalimu amri na kuagiza wabunge wa tabaka zote tatu kukutana. Kufikia hapo, kile kilichoanza kama bunge lililoitishwa kushauri tu, lilikuwa limegeuka kuwa serikali ya kitaifa.


Wakati bunge la umoja wa kitaifa likijadili nini cha kufanya, mmoja wao kutoka tabaka la wenye “nasaba bora” alitoa mawazo kwamba, “wakulima walikuwa wakiasi dhidi ya ukandamizaji, na kwamba, badala ya kwenda kinyume nao, bunge lipambane na udhalimu huo”.


Agosti 4, 1789, bunge lilifuta maslahi na marupurupu yote manono ya tabaka mbili za kwanza. Na kama hatua ya kwanza kwa kazi ya kuandika katiba, bunge (au bunge la katiba kama lilivyokuja kujulikana) lilitoa azimio juu ya haki za binadamu na za raia.


Azimio hilo liliweka misingi mikuu ya serikali ambayo katiba iliyotarajiwa ilitakiwa kuzingatia, kama ifuatavyo:


Kwanza: Binadamu huzaliwa na kubakia huru na mwenye haki sawa.


Pili: Haki hizo ni haki asilia na ni pamoja na uhuru wa mtu binafsi, umiliki wa mali, usalama na haki ya kukataa kukandamizwa.


Tatu: Sheria ni kielelezo cha matakwa ya wananchi. Kila raia ana haki kushiriki yeye mwenyewe, au kupitia wawakilishi (wabunge) wake katika kuzitunga.


Nne: Mtu asituhumiwe, asikamatwe au kufungwa ila kwa kushitakiwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria.


Chini ya azimio hili, mambo kama uvumilivu wa kidini, uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, yalitajwa kuwa moja ya mihimili ya uhuru wa mtu na kwa serikali yenye uhalali wa kutawala.


Septemba 1791, katiba iliyokuwa ikisubiliwa kwa hamu na wananchi, ilikamilika. Ilitoa na kufafanua kwa mara ya kwanza katika historia, mgawanyo wa madaraka kati ya utawala, bunge na mahakama. Kazi ya kutunga sheria ilikabidhiwa kwa bunge.


Jambo moja lisilo la kawaida lililofanywa na bunge hilo la katiba ni kwamba, baada ya kukamilisha kazi yake na kabla ya kujivunja, lilitangaza wajumbe wake kutostahili kugombea ubunge wa bunge jipya.


Katiba ni mapambano; haiji kwa ridhaa ya watawala. Mfalme Louis wa XVI alijaribu kuligawa Bunge ili lisipate muafaka juu ya katiba wakilishi kwa ajili ya wananchi wote ili kumwezesha kuendeleza udikteta wake kwa manufaa yake na maswahiba wake. Bila nguvu ya umma wa wanyonge, inayoshinda nguvu ya mtutu wa bunduki, Ufaransa isingepata Katiba bora na yenye kuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu. Baada ya hapo, dunia yote, hadi sasa, iliiga katiba hiyo ya Ufaransa.


Yaliyotokea na yanayotokea hapa nchini kuhusu historia ya michakato ya katiba hayatofautiani na yaliyotokea Ufaransa.

Lubanga ahukumiwa miaka 14 Gerezani

Thomas Lubanga
Thomas Lubanga
Mbabe wa kivita kutoka Congo, Thomas Lubanga, amehukumiwa kifungo cha miaka 14, baada ya kupatikana na hatia ya kuwasajili watoto katika jeshi lake kati ya mwaka wa 2002 na 2003.
Lubanga alipatikana na hatia na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC mwezi Machi mwaka huu.
Hukumu hiyo ndiyo ya kwanza kutolewa na mahakama hiyo ya ICC iliyoundwa miaka 10 iliyopita.
Lubanga amekanusha mashtaka yote dhidi yake akisema hakuna kosa alilofanya na kwamba hakuunga mkono watoto kutumiwa kama wanajeshi.
Lakini majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo, walikubaliana kwa kauli moja kuwa Lubanga alikuwa na hatia.

Zaidi ya watu 60,00 waliuawa

Shirika la kutetea haki za kibinadam, la Human Rights Watch, limedai kuwa zaidi ya watu 60,000 waliuawa kwenye mzozo kati ya watu ya kabila la Hema na Lendu, mkoani Ituri, Kaskazini Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mwezi juni mwaka huu, aliyekuwa mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo ICC, Louis Moreno Ocampo aliomba mahakama hiyo kumhukumu bwana Lubanga zaidi ya miaka 30 gerezani.
Kuhukumiwa kwa bwana Lubanga kumehusishwa na machafuko yanayoendelea nchini Congo.
Wanajeshi wa waasi wanaopinga serikali wamekaribia mji wa Goma Mashariki mwa nchi hiyo.
Kiongozi wa waasi hao ni Generali Bosco Ntaganda, ambaye pia anasakwa na mahakama hiyo ya ICC.

Uchina yamfunga Padre kwa kujiuzulu


Askofu wa Uchina
Askofu wa Uchina
Askofu mpya kabisa kutawazwa imearifiwa kuwa anashikiliwa na mamlaka ya Uchina baada ya kutangaza kuwa anajiuzulu kutoka Kanisa Katoliki linalokubalika na Mamlaka ya Uchina.
Thaddeus Ma Daqin, Askofu wa Shanghai, alitangaza hatua yake ya kujiuzulu kutoka Chama kijulikanacho kama China Patriotic Association (CPA) siku ile ambapo alitawazwa wiki iliyopita.
Duru za Kanisa Katolika na vyanzo vingine vya kidini vimesema kuwa kiongozi huyo wa dini anashikiliwa ndani ya Seminariyo moja karibu na Shanghai.
Kwa mda mrefu kumekuwepo hali ya kutofahamiana baina ya Uchina na Vatican.
Vatican, iliyomteuwa Askofu Ma, haitambui chama cha CPA kinachokinzana na Kanisa Katoliki na Kanisa Katoliki nchini Uchina halitambui Mamlaka ya Papa.
Waumini wanaokadiriwa kutimu milioni 10 wa huko Uchina wamegawika kati ya wafuasi wa Papa na upande wa pili ukikubaliana na kundi la Chinese Patriotic Catholic Association (CPA).
Taarifa zinasema kuwa Askofu Ma aliuambia ummati wa watu 1,000 kuwa ameamua kujiuzulu ili awezew kushughulikia majukumu yake mapya. Tangazo lake hilo lilifuatiwa na makofi ya waumini , kwa mujibu wa habari za gazeti linalochapishwa huko HongKong la South China Morning Post.
Lakini wadadisi wanasema kuwa hatua hio ilionekana na wakuu wa Uchina kama kejeli na kudharau udhibiti wa Dola la Uchina juu ya viongozi wa Kanisa Katoliki na wengine.

Tuesday, July 10, 2012

SHIRIKA LA MAENDELEO BUMBULI

 

Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Napenda kuwatangazia wana-Bumbuli kwamba ile ahadi niliyotoa wakati wa kampeni – ahadi ya kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli – imetimia. Shirika limepata usajili, limefungua ofisi, lina watumishi wa mwanzo na tayari ipo miradi minne ambayo utekelezaji wake utaanza mara moja. Tutazindua Shirika hili tarehe 4 Agosti 2012, katika mkutano wangu na wana-Bumbuli waishio Dar es Salaam na mikoa ya jirani, na baadaye katika mikutano na wananchi jimboni Bumbuli.
Chimbuko
Nilipoamua kugombea Ubunge wa Bumbuli mwaka 2010, niliamua kwamba katika utumishi wangu kama Mbunge nitashirikiana na Wana-Bumbuli pamoja na marafiki na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii Bumbuli. Jimbo letu ni kati ya majimbo yaliyo nyuma kimaendeleo kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhitaji jitihada za ziada – zaidi ya zile za Serikali. Katika kufikia lengo hilo, niliahidi kuanzisha Shirika litakaloratibu shughuli za maendeleo katika Jimbo.
Nilifikia uamuzi wa kuanzisha Shirika nikitambua kwa dhati uwepo wa jitihada nzuri za serikali katika kuboresha maisha ya watu wa Bumbuli nikitegemea pia serikali kuendeleza jitihada zaidi. Hata hivyo natambua kwamba kazi ya maendeleo si kazi ya serikali pekee, inahitaji ushiriki wa kila mmoja na hasa sekta binafsi ili kuisadia juhudi za serikali kufikia malengo ya maendeleo. Nilitaka kuchambua uwezo wa watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali katika kupanua wigo wa ajira na shughuli za kipato kwa watu wa Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii.
Mpango wa Mageuzi Bumbuli
Mpango huu ulitokana na mawazo niliyokuwa nayo nilipoamua kugombea ubunge juu ya haja kuunganisha jitihada za wenyeji wa Bumbuli, wafanyabiashara na taasisi za hapa nchini, na wawekezaji kutoka nje katika kufanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Niliamini jitihada za sekta binafsi zikioana na mipango ya maendeleo ya serikali kutachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa wana-Bumbuli na hivyo kupanua wigo wa ajira na shughuli za kibiashara za uzalishaji mali katika Jimbo.
Malengo ya mpango wa kuikwamua Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii ni kama ifuatavyo:
1. Kuongeza pato la wakulima wa Bumbuli kutokana na mazao wanayovuna kwa kuboresha mbinu za kilimo, mbinu za kuhifadhi mazao, na hatua mahsusi za kuongeza thamani ya mazao hayo (value-addition).
2. Kuwavutia wawekezaji kujenga taasisi au shule itakayokuwa na wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine watakaotumia bidhaa zinazozalishwa Bumbuli, hivyo kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi.
3. Kuleta huduma za kifedha kwa kuanzisha taasisi ya fedha Bumbuli ambayo hatimaye itakuwa benki ya wananchi wa Bumbuli ambayo itatoa mikopo kwa masharti nafuu.
4. Kuchukua hatua mahsusi za kuhifadhi mazingira ya Milima ya Usambara kwani maisha na maendeleo ya kiuchumi ya watu wa Bumbuli yanategemea sana mazingira na mandhari ya milima ya Usambara.
5. Kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli litakalokuwa na jukumu la kubuni, kuratibu na kusimamia uendeshaji wa shughuli zilizoainishwa hapo juu. Shirika hili ndilo litakalokuwa kiini cha mtandao wa kijamii wa uchumi kwa Bumbuli.
Malengo haya yamekusudiwa kuwanufaisha wananchi kwa kuanzisha mtandao wa kimataifa wa kibiashara ambapo wadau mbalimbali watashiriki; na hatamu za uchumi zikishikiliwa na watu wa Bumbuli wenyewe.
Shirika la Maendeleo Bumbuli
Shirika la Maendeleo ya Bumbuli ni shirika la maendeleo lisilotengeneza faida lenye lengo la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya Jimbo. Shirika hili limesajiliwa kama kampuni yenye ukomo wa dhamana, na litafanya biashara ili kulipia gharama za uendeshaji na faida inayopatikana itatumika kugharamia miradi ya maendeleo ili kufikia malengo ya kijamii ya Mkakati wa Mageuzi ya Uchumi wa Bumbuli. Shirika litakuwa na kazi zifuatazo;
1. Kuihamasisha sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya Bumbuli kwa kuwekeza katika maeneo mblimbali. Uwekezaji huu utahusisha wafanyabiashara wa ndani na wale wa kigeni na Shirika litajihusisha zaidi katika kutoa msaada wa kitaalamu, na kuratibu mtandao wa kibiashara utakaoenea kuanzia ngazi ya wilaya, taifa na kimataifa.
2. Kubuni na kuitangaza ‘Chapa Lushoto’ (Lushoto Brand) pamoja na kutayarisha mafunzo kwa wakulima juu ya kutayarisha mazao yao ili yapate kuwa na thamani bora zaidi. Shirika hili litajenga mfumo utakaosaidia kununuliwa kwa mazao ya wakulima na masoko ya bidhaa, muundo utakaotumiwa na wafanyabiashara binafsi.
3. Kuvutia uwekezaji kwa njia ya kuitangaza Bumbuli pamoja na kuishauri halimashauri na serikali za mitaa kuhusu maeneo ya kuwekeza na miundombinu ya kuboresha ili kuvutia uwekezaji zaidi.
4. Kutafuta fedha kwa ajili ya uwekezaji wa kijamii na kibiashara na kutoa msaada wa kihuduma kwa makampuni ya biashara ya nyumbani na uwekezaji wa kutoka nje.
5. Kuratibu mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wadau mbalimbali wa maendeleo Bumbuli.
6. Kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mpango wa Maendeleo na Mpango wa uwekezaji.
Shirika litaongozwa na bodi itakayokuwa na watu kati ya nane na kumi na moja na kuendeshwa na timu ya watu watano ambao watakuwa ni, Mkurugegenzi Mtendaji, Mweka Hazina, Wachambuzi wawili na Mhasibu.
Miradi ya Mwanzo ya Shirika la Maendeleo Bumbuli
1. Mradi wa Kituo cha Kukusanya, Kusafisha, Kugredi, Kupaki na Kutafuta Masoko ya Mboga na Matunda ya Bumbuli (Bumbuli Packing House)
Wilaya ya Lushoto, jimbo la Bumbuli likiwemo, inasifika kwa kilimo cha mboga na matunda. Hata hivyo, asilimia hamsini (50%) ya mboga na matunda yanayolimwa Bumbuli yanaharibika – kwa kutokufika sokoni au kutopata soko la uhakika. Hata yale mazao yanayonunuliwa, wakulima wanapata mapato kidogo sana ambayo hayaendani na thamani ya jasho lao.
Mradi wa Bumbuli Packing House, ambao utajiendesha kibiashara, una dhamira ya kumaliza tatizo hili. Pamoja na hili mradi huu utawawezesha wakulima kwa pembejeo – mbegu, mbolea, pampu, nk – na mafunzo ili wazalishe mboga na matunda bora zaidi ya kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.
Mradi huu, katika awamu ya kwanza, utagharimu shilingi milioni 780. Utafiti wa Kibiashara (Market Analysis Survey) umefanyika, Andiko la Kibiashara limekamilika. Na majadiliano na wadhamini kupata fedha hizi yamefikia mwisho ambapo ndani ya mwezi mmoja fedha hizo zitapatikana, na baada ya maandalizi kukamilika (ikiwemo kupata professional management), mradi utaanza.
2. Mradi wa Kiwanda cha Kusindika Mboga na Matunda
Shirika liko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kukifufua upya kiwanda cha kusindika Mboga na Matunda (Natural Choice) kilichopo Soni, jimbo la Bumbuli, ambacho mwanzoni kwa miaka ya 2000 kilikuwa na sifa kubwa ya kutoa bidhaa nyingi, bora na za thamani kubwa.
Mradi huu utaenda hatua ya mbele zaidi ya Bumbuli Packing House kwa kutengeneza juisi, jams, concentrates na bidhaa nyingine za mboga na matunda kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi. Mradi huu, sio tu utatoa ajira kwa watu wa Bumbuli, bali pia utahakikisha soko la uhakika kwa mboga na matunda ya Lushoto linapatikana na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na hivyo kuwaongezea kipato.
3. Mradi wa Kutoa Mikopo kwa Masharti Nafuu (Bumbuli Microfinance Institutition)
Jimbo la Bumbuli halina tawi la benki yoyote na huduma ya fedha ni tatizo kubwa. Shirika la Maendeleo Bumbuli limeomba leseni kutoka Benki Kuu kuanzisha taasisi ya fedha kwa ajili ya ukopeshaji kwa masharti nafuu na pamoja na huduma nyingine za fedha. Andiko la Mradi huu limefanywa kitaalam sana, baada ya utafiti wa karibu miezi nane kuhusu njia muafaka ya kutoa huduma ya fedha kwa masharti nafuu kwa watu wa Bumbuli. Mradi huu utagharimu shilingi milioni 450 kwa kuanzia na baada ya miaka mitatu mtaji utaongezwa na kufikia shilingi bilioni 1.6. Wakati tunasubiri usajili na leseni kutoka Benki Kuu tayari wapo wafadhili ambao, baada ya kusoma andiko letu, wameonyesha nia ya kusaidia mradi huu.
Msingi wa mradi huu ni kuwezesha vikundi vya kuweka na kukopeshana fedha ambavyo tayari vipo lakini vina mtaji mdogo, kutoa mafunzo ya fedha kwa vikundi hivi, na kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi vingine. Kipaumbele na nafuu ya mikopo itatolewa zaidi kwa vikundi vitakavyotumia fedha hizi kwa uzalishaji mali na shughuli ambazo zitaajiri watu wengine.
4. Mpango wa Malipo kwa Kufanya Vizuri kwa Shule za Sekondari (Cash-On-Delivery for Secondary Education in Bumbuli)
Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC) litakavyotekeleza program ya msaada ya Malipo kwa kufanya vizuri** au cash on delivery (COD), ambayo itaongeza umakini na tija kwenye kujifunza na matokeo ya mitihani katika shule za sekondari jimboni Bumbuli. Kulingana na utafiti wetu, jimbo la Bumbuli liko kwenye hali ya kukata tamaa ya kupata msaada kwenye Sekta yake ya Elimu ya Sekondari. Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC) litatekeleza program ya majaribio ya malipo kwa kufanya vizuri (COD), ya miaka mitatu ambayo itafanya malipo kulingana na idadi ya wanafunzi ambao wamefaulu Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne. Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC) linalenga kuboresha matokeo ya kujifunza/elimu katika jimbo la Bumbuli kupitia program hii ya kutoa motisha. Program hii itahusu Shule za Sekondari za Serikali za Kata.
Malipo kwa kufanya vizuri (COD) ni utaratibu mpya kutoa msaada ambapo wafadhili hutoa pesa kwenye maendeleo yanayopimika kwa kuangalia matokeo maalum. Unahusianisha moja kwa moja malipo na matokeo maalum, ikiwapatia watendaji/wapokeaji motisha ya kuongeza nguvu zao za kufanyakazi ili kufikia maendeleo.
Msingi na uhalali wa wazo la CDO, ulioanzishwa awali na Kituo cha Maendeleo ya Kimataifa(Center for Global Development) mjini Washington, umejikita kwenye mtazamo kwamba kazi za maendeleo ni lazima zitathminiwe kwenye athari (impact) zinazoletwa. Mbinu inawakilisha mabadiliko kutoka kufuatilia nguvu na rasilimali ambavyo mashirika huwekeza katika kutoa misaada - 'nyenzo/rasilimali', na pia shughuli na vifaa/vitendeakazi vinavyotokana na uwekezaji huo - 'matokeo'. Badala yake, mbinu hii inalenga kujikita kuangalia namna gani maisha ya watu masikini yameweza kubadilishwa kutokana na uwekezaji kwenye sekta au eneo fulani la maendeleo (afya, elimu, n.k).
Mnamo mwezi Septemba 2011, Shirika la Maendeleo Bumbuli lilifanya utafiti wa kina juu ya mazingira ya kujifunzia Bumbuli na kugundua kwamba shule nyingi, walimu, na wanafunzi wa Bumbuli hawana motisha wala rasilimali zinazohitajika kuwawezesha wafanye vizuri kama inavyotarajiwa.
Kwa wastani, kila shule iliyotoa data za matumizi ya pesa ilionyesha ni Sh. 5,268 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka 2010 (kiasi kilichotarajiwa kwa shule za Sekondari ni shilingi 25,000 kwa kila mwanafunzi). Pamoja na hayo, utafiti ulionyesha kuwa ni 71% tu ya walimu walikuwepo shuleni, ambapo ni 19% tu walikutwa madarasani. Utafiti huo ulionesha kuwa walimu hupata mishahara yao kwa wakati. Wastani wa mshahara halisi wa mwalimu wa Bumbuli ni Sh.395,000 kutoa malipo ya deni ya Sh.74,000 kila mwezi. Wengi walionesha kuwa na shughuli ya ziada ya kiuchumi (67%), hasa kilimo (90%). Wengi wao (98%) walidai kutokuhusishwa katika hatua za kupanga bajeti za shule. Wastani wa Pato la Mtanzania anayeishi kijijini (ikiwemo Bumbuli) ni Sh.152,000 (HBS, 2010). Wakati 89% ya wanafunzi wanaonesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi wa familia, bado 70% wanafanikiwa kupata muda kidogo wa kukamilisha kazi zao za masomo wakiwa nyumbani, huku 34% inaonesha hawakufika shule kwa mwezi uliopita kutokana na kusaidia shughuli za nyumbani. Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne ya mwaka 2011 kwa Shule za Bumbuli yalikuwa mabaya sana. Kati ya wanafunzi 1,327 waliofanya mtihani, hakuna aliyepata Division 1, waliopata Division 2 ni wanne, waliopata Division 3 ni 39, na waliobakia, yaani wanafunzi 1,274, walipata Division 4 na 0.
Pamoja na hatua mahsusi ambazo Serikali inachukua kuboresha elimu nchini na kuongeza ufaulu, Shirika la Maendeleo Bumbuli, kupitia Program hii ya COD, linataka kuonesha kwamba fedha zinaweza kugawika vizuri na kwa usahihi ili kuboresha elimu kwa kupima kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Hatua na mikakati inayopendekezwa
Program ya COD kwa Shule za Sekondari Bumbuli itahusisha makubaliano kati ya Shirika la Maendeleo Bumbuli, Shule za Sekondari Bumbuli na Halmashauri ya Wilaya kulipa jumla ya kiasi cha Dola za kimarekeni 100 kwa kila mwanafunzi anayefaulu mitihani ya kidato cha IV kwa daraja la I-III. Malipo ya COD yatafanyika baada ya uthibitisho wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. Fedha zitapelekwa Halmashauri ya Wilaya, Shule za Sekondari na kwa walimu na wanafunzi. Fedha zitakazogawiwa kwa shule zitatumika kwa ajili ya mahitaji ya kielimu ya shule kama zilivyowekewa vipaumbele na Bodi za Shule.
Watakaonufaika na mradi:
Kwa kila mwanafunzi atakayefaulu mtihani (Div I-III) anapomaliza kidato cha nne, Shirika la Maendeleo Bumbuli kupitia program ya COD litatoa malipo yafuatayo:
1. Walimu: Tsh 60,040/= kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
2. Wanafunzi: Tsh 50,500/= Kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
3. Shule: Tsh 31,600/= Kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
4. Halmashauri ya Wilaya: Tsh 15,800/= kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
Vipimo na Ukaguzi:
Data za mitihani kuanzia mwaka 2011 zitatoa msingi wa awali, na msingi huo utakuwa ukibadilishwa kila mwaka na ufanisi wa utendaji wa shule, hivyo kila mwaka unakuwa msingi kwa ajili ya malipo ya mwaka ujao wa. Kiashiria cha matokeo kitakuwa idadi ya wanafunzi ambao wamefaulu kidato cha nne kwa kupata daraja la I-III. Ili kuyadumisha matokeo hayo, hatua mbalimbali zitakuwa vikiripotiwa kila mwaka na shule na halmashauri. Mkataba, matokeo, na taarifa nyingine zitawekwa wazi kwa wananchi ili kuongeza uwajibikaji wa wafadhili na wapokeaji
Shirika la Maendeleo Bumbuli halina nia ya kusema kwamba COD ndio suluhisho pekee la tatizo la maendeleo ya elimu au ufumbuzi wa matatizo yote katika mfumo wa elimu nchini lakini tunaamini inaonesha matarajio ya kutosha kuona thamani ya kujaribu, kujifunza na kutathmini.
Uendelevu wa program
Ili program iwe endelevu, Shirika la Maendeleo Bumbuli(BDC) litaweka mfumo thabiti wa kufanya tathimini na kutoa mrejesho, ambao utatumika kama zana ya kupimia uwajibikaji, na kuendeleza uwazi. Pia ni muhimu kuzingatia ushirikishwaji wa wenyeji wa Bumbuli na umiliki wa program ya COD. Hili linaweza kufanikiwa kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha elimu bora kama uwekezaji wa wenyeji, na Mtandao wa Wahitimu wa Shule za Sekondari Bumbuli kwa ajili ya fedha za COD. Zaidi sana, Shirika la Maendeleo Bumbuli litahusisha na kutumia Bodi za Shule, ambazo zinahusisha wazazi na walimu. Hii ndiyo njia itakayowafanya watu wa Bumbuli wathamini juhudi zao wenyewe katika kuboresha jamii zao.
5. Kambi ya Wanafunzi Wanaojiandaa na Mtihani wa Kidato cha Nne 2012
Kuanzia tarehe 4 Agosti hadi 5 Septemba, wakati wa likizo za masomo, Shirika limeandaa kambi maalum kwa matayarisho ya vijana wanaojiandaa na mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu. Kambi hii itakuwepo kwenye Kituo cha Elimu Soni, ambacho kina mandhari, mazingira na eneo la kutosha kufundishia na kuishi wanafunzi katika kipindi hiki.
Kila siku, wanafunzi hao watapigwa msasa kwa masomo ambayo hawakupata fursa ya kuyasoma vizuri katika mwaka wa shule, watafundishwa mbinu za kufanya mitihani (ikiwemo time-management), na kufanya revision ya mitihani ya Kidato cha Nne ya kuanzia mwaka 1984 hadi sasa. Shirika litatafuta walimu wenye sifa za kufundisha masomo ya Hesabu, Kiingereza, Historia, Kemia, Fizikia na Biolojia, hata nje ya Jimboni na kuwalipa posho kuja kufundisha kwenye kambi. Pia tutaomba watu mbalimbali, ikiwemo walimu wastaafu, wenye moyo wa kujitolea waje kufundisha kambi hii.
Mwisho
Hadi sasa Shirika la Maendeleo Bumbuli halijapata mfadhili au ufadhili kutoka kokote au kwa mtu yoyote. Miradi hii niliyoitaja ndio iko katika hatua za kupata ufadhili. Fedha ambazo zimetumika hadi sasa kuanzisha Shirika, kuweka ofisi, kuajiri watumishi wa muda na kufanya utafiti na kutengeneza maandiko ya miradi zimetokana na mkopo niliouchukua kama Mbunge, ikiwemo mkopo wa gari ambao sikuutumia kununua gari bali kuanzisha Shirika.
Napenda kutoa mwito kwa wana-Bumbuli wenzangu na Watanzania kwa ujumla kusaidia kuchangia maendeleo ya Jimbo la Bumbuli, hasa kwa miradi ambayo hatukuitafutia ufadhili kama huu wa COD na kambi. Kwa kuchangia unaweza kutumia namba ya M-PESA 0762088050. Kwa maelezo zaidi kuhusu Shirika la Maendeleo Bumbuli, tuma barua pepe: getinvolved@bumbuli.org au piga simu: +255 22 2129821/6 au tuma fax: +255 22 2129796
Katika miezi ijayo, BDC pia itatekeleza miradi ya kitaifa yenye manufaa kwa maendeleo na utawala bora kwa nchi yetu. Naamini nchi yetu itapiga hatua za maendeleo kwa kasi zaidi kama kila mmoja wetu, kwa nafasi na uwezo wake, atathubutu, lakini pia kama sote tutasaidiana katika kuchangiana na kupeana mawazo kuhusu shughuli za maendeleo.

January Makamba
Mbunge Bumbuli

Nafasi za Masomo University of Oldenburg,Germany


 
Kwa wale wanaohitaji kujiunga na elimu ya juu nchini Ujerumani.
Kuanzia B.A,Bsc,M.A mpaka Phd Watanzania tumieni nafasi hizi,
chuo kinapokea wanafunzi hata kwa vijana wa Kitanzania wenye
kumaliza kidato cha sita wana nafasi ya kujiunga na chuo hiki,
maelezo zaidi,
Tafadhali wasiliana na anuani hii hapa chini:

International Student Office
Carl von Ossietzky Universität Oldenburg
Ammerländer Heerstr. 114-118,
26129 Oldenburg
Germany
Simu :+49-(0)441-798-2479
fax : +49(0)441 7982461
Pia fomu za maombi zinapatikana online katika link hii chini: