Bahati mbaya sio wote tuna ndugu, jamaa na marafiki ambao kazi zao zinawapa mwanya wa kuona kinachozalishwa na mfumo wa elimu nchini. Hata hivyo, wakati tunaanza kuelewa kinachoendelea kupitia kwao tunakuwa tumechelewa. Tumechelewa sana. Kwa sababu tunakuwa tayari tumeshapoteza kizazi; tunakuwa tunaangalia matokeo ya makosa yaliyokuwa yakifanywa kwa kipindi kifefu.
Juhudi za asasi kama Twaweza/Uwezo na Tamasha Vijana, kufanya tafiti za kina na kuonesha wapi mapungufu yalipo hasa, ni nzuri na zinahitaji heko badala ya kuzikebehi kwa ‘majibu ya kisiasa’. Zinapaswa kutumiwa katika uundaji na mabadiliko ya mitaala na mfumo mpya wa elimu unaoakisi mwelekeo wa ulimwengu huu wa leo.
Pia, napenda kuchukua fursa hii kuhoji: Kwa nini hatukuwa na vigezo vya kutuambia mwelekeo wa elimu katika ngazi mbalimbali? Yaani, hizi ripoti zingetakiwa ziwe zinatoka angalau kila baada ya miaka kadhaa tangu siku sekta ya elimu na wizara husika zilipotengemaa. Hakuna mtu aliyewahi kufikiria hilo? Kama nilivyosema awali, ni dhahiri kuwa mapungufu tunayoyaona sasa hivi ni matokeo ya mapungufu na makosa ya muda mrefu.
Au bado tunaamini ya kwamba mitihani ya mwisho pekee ndio kipimo thabiti cha elimu?
Kwa upande mwingine, wengi wetu — mtu mmoja mmoja — hatuna hulka ya
kufuatilia maendeleo ya wadogo zetu, ndugu zetu na watoto wetu mara kwa
mara. Wengi tunasikia malalamiko kutoka kwa wengine, lakini hatushtuki
hadi pale watoto wetu wanapopata madaraja ya chini kabisa kwenye mitihani ya mwisho (hasa ya kidato cha nne na sita).Kama umefanya utafiti au umesoma ripoti za tafiti mbalimbali, utakubaliana nami kuwa hatuwatendei haki vijana ambao wapo mashuleni sasa hivi. Sehemu kubwa hawaandaliwi kukabiliana changamoto za dunia ya sasa.
Wapo wenye mawazo tofauti, kuwa tunapiga hatua; vijana wengi zaidi sasa hivi “wanapata elimu”. Bahati mbaya ulimwengu wa leo hauna mipaka. Nchi yetu sio kisiwa. Vijana wa leo hii wanashindana na vijana kutoka kona mbalimbali za dunia. Kwa mantiki hiyo, kama wengine wanaendelea kwa kasi kubwa kuliko sisi, basi sisi tunarudi nyuma!
Mapungufu tunayoyaona ni mengi, lakini wakati waliopo kwenye sekta ya elimu wakijaribu kuyatambua na kuondokana nayo, ni wajibu wetu — mtu mmoja mmoja — kujaribu kufanya kila tunachoweza kuokoa wengi kadri tunavyoweza, kwa kuwa mabadiliko yanayotakikana yatachukua miaka mingi.
Kwa mtazamo wangu, donda ndugu ni sisi kama jamii kwa ujumla kutoheshimu taaluma ya ualimu. Hatujaweza kuwavutia wengi wanaofanya vizuri mashuleni kuingia kwenye fani ya ualimu. Zaidi ya hayo, walimu wachache tulionao hawapewi motisha ya aina yoyote ile.
Ukiacha upungufu wa zana za kufundishia, n.k., kuna mdahalo mzito wa muda mrefu wa lugha ipi itumiwe (sekondari na vyuoni): Kiswahili au Kiingereza?
Tukumbuke kuwa kwenye taaluma yoyote ile, kitu muhimu ni ujenzi wa “msingi”. Hapa namaanisha, kwa mfano kwenye sayansi, “msingi” ni tabia ya udadisi, jinsi mtu anavyofikiri na anavyokabili tatizo fulani. Katika hatua ya ujenzi wa tabia ya udadisi, awali ya yote mwanafunzi anapaswa kuwa na ufahamu wa mambo yanayomzunguka. Na udadisi au ufahamu huambatana na ujenzi wa taswira fulani kichwani.
Je, elimu inamsaidia mwanafunzi kuwa mdadisi? Lugha inayotumiwa inarahisisha zoezi la kujenga msingi, au tabia ya udadisi?
Unapomfundisha mwanafunzi wa kidato cha kwanza kuhusu mwendo kasi, atakuelewa vizuri ukitumia mifano ya gololi, ndulele au billiards? Ukitumia mfano ya billiards pekee, mwanafunzi atatumia nguvu nyingi kukariri (kwa kuwa hajui billiards ni nini) badala ya kuanza kujenga taswira na uelewa wa mwendo kasi.
Mabadiliko ya matumizi ya lugha kwenye masomo kutoka darasa la saba hadi kidato cha kwanza huathiri wanafunzi wengi mno. Wapo wachache wanaouruka hiki kihunzi bila matatizo, ila wengi hupata msaada kwa namna moja au nyingine. Wenye bahati tulikuwa na walimu wenye uwezo wa kutuelezea vizuri kwa Kiswahili rahisi kila palipohitajika. Wenye bahati zaidi tulikuwa tuna wazazi ambao waliweza kutusaidia kujenga taswira ya vitu kama electron kwa kutumia Kiswahili.
Bahati mbaya wengi hawana hizo bahati, hivyo sehemu kubwa ya juhudi zao huelekezwa kwenye kukariri maelezo ya Kiingereza bila kuelewa. Hii ni moja ya vyanzo vya misingi mibovu ambayo huja kuanza kuota nyufa wanafunzi wanapofika ngazi za juu.
Kama moja ya njia ya kutatua tatizo la matumizi ya lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao bado hawajakimudu vizuri, kuna kitabu kipya kinachoitwa “Enjoy Chemistry, Furahia Kemia” kilichochapwa hivi karibuni. Kitabu hiki kimeandikwa maalumu kwa ajili ya wanafunzi wanaozungumza lugha ya Kiswahili wanaotaka kujifunza Kemia,
na wakati huohuo wapate kumudu lugha ya Kiingereza ili kufanya majaribio na mitihani ya kufuzu elimu ya sekondari.
Kwa upande wa uhaba wa vifaa vya maabara, kitabu hiki kina maelezo ya kufanya majaribio ya Kemia ambayo yatamwezesha mwanafunzi kujifunza mwenyewe. Maelezo ya kitabu yanasema: “Kwa kuwa shule nyingi za sekondari zina uhaba mkubwa wa vifaa vya maabara maalumu kwa ajili ya somo la sayansi lenye majaribio mengi kama ilivyo Kemia, kitabu hiki pia kinaweka mkazo kwenye mbinu ya fanya-mwenyewe. Mbinu hii itawasaida wanafunzi kuelewa Kemia kwa kina na wakati huohuo kulifurahia somo. Njia hii itawapatia wanafunzi walio kwenye shule zisizo na vifaa vya kutosha fursa sawa ya kufanya majaribio ya Kemia kama waliyonayo wanafunzi walio na bahati ya kuwa katika shule yenye vifaa vingi vya maabara.”
Ni muhimu kusisitiza kuwa kitabu hiki hakibadilishi wala kupindisha mitaala ya Kemia nchini.
Wakati wadau wa elimu wakiendelea kufanya midahalo na mijadala ya mabadiliko katika sekta ya elimu na mitaala, juhudi kama hizi zinatia moyo kwa kuwa naamini zitasaidia kuokoa vijana kadhaa.
Tafadhali, pitia kitabu hiki kisha tupe maoni yako hapo chini. Pia, wataarifu na wengine na wakaribishe kupiga kura juu ya lugha gani itumiwe kufundisha wanafunzi wa ngazi ya sekondari.
Imetolewa na Mzumbe
No comments:
Post a Comment