Kwikwi husababishwa na nini?
Baada
ya kusoma makala inayohusu kijana mmoja aliyesumbuliwa na kwikwi kwa
zaidi ya miaka miwili na nusu, na baadaye kutibiwa tatizo hilo kwa
kufanyiwa upasuaji wa ubongo na kutolewa tezi, nimeamua leo nizungumzie
kwikwi.
Kwiki ni kitendo kisichozuilika ambacho hutokana na kusinyaa
kwa kuta za kiwambo cha moyo au diaphragm. Kwa kawaida kwikwi ni
kitendo kinachojirudia rudia mara nyingi. Sauti ya 'hic' inayotokea
wakati unapokuwa na kwikwi husababishwa na kidaka tonge (epiglottis)
ambacho hufunga haraka wakati hewa inapoingia kwenye koo. Kupiga kwikwi
kwa kawaida hakuna maumivu lakini mara nyingine husumbua hasa
inapoendelea kwa muda mrefu. Kwikwi ya kawaida huweza kutulizwa kwa
kunywa maji, lakini wakati mwingine kufanya hivyo hakusaidii.
Zifutazo ni sababu zinazoweza kukuletea kwikwi
1. Kula kwa haraka.
2. Kula chakula cha moto na kunywa maji baridi baada yake.
3. Kulia au kukasirika.
4. Kula chakula chenye viungo vingi au pilipili.
5. Kula chakula cha moto sana.
6. Kunywa pombe au soda kwa wingi.
7. Kukohoa sana.
8. Kucheka kupita kiasi.
9. Kufurahi sana, kusisimka au kupatwa na msituko.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, vitu ambavyo vinakiletea karaha
kiwambo cha moyo au diaphragm husababisha kwikwi. Kuna sababu nyingi
ambazo husababisha jambo hilo na hizo tulizotaja hapo juu ni miongoni
mwazo,ambapo matokeo yake ni humfanya mtu apige kwikwi. Kwikwi kwa
kawaida huisha baada ya dakika chache au hata sekunde. Lakini iwapo
kwikwi itaendelea kwa masaa au kwa siku, huweza kuwa ni tatizo muhimu la
kitiba na pengine hali kama hiyo inaweza ikawa inasababiswa na ugonjwa.
Kuna baadhi ya watu hupata kwikwi sana wakati wa ujauzito, baada
ya kufanyiwa operesheni na hata watoto wachanga pia hupatwa na kwikwi
mara kwa mara. Wajawazito hupata kwikwi sana mwishoni mwa miezi mitatu
ya mwanzo ya ujauzito na mwanzoni mwa miezi mitatu ya pili. Kwikwi
hutokea wakati wa ujauzito ni kwa sababu wakati huo uwezo wa kuvuta hewa
ndani ya mapafu na kutoa nje huongezeka kwa asilimia 30 hadi 40
ikilinganishwa na hali ya kawaida. Hakuna sababu inayojulikana
inayosababisha kwikwi kwa watoto wachanga, na wazazi wanashauriwa
wasitiwe hofu na suala hilo. Hii ni katika hali ambayo kwikwi baada ya
upasuaji husababishwa na nusu kaputi au anesthesia.
No comments:
Post a Comment