MAELFU WAJITOKEZA KUMZIKA, WATU 600 WAPOTEZA FAHAMU, POLISI WASEMA HAWAKUTARAJIA UMATI MKUBWA HIVYO
MAELFU
ya waombolezaji jana walijitokeza katika mazishi ya msanii nguli wa
filamu Tanzania Steven Kanumba (28), yaliyofanyika katika Makaburi ya
Kinondoni, Dar es Salaam. Alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi ya
Aprili 7, mwaka huu.Kabla ya kuzikwa, mwili wa marehemu Kanumba
ulipelekwa katika Viwanja vya Leaders ili kuwawezesha waombolezaji kutoa
heshima za mwisho. Hata hivyo, ni wachache waliobahatika kupata fursa
hizo baada ya kutokea msongamano mkubwa ulioifanya kamati ya maandalizi
ya mazishi hayo kusitisha mchakato huo.
Inakadiriwa kuwa
waombolezaji wapatao 600 walianguka kutokana na ama msongamano au
majonzi ya kifo hicho cha ghafla cha msanii huyo.
Makamu wa Rais,
Dk Mohamed Gharib Bilal, Mke wa Rais, Salma Kikwete na Waziri wa
Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe walikuwa wa kwanza kutoa
heshima zao za mwisho na kufuatiwa na viongozi wengine wakiwamo wabunge.
Baada ya viongozi hao kutoa heshima zao za mwisho, Dk Bilal na
Mama Kikwete waliondoka na kwa mujibu wa ratiba, ilikuwa zamu ya
waombolezaji wengine kuaga.
Hata hivyo, kulitokea msongamano
mkubwa wa watu kila mmoja akitaka kulifikia jeneza na kulishika. Ilibidi
vyombo usalama na walinzi binafsi kufanya kazi ya ziada kurejesha hali
ya utulivu katika eneo hilo.
Kutokana na utaratibu mbovu katika
kuendesha shughuli hiyo, ratiba ilikatishwa na mwili kuondolewa saa 6:30
kupelekwa makaburini. Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi iliyokuwa
imetolewa juzi, muda wa kuaga ulipangwa kuanza saa 6:00 hadi saa 9:00
alasiri.
Badala yake, waombolezaji walitakiwa kujipanga kando ya
Barabara ya Tunisia ambako gari lililobeba mwili wa msanii huyo lilipita
kuelekea makaburini.
Haikuwa kazi rahisi kwa waombolezaji hao
ambao baadhi walifika hapo alfajiri kwa ajili ya kutoa heshima zao
mwisho kukubaliana na agizo hilo.
“Hatuwaelewi hawa. Sisi
hatukuja kuliona jeneza tunataka kumuona ili tujue kama kweli amekufa.
Hawa walioandaa utaratibu huu mbovu ni kina nani jamani au wameshindwa
kazi?” alisema mmoja wa waombolezaji na kisha kuangua kilio.
Baada
ya hali kutulia umati huo wa waombolezaji ulianza kulisindikiza gari la
marehemu kwa nyuma huku wengine wakitaka jeneza hilo lishushwe ili
walibebe.
Wakati msafara huo ukielekea makaburini, baadhi ya
waombolezaji walikuwa wakianguka na wengine kuzirai baada ya kuona
jeneza na kuwafanya watoa huduma wa Msalaba Mwekundu kufanya kazi kubwa
ya kuwasaidia na kuwapeleka baadhi yao hospitali.
Licha ya umbali
kati ya Viwanja vya Leaders na Makaburi hayo ya Kinondoni kuwa karibu,
msafara huo ulichukua takriban saa mbili kufika kutokana na kwenda
taratibu ili kutoa fursa kwa waombolezaji ambao baadhi yao walilazimika
kupanda juu ya miti, kutoa heshima zao.
Baada ya kufika
makaburini, iliwalazimu polisi kuongeza nguvu kudhibiti umati huo na
kutoa fursa kwa ibada ya mazishi kuendeshwa kama ilivyopangwa.
Wazirai
Mwenyekiti
wa Kamati ya Tiba ya mazishi hayo, Dk Nassoro Ally alisema watu wapatao
600 walizirai katika viwango tofauti kutokana na sababu mbalimbali
ikiwamo ya watu kujaa na kubanana na hivyo kukosa hewa.
“Watu
wamebanana na kukanyagana. Wemekosa hewa na wengine kati yao
wanakabiliwa na matatazo ya kiafya, ugonjwa wa pumu, shinikizo la damu
ingawa wapo waliokanyagana na kuanguka kutoka katika miti na kupoteza
fahamu,” alisema Dk Ally.
Baadhi ya waombolezaji waliozirai ni pamoja na wasanii Wema Sepetu, Jacqueline Wolper na Irene Uwoya.
Wema alizirai baada ya kufika makaburini na Wolper alifikwa na hali hiyo katika Viwanja vya Leaders.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema watu waliopoteza fahamu hawazidi 30.
Alisema
watu waliofika kuaga mwili huo walikuwa ni zaidi ya matarajio yao na
kuongeza kwamba kwa mazingira shughuli hiyo, eneo hilo lilikuwa dogo
akisema sehemu muafaka ilipaswa kuwa Uwanja wa Taifa.
Kauli za viongozi
Akitoa salamu kwa niaba ya Serikali, Dk Nchimbi alisema huu ni mwaka wa mwisho kwa wasanii kuibiwa kazi zao.
Dk
Nchimbi ambaye katika salamu zake pia alitoa ubani wa Sh10milioni kwa
niaba ya Serikali, alisema wizara yake ikishirikiana na Wizara ya Fedha,
Wizara ya Kazi na Ajira na Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff),
wameshakutana na kujadiliana namna ya kuzuia wizi katika kazi za
wasanii.
“Mwaka huu ndiyo mwisho wa kazi za wasanii kuibiwa na
nilipenda sana kuona Kanumba akishuhudia jitihada hizi ambazo tumekuwa
tukizifanya naye kama mdau mkubwa wa sekta hii,” alisema Dk Nchimbi na
kuongeza:
“Jitihada ambazo amezifanya Kanumba enzi za uhai wake
ni dhahiri zimejionyesha leo. Mmejitokeza kwa wingi kuja kumuaga hivyo
wasanii mnaobaki mnatakiwa kuiga kile alichokuwa akikifanya.”
Rais
wa Taff, Simon Mwakifwamba alisema marehemu Kanumba ameacha pengo kubwa
katika tasnia ya filamu kutokana na mchango wake mkubwa aliouonyesha
katika kipindi kifupi cha uhai wake.
“Kanumba alikuwa balozi
pekee wa filamu nchi za nje. Aliitangaza nchi yetu kupitia tasnia ya
filamu hivyo tutamkumba daima kwa kutuonyesha njia,” alisema
Mwakifwamba.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
amewataka wasanii nchini kufuata nyayo za Kanumba na kumkumbuka msanii
huyo milele.
“Watanzania wengi wana majonzi makubwa lakini
watambue kwamba ni kazi ya Mungu. Kinachotakiwa sasa hili litumike kama
somo kwa wasanii wengine kwani leo tunashuhudia Kanumba akiagwa kama
mfalme kutokana na kazi yake nzuri aliyokuwa anaiwasilisha kwa
Watanzania,” alisema Nape.
Askofu wa Kanisa la African Inland
Church (AIC), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Charles Salala alisema
msiba wa Kanumba ni pigo kwa taifa na kuwaasa Watanzania kutenda mambo
mema ili kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii.
“Leo tupo katika msiba
wa mtu ambaye alikuwa ana mchango mkubwa kwa jamii, ndiyo maana
tunashuhudia umati mkubwa wa watu ukiwa umekusanyika hapa, lakini jambo
ambalo sisi kama binadamu tunatakiwa kufanya ni kuishi maisha mema na
kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ,” alisema na kuongeza:
“Marehemu
Kanumba aliwahi kuhudumu katika kanisa hili na alikuwa ni mtu mwenye
upendo kwa kila mtu ndiyo maana leo maelfu ya Watanzania tupo hapa
kumsindikiza ndugu yetu katika safari yake ya mwisho.”
Habari na Mwananchi,Video na Dj Choka.
No comments:
Post a Comment