NJOMBE

NJOMBE

Monday, April 2, 2012

Wabunge wa Chadema wacharangwa mapanga

WABUNGE wawili wa Chadema wamejeruhiwa vibaya kwa mapanga na mashoka huko Mwanza katika tukio lililotokea saa nane usiku katika eneo la Ibanda Kabuhoro baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM usiku wa kuamkia uchaguzi wa diwani Kata ya Kirumba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alisema jana kwamba mbali na wabunge hao, Samson Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatory Machemuli wa Ukerewe, wengine walioshambuliwa ni pamoja na Ahmed Waziri ambaye inasemekana kuwa ni kada wa UVCCM aliyekatwa kiganja chake cha mkono wa kulia.

Wengine ni Haji Mkweda (21), ambaye alijeruhiwa mguu wa kulia, Judhith Madaraka (26), aliyechomwa kisu kwenye titi lake la kushoto na mkono wa kushoto, Ivory Mchimba (26), aliyejeruhiwa kichwani na mdomoni. Majeruhi wote ukiondoa wabunge hao na Waziri, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure.

Awali, wabunge hao walilazwa katika Hospitali ya Rafaa Bugando lakini baadaye walisafirishwa kwa ndege kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam. Kwa upande wake, Waziri amelazwa Bugando.

Mbali ya Mwanza, katika uchaguzi mwingine wa udiwani Kata ya Kiwira, Mbeya nako damu ilimwagika baada ya watu kadhaa kushambuliwa kwa mapanga na nodo. Katika tukio hilo polisi imewatia mbaroni watu 10.

Kamanda Barlow alisema katika vurugu hizo magari matatu likiwemo la Kiwia yaliharibiwa.

Alisema polisi ilipata mapema taarifa za tukio hilo lakini ilichelewa kufika kutokana na eneo hilo kuwa lenye mawe na milima hivyo kufika wakati tayari wabunge wameshajeruhiwa vibaya na mali hizo kuharibiwa.

“Kiwia alionekana kushambuliwa kichwani na kitu chenye ncha kali na magari nayo yakiwa yameharibiwa vibaya. Kwa mazingira hayo ya usiku na hali ilivyotokea, jeshi langu linafanya uchunguzi wa kina kuweza kujua kiini cha vurugu hizo, lakini tumewaelekeza wenzetu wa Takukuru kufuatilia kujua kama mazingira ya wabunge hao kutembea usiku huo yalikuwa na uhusiano wowote na masuala ya rushwa,” alisema.

Bunge latoa tamko
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alithibitisha taarifa za kuvamiwa kwa wabunge hao na kusema wamepelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Ndugai alisema utaratibu ulivyo ni kwamba mbunge yeyote akiumia, Bunge ndilo linaloshughulikia matibabu yake na ni katika hospitali za Serikali tu.

“Nimepata taarifa hizo na tumetuma timu yetu ya Bunge kwenda kushughulika suala hilo. Mara ya kwanza nilisikia ni mbunge mmoja tu ndiye aliyepelekwa Dar es Salaam, lakini baadaye nikaambiwa ni wote wawili hivyo tunafuatilia kujua hali zao,” alisema Ndugai

Chadema
Akizungumzia tukio hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku baada ya kutokea kundi la watu ambao idadi yao haijajulikana na kuanza kuzuia gari la Mbunge Kiwia, huku wakilishambulia kabla ya kulimwagia gesi ya kuwasha baada ya kuvunja vioo kisha kumtoa na kuanza kumshambulia.

“Kabla ya kushambuliwa baada ya kuona gari lake limevamiwa alibahatika kumpigia simu Machemli akimwomba awahi eneo alilokuwepo, naye alipofika alijikuta akiwa mikononi mwa vijana hao na kushambuliwa pia,” alisema Zitto na kuongeza:

“Wakati tukio hilo linatokea, askari wa jeshi la polisi walikuwa katika maeneo hayo lakini walishindwa kutoa msaada kitu ambacho kilitushangaza.”

Chadema jana kilitoa tamko kulaani tukio hilo kikisema ni kitendo kinachopaswa kukemewa na wapenda amani na demokrasia ya kweli wote.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema katika taarifa yake kuwa Chadema hakitaishia kulaani na kusikitika, bali kitachukua hatua stahiki ili kukomesha vitendo hivyo.

Mwenyekiti wa CCM

Tukio hilo limekuja siku saa chache baada ya Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina kukaririwa akiwaagiza wana CCM, kwa ujumla kutowavumilia Chadema akidai kuwa wamekuwa watu wa vurugu akisema katika uchaguzi uliopita waliaachia wakafanya walivyotaka ikiwemo kuchoma ofisi za CCM.

Mabina ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni alisema: “Nawaambia wafuasi wa CCM hakuna kuwaogopa Chadema, lazima tupambane nao kwa hili.”

Jana Mabina, alikiri kuwa na taarifa ya tukio hilo na kusema: “Chadema wamezoea fujo. Bila ya kufanya fujo hawawezi kushinda, sasa angalia usiku wa manane walikuwa wanafanya nini?” alihoji na kuendelea:

“Kama siyo kutoa rushwa, ninachojua wao ndiyo walianza kushambulia vijana wangu, mfano huyu mmoja (Ahmed) wamefanikiwa kumvunja mkono na hivi tunavyoongea ameingizwa chumba cha upasuaji kufanyiwa oparesheni mkono wake.”

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana kuwa anazo taarifa za tukio hilo lakini asingependa kulizungumzia kwa kuwa chama kimejipanga kuzungumza na waandishi wa habari leo.

Mapanga Mbeya

Huko Mbeya, watu wanne waliokuwa wakitoka katika kituo cha kupigia kura cha Kiwira Mjini wamejeruhiwa kwa kukatwa mapanga katika eneo la Hilondo ambalo ni maarufu kwa machimbo ya mchanga.

Waliojeruhiwa ni John Andengenye (26), Daud Hamis (27), Jacob Kalua (30) na mwingine ambaye hakutambuliwa mara moja.

Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Makandana, Rungwe Grace Kapungu alithibitisha watu hao kufikishwa katika hospitali hiyo ya wilaya kwa ajili ya matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa watu 10 wamekamatwa wakihusishwa nalo.

Habari hii iemandikwa na Sheilla Sezzy, Mwanza; Godfrey Kahango, Mbeya na Frederick Katulanda, Geofrey Nyang'oro, Boniface Meena Dar.
Habari na Mwananchi.

No comments:

Post a Comment