NJOMBE

NJOMBE

Friday, September 7, 2012

Obama apigiwa debe na Bill Clinton

 

Rais mstaafu Bill Clinton na Barack Obama
Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton amemtetea vikali mgombea urais wa chama cha Democrats nchini Marekani Barack Obama.
Katika hotuba iliyochukua muda wa dakika 50 katika kongamano la chama hicho linalofanyika mjini Charlotte, North Carolina, Clinton alikosoa sera za uchumi za chama pinzani cha Republican.
 Bill alisisitiza kuwa sera ya uchumi ya Barack Obama imeweza kuimarisha uchumi wa nchi hiyo ambao ulikuwa umedorora. Bwana Clinton alimaliza hotuba yake kwa kumteua rais Obama kuwa mgombea rasmi wa urais wa chama.
Rais Obama atamenyana na mgombea wa chama cha Republican Mitt Romney katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Novemba.
Hotuba ya Clinton ni dalili ya kuimarika kwa uhusiano kati yake na Obama na pia kama juhudi za kupiga jeki mvuto wa obama miongoni mwa wazungu wanaofanya kazi.
Kura za maoni zinaonyesha kuwa wapiga kura wa chama hicho wamekuwa waangalifu sana kuhusu sera za Obama lakini Clinton ana rekodi nzuri ya kuwashawishi watu kumuunga mkono Obama.
Clinton aliambia wafuasi wa chama '' Amueni nchi mnayotaka kuishi. Ikiwa mnataka viongozi wasio wajali basi pigieni kura chama cha Republican. Mkitaka nchi yenye nafasi nyingi na ambayo majukumu yanagawanywa, basi sote tuko pamoja. Lazima mumpigie kura Barack Obama na makamu wake Joe Biden."
Bwana Clinton alikosoa vikali chama cha republican kwa kuzuia juhudi za uchepuzi wa uchumi na badala yake kujihusisha na mijadala kuhusu sera.
Kura za maoni zinaonyesha Barack Obama akiongoza kwa asilimia 47 huku mpinzani wake Mit Romney akimfuata kwa asilimia arobaini na sita.

Wachimba migodi waachiliwa huru

Wachimba migodi waachiliwa
Karibu wafanyakazi wote wa migodi ya madini nchini Afrika Kusini waliokamatwa katika vurugu za mwezi uliopita wameachiliwa.
Watu arobaini na wanne waliuawa katika vurugu hizo zilizowahusisha polisi na wafanyakazi wa migodi ya madini ya dhahabu ya Marikana.
Hatua hiyo imekuja wakati vyama vingi vya wafanyakazi wa migodi vimetiliana saini na kampuni ya migodi kumaliza mgomo ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya machimbo ya platinum.
Lakini makubaliano hayo hayakutiwa saini na chama muhimu kisichotambuliwa, ambacho ni kitovu cha mgogoro huo.
Kutoka katika vilima kuzunguka mji wa Rustenberg unaweza kuona machimbo yaliyosambaa, yakiwa yamezungukwa na kambi za maskwota, ambamo wanaishi wafanyakazi wa migodi hiyo na familia zao.
Hapa ndipo inapotoka asilimia sabini na tano ya madini ya dhahabu nyeupe ijulikanayo kama platinum inayozalishwa duniani.
Chama chao cha Taifa cha Wafanyakazi wa Migodi, kinachotambuliwa kisheria, kinaonekana kuwa karibu karibu sana na kampuni iliyosajiliwa Uingereza ya Lonmin.
Pia kinaonekana kuwa karibu zaidi na Rais Jacob Zuma. Kwa hiyo wafanyakazi wameelekeza macho yao kwa chama cha AMCU - chama ambacho hakitambuliwi na kampuni hiyo.
AMCU ilikuwa katika mazungumzo ya siku nzima hapo jana, yaliyosuluhishwa na makanisa na serikali. Lakini makubaliano yalipofikiwa wajumbe wa chama hicho cha AMCU walitoka nje. Kitu walichotaka ni kuboresha malipo yao na hakuna la kujadili zaidi.
Malalamiko yao yamechukuliwa na Julius Malema, ambaye alifukuzwa kutoka chama cha ANC wakitafuta mahali pa kusimamia malalamiko yao.
Na vikundi vingine vya mrengo wa kushoto vinawaunga mkono wachimba migodi hao.Lakini bei ya madini ya platinum ambayo imekuwa ikianguka kwa asilimia ishirini kwa mwaka mmoja uliopita, kampuni hiyo inasema haina uwezo wa kuwalipa zaidi wafanyakazi wa migodi hiyo.

Minara ya mawasiliano ya simu yashambuliwa

 

Ramani ya Nigeria
Takriban Minara 24 ya kurushia mawasiliano ya simu za mkononi imevamiwa kote nchini Nigeria.
Msemaji wa jeshi ameripotiwa akilaumu kundi la wapiganaji la Boko Haram kwa uvamizi huo wa kwanza wa aina yake dhidi ya kampuni tisa za huduma za simu.
Wataalamu wanasema kuwa uharibifu huo utagharimu kampuni hizo mamilioni ya dola.
Milio ya risasi na milipuko ilisikika huku moto mkubwa ukiteketeza minara hiyo Mjini Kano sawa na miji ya Maiduguri, Gombe na Bauchi.
Uvamizi mwingine ulitokea mjini Potiskum.
Msemaji wa jeshi mjini Maiduguri Luteni Kanali Sagir Musa, aliambia BBC kuwa maafisa wa usalama walishuku kundi la Boko Haram kwa uvamizi huo.
Kwa mujibu wa Luteni Kanali Musa, hii ni mbinu mpya ya mashambulizi ambayo imeanza kutumiwa na kundi hilo.
Siku ya Jumatano, kampuni tisa ziliripoti uharibifu uliofanyiwa minara yao 24. Duru zinaarifu kuwa baadhi ya kampuni zilizolengwa ni MTN ya Afrika Kusini pamoja na ile ya himaya ya nchi za kiarabu, Etisalat.
Boko Haram lilianza kufanya mashambulizi mwaka 2009 wakitaka sheria za kiisilamu kutumika, wakishambulia majengo ya serikali , makanisa na kuwaua wahubiri wa kiisilamu wenye msimamo wa kadri.

Wahamiaji wa kiafrika waombewa hifadhi Israel

Wahamiaji wa kiafrika nchini Israel
Shirika la kuwahudumia wakimbizi la umoja wa mataifa, UNHCR, limeomba Israel kuruhusu kikundi cha wahamiaji wa kiafrika kuingia nchini humo.
Wahamiaji hao wamekwama katika mpaka wa nchi hiyo na Misri kwa wiki moja sasa.
Wamekuwa wakitumia karatasi za plastiki kujikinga na jua kali ya jangwani
Waziri wa mambo ya ndani wa Israeli Eli Yishai, anasema sio kwamba hawahurumii wahamiaji hao kwa sababu ya masaibu wanayopata, lakini hofu yake ni kuwa ikiwa wataruhusiwa kuingia Israel, huenda hatua hiyo ikiwafanya mamia ya wahamiaji wengine kuingia nchini humo.
Israel imekuwa na visa vya ubaguzi wa rangi kwa wahamiaji wa kiafrika serikali ikiwafananisha na saratani.
Mnamo mwezi Juni, wahamiaji wanne wa kiafrika walijeruhiwa baada ya makaazi yao kuteketezwa na watu walioaminika kuwa wenyeji mjini Jerusalem.
Baada ya shambulio hilo ukawekwa ujumbe ukutani kuwataka wageni kuondoka eneo hilo. Katika siku za karibuni kumekua na hisia kali nchini Israel kuhusu jinsi ya kushughulikia wahamiaji elfu 60 kutoka Afrika.
Sheria mpya ilipitishwa nchini Israel kuwapa mamlaka maafisa wa uhamiaji kuwazuilia korokoroni wahamiaji haramu kwa miaka mitatu.Waathiriwa wa shambulio la wakati huo walikuwa raia wa Eriterea ambapo walipata majeraha ya moto mikononi.
Msemaji wa polisi nchini Israel Micky Rosenfeld aliambia BBC kwamba sio siri waafrika weusi wamekuwa wakilengwa na wenyeji.
Katika majuma ya karibuni ghasia zilitokea miji kadhaa ya Israel wanakopatikana wahamiaji wa kiafrika. Kusini mwa jiji kuu Tel Aviv biashara za waafrika zilishambuliwa huku waafrika wenyewe wakikejeliwa hadharani.
Polisi wanasema takriban wahamiaji elfu 60 wa kiafrika wanaishi Israel ambapo 35,000 wakikaa Tel Aviv na 5,000 wakiwa mjini Jerusalem.

Michelle Obama amuombea mumewe kura

Mkewe rais Obama , Michelle akihutubia kongamano la Democrats
Mkewe Rais wa Marekani, Barack Obama, Michelle, amehutubia kongamano la chama tawala cha Democratic ambapo alitetea haki ya mumewe kupewa nafasi kutawala taifa hilo kwa muhula wa pili.
Akiongea Kaskazini mwa Jimbo la Carolina, alimtaja mumewe kama mtu anayeelewa matatizo yanayowakumba wamarekani.
Alitetea hatua ya mumewe ya kuanzisha mpango maalumu wa bima ya afya ulioleta utata mwingi sana hasa miongoni mwa wanachama wa chama cha upinzani cha Republican walioupinga.
Alisema kuwa mumewe alinuia kutoa nafasi sawa ya matibabu kwa wote. Hata hivyo alikiri kuwa mageuzi aliyoahidi mumewe miaka minne iliyopita yalikuwa magumu kuyatekeleza lakini akasisitiza kuwa yatafaulu baadaye.
Rais Obama atahutubia kongamano hilo baadaye juma hili, ambapo atakubali rasmi kuwa mgombea wa Urais wa chama cha Democratic.

Thursday, September 6, 2012

Maharamia waiteka meli ya mafuta Nigeria


Meli kubwa ya mafuta
Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la wanamaji nchini Nigeria, Jerry Omodara, haijulikani iliko meli hiyo na kwamba juhudi za kuitafuta zinaendelea.
Shirika la kimataifa la mabaharia, liliambia shirika la habari la AFP kwamba mabaharia 23 walikuwa kwenye meli hiyo wakati ilipotekwa na walikuwa wamejifungia ndani ya chumba kimoja salama wakati wa tukio hilo.
Wadadisi wanasema kuwa visa vya uharamia vimekithiri katika maeneo mengi ya Afrika Magharibi.
Shirika la kimataifa la mabaharia, linasema liliweza kurekodi visa kumi na saba vya utekaji nyara wa meli nchini Nigeria, katika miezi ya kwanza sita ya mwaka huu. Linasema kumekuwa na ongezeko kubwa la visa hivyo ikilinganishwa na mwaka 2011.
Mkuu wa kituo cha shirika hilo cha kuripoti visa vya uharamia nchini Malaysia, Noel Choong, amesema kuwa wale waliofanya kitendo hicho, huenda ni kundi moja la maharamia walioteka nyara meli za mafuta nchini Togo mwezi jana, kuiba mafuta na baadaye kuwaachilia mabaharia waliokuwa kwenye meli hiyo.
Luteni Omodara anasema kuwa helikopta moja inatumiwa kuisaka meli hiyo katika juhudi za kuikoa.
Mwaka jana Nigeria na nchi jirani ya Benin zilianza mpango wa pamoja wa kuweka usalama baharani ili kupambana na uharamia.

Watu 34 wafariki kiwandani nchini India

Kiwanda cha fataki nchini India
Watu 34 wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa katika moto mkubwa uliotokea katika kiwanda cha fataki kusini mwa jimbo la Tamil Nadu, nchini India.
Moto huo katika kiwanda cha Om Shakti ulisababisha milipuko kadhaa ya fataki na moshi mkubwa kwenye kiwanda hicho kilichoko mjini Sivakasi, kitovu cha viwanda vya fataki nchini India.
Mji huo una mamia ya viwanda na hutengeza asilimia tisini ya fataki nchini humo.
Kwa mujibu wa afisaa mkuu wa polisi wilayani Virudhunagar, ambako mji wa Sivakasi uko, idadi ya waliofariki ilipanda hadi watu 34.
Aliongeza kuwa baadhi ya waathiriwa walikuwa wafanyakazi wa viwanda ingawa wengi walikuwa wenyeji wa vitongoji vya eneo hilo.
"baada ya mlipuko, watu walienda kiwandani kujionea na kwa bahati mbaya waliofika kushuhudia tukio hilo nao pia wakateketea'' alisema afisaa huyo.
Bwana Hoda alisema kuwa leseni ya kampuni hiyo ilikuwa imefutiliwa mbali kwa muda kwa sababu ya kukiuka sheria za usalama wa wafanyakazi na kwamba hakuna kazi ilipaswa kuwa inafanyika kiwandani humo hii leo. Aliongeza kuwa polisi wanamsaka mwenye kiwanda hicho.
Awali bwana Hoda aliambia BBC kuwa wazima moto walishindwa kuingia kiwandani kwa sababu milipuko ilikuwa bado inasikika.
"kuna joto jingi sana na hali ni ngumu kwa watu kuweza kuingia ndani ya jengo hilo. Kiwanda kina akiba kubwa ya fataki na milipuko bado inasikika'' alisema bwana Hoda.
Bado haijajulikana kilichosababisha moto huo.

Al-Senussi akabidhiwa kwa watawala wa Libya

Abdallah al-Senussi
Serikali ya Mauritania imewakabidhi maafisa wa utawala wa Libya aliyekuwa mkuu wa ujasusi nchini humo, Abdullah al-Senussi
Libya inataka kumfungulia mashtaka bwana Senussi kwa makosa aliyoyafanya chini ya utawala wa hayati Muamar Gaddafi.
Mapema mwezi huu rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz alisema kuwa bwana Sanusi aliyekuwa amekimbilia nchini humo, sharti kwanza akabiliwe na sheria kwa makosa ya kuingia Mauritania kinyume na sheria.
Senussi alitoroka Libya baada ya mapinduzi ya mwaka jana ambayo yalimng'oa mamlakani Muammar Gaddafi.
Pia anatakiwa na Ufaransa pamoja na mahakama ya kimataifa kuhusu haki za bianadamu ICC kwa makosa ya kukiuka haki za binadamu.
Ripoti za kukabidhiwa kwake kwa watawala wa Libya, zilitolewa na televisheni ya taifa pamoja na shirika rasmi la habari la Mauritania.
Kulingana na ripoti, bwana Senussi alikabidhiwa kwa wajumbe wa Libya walioongozwa na waziri wa sheria na haki wa nchi hiyo. Lakini hadi sasa bwana Senussi hajulikani aliko.

Wednesday, September 5, 2012

Ajali mbaya ya barabarani Morocco

Majeruhi waliookolewa kutoka kwa basi hiyo
Takriban watu 42 wamefariki baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuanguka katika Korongo kusini mwa Morocco.
Zaidi ya abiria wengine ishirini walipata majeraha mabaya.
Basi hilo lililokuwa linasafiri kati ya miji ya Marrakesh na Zagora, lilianguka umbali wa mita 150 kutoka barabarani
Wengi wa abiria waliokuwa wanasafiri kwenye basi hilo wanaaminika kuwa raia wa Morocco. Haijulikani ikiwa kuna majeruhi wowote wa kigeni walikuwa kwenye basi hilo.
Duru zinaarifu kuwa ajali hiyo ilitokea katika eneo lenye milima mapema leo asubuhi.
Bado haijulikani kilichosababisha ajali yenyewe ingawa afisaa mmoja mkuu anasema kuwa uchunguzi umeanzishwa.
Takriban watu 24 walijeruhiwa , ishirini na moja kati yao wakikimbizwa hospitalini mjini Marrakesh na waliosalia wakipelekwa hospitalini mjini Ouarzazate.
Katika taarifa yake, mfalme wa nchi hiyo Mohammed wa sita, alitoa rambi rambi zake kwa familia za waathiriwa na kuahidi kulipia usafiri na gharama za mazishi.
Mwezi Julai mwaka jana, ajali mbili tofauti za basi nchini humo zilisababisha vifo vya watu 26.
Zaidi ya watu 4,000 walifariki katika ajali tofauti za barabarani nchini Morocco mwaka jana kulingana na takwimu za wizara ya usafiri nchini humo.

Jeshi la Kenya lashambulia Kismayo

Mwanajeshi wa Kenya
Jeshi la wanamaji la Kenya limekiri kuwa lilishambulia mji wa Kismayo siku ya Jumatatu
Msemaji wa jeshi la Kenya kanali, Cyrus Oguna, aliambia BBC kuwa shambulizi hilo la hapo jana ni sehemu ya harakati za Muungano wa Afrika, dhidi ya wanamgambo wa Al Shabaab.
Wakaazi wa mji huo ambao unadhibitiwa na kundi la wapiganaji wa al-Shabaab, waliambia BBC kuwa walisikia milipuko katika meli zilizoko baharini.
Awali wanajeshi wa Kenya wakishirikiana na wale wa Ulaya na vikosi maalum vya Marekani walikana kuhusika na mashambulizi hayo.
Hata hivyo Duru zinasema kuwa sasa wameanza kupambana na wanamgambo wa Al Shabaab wanaodhibiti mji huo.
Wakati huohuo,duru zinaarifu kuwa kundi la Al shabaab nalo linajiandaa kwa mapambano hayo.
Al Shabaab hutumia mji huo kuingiza silaha zao kutoka nje na pia huwatoza kodi wafanyabiashara wanaotumia bandari hiyo kujikimu kimaisha.
Kismayo ndio mji mkubwa pekee uliosalia kudhibitiwa na Al Shabaab .
Wanajeshi wa Somalia wanaoshirikiana na wale wa Kenya wanaripotiwa kuukaribia mji huo wakiwa tu umbali wa kilomita hamsini kutoka mjini humo wakati wanajeshi wa Kenya wakisema kuwa wao wangali mbali sana na mji huo.
Inaarifiwa wasiwasi umekumba mji huo wakaazi wakisubiri mapambano ya kuudhubiti mji huo ambao ndio ngome kuu ya Al Shabaab.

Wakimbizi wanaotoroka Syria waongezeka

Wakimbizi kutoka Syria
Zaidi ya wakimbizi 100,000 wa Syria waliitoroka nchi yao mwezi Agosti pekee, hii ikiwa ndio idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kutoroka Syria tangu vita kuanza mwezi Machi .
Msemaji wa umoja wa Mataifa nchi humo amesema kuwa watu hao wanakimbilia nchi jirani.
Taarifa hii ya kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi wanaotoroka Syria ilielezewa kwenye mkutano kati ya rais Bashar al Assad na afisaa mkuu mtendaji wa shirika la msalaba mwekundu kuhusu hali ya misaada kwa Syria.
Misaada imeanza kupungua mjini Allepo mojawapo ya maeneo ambako mapigano yanaendelea, huku ikisemekana kuwa vigumu kuweza kufikia sehemu nyingi za mji.
Watu watano waliuawa leo katika mkoa wa kaskazini , siku moja tu baada ya watu wengine 25 kuuawa katika shambulizi la angani.
Wanaharakati wa upinzani walisema kuwa watu wengi walijeruhiwa katika shambulizi la makombora lililofanywa na majeshi katika eneo la Darat Izza mjini Allepo.
Wakimbizi wa Syria wakiwa kambini nchini Jordan
Kamanda mmoja wa jeshi ameripotiwa akiahidi kuwa atafanya kila awezalo kudhibiti mji huo katika siku kumi zijazo.
Afisaa mkuu mtendaji wa shirika la msalaba mwekundu anatarajiwa kukutana na maafisa wengine wakuu wa serikali ya Syria pamoja na kuzuru baadhi ya vitongoji vya mji mkuu Damascus vilivyoathiriwa na mapigano.
Hata hivyo hakuna maelezo yoyote yametolewa kuhusu mazungumzo ya bwana Maurer na Assad lakini msemaji wa shirika hilo, Cecilia Goin aliambia BBC kuwa shirika hilo linatazamia kuongeza juhudi zake za misaada kote nchini Syria.

Tuesday, September 4, 2012

Wachimba Migodi 122 waachiliwa Afrika Kusini


Wachimba migodi walioachiliwa
Wachimba migodi mia moja ishirini na wawili wa kampuni ya Lonmin yenye kuchimba madini ya Platinum wameachiliwa huru na Mahakama ya Kharankuwa iliyoko kaskazini mwa Pretoria.
Mara tu baada ya kuachiliwa wachimba migodi hao walikaribishwa nje ya mahakama na wenzao ambao walionekana kuimba nyimbo za kushangilia na kuwaelekeza katika eneo kulikotokea mauaji
Hatua ya kuachiliwa kwa wachimba migodi inakuja baada ya viongozi wa mashtaka kufutilia mbali mashtaka dhidi ya wachimba migodi 270 kufutia shinikizo za umma.
Wachimba migodi wa kwanza hao walikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya wenzao 34 waliouawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi.
Wakili wa wachimba migodi hao Bi Mapuli Kesi, alifurahia uamuzi huo wa mahakama na kunukuliwa akisema, "mimi ninayo furaha kubwa na ni ushindi mkubwa kwa kundi letu. Tumefanya kazi kubwa kufikia hapa tulipo."
Mwandishi wetu wa Afrika Kusini, Omar Mutasa, aliyekuweko mahakamani wakati kundi la kwanza la wachimba migodi lilipoachiliwa huru, alisema wachimba madini hao walilalamikia kile walitaja kuwa mateso mikononi mwa maafisa wa polisi.
Mmoja wao ambaye hakutaka kusema jina lake aliambia BBC, "polisi walikuwa wakali sana wakisema tusiwatazame na wakati mwingine walikuwa wakitutoa nguo na kutupiga marungu."
Hapo jana polisi waliwapiga riasasi na kuwajeruhi wachimba migodi wanne katika tukio tofauti .
Inadaiwa kuwa polisi walitumia risasi za mipira kuwatawanya waandamanaji katika Mgodi mwingine wa Gold Miners wanaogoma wakidai nyongeza ya mishahara ndipo wanne hao walipojeruhiwa.
Kisa hiki kinafuatia kuuwawa kwa wachimba migodi wengine 34 wakati walipopigwa risasi na polisi wiki mbili zilizopita.
Mazungumzo yanayolenga kusitisha mgomo wa wachimba migodi hao wa mgodi wa madini ya Platinum wa Marikana, vile vile yalitarajiwa kuanza hapo jana.
Polisi wanadai kuwa walilazimika kuwafyatulia risasi wachimba migodi hao kama hatua ya kujilinda kwani na wao walikuwa wamejihami kwa mapanga wakati wakikabiliana nao.
Mgomo wao ulioitishwa kulalamikia nyongeza ya mishahara pamoja na kutaka chama chao kipya cha wafanyakazi kutambuliwa, ungali unaendelea huku mgodi ukisalia kufungwa kwa wiki tatu sasa.
Hata hivyo kampuni inayomiliki mgodi huo, Lonmin, ambayo ndio ya tatu kwa ukubwa wa uzalishaji wa madini hayo, imesema kuwa mgomo huo ni haramu.
Lakini imetupilia mbali matakwa yake kuwa ikiwa wafanyakazi hao hawatarejea kazini , watafutwa kazi.
Baada ya ufyatuliaji risasi, viongozi wa mashtaka wa serikali, walitumia kanuni ya enzi ya ubaguzi wa rangi ya kosa la ujumla kuweza kuwafungulia mashtaka wachimba migodi 270 waliokamatwa wakati wa vurugu baada ya mgomo wao kuwalazimisha polisi kuwafyatulia risasi.
Kanuni hiyo ilitumika na walowezi wa kizungu wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi kuwanyanyasa wapinzani wao waafrika weusi.

Ustaarabu na Ushenzi ni vitu vinavyofanana

Ustaarabu...

Ustaarabu na ushenzi ni vitu vinavyo fanana sana. Na wala sio rahisi kupambanua upi ni ustaarabu hasa na upi ni ushenzi. Kwa maana kile kinachoitwa ustaarabu kwa mtu mmoja kinaweza kuwa ushenzi kwa mtu mwingine na ushenzi kwa huyu unaweza kuwa ustaarabu kwa yule.
Mdada asilia

Si ajabu wakoloni walipokuja waliuita utamaduni wetu eti ni wa kishenzi. Tunapoishi katika jamii tunaupima ustaarabu kutokana na kawaida (norms) ya watu wanao tuzunguka. Tatizo ni kwamba mara nyingine huo tunaouita ustaarabu kumbe ndio ushenzi hasa kuliko ule tunaodhania kuwa ndio ushenzi.

Halle Berry
Inanishitua sana ninaposikia kampeni za kuhimiza kukubalika kwa ndoa za jinsia moja. Inanishangaza ninapoona viongozi wa dini na watu wanaoheshimika sana wakisisitiza wanaume wanaojifanya wanawake na wanawake wanaojifanya wanaume wapewe haki ya kufunga ndoa na kuheshimiwa kama wanandoa wengine kwa sababu eti huo ndio ustaarabu.  Inanisumbua ninapoona wanawake na wanaume wakijitembeza mitaani kuuza uroda kana kwamba ni njugu kwa madai kwamba huo ni ustaarabu...

Jeniffer Lopez

Inaniuma sana ninapoona wezi wa mali ya umma wakitukuzwa, kushangiliwa, kulindwa na kupewa nafasi zajuu zaidi za uongozi kwa sababu eti huo ndio ustaarabu...Inanikera ninapoona viongozi wanazidi kujilimbikizia mali, kujenga himaya za kifalme, kutumia mabilioni ya shilingi za wavuja jasho kwa matumizi yasiyo ya lazima huku wakiwaacha wananchi wakiteseka kwa kukosa huduma muhimu kama afya (matibabu) umeme, maji, na usafiri wa kuaminika mijini. Inanitia kichefuchefu kwamba madaktari wetu wanafikia kugoma kwa madai ya fedha huku wanasiasa wakilimbikiziwa posho kiasi cha kuogopa kuzipokea kwa aibu...huu nao ni ustaarabu. 

Lady Gaga

Zaidi ya yote inaniuma sana ninapoona watoto wetu wakifundishwa ubinafsi, kutothamini utu, kutomuogopa Mungu kwa imani kwamba hayupo (ha exist) na kupewa uhuru mkubwa kuliko mtoto anaostahili kuwa nao kwa kisingizio cha haki za watoto, eti  nao ni ustaarabu...Wallah kama huu ndio ustaarabu ni bora turudi kwenye kutembea uchi maana naamini watu walikuwa wastaarabu zaidi kuliko sasa...
 

Televisheni ya Misri yaruhusu hijabu

Wanawake wa Misri waliovaa hijabu, wakipiga kura mwezi May
Serikali ya Misri imeondoa amri iliyopiga marufuku wasomaji habari kwenye televisheni kuvaa hijabu.
Jumapili taarifa ya habari ya mchana kwenye televisheni ya taifa ilisomwa na mwanamke, Fatma Nabil, ambaye alifunika kichwa na kitambaa cha rangi ya maziwa.
Afisa wa televisheni ya Misri alisema wanawake sasa wataambiwa nao wafuate, na kwamba hawatahatarisha kazi zao wakivaa hijabu.
Amri ya marufuku iliwekwa na serikali zilizopita za Misri.
Baadhi ya wasomaji wa habari waliishtaki televisheni ya taifa na walishinda, lakini baada ya hapo hawakuruhusiwa kuonekana mbele ya kamera.

Mshirika wa Aboud Rogo ajikabidhi kwa polisi

Mtu anayesemekana kuwa mshirika wa karibu wa mhubiri aliyeuawa wiki jana mjini Mombasa, Kenya, Sheikh Aboud Rogo, amefikishwa mahakamani kwa kosa la uchochezi wa ghasia na kufanya mauaji.
Abubaker Sharif anayejulikana kwa jina lengine kama Makaburi, awali alikuwa amedai kuwa maisha yake yamo hatarini na hata kudai kuwa maafisa wa serikali walikuwa na njama ya kumuua.
Polisi wanasema walikuwa wametoa kibali cha kumkamata ingawa Abubakar aliweza kujikabidhi mwenyewe kwa polisi.
Hata hivyo amekana madai hayo dhidi yake.