NJOMBE

NJOMBE

Thursday, February 2, 2012

Mbunge ahoji Bodi ya Mikopo kupewa fedha nyingi


MBUNGE wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (CHADEMA), amehoji sababu za serikali kutoa fedha nyingi kwa Bodi ya Mikopo ya Vyuo vya Elimu ya Juu wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu. Mbunge huyo alisema wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu serikali imetoa fedha nyingi kwa Bodi ya Mikopo, wakati ambao hakuna uchaguzi pesa zinapungua.
Kutokana na hali hiyo, Mtinda alitaka kujua ni kuna uwiano gani wa kimapato na kwanini mikopo ya wanafuzi wa vyuo isipitie moja kwa moja kwenye akauti zao badala ya akauti za vyuo ambazo hutumiwa vibaya na wahasibu kwa kutumia majina feki.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema si kweli kuwa mapato ya serikali yanapanda wakati wa Uchaguzi Mkuu na kusababisha fedha nyingi kupelekwa katika Bodi ya Mikopo.
Kawambwa alisema serikali inapeleka fedha kwenye Bodi ya Mikopo kulingana na mapato yaliyopo na wala si kutegemea kipindi cha uchaguzi kama alivyosema mbunge huyo.
Alidai kuwa serikali haitabadilisha msimamo wake wa kutuma fedha katika vyuo kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza hali ya kutuma fedha kwenye akaunti ya mwanafunzi ambaye aliacha masomo muda mrefu.
Hata hivyo Dk.Kawamba alisema kuwa serikali itahakikisha inasimamia vema fedha hizo ili zitumike kwa makusudi tarajali na si vinginevyo.

bil.117/- zahitajika ujenzi wa U/Ndege Msalato

SERIKALI imesema inahitaji sh bilioni 116.95 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya wa ndege uliopo Msalato mkoani Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athman Mfutakamba, alipokuwa akijibu swali na Mbunge wa Bahi, Omary Badwel (CCM) aliyetaka kujua ujenzi wa uwanja huo utaanza lini.
Badwel alihoji kiwanja hicho kinatarajiwa kuwa na ukubwa gani kulingana na mahitaji ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.
Mfutakamba alisema serikali inatambua umuhimu wa kuwa na kiwanja kikubwa cha kisasa cha ndege mkoani hapa.
Alisema kutokana na hilo hatua za awali za ujenzi huo zilianza ikiwamo kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato kwa gharama ya sh milioni 715.5 kupitia msaada wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo kwa Afrika (BADEA).
Alisema serikali imekamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo ambapo wananchi 1,432 wameshalipwa.
“Kazi ya kusafisha maeneo yatakayojengwa miundombinu ya kiwanja kama vile barabara ya kurukia ndege, jengo la abiria na miundombinu mingine ya kiwanja imekamilika,” alisema.
Alisema kwa sasa wanaendeleza majadiliano na washirika wa maendeleo ya taasisi mbalimbali za kifedha kwa ajili ya kukusanya fedha za ujenzi wa uwanja huo.

CCM waweka kambi karibu na CHADEMA

WAKATI kampeni za vyama mbalimbali zikiwa zinaendelea katika Jimbo la Uzini, Visiwani Zanzibar za kumsaka mwakilishi wa jimbo hilo, Chama cha Mapinduzi (CCM), nacho kilihamishia ngome yake hatua chache kutoka ilipo ngome ya CHADEMA.
Mwandishi wetu alishuhudia makada wa chama hicho wengine wakiwa wamevalia sare za CCM majira ya saa moja jioni wakiwa wanashusha vyombo na vyakula mbalimbali kutoka katika gari.
Mmoja wa wakazi wa Uzini, aliliambia Tanzania Daima kuwa kutokana na ukaribu wa kambi hizo mbili kuna hatari kubwa ya kuwapo kwa vurugu baina ya wafuasi wa vyama hivyo.
“Hawa jamaa ni sawa na Simba na Yanga, naliomba Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi eneo hili kwani wakati wowote mambo yanaweza kubadilika,” alisema.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, alisema uamuzi wa CCM kukaa karibu na kambi ya chama hicho si mzuri na unaonyesha walivyo wachokozi.
Lwakatare alisema chama chao kimejipanga vilivyo kwa lolote litakalotokea na kuwaonya CCM kuwa wasithubutu kuanzisha fujo na Jeshi la Polisi kuwa macho kwa kuwapo dalili za uchokozi za CCM.

Sumaye ang’ang’aniwa bungeni

MBUNGE wa Mvomero, Amos Makalla (CCM), amemtuhumu Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kwamba amekwapua ekari 326 za shamba la ushirika la wilayani Mvomero lililopaswa kugawanywa kwa wanakijiji wa Mvomero, mkoani Morogoro.
Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo alihoji utaratibu uliotumiwa na serikali kumuuzia Sumaye shamba hilo badala ya kuwapa wananchi kipaumbele.
Makalla alitoa tuhumu hizo jana wakati akiuliza swali bungeni katika kipindi cha maswali na majibu ambapo pia aliitaka serikali itoe tamko kuhusu shamba hilo kwakuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni zake mwaka 2010, aliwahi kuahidi kushughulikia kero hiyo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole-Medeye, alisema kuwa shamba hilo lenye hati namba 21919, lililoko katika Kijiji cha Mvomero, Wilaya ya Mvomero, linamilikiwa na mke wa Sumaye, Esther Sumaye kihalali.
Alisema kabla ya shamba hilo kumilikiwa na Esther Sumaye, lilikuwa likimilikiwa na Onasaa Waryaeli Kisanga na Mesaki Josiah Ndanshau, wakitumia jina la Mvomero River Farm Limited kwa hati namba 211919.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, kumbukumbu zilizoko kwenye wizara yake zinaonyesha kuwa awali shamba hilo lilikuwa likimilikiwa na Mvomero River Farmers Limited ya Morogoro kuanzia mwaka 1978 hadi Julai 1985 lilipohamishiwa kwa Kampuni ya Wami & Magole Farmers Co-operative Society ya Morogoro.
Alisema Machi 1966 Kampuni ya Wami & Magole Farmers Cooperative Society Limited, ilibadili jina na kuitwa Morogoro Farmers Primary Society Limited.
“Aidha, tarehe 27, Novemba 2001, Morogoro Farmers Primary Co-operatives Ltd, walimuuzia Esther Sumaye shamba hilo na baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipa ushuru kwa serikali, uhamishwaji wa miliki ulikamilishwa mwaka 2002 kwa mujibu wa kifungu cha 61 cha sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999,” alisema naibu waziri.
Kwa kuwa Esther Sumaye ana miliki shamba hilo kihalali na kuliendeleza kwa kuzingatia masharti ya hatimiliki, waziri alisema serikali inaheshimu haki zake na kwenye ibara ya 24 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Alisisitiza kuwa kwa kuwa mwenye shamba aliamua kumuuzia Sumaye na kuwanyima wananchi, serikali inaheshimu haki hiyo na kuongeza kuwa shamba hilo ni mali ya Sumaye.
Kwa muda mrefu sasa, Sumaye na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa wamekuwa wakilalamikiwa kujitwalia maeneo makubwa ya ardhi kifisadi mkoani Morogoro, hivyo wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiomba serikali iwapokonye vigogo hao na kuligawa kwa wananchi.
Hata hivyo Sumaye amepata kujitokeza hadharani mara nyingi kupinga madai kwamba amepora ardhi hiyo na badala yake amekuwa akisisitiza kuwa ana miliki kihalali.

Wednesday, February 1, 2012

Mgomo wa madaktari kutikisa Bunge leo


SERIKALI leo inatarajia kutoa kauli bungeni juu ya hatma ya mgomo wa madaktari unaoendelea nchini ambapo umedumu kwa wiki mbili sasa.
Akizungumza kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge jana, Spika wa Bunge, Anna Makinda, alisema kuwa serikali imeshapata maombi kwa ajili ya kutoa kauli  juu  ya mgomo huo ulioleta athari kubwa nchini.
Spika alitoa kauli hiyo wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, aliyetaka kujua serikali inatoa kauli gani juu ya mgomo wa madaktari nchini.
Zitto aliitaka serikali kutoa kauli juu ya mgomo huo pia ni lini madaktari hao wangelipwa haki zao.
Akijibu hoja hiyo Makinda alisema kuwa tamko la serikali litatolewa leo na hali hiyo inatokana na kuwepo kwa utaratibu unaotaka kauli ya serikali katika suala hili, upitie kanuni na taratibu za kibunge.
“Kwa kuwa serikali ilishapokea maombi ya kutoa tamko ni lazima waziri aandike tamko hilo na kulichapisha ili anapolisoma bungeni, liwe limeandikwa na liweze kusomwa na wabunge wote,” alisema.
Mbali na hilo alisema ni lazima pia tamko hilo lipitie katika kamati ya uongozi ya Bunge ili liweze kujadiliwa na baada ya hapo, litapelekwa kwa Spika na kutoa baraka za kuileta bungeni.
Wakati serikali ikijiandaa kutoa tamko bungeni, tayari serikali hiyo hiyo kupitia kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilishatoa kauli na kuwapa madaktari hao saa 24 warejee kazini, vinginevyo wahesabu kwamba wamejifuta kazini.
Pamoja na tamko hilo la vitisho, bado madaktari hao wameendelea na mgomo wao hadi jana na vifo vingi vimeripotiwa kutokea sehemu mbalimbali nchini kutokana na mgomo huo.

Wanajeshi waanza kazi Muhimbili

MADAKTARI wanajeshi 15, kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), jana walianza  kutoa huduma za kitabibu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Madaktari hao walipelekwa katika Idara ya Magonjwa ya Dharura huku Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Haji Mponda akiahidi kuongeza wengine 80 kutoka wizarani kwake.
Mwandishi wetu alitembelea baadhi ya wodi katika hospitali hiyo na kuona wagonjwa wasiozidi 10, ilhali wodi hizo zinachukua kati ya wagonjwa 80 hadi 90.
Mmoja wa wagonjwa aliyelazwa katika jengo la Kibasila, wodi namba 14, ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema  jana asubuhi daktari mmoja alipita na kumchoma sindano.
Katika Jengo la Kibasila, wodi namba 12, msimamizi wa wodi hiyo, bila kujua kuwa alikuwepo mwandishi wa habari hizi, alisikika akimwambia mfanyakazi mwingine wa hospitali hiyo, wauguzi tokea juzi hawapo wodini kwa kuwa wako kwenye mkutano wao unaoendelea.
Awali akizungumza na waandishi wa habari, ofisa habari wa hospitali hiyo, Aminaeli Eligaesha, alisema juzi katika eneo hilo la Idara ya Magonjwa ya Dharura, ambako wamewekwa madaktari hao wa JWTZ, wagonjwa hawakupokelewa kutokana na mgomo uliopo.
Alibainisha kuwa mkuu wa idara hiyo, Profesa Victor Mwafongo, aliamua kuomba msaada na ombi hilo liliitikiwa vema kwa madaktari  wa JWTZ kupelekwa hospitalini hapo jana.
“JWTZ wametupatia madaktari 15, wameripoti leo (jana) saa mbili asubuhi, sasa hivi wanatembea kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali,” alisema Aligaesha.
Alisema madaktari hao wanajeshi waliofika hospitalini hapo wote ni mabingwa kwa kuwa wako wenye fani ya upasuaji, magonjwa ya wanawake, watoto na meno.
Alitoa wito kwa Watanzania kuwapeleka wagonjwa hospitalini hapo, kwa kuwa hali hivi sasa imetengamaa na kwamba mambo mengine yanaendelea kurekebishwa.
Waziri wa Afya
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, alifika hospitalini hapo, jana asubuhi kuangalia athari za mgomo huo uliodumu kwa takriban wiki mbili sasa.
Alisema baada ya hali ya hospitalini hapo kusuasua serikali imepeleka wanajeshi hao na pia wizara yake inatarajia kupeleka madaktari 80 ambao watatawanywa kwenye vitengo tofauti kuongeza nguvu kwa wachache waliopo.
Waziri huyo alisema mlango wa serikali wa kuzungumza na madaktari hao bado uko wazi, kwa kuwa kuna taratibu za kufuata kwa watumishi wa umma ili wazungumze na kufikia muafaka.
Wanaharakati wazungumza
Wanaharakati  hapa nchini wametoa wito kwa serikali na madaktari kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili huduma za afya zitolewe kama ilivyokuwa kabla ya mgomo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sikika, Irene Kiria, aliitaka serikali iache kulifanya suala hilo kuwa la kisiasa bali walipe uzito kwa sababu linagusa uhai wa wananchi wengi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alihoji kauli aliyoitoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwa kama madaktari wasingerudi kazini, serikali ingetumia wanajeshi.
Dk. Kijo-Bisimba, alihoji kama hospitali za majeshi nchini zina madaktari wa kutosha kwa nini hawatoi huduma kwa watu wakati taifa lina upungufu wa madaktari kwa zaidi ya asilimia hamsini.
“Madaktari hao watakapoondolewa kwenye hospitali zao, je huduma katika hospitali hizo walizotoka zitakuaje?
“Je madaktari wa jeshi malipo yao yanatofautiana na madaktari wetu wa kawaida? Gharama za kuwapeleka kwenye hizo hospitali na kuwatunza hazitakuwa zimeongeza mzingo mwingine kwa taifa?” alihoji mkurugenzi huyo.

Madaktari, serikali zungumzeni - Wahariri

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limeshauri serikali na madaktari kukaa katika meza moja ya mazungumzo ili kutafuta muafaka wa mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.
Taarifa ya TEF iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wake, Neville Meena, ilisema majadiliano hayo yatakayofikiwa na pande hizo mbili, yalenge kutatua matatizo ya madaktari, lakini pia yazingatie uwezo wa serikali.
Meena alisema lengo liwe kuwawezesha madaktari kadiri uwezo wa serikali unavyoruhusu sambamba na kuwaokoa wagonjwa wanaokabiliwa na hatari kubwa kwa sababu ya kukosa tiba.
“Madaktari wakubali kurejea kazini haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya watu ambao wanapoteza maisha kutokana na kukosa tiba, wakati wagonjwa wakiwa si sehemu ya mgogoro uliopo,” alisema katibu huyo.
Vile vile, Meena aliishauri serikali kufuta amri zake zote dhidi ya madaktari ambao hawakuripoti kazini juzi, ili kuwezesha mazungumzo ya pande zote mbili kufanyika.
“Baada ya maafikiano kuwapo, usiwepo mpango wowote wa wazi au wa kificho wa kuwaadhibu kwa namna yoyote ile viongozi wa madaktari waliogoma kwani tunaamini kwamba madai yao yalikuwa halali,” alisema.

Slaa akutana na JK

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa tamko iwapo ameridhia wananchi waendelee kufa kwa kukosa huduma za afya kwa kukataa kuwaongezea posho madaktari huku akiidhinisha posho ya sh 330,000 kwa siku kwa wabunge.
Amesema Rais Kikwete amekuwa mgumu kuongeza posho kwa watu wanaotoa huduma muhimu kama madaktari na walimu, lakini amekuwa mwepesi kwa wanasiasa ambao hukaa kimya bungeni na wengine kuishi kupiga makofi.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akizungumza na Tanzania Daima, kwa njia ya simu. Dk. Slaa alisema iwapo Rais Kikwete hatatoa tamko kuhusu suala hilo, CHADEMA itayatumia majukwaa kuwaeleza wananchi.
Alisema CHADEMA imekuwa ikilaumiwa kwa kuishtaki serikali kwa wananchi kila inaposhindwa kuwajibika lakini hivi sasa hawatakali wala kuogopa lawama hizo kwakuwa hazina msingi.
“Sasa imetosha. Rais Kikwete atoe tamko  kama ameidhinisha wananchi waendelee kufa kwa kugoma kupandisha posho ya sh 10,000 kwa madaktari na kuwaongezea wabunge.  Hivi anataka nchi iendelee hivi hadi lini?” alihoji.
Alisema kuwa madaktari wengi nchini wanafanya kazi katika mazingira magumu huku wakihatarisha maisha yao kutokana na kuwapo katika hatari ya kuambukizwa magonjwa, lakini serikali haiwajali kwa kiwango inachowajali wanasiasa.
Alibainisha kuwa serikali inapaswa kulaumiwa kwa hali inayoendelea sasa nchini kwa wananchi kufa kutokana na kukosa huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali hapa nchini.
Aliongeza kuwa mgomo wa madaktari umeonyesha kuwa serikali imekosa umakini katika vipaumbele vyake na hivyo kuwafanya wananchi waishi maisha ya taabu kila kukicha.
“Rais Kikwete alipaswa kukaa chini na kuziongezea posho kada zote … sasa hakuna uwiano, jambo ambalo ni hatari kwa nchi. Mwaka 2007 niliwahi kusema bungeni kuwa kuna bomu litalipuka, Pinda (Waziri Mkuu, Mizengo Pinda) alikataa,” alisema.
Juzi, Waziri Mkuu alikaririwa akisema kuwa Rais Kikwete ameidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) kwa wabunge kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 kwa siku.
Kuidhinishwa kwa posho hiyo kunafanya sasa mbunge kupokea sh 330,000 kwa siku. Sh 200,000 ikiwa ni posho ya kikao, sh 80,000 posho ya kujikimu na sh 50,000 nauli.
Pinda  alitoa taarifa hiyo katika kikao cha utangulizi cha wabunge ambako inaelezwa kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), na mbunge wa Bumbuli, January Makamba (CCM) walipinga suala hilo.
Mjadala wa kupanda kwa posho hizo umeligawa taifa tangu kuibuliwa kwake huku baadhi ya makundi yakipinga ongezeko hilo.
Jana Spika wa Bunge, Anna Makinda, alisema posho hizo mpya zimeanza kulipwa kuanzia jana baada ya kupitishwa na ngazi zinazohusika.

JK aahidi kujenga mahakama Arusha


RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali itagharimia ujenzi wa makao makuu ya kudumu ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (ACHPR) mjini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari  na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema, Rais Kikwete anaunga mkono mageuzi yanayokusudiwa kufanywa kwenye muundo wa mahakama hiyo.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa ujenzi huo unalenga kuiwezesha mahakama hiyo kuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuzitolewa uamuzi kesi za makosa ya jinai sawa na mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ya mjini The Hague, Uholanzi.
Ahadi hiyo ya Rais Kikwete aliitoa wakati akizungumza na ujumbe wa majaji wa mahakama hiyo, wakiongozwa na rais wake, Jaji Gerald Niyungeko, mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Kikwete aliwaambia majaji kufikiria kuwa na mchoro wa jengo zuri lenye hadhi la mahakama hiyo, kwani itakuwa ni mahakama ya bara zima na wala siyo ya Tanzania pekee.
Rais pia aliwaahidi kuwa serikali itaongeza kasi ya kutafuta ardhi kwa ajili ya ujenzi wa mahakama hiyo mjini Arusha, kutokana na mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa AU uliomalizika jana kukubaliana ujenzi mjini humo.
Jaji Niyungeko alimweleza Rais Kikwete kuhusu shughuli za mahakama hiyo, ambapo aliishukuru serikali kwa mchango wake mkubwa katika kuunga mkono shughuli za mahakama hiyo.
Jaji huyo alisema mahakama hiyo sasa imeanza kupokea kesi nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo ambapo kwa kipindi cha mwaka jana ilipokea kesi 14, ikiwamo moja kutoka Tanzania, na maombi mawili ya kuitaka mahakama hiyo kutoa ushauri wa kisheria.

Halmashauri Singida zaongoza kwa rushwa

HALMASHAURI za wilaya na manispaa mkoani Singida zimeendelea kuongoza kwa matukio 58 dhidi ya malalamiko 85 ya kuomba na kupokea rushwa katika kipindi cha mwaka jana.
Halmashauri hizo ambazo zinadaiwa kuwa zimejaa wabadhirifu wa mali za umma, zimeongoza kwa kulalamikiwa kwa matukio hayo ikiwa ni asilimia kubwa ikilinganishwa na ofisi nyingine.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida, Julliane Kallasa, alisema jeshi la polisi linashika nafasi ya pili kwa kuripotiwa kuwa na matukio tisa.
Alitaja taasisi nyingine na idadi ya malalamiko yake yakiwa kwenye manbano kuwa ni mahakama (1), taasisi binafsi (7) na taasisi zinginezo (10).
Alisema vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kwa mwaka jana, viliongezeka na kufikia 85 tofauti na mwaka juzi ambapo zilikuwa 80.
Pamoja na mambo mengine alisema mwaka jana jumla ya kesi nne zilifunguliwa mahakamani ikilinganishwa na kesi mbili za mwaka juzi.
“Kesi moja ilitolewa hukumu mwaka jana ambapo mtuhumiwa Elipharaja Hamisi  Omari, Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Shati wilayani Iramba, alipatikana na hatia ya kuomba na   kupokea rushwa. Alihukumumiwa adhabu ya kutumikia jela miaka mitatu,” alisema Kallasa bila kutaja aina ya rushwa na kiasi alichopokea mshtakiwa.
Mkuu huyo wa Takukuru alisema katika kesi zingine mbili za watuhumiwa Wilson Ngasa Gasule toka sekretarieti ya mkoa wa Singida na Gerwin Lyaheja toka ofisi ya mkuu wa wilaya, hawakupatikana na hatia na waliachiwa huru na mahakama ya mkoa.
Akifafanua, alisema washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kutumia nyaraka ili kumdanganya mwajiri wao wajipatie fedha, kitendo ambacho ni kinyume na sheria no.22 ya PCCA ya mwaka 11/2011.
“Pia mtuhumiwa Khalifa Abdala Kisumo, ofisa tabibu wa hospitali ya mkoa wa Singida, naye aliachiliwa huru na mahakama baada ya kushahidi kushindwa kumuunganisha na kosa la kuomba na kupokea rushwa,” alisema.
Alitoa wito kwa viongozi na watendaji katika mkoa wa Singida kusimamia vizuri rasilimali za umma ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mwenyekiti CCM ampa kipigo katibu wake

HALI ya kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Maswa, mkoa wa Shinyanga, si shwari kutokana na mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, Peter Bunyongoli, kumpatia kipigo katibu wake, Omari Kilolo, baada ya kutofautiana katika kikao cha kamati ya siasa.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho na kuthibitishwa na baadhi ya wajumbe kilichofanyika katika ofisi ya katibu wa CCM wilaya  iliyoko mjini humo  zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Jumatano iliyopita, majira ya saa 7:30 mchana.
Wajumbe hao wakizungumza na waandishi wa habari mjini Maswa jana kwa masharti ya kutotajwa majina, walieleza chanzo cha katibu huyo kupata kipigo ni hoja iliyokuwa ikijadiliwa ya matumizi ya fedha sh milioni 26 zilizotokana na malipo ya mnara wa simu za mikononi wa kampuni ya Vodacom ulioko juu ya jengo la ghorofa moja la ofisi hiyo.
Viongozi hao waliendelea kushutumiana juu ya matumizi mabaya ya fedha hizo huku kila mmoja akimtupia lawama mwenzake, jambo ambalo lilizua mtafaruku mkubwa ndani ya kikao hicho.
“Wakati tukiendelea na hoja hiyo viongozi hao kila mmoja alianza kumtupia lawama  mwenzake juu ya matumizi mabaya ya fedha hizo ambazo zilianza kutumika tangu katika kampeni za uchanguzi mkuu uliopita,” alisema mjumbe mwingine.
Habari zaidi zinazidi kueleza kuwa katibu huyo aliendelea kumtupia lawama mwenyekiti wake kwa kushindwa kukisimamia chama tangu aliposhindwa ubunge wa jimbo la Maswa Mashariki na Mbunge wa sasa Sylvester Kasulumbayi (CHADEMA), hivyo kukitelekeza hadi alipoibukia katika kikao cha kamati ya siasa na kumtupia lawama juu ya matumizi ya fedha za mnara.
Kauli hiyo ndiyo iliyompandisha hasira mwenyekiti huyo na kusimama na kuanza kumshambulia kwa kumpiga ngumi, jambo ambalo liliwashangaza wajumbe na ndipo Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Kapteni James Yamungu alipotaka busara itumike katika kufikia muafaka jambo hilo.
“Akizungumzia tukio hilo, katibu wa CCM wilaya ya Maswa, Omari Kalolo, alikiri kupata kipigo kutoka kwa mwenyekiti wake na kusisitiza kuwa kitendo alichokifanya hakipaswi kufanywa na kiongozi.
“Ni kweli mwenyekiti wangu amenipiga ngumi tukiwa ndani ya kikao cha kamati ya siasa, nimesikitika sana,  kwani jambo hili si siri kwani kwa sasa kila mtu analifahamu na kitendo alichokifanya hakikupaswa kufanywa na kiongozi aliyepewa dhamana ya kusimamia ilani ya chama chenye kuongoza dola,” alisema.
Alipotafutwa kwa njia ya simu mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa, Peter Bunyongoli, kuzungumzia tukio hilo simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita mara kwa mara bila kupokelewa.

CHADEMA:Waonya juu ya Raza

Msimchague Raza si mwadilifu
BAADA ya  Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutupilia mbali pingamizi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kusimamishwa kwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mohamed Raza, kutokana na kuvunja sheria ya uchaguzi katika kipengele cha uchukuaji fomu, chama hicho kimewataka wananchi kutomchagua mgombea huyo kwa kuwa sio mwadilifu.
Kauli hiyo ilitolewa jana  katika kijiji cha Dagaa na Manzese, visiwani hapa na meneja wa kampeni wa CHADEMA, Saidi Mzee, na kuongeza kuwa
Raza alishindwa kulipa sh 1,500 kwa ajili ya fomu, hivyo ni wazi ameshaiibia nchi na ataendelea kuiibia.
Alisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kumchagua Raza kwa kuwa anawania nafasi hiyo kwa ajili ya kupata urahisi wa kupitisha bidhaa zake na si kuwakomboa wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alisema watakaposhika nchi wataruhusu biashara ya gongo na kwamba kabla ya kukuzwa  itaboreshwa ili iweze kuwaingizia wananchi kipato.
Dk. Slaa alisema nchini  Uganda pombe hiyo imekuwa ikiwanufaisha watengenezaji ambao wanaiuza ndani na nje ya nchi yao, hivyo haoni sababu ya Tanzania kuendelea kuizuia.
Kuhusu upandaji holela wa bei ya sukari, Dk. Slaa alisema hali hiyo inasababishwa na ndoa kati ya CUF na CCM na kuongeza kuwa CUF kwa sasa haiwezi kutetea tena wananchi.
Alisema CHADEMA imeamua kuingia visiwani humo baada ya CUF kushindwa kukemea maovu kwa muda mrefu na kueleza kuwa wanaamini mgombea wao Ali Mbarouk Mshimba atafanya vizuri wakimchagua.
Dk. Slaa aliahidi kampeni zao zitaendelea nyumba kwa nyumba hadi usiku wa manane mpaka kieleweke na kuongeza kwamba  2015 lengo la chama hicho ni kushika baraza la wawakilishi.
Kwa upande wake mgombea Ali Mbarouk Mshimba, aliwataka wakazi hao kumpa kura za ndio kwa kuwa ni mzaliwa wa Uzini na pia anafahamu shida za wananchi.
“Mnajua wazi CCM imeua sera za chama cha Afro Shirazi party, hivyo itumieni hii fimbo ya karibu kuua nyoka badala ya mbali inaoishi Mji Mkongwe,” alisema

Mbunge CCM ahoji mshtaki kumhudumia mshtakiwa

MBUNGE wa Viti Maalumu Agnes Hokololo (CCM) jana aliitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu washtaki kuendelea uwahudumia washtakiwa wao.
Mbunge huyo alitaka kujua hali hiyo kutokana na kile alichokieleza kuwa ni usumbufu na baadhi ya watu wanashindwa kuwapeleka watu mahakamani kuhofia gharama hizo.
“Hivi hii serikali haioni kuwa kumhudumia mshtakiwa kwa kutumia gharama za mshtaki wake unakuwa ni mzigo?’’ alihoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Balozi Khamis Kagasheki alikiri kuwa utaratibu huo upo kwa muda mrefu na kusema serikali inautazama kwa karibu sasa.
Hata hivyo katika hali ya kawadia Kagasheki alisema hata yeye hana majibu ya kama utaratibu huo ni sahihi au si sahihi lakini anachojua ni kwamba ulikuwepo tangu mwanzo.
Kuhusu kuunga mkono juhudi za wananchi katika ujenzi wa vituo vya polisi kila kata, Balozi Kagasheki alisema ni mpango wa serikali katika kuimarisha ulinzi.

Feza za rada Bil.18/- kununua madawati

Kutoka Bungeni Dodoma

SERIKALI imesema sh 18.4 bilioni kutoka katika fedha zilizorudishwa za rada zitanunua madawati kwa shule za msingi na sekondani nchini.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI-Elimu) Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Martha Mlata (CCM).
Mlata alitaka ufafanuzi ni kiasi gani cha fedha kilichotengwa kutokana na fedha za rada kitakachotumika kupunguza tatizo la madawati kwa shule nyingi nchini.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Musoma Mjini Vicent Nyerere (CHADEMA) alitaka kujua serikali imejipanga vipi kukabiliana na upungufu wa madawati kwa shule zote nchini.
Naibu Waziri alisema mwaka wa fedha 2009/10 serikali ilitoa kiasi cha sh bilioni moja kwenda katika mamlaka za serikali za Mitaa kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa shule za sekondari.
Mwaka 2010/11 serikali ilitoa tena sh bilioni tatu kwa ajili ya kununua madawati kwa shule za msingi kwa utaratibu wa kupeleka fedha kwenye halmshauri.
Hata hivyo alisema walimu wakuu wa shule nchini wamepewa mamlaka ya kutumia fedha zinazotengwa kufanyia ukarabati madawati yanayoharibika.
Kwa upande wake Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Mkuchika alisema kuwa serikali iko mbioni kukamilisha waraka utakaosambazwa na Waziri Mkuu nchi nzima kuelezea kuwa huu ni mwaka wa kumaliza tatizo la madawati kwa shule zote.

Mil.12/- zawafuta jasho walioharibiwa mashamba

JIBU LA SWALI LA MBUNGE Biharamulo magharibi


KIASI cha sh milioni 12.4 zimetumika kuwafuta machozi wakulima wenye mashamba yaliyoharibiwa na wanyamapori wilayani Karagwe, Kagera.
Fedha hizo zimetolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo jumla ya wakulima 124 walinufaika.
Aidha, wizara hiyo imelipa jumla ya sh mil. 12.4 kwa ajili ya kufuta machozi na jasho kwa wananchi waliopata madhara kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict Ole-Nangoro, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Biharamulo Magharibi Dk. Anony Mbassa (CHADEMA) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Mbunge huyo alitaka kujua pamoja na mambo mengine, iwapo wananchi wanaopakana na Hifadhi ya Burigi kama wamelipwa fidia kutokana na uharibifu wa mashamba na madhara kwa binadamu unaofanywa na tembo, nyati na wanyama wengine wakali.
Alitaka kujua kiasi cha fidia kilicholipwa kati ya mwaka 2000 na mwaka 2011.
Akijibu swali hilo Ole-Nangoro alisema jumla ya wananchi saba wamelipwa fedha za kifuta machozi kwa madhara waliyopata kutokana na wanyamapori wakali katika wilaya za Ngara na Karagwe.
“Tangu mwaka 2005 hadi 2006 kiasi cha sh 250,000 kililipwa kwa familia za marehemu wanne waliouawa na tembo na watatu waliojeruhiwa,” alisema naibu waziri huyo.
Alisema wizara hiyo hutoa asilimia 25 ya fedha zinazotokana na mapato ya uwindaji wa kitalii katika pori la Akiba la Burigi kila mwaka ambapo hupelekwa kwenye halmashauri za wilaya husika kwa ajili ya maendeleo ya jamii.