
Marehemu Kanumba
NI BAADA YA JOPO LA MADAKTARI MUHIMBILI KUMFANYIA UCHUNGUZI, BABA YAKE AZUNGUMZA, WABUNGE WAMLILIA Florence Majani na Suzzy Butondo
MSANII
nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba amefariki dunia kutokana na
tatizo la mtikisiko wa ubongo linalojulikana kitalaamu kama Brain
Concussion, taarifa za kitabibu zimeeleza. Taarifa hizo za ndani,
zilizopatikana jana baada ya jopo la madaktari bingwa watano wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo,
zimeeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara
moja au baada ya siku kadhaa. Mmoja wa madaktari hao ambaye aliomba jina
lake lisitajwe gazetini alisema waligundua tatizo hilo baada ya
kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.
“Tulianza
kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa
6:45 mchana na tukagundua kuwa marehemu alifariki kutokana na mtikisiko
wa ubongo kwa kitaalamu, Brain Concussion,” alisema daktari huyo.
Alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo ambao husababisha kufeli kwa
mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure) “Kilichomuua hasa ni
mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu ya nyuma ya
ubongo (cerebrum), huua kwa haraka” alisema daktari huyo na kuongeza
kuwa mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa
upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wake.
“Baada ya ubongo
wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndiyo maana
tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake
yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo ndizo dalili
za kufeli kwa mfumo wa upumuaji.”
“Mtu aliyepata mtikisiko wa
ubongo huweza kutokwa na mapovu mdomoni na hukoroma kabla ya kukata roho
na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki.”
Daktari
mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo ambaye pia aliomba jina lake
lisitajwe alisema ubongo wa mwigizaji huyo ulikuwa umevimba na kushuka
karibu na uti wa mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji.
Alisema
sehemu ya maini na majimaji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine
katika mwili huo.
Baba mzazi azungumza Baba mzazi wa mwigizaji
huyo, Charles Musekwa Kanumba alisema kwamba alipata taarifa za kifo cha
mwanawe Jumamosi saa 10:00 alfajiri baada ya kupigiwa simu na dada wa
marehemu, Sara Kanumba. “Sara aliniuliza: ‘Una taarifa yoyote kuhusu
mwanao Kanumba?’ Nikamjibu kuwa sina taarifa yoyote, ndipo aliponieleza
habari za kifo hicho. Aliniambia Kanumba hatupo naye tena amefariki kwa
kuanguka, amekorofishana na mpenzi wake.” alisema taarifa hizo
zilimsababisha aishiwe nguvu kwa kuwa kilikuwa kifo cha ghafla… “Basi
kuanzia hapo, nilianza kupigiwa simu za kupewa pole, ndipo nilipoamini
kumbe mwanangu amefariki.”
Akizungumzia kuchelewa kufika
msibani, alisema kumetokana na tatizo la mawasiliano. Awali, alikuwa
amepanga mtoto wake Kanumba akazikiwe Mwanza kwa babu yake ndiyo maana
hakufika mapema msibani. “Nilikuwa nimepanga apitishwe hapa kwangu
Shinyanga aagwe, halafu tumpeleke Mwanza kwa babu yake kumzika huko
lakini alipokuja mama yake alinishauri kuwa huko kutakuwa na nafasi
ndogo kwa sababu watu ni wengi pia alikuwa na marafiki wengi, wengine wa
kutoka nje ya nchi kwa hiyo alinishawishi na tukakubaliana kumzika Dar
es Salaam,” alisema.
Pia alikanusha uvumi kuwa hajafika msibani
kwa kuwa walikuwa na ugomvi na marehemu akisema walishamaliza tofauti
zao. Alisema anatarajia kufika leo usiku tayari kushiriki mazishi hayo.
Wabunge
kilio Jana, baadhi ya wabunge waliofika nyumbani kwa marehemu Kanumba
waliangua vilio wakati walipotoa salamu zao za rambirambi.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Martha Mlata hakuzungumza na badala yake aliimba
kipande cha wimbo uliozungumzia kifo na maneno ya wimbo huo yalionekana
kuwagusa wafiwa na kusababisha vilio kuanza upya huku baadhi wakipoteza
fahamu.
Mbunge mwingine, Neema Mwinyimgaya aliongeza majonzi
masibani hapo alipounganisha msiba huo na wa mama yake… “Mama yangu
amefariki miezi mitatu iliyopita, huko uliko mama, nakuomba umpokee
kijana mwenzetu,” alisema mbunge huyo na kushindwa kuendelea.
Wabunge
wengine waliohudhuria msiba huo ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini),
Aboud Juma (Kibaha Vijijini), Mussa Azan Zungu (Ilala), Abbas Mtemvu
(Temeke), Peter Serukamba (Kigoma Mjini) na Ritha Kabati (Viti Maalumu).
Kova
na mchango wa Kanumba Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema anakumbuka mchango wa Kanumba katika kuzuia
uhalifu jijini.
“Tulishirikiana naye pamoja na wasanii wengine
kuandaa bonanza maalumu ambalo lilidhamiria kukabiliana na uhalifu hapa
jijini na kwa kweli mchakato ule ulifanikiwa kwani uhalifu ulipungua kwa
kiasi kikubwa” alisema Kova.
“Kifo chake kimekuwa cha ghafla mno na
nafikiri kujiweka tayari (kiimani) ni jambo ambalo kila mmoja anatakiwa
kuwa makini nalo katika maisha yake,” alisema Kova.
Ratiba ya mazishi
2:30
- Msafara kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Barabara ya Umoja
wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club.
3:30 - Misa ya kumuombea na salamu mbalimbali.
6:00 – Kuaga
9:00 - Kuelekea Makaburi ya Kinondoni kupitia Barabara ya Tunisia
SAHIHISHO
Rais
Jakaya Kikwete jana alilazimika kubadili ratiba yake ya safari za ndani
ya nchi ili kwenda kujumuika na waombolezaji wengine katika msiba wa
msanii nguli, Steven Kanumba na hakuwa na safari nje ya nchi kama
ilivyoripotiwa na gazeti hili jana. Mhariri
Habari na Mwananchi