NJOMBE

NJOMBE

clock

Wednesday, April 11, 2012

Safari ya mwisho ya Kanumba

MAELFU WAJITOKEZA KUMZIKA, WATU 600 WAPOTEZA FAHAMU, POLISI WASEMA HAWAKUTARAJIA UMATI MKUBWA HIVYO

MAELFU ya waombolezaji jana walijitokeza katika mazishi ya msanii nguli wa filamu Tanzania Steven Kanumba (28), yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam. Alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu.Kabla ya kuzikwa, mwili wa marehemu Kanumba ulipelekwa katika Viwanja vya Leaders ili kuwawezesha waombolezaji kutoa heshima za mwisho. Hata hivyo, ni wachache waliobahatika kupata fursa hizo baada ya kutokea msongamano mkubwa ulioifanya kamati ya maandalizi ya mazishi hayo kusitisha mchakato huo.

Inakadiriwa kuwa waombolezaji wapatao 600 walianguka kutokana na ama msongamano au majonzi ya kifo hicho cha ghafla cha msanii huyo.

Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Mke wa Rais, Salma Kikwete na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe walikuwa wa kwanza kutoa heshima zao za mwisho na kufuatiwa na viongozi wengine wakiwamo wabunge.

Baada ya viongozi hao kutoa heshima zao za mwisho, Dk Bilal na Mama Kikwete waliondoka na kwa mujibu wa ratiba, ilikuwa zamu ya waombolezaji wengine kuaga.

Hata hivyo, kulitokea msongamano mkubwa wa watu kila mmoja akitaka kulifikia jeneza na kulishika. Ilibidi vyombo usalama na walinzi binafsi kufanya kazi ya ziada kurejesha hali ya utulivu katika eneo hilo.

Kutokana na utaratibu mbovu katika kuendesha shughuli hiyo, ratiba ilikatishwa na mwili kuondolewa saa 6:30 kupelekwa makaburini. Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi iliyokuwa imetolewa juzi, muda wa kuaga ulipangwa kuanza saa 6:00 hadi saa 9:00 alasiri.

Badala yake, waombolezaji walitakiwa kujipanga kando ya Barabara ya Tunisia ambako gari lililobeba mwili wa msanii huyo lilipita kuelekea makaburini.

Haikuwa kazi rahisi kwa waombolezaji hao ambao baadhi walifika hapo alfajiri kwa ajili ya kutoa heshima zao mwisho kukubaliana na agizo hilo.

“Hatuwaelewi hawa. Sisi hatukuja kuliona jeneza tunataka kumuona ili tujue kama kweli amekufa. Hawa walioandaa utaratibu huu mbovu ni kina nani jamani au wameshindwa kazi?” alisema mmoja wa waombolezaji na kisha kuangua kilio.

Baada ya hali kutulia umati huo wa waombolezaji ulianza kulisindikiza gari la marehemu kwa nyuma huku wengine wakitaka jeneza hilo lishushwe ili walibebe.

Wakati msafara huo ukielekea makaburini, baadhi ya waombolezaji walikuwa wakianguka na wengine kuzirai baada ya kuona jeneza na kuwafanya watoa huduma wa Msalaba Mwekundu kufanya kazi kubwa ya kuwasaidia na kuwapeleka baadhi yao hospitali.

Licha ya umbali kati ya Viwanja vya Leaders na Makaburi hayo ya Kinondoni kuwa karibu, msafara huo ulichukua takriban saa mbili kufika kutokana na kwenda taratibu ili kutoa fursa kwa waombolezaji ambao baadhi yao walilazimika kupanda juu ya miti, kutoa heshima zao.

Baada ya kufika makaburini, iliwalazimu polisi kuongeza nguvu kudhibiti umati huo na kutoa fursa kwa ibada ya mazishi kuendeshwa kama ilivyopangwa.

Wazirai

Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya mazishi hayo, Dk Nassoro Ally alisema watu wapatao 600 walizirai katika viwango tofauti kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya watu kujaa na kubanana na hivyo kukosa hewa.

“Watu wamebanana na kukanyagana. Wemekosa hewa na wengine kati yao wanakabiliwa na matatazo ya kiafya, ugonjwa wa pumu, shinikizo la damu ingawa wapo waliokanyagana na kuanguka kutoka katika miti na kupoteza fahamu,” alisema Dk Ally.

Baadhi ya waombolezaji waliozirai ni pamoja na wasanii Wema Sepetu, Jacqueline Wolper na Irene Uwoya.

Wema alizirai baada ya kufika makaburini na Wolper alifikwa na hali hiyo katika Viwanja vya Leaders.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema watu waliopoteza fahamu hawazidi 30.

Alisema watu waliofika kuaga mwili huo walikuwa ni zaidi ya matarajio yao na kuongeza kwamba kwa mazingira shughuli hiyo, eneo hilo lilikuwa dogo akisema sehemu muafaka ilipaswa kuwa Uwanja wa Taifa.

Kauli za viongozi
Akitoa salamu kwa niaba ya Serikali, Dk Nchimbi alisema huu ni mwaka wa mwisho kwa wasanii kuibiwa kazi zao.
Dk Nchimbi ambaye katika salamu zake pia alitoa ubani wa Sh10milioni kwa niaba ya Serikali, alisema wizara yake ikishirikiana na Wizara ya Fedha, Wizara ya Kazi na Ajira na Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff), wameshakutana na kujadiliana namna ya kuzuia wizi katika kazi za wasanii.

“Mwaka huu ndiyo mwisho wa kazi za wasanii kuibiwa na nilipenda sana kuona Kanumba akishuhudia jitihada hizi ambazo tumekuwa tukizifanya naye kama mdau mkubwa wa sekta hii,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Jitihada ambazo amezifanya Kanumba enzi za uhai wake ni dhahiri zimejionyesha leo. Mmejitokeza kwa wingi kuja kumuaga hivyo wasanii mnaobaki mnatakiwa kuiga kile alichokuwa akikifanya.”

Rais wa Taff, Simon Mwakifwamba alisema marehemu Kanumba ameacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu kutokana na mchango wake mkubwa aliouonyesha katika kipindi kifupi cha uhai wake.

“Kanumba alikuwa balozi pekee wa filamu nchi za nje. Aliitangaza nchi yetu kupitia tasnia ya filamu hivyo tutamkumba daima kwa kutuonyesha njia,” alisema Mwakifwamba.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amewataka wasanii nchini kufuata nyayo za Kanumba na kumkumbuka msanii huyo milele.

“Watanzania wengi wana majonzi makubwa lakini watambue kwamba ni kazi ya Mungu. Kinachotakiwa sasa hili litumike kama somo kwa wasanii wengine kwani leo tunashuhudia Kanumba akiagwa kama mfalme kutokana na kazi yake nzuri aliyokuwa anaiwasilisha kwa Watanzania,” alisema Nape.

Askofu wa Kanisa la African Inland Church (AIC), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Charles Salala alisema msiba wa Kanumba ni pigo kwa taifa na kuwaasa Watanzania kutenda mambo mema ili kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii.

“Leo tupo katika msiba wa mtu ambaye alikuwa ana mchango mkubwa kwa jamii, ndiyo maana tunashuhudia umati mkubwa wa watu ukiwa umekusanyika hapa, lakini jambo ambalo sisi kama binadamu tunatakiwa kufanya ni kuishi maisha mema na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ,” alisema na kuongeza:

“Marehemu Kanumba aliwahi kuhudumu katika kanisa hili na alikuwa ni mtu mwenye upendo kwa kila mtu ndiyo maana leo maelfu ya Watanzania tupo hapa kumsindikiza ndugu yetu katika safari yake ya mwisho.”
Habari na Mwananchi,Video na Dj Choka.

No comments:

Post a Comment